Jumapili ya Huruma ya Mungu: Injili, Umoja, Ekaristi na Sala!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari masomo ya dominika ya Pili ya Pasaka, dominika ambayo pia inaitwa dominika ya Huruma ya Mungu. Kristo mwenyewe analialika Kanisa zima kuitazama Huruma yake kuu kwa wanadamu na kwa ulimwengu mzima kuwa ni tunda la kipasaka, ni tunda la ufufuko wake. Hata katika kipindi hiki ambacho dunia imejaa hofu na uchungu mkubwa kwa janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mungu anajidhihirisha kuwa yupo nasi na Huruma yake haijakoma kutuimarisha, kutufariji na kututakasa. Somo la kwanza (Mdo. 2:42-47) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Kimsingi kitabu hiki kinaelezea hali ya kanisa la mwanzo ilivyokuwa baada ya ufufuko wa Kristo. Jambo linalojitokeza waziwazi ni kuwa baada ya Kristo kufufuka, mitume walianza mara moja na tena kwa ujasiri mkubwa kumhubiri Kristo. Somo hili la leo linaonesha sasa matokeo ya mahubiri yao hayo kuwa ni kuongezeka kwa waamini na kujengeka kwa jumuiya ya kwanza ya wakristo. Ni hapa ndipo lilipo chimbuko la kibiblia la muundo wa kichungaji tulionao hadi sasa, yaani muundo wa Jumuiya ndogondogo za Kikristo. Katika kipindi cha Mitume, Jumuiya ndogo ndogo ndio ulikuwa muundo wa Kanisa lenyewe.
Somo linajikita kueleza mihimili minne ya jumuiya hiyo: fundisho la mitume, ushirika, kuumega mkate na sala. Fundisho la Mitume ndiyo Habari Njema waliyoihurubiri, yaani Kristo mwenyewe. Jumuiya ya kikristo ni lazima imuelewe Kristo ili iweze kujikita vema katika msingi wa imani na maisha aliouacha. Msingi wa ushirika ni umoja na mshikamano unaopaswa kuonekana kwa nje katika maisha ya wanajumuiya. Hiki ndicho kiliwasukuma kuweka vitu vyao vyote pamoja na kuishi kama familia moja. Kuumega mkate ni adhimisho la Ekaristi, yaani Misa Takatifu. Adhimisho hili lilikuwa ni kuifanya hai kati yao Pasaka ya Bwana, yaani kumbukumbu la Mateso, Kifo na ufufuko wa Kristo , adhimisho ambalo ndio kiini cha maisha ya Mkristo. Na mwisho ni msingi wa sala, muungano wa kiroho kati yao na Mungu. Somo hili kwetu ni mwaliko wa kuzipima jumuiya zetu za Kikristo chini ya mihimili hiyo minne ya Jumuiya ya kwanza ya kikristo. Ni mwaliko pia wa kujibidiisha kuzifanya upya ili ziweze kuakisi roho ile ile ya jumuiya ya mitume katika mazingira yetu ya sasa.
Somo la pili (1Pet 1:3-9) ni kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa watu wote. Katika waraka huu, Petro anawaandikia wakristo wapya, yaani wale ambao ni punde tu wamepokea ubatizo. Utamaduni uliokuwapo ni kuwa mafundisho ya ubatizo yalitolewa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ilikuwa ni mafundisho ya kuwaandaa wakatekumeni kupokea ubatizo na awamu ya pili ilikuwa ni mafundisho waliyopewa baada ya ubatizo. Haya yaliitwa “mistagojia” na ndiyo yalikuwa mafundisho ya kina kuhusu imani waliyoikiri na kuipokea kwa ubatizo. Mtume Petro katika mafundisho yake haya anawaonesha wabatizwa kuwa ubatizo walioupokea ni tunda la ufufuko wa Kristo. Ni kwa sababu ya ufufuko wa Kristo, wote wanaobatizwa wanapata urithi usioharibika, uliokuwa umeandaliwa tayari mbinguni. Na hiyo ni sababu tosha ya kila mbatizwa kujawa na furaha.
Hata katika furaha hiyo, Mtume Petro haachi kuwakumbusha kuwa safari ya imani waliyoianza kwa ubatizo inaambatana na majaribu na magumu mbalimbali ya kiimani. Anayalinganisha majaribu hayo na tendo la kusafisha dhahabu. Ili kupata dhahabu halisi ambayo haijachanganyikana na madini mengine, jiwe la dhahabu hupitishwa kwenye moto mkali ili liyeyuke na kujichuja. Petro anachukulia mfano huo huo na kuelezea kuwa majaribu ya kiimani hulenga kuichuja na kuisafisha imani. Yeye anayevumilia pamoja na Kristo katika majaribu hayo, ataifikisha salama imani hiyo katika siku ya mwisho.
Injili (Yoh. 20:19-31) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Yohane. Yesu anadhihirisha ufufuko wake kwa kuwatokea wanafunzi wake. Tendo hili linakuwa ni uthibitisho kuwa kweli amefufuka na siyo kwamba mwili wake uliibwa kutoka kaburini. Yesu anawatokea wanafunzi milango ikiwa imefungwa na wao wakiwa ndani kwa hofu. Anatambulisha itakayokuwa namna yake mpya ya kuwa pamoja na wanaomwamini. Anaweza kuingia mahala popote katika moyo wa kila ambaye ana kiu naye. Anapoingia anawasalimu “Amani iwe kwenu”. Kwa salamu hii anatangaza kuanza kwa awamu mpya, awamu ya uwepo wa amani iliyokuwa imekosekana ulimwenguni kwa sababu ya kuenea kwa utawala wa dhambi na mauti. Yesu kwa ufufuko wake ameishinda dhambi na ameyashinda mauti hivyo ni haki kabisa sasa kutangaza amani. Kile kilichoashiriwa na malaika, walipoimba usiku ule alipozaliwa, utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mapema, sasa kwa ufufuko wake amekitimiza. Ndivyo alivyotumwa na Baba na sasa Yeye naye anawatuma wanafunzi wake waieneze duniani.
Tangazo hilo la amani linafuatiwa na tendo lingine kubwa zaidi, anawavuvia Roho Mtakatifu na anawapa mamlaka ya kuadhimisha Sakramenti ya maondoleo ya dhambi. Lugha ya kibiblia inayotumika, yaani “kuwaondolea dhambi na kuwafungia dhambi” inamaanisha kuwapa mamlaka kamili, na kwa mamlaka hayo wanafunzi wake hao watatenda vile vile kama anavyotenda yeye mwenyewe. Simulizi la Mtume Tomaso ambaye hakuwapo Yesu alipotokea na ambaye alipokuja akasema hataamini hadi aone makovu ya misumari katika mwili wa Yesu, linakuja ili kukazia jambo moja muhimu ambalo ni imani. Bila imani ni vigumu kuuona uwepo wa Yesu kama walivyouona wanafunzi wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu; bila imani ni vigumu kuona kuwa amani ya kweli duniani ni ile tu iliyo na msingi wake katika Kristo na tena bila imani ni vigumu kuiona nguvu waliyopewa Mitume ya kuondolea dhambi kwa huduma ya kanisa. Yesu anaalika kuwa na paji la imani anaposema “wewe kwa kuwa umeniona umesadiki, wana heri wale wasiiona wakasadiki”. Imani ni ufunguo wa kuyapokea matunda ya ufufuko wa Kristo.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika hii ya pili ya Pasaka inatupatia nafasi ya kuadhimisha sherehe ya Huruma ya Mungu. Kristo mwenyewe aliagiza kuadhimishwa kwa sherehe hii pale alipomtokea Mtakatifu Faustina na kumwambia; “Dominika inayofuatia dominika ya Pasaka ninataka iadhimishwe Sherehe ya Huruma ya Mungu. Mwanangu, utangazie ulimwengu wote juu ya Huruma yangu isiyo na kikomo. Katika siku hiyo nitafungulia milango yote ya Huruma yangu na roho itakayopokea Maungamo na Ekaristi Takatifu siku hiyo itapata maondoleo ya dhambi pamoja na adhabu zake zote.” Baba Mtakatifu Francisko anafundisha kuwa “huruma ndilo jina lingine la Mungu”. Hii ni kweli kwa sababu historia nzima ya wokovu wa mwanadamu, ni historia inayomfunua Mungu kuwa ni Bwana aliyejaa Huruma na neema (Rej Zab. 103:8).
Tunaweza kusema pia kuwa kama jinsi ambavyo Mitume walikuwa wamejifungia ndani kwa hofu, ndivyo pia mwanadamu katika mwendo wa maisha amejikuta amejifungia ndani yeye mwenyewe kwa sababu ya udhaifu wake wa kibinadamu na kupoteza kabisa tumaini la kuinuka na kuanza upya safari ya kuishi kitakatifu. Sherehe ya leo inamkumbusha mwanadamu aliyejikatia tamaa katika udhaifu wake, mahangaiko ya Yesu kama alivyojifunua kwa Mtakatifu Faustina, “kwa nini watu wangu wanapotea wakati huruma yangu ipo”? Ni sherehe inayotualika basi kutambua uwa huruma ya Mungu ni kubwa kuliko udhaifu wa mwanadamu. Na yeyote anayeikimbilia kwa toba ya kweli na moyo wa kujibandua kutoa maisha ya dhambi, ataikuta wazi daima milango ya Huruma na ataikuta wazi mikono ya Baba mwenye Huruma tayari kumpokea na kumkaribisha ndani kama katika mfano wa Mwana Mpotevu (Lk. 15). Adhimisho la Sherehe hii huruma ya Mungu liwe kwetu kichocheo cha kukuza imani na kutufanya wenyewe kuwa vyombo vya Huruma ya Mungu kati ya wenzetu.