Jumapili ya Mchungaji Mwema: Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani 2020
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Leo Mama Kanisa anaadhimisha Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka sanjari na maadhimisho ya Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya unaongozwa na kauli mbiu: “Jipeni Moyo Ni Mimi Msiogope: Maneno ya Miito”: Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa. (Rej. Mt.14:22-33). Pentekoste ni tukio ambalo limeleta mageuzi makubwa katika historia na maisha ya Mitume wa Yesu na Kanisa katika ujumla wake. Leo tunakutana na Mtakatifu Petro Mtume, aliyepyaishwa kwa nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu, kiasi cha kuuvua ule utu wake wa kale uliochakaa kwa woga uliopelekea hata kumkana Kristo Yesu mara tatu! Katika hotuba yake ya kwanza, Mtume Petro anamwelezea Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ndiye Bwana, Masiha na Mkombozi wa Ulimwengu.
Fumbo la Pasaka ni kiini na chemchemi ya imani, toba na wongofu wa ndani. Kumbe, Wakristo wanapaswa kumfuasa kwa uaminifu na udumifu ili Kristo Mfufuka aweze kuyapyaisha maisha yao kadiri ya Mafundisho yake. Kwa ushuhuda huu, Petro Mtume, aliyetambulikana na wengi kama mvuvi wa Galilaya analipatia Kanisa la mwanzo Wakristo wapya elfu tatu, baada ya kumwongokea Kristo Mfufuka. Somo la Pili linamwonesha Mtume Petro akiwahubiria waamini waliokwisha kubatizwa kwa Maji na Roho Mtakatifu na sasa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Anawataka Wakristo kuwa ni mashuhuda na vyombo vya imani tendaji kwa kuendelea kujikita katika wema na udumifu mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu katika utakatifu, haki na msamaha ili kuweza kushikamana na kudumisha mafungamano na Kristo Yesu, ambaye amejitanabaisha kuwa ni Mchungaji mwema!
Katika Injili, Kristo Yesu anafafanua sifa za Mchungaji mwema, anayetambulikana kwa njia ya huduma, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, kiasi cha kuyamimina maisha yake ili yawe ni chemchemi ya maisha mapya na uzima wa milele. Ni Mchungaji anayejitaabisha kuwapeleka kondoo wake nje kwenye malisho ya kijani kibichi na kando ya maji ya utulivu, huwaongoza. Kristo ni mchungaji mwema, anayeguswa na mahangaiko ya waja wake: kiroho na kimwili. Kwanza kabisa anawaonea huruma, anawasamehe, anawatakasa na kuwaondolea dhambi zao, kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu mdhambi lakini mpendelevu machoni pa Mungu. Yesu ni mchungaji mwema, aliyewalisha na kuwanywesha watu, kiasi cha kuwarejeshea tena ile furaha iliyokuwa inaanza kutoweka taratibu kama umande wa asubuhi. Ni Mchungaji mwema anayesikiliza kwa makini na kutoa dira na mwongozo wa maisha kwa njia ya Mafundisho yake na muhtasari wa Mafundisho haya ni Amri Kuu ya Upendo, Sala ya Baba Yetu na Heri za Mlimani.
Ni mchungaji mwema kiasi kwamba, Kondoo wake wanaifahamu sauti yake! Waswahili wanasema, miruzi mingi humchanganya Mbwa! Huu ni mwaliko na wajibu wa Kondoo wa Kristo kumjifunza Kristo Yesu na hatimaye, kuanza ujenzi wa utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini Neno la Mungu linalopaswa kuwa kweli ni dira na mwongozo wa maisha ya Wakristo. Waamini waitambue sauti ya Kristo Yesu kupitia kwa viongozi wa Kanisa, matukio na historia ya maisha yao! Wachungaji wawe thabiti na imara katika imani. Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba, “Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika”. Ukweli unaotolewa na kushuhudiwa na Kristo Yesu ndio utakaowaweka waja wake huru. Yesu anasema “Jipeni Moyo Ni Mimi Msiogope”. Kristo Yesu ndiye mchungaji mwema anayeweza kutuokoa kutoka katika Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, hofu na mashaka, ikiwa kama tutaweza kuwa na ubavu wa kusoma alama za nyakati kwa kufikiri na kutenda kwa busara! Tumwombe Mwenyezi Mungu ili aweze kulijalia Kanisa lake vijana wenye ari na moyo mkuu; wema na watakatifu watakaoweza kujitosa katika miito mbali mbali ndani ya Kanisa.