Jumapili ya Huruma ya Mungu: Madonda Matakatifu ya Yesu!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma
Amani na Salama! Sehemu ya Injili Takatifu ya Jumapili ya Huruma ya Mungu imegawanyika katika sehemu kuu mbili, kwanza ni Yesu anawavuvia Roho Mtakatifu wafuasi wake na hivyo kuwapa uwezo dhidi ya uovu na yule mwovu, na ndio kuwaondolea watu dhambi. Na sehemu ya pili ni ile ya Mtume asiyeamini bila kuona na kugusa madonda yake Yesu, ndiye Tomaso Pacha. Mwinjili Yohane anamtambulisha kama pacha, ndio kusema ni pacha wa kila mwamini na kila mmoja wetu, ni kielelezo cha kila mmoja wetu kama tutakavyoona katika tafakari yetu ya leo. Yesu kabla ya kuwavuvia Roho Mtakatifu, anawasalimu wanafunzi wake kwa kuwatakia amani. Kristo Mfufuka pia nasi leo anatusalimu kwa kututakia amani na hasa sisi tunaosafiri leo katika nyakati hizi ngumu katika historia ya mwanadamu, nyakati ambazo tunajifungia ndani kwa hofu na mashaka makubwa, si hofu kama ile ya wanafunzi wa mwanzo wa Yesu wakiwaogopa wayahudi bali sisi leo kwa hofu ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.
Kristo Mfufuka anatutakia amani na hivyo kuishinda kila aina ya hofu na mashaka tunayokuwa nayo katika maisha yetu ya siku kwa siku. Niliwaalika Dominika iliyopita kuwa turejee katika Pasaka ile ya mwanzo kabisa, ambapo Mitume hawakuisherekea katika Makanisa makubwa tunayokuwa nayo leo bali pale nje ya kaburi lililokuwa wazi, wengine wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu na mashaka makubwa. Kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake, Bwana wetu Yesu Kristo tayari anawafundisha wanafunzi wake kuwa Yeye ndio Uzima na Ufufuo. Hivyo baada ya ufufuko wake anapowatokea wanafunzi wake siku ile ya kwanza ya Juma anawadhihirishia waziwazi Mitume wake kuwa kweli ni Mzima na kuwasalimu kwa kuwatakia amani iwe nao. Ni kweli Yeye mzima! Tukiwa na imani kwake hatuna sababu ya kuwa na mashaka wala wasiwasi wa chochote kile, kwani tuna hakika kuwa Kristo ni mzima hata kama tutakufa tutaishi milele. Na hata anawapa zawadi ya Pasaka Mitume wake kwa kuwavuvia Roho Mtakatifu.
Ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu wanapokea uwezo wa kusamehe dhambi, kuwa wagawaji wa Huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake, na ndio kwa msamaha wa dhambi nasi tunapata kushiriki uzima wa kweli, yaani maisha ya urafiki na neema. Mtakatifu Yohane Paulo II aliitenga Dominika ya Pili ya Pasaka kuwa ni Dominika ya Huruma ya Mungu. Kristo anakufa na kufufuka ili sisi tupate uzima wa milele. Kipindi cha Pasaka ni wakati mzuri tunaalikwa kutafakari upendo na huruma ya Mungu. Upande wa pili tunakutana na Mtume Tomaso kama kielelezo cha wale wote wanaopata ugumu katika safari ya kuamini ufufuko wa Kristo. Tomaso kinyume na wanafunzi wengine wa Yesu waliokuwa wamejifungia ndani kwa hofu, yeye anatoka nje bila woga wala hofu, lakini pia tunajiuliza alikwenda wapi? Hatujui kwa hakika kwa nini Mwinjili Yohane anamtumia Mtume Tomaso kama kielelezo kwani kwa hakika ugumu ule haukuwa wa Mtume Tomaso peke yake na hata zaidi sana kumwonesha Tomaso kuwa hakuwa na hofu ya Wayahudi na kujikuta hayupo wakati Kristo Mfufuka alipowatokea wanafunzi wake.
Mwinjili Yohane anatuonesha tangu mwanzoni kuwa wanafunzi au wafuasi wa Yesu walimwona Yesu Mfufuka. Neno kuona katika lugha ya Kigiriki linaweza kueleweka kama ‘’blepo’’ (βλεπω) likiwa na maana ya kuona kwa macho ya kawaida au macho ya nyama, lakini Mwinjili Yohane hatumii neno hilo na badala yake anatumia neno ‘’orao’’ (οραω), likiwa na maana sio tu kuona kwa macho ya nyama bali kuona na kutambua kiundani, ni sawa na kung’amua, hivyo ni sawa na kusema walimng’amua Kristo Mfufuka, ndio kuona na kung’amua kwa jicho la imani. Haitoshi tu kumuona Kristo Mfufuka bali tunaalikwa kumtambua, kumng’amua katika undani wa maisha yetu. Mwinjili Marko anathibitisha hilo pale anapotuonesha kuwa Kristo Mfufuka anawatokea Mitume na kuwaonya juu ya kutokuamini kwao. (Marko 16:14) Mwinjili Luka naye anatuonesha kuwa Kristo Mfufuka anapowatokea Mitume wake wanafadhaika na kuwa na woga. (Luka 24:38) Na Mwinjili Mathayo naye kwa upande wake anatuonesha kuwa aliwatokea Mitume wake katika Mlima Galilaya na baadhi yao walikuwa bado hawajaamini. (Mathayo 28:17). Hivyo kwa kuangalia Injili pacha tunaona wazi kuwa wote walikuwa na mashaka ya kuamini na hivyo siyo Tomaso mtume peke yake kama anavyotuonesha Mwinjili Yohane.
Mwinjili Yohane anapoandika Injili yake ni karibia mwaka 95 BK, na hivyo ni kitambo tangu Mtume Tomaso alipofariki kifo dini. Si lengo la Mwinjili Yohane kutuonesha au kutupa picha hasi ya imani ya Mtume Tomaso. Kwa makusudi mazima anapowaandikia kizazi cha tatu cha wakristo, hivyo wengi wao kama si wote hawakumuona Kristo Mfufuka kwa macho yao na hata wengine hawakufahamu hata Mitume waliokutana na Kristo Mfufuka. Hivyo kwao ilikuwa ngumu kuamini na hivyo walibaki na mashaka makubwa juu ya ufufuko wake Kristo. Wakati Wainjili wa Injili pacha wanatuonesha waziwazi kuwa Mitume wote walikutwa na ugumu wa kuamini na hata baada ya kutokewa wengine walibaki na mashaka. Hivyo safari yao ya imani tunaona ni ngumu na ya kukatisha tamaa wakati fulani. Na ndio hapo tunaona Mwinjili Yohane anamtumia Mtume Tomaso kama kielelezo si kwake peke yake bali kwetu sote linapokuja swala la kuamini juu ya “Kerygma” ya Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo.
Kristo anapowatokea wafuasi wake siku ile ya kwanza ya juma hawaaliki kumwangalia uso au sura yake ili wamtambue bali anawaonesha mikono yake na ubavu wake. Kitambulisho cha Kristo Mfufuka ni mikono na ubavu wake. Ni upendo na huruma yake. Na ndio anatualika nasi katika kipindi hiki kuangalia mikono na ubavu wake, ni katika mikono yake na ubavu tunauona upendo na huruma yake ya Kimungu, tunauona wokovu wetu. Wanafunzi wa Yesu hawaishii tu kuona makovu katika mikono na ubavu wake bali zaidi sana upendo na huruma ya Mungu kwa kila mmoja wetu, ni kuona kwa jicho la imani, ndio ‘’orao’’ kama tulivyoona hapo juu. “Kerygma" ya ufufuko sio ukweli wa kisayansi hivyo kuweza kudhibitishwa kwa njia za ufahamu au akili zetu za kibinadamu, hivyo kuweza kuushika na kuuona kwa macho yetu ya kibinadamu. Ni lengo la Mwinjili Yohane kuwa Kristo Mfufuka yu hai ila si tena na mwili ule wa nyama bali sasa na mwili wa ufufuko, mwili wa utukufu na ndio maana tunaona mara kadhaa anawatokea wale watu wake wa karibu alioambatana nao kila siku na bado hawakuweza kumtambua. Kristo Mfufuka sasa ana mwili wa utukufu usioshikika wala kuonekana kwa macho ya kimwili bali tunaweza kuuona na kuushika kwa jicho la kiimani tu. Imani tu itoshe!
Sisi leo tungeweza kusema heri wao waliomuona kwa macho Kristo Mfufuka ila Kristo anabadili mantiki yetu ya kibinadamu kuwa heri wanaoamini bila kuona wala kugusa. Mwinjili Yohane anamtumia Mtume Tomaso mara kadhaa katika Injili yake kama mfano wa yule anayekuwa na ugumu katika kuelewa na kuamini katika mafundisho na leo juu ya Kerygma ya Ufufuko. Wakati Yesu anapomjalia tena uzima Lazaro tunaona Mtume Tomaso anawaalika Mitume wengine waende pamoja na Yesu ili wafe naye. (Yohane 11:16) Na hata katika karamu ya mwisho tunaona anapata shida kuelewa mafundisho ya Yesu kama Njia. (Yohane 14:5) Mtume Tomaso pia ni kielelezo cha Wayahudi ambao daima walitaka ishara kadiri ya Mtume Paulo. (1 Wakorintho 1:22) Na hata Mwinjili Yohane pia anaonesha jinsi Yesu alipokuwa anawaonya wasikilizaji wake kuwa wasipoona miujiza na ishara kamwe hawataamini. Baada ya safari ngumu ya imani kwa Mtume Tomaso tunaona mwishoni Mwinjili Yohane anatuonesha jinsi alivyoweza kukiri imani yake mbele ya Kristo Mfufuka. Na ni moja ya Kukiri Imani ya mmoja mwenye Imani thabiti kabisa kwa Kristo na ndiyo Mtume Tomaso anakiri juu ya Umungu wake Kristo. Anamtambua Kristo Mfufuka kama Bwana na Mungu. Na ndio daima katika Agano la Kale tunaona Wayahudi wanamtambua Mungu kama Bwana wao. (Zaburi 35:23)
Na ndio tunaona katika Kanisa leo sio tu mahali pa maskini na wagonjwa lakini pia kwa ajili ya hata wale wanaokuwa katika ugumu wa kuamini au wasio na imani, wenye mashaka na wasiwasi. Na ndio hao Mtume Paolo anawatambua kama wadhaifu ambao wanakwazika kirahisi hivyo hawana budi kusaidiwa na kuongozwa katika ukweli wote. Na ndio Mwinjili Mathayo anawatambua kama wadogo nao pia hawana budi kulindwa na makwazo. Ni wajibu wetu leo kuwaongoza wale wanaokuwa wadogo na dhaifu katika imani ili nao wafikie kuamini katika “Kerygma” ya ufufuko wake Kristo. Hitimisho la Injili ya Yohane anatuonesha sababu za kuandika Injili hii. Anatuambia kuwa anaandika baadhi tu ya ishara kwani kuna ishara nyingi alizifanya Yesu ila anatuchagulia baadhi tu kwa nia ya kutusaidia kufikia imani kwa Kristo Mfufuka. Ishara hizi daima zinamfunua Yesu kuwa ni Kristo wa Mungu, ni sura halisi ya Mungu. Ni kwa kuwa katika umoja na jumuiya nzima ya Kanisa nasi daima tunakutana na Kristo Mfufuka na ndio makusanyiko yetu ya kila Dominika. Nje ya jumuiya kama Mtume Tomaso hatuwezi kukutana na Kristo Mfufuka. Ni katika Meza ya Neno lake na Ekaristi nasi leo tunakutana na Kristo Mfufuka. Tunaalikwa daima kusafiri na kutembea pamoja na jumuiya, yaani Mama Kanisa ili tuweze kukutana na kumkiri Kristo Mfufuka.
Dominika ya leo pia tunaalikwa kuwa mikono na ubavu wa Kristo Mfufuka, kuwa wajumbe na mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu katika maisha yetu ya siku kwa siku na hapo kweli tunakuwa watu wa ufufuko. Haitoshi kuimba Alleluiya na wakati tunafunga mikono yetu na ubavu wetu kwa wale wanaotujia ili waonje upendo na huruma yake Kristo Mfufuka. Maisha yetu ili kumshuhudia Kristo Mfufuka ni mwaliko wa kuwaonesha wengine mikono na ubavu wa Kristo Mfufuka, kila mmoja wetu kama mfuasi wa Kristo hatuna budi kuwa mikono na ubavu wa Kristo Mfufuka, kuwa wajumbe wa huduma ya upendo na huruma yake kwa watu wote. Tunaalikwa kuwa faraja na amani kwa wale wote wanaokuwa mbali na jumuiya ile ya Kristo Mfufuka, mbali na ukweli ule wa Kristo Mfufuka. Maisha ya ‘’koinonia’’ ndio maisha ya ushahidi ya ufufuko wake Kristo, ndio maisha ya kuishi kindugu na kwa kupendana na kujaliana. Nawatakia tafakari njema na Dominika njema ya Huruma ya Mungu. Pasaka njema!