Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili III ya Kipindi cha Pasaka: Muhimu: Safari ya Waamini! Liturujia ya Neno la Mungu, Liturujia ya Ekaristi na Ushuhuda wa maisha ya waamini! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili III ya Kipindi cha Pasaka: Muhimu: Safari ya Waamini! Liturujia ya Neno la Mungu, Liturujia ya Ekaristi na Ushuhuda wa maisha ya waamini! 

Tafakari Jumapili III ya Pasaka: Safari! Neno! Ekaristi! Ushuhuda

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya III ya Kipindi cha Pasaka ni mwaliko kwa Wafuasi wa Kristo Yesu kufunga safari ya maisha ya kiroho, ili kuweza kukutana na Kristo Mfufuka anayewafafanulia Liturujia ya neno la Mungu, ili hatimaye, katika maadhimisho ya Liturujia ya Ekaristi, waweze kukutana na Kristo Mfufuka katika maumbo ya Mkate na Divai! Tayari kumshuhudia Kristo Mfufuka!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Wafuasi wawili wa Emau nao kama ilivyo desturi ya wayahudi wengine walifika pia Yerusalemu kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe za Pasaka ya Kiyahudi. Hivyo wakiwa huko pia wanashuhudia matukio ya kuhukumiwa, kuteswa na hata kufa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Mwinjili Luka anawatambulisha pia kama wanafunzi na wafuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo, aliyekuwa Mwalimu wao, nabii mwenye nguvu katika matendo na maneno. Baada ya kumaliza Sherehe zile zilizogubikwa na majonzi ya mateso na kifo cha Bwana na Mwalimu wao wanaamua kurejea makwao, lakini siku ile ya kwanza ya Juma mapema asubuhi wanapata taarifa kuwa kaburi li wazi kwani wanawake walikwenda kaburini na kukutana na malaika na kuwatangazia kuwa Yesu amefufuka, yu hai mzima! Pamoja na kusikia Habari zile njema bado wanasukumwa kurejea makwao ili kuendelea na maisha yao ya kawaida. Wakiwa njiani ndio wanakutana na msafiri anayeambatana nao. Wataalamu wa Maandiko Matakatifu leo wanaibua mjadala mkubwa juu ya uwepo na umbali wa kijiji kinachotambulishwa kama Emau.

Ni kweli kuna kijiji kinachojulikana kama Emau lakini hakipatikani umbali wa kilometa 12 kutoka Yerusalemu bali takribani kilometa 30 kutoka Yerusalemu. Si tu tunakutana na utambulisho sahihi wa kijiji kile lakini hata uharaka wa wafuasi wale wa kurejea mara moja katika maisha yao ya awali bila kuchukua muda wa kufuatilia na kujiridhisha juu ya habari za Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Daima yafaa tukumbuke Mwinjili Luka anapoandika sio lengo wala shabaha yake kutupa kweli za kihistoria au kijiografia kwa nafasi ya kwanza bali kweli za kitaalimungu. Hivyo kwetu leo Emau ya kiroho ni kila tunapokuwa na kusanyiko la Kiliturujia kila Dominika, ni hapo tunakutana na Kristo Mfufuka katika ukamilifu wake na ndio katika Neno lake na katika kuumega mkate, ni hapo Kristo mfufuka anakaa katikati yetu na kutuonesha mikono na ubavu wake. Lakini kama wafuasi kwa nini walishindwa kumtambua Yesu njiani? Na Mwinjili anatumia lugha ya kusema kuwa macho yao yalikuwa yamefungwa katika kumtambua Yesu. Na pia kwa nini Mwinjili anamtaja kwa jina mmoja wa wale wafuasi na mwingine hamtaji? Je, Mwinjili amesahau jina la yule wa pili au nini hasa lengo na shabaha yake ya kumtaja mmoja tu?

Wanarejea tena Yerusalemu na kuwasimulia Mitume kuwa wamemuona Kristo Mfufuka na wao wanajuzwa pia kuwa Kristo Mfufuka amewatokea mitume. Na hata wanapokuwa katikati ya mazungumzo hayo Yesu anakuja na kukaa kati yao, na hata sasa bado wanabaki na hofu na uoga na kudhani kuwa ni mzimu, kwani bado hawakuwa wanaamini. Hata Yesu anawaalika kuamini kuwa sio mzimu kwani anakula samaki na mkate mbele yao. Kwa kweli kila mara tunasoma Maandiko na hasa juu ya Ufufuko wa Yesu Kristo tunaona ugumu unaotushangaza hata baada ya kuwatokea wanakuwa na mioyo na safari ndefu ya imani juu ya Kristo Mfufuka. Ni kutokana na kushindwa kusoma vema Maandiko tunajikuta hata nasi katika mazingira magumu ya kupata ujumbe kusudiwa. Ninawaalika kila mara tunaposoma Maandiko Matakatifu kusoma sio kama masimulizi ya kihistoria hata kama Mwinjili anatupa pia kweli za kihistoria bali kusoma na kuona kweli za kiimani, kweli za kitaalimungu zinazokusudiwa kila mara na Mwinjili kwa nafasi ya kwanza. Aliwafungua akili zao, ndio kazi ya Neno la Mungu kutufungua akili zetu ili tuweze kufikia ukweli wa imani, ni mdahalo na majadiliano ya kirafiki kati ya Mungu na mwanadamu, kama vile walivyozungumza walipokuwa njiani pamoja na Kristo Mfufuka ndivyo anatuvyotualika nasi leo kufanya majadiliano yale yale tunapokuwa katika safari yetu ya imani hapa duniani. Hatuna budi kumsikiliza ili atufafanulie na kutufundisha Neno la Mungu kwani ni taa ya kutuongoza katika maisha yetu.

Walipokuwa mezani pamoja na huyu msafiri anatwaa mkate, anabariki na kuumega na kuwapa. Na hata kabla ya kuketi pale mezani msafiri huyu anawaalika na kuwafafanulia Maandiko Matakatifu kuanzia Musa na Manabii, mpaka mioyo yao ikawaka kule njiani. Ndio kusema ni Adhimisho kamili la Ekaristi, linalokuwa na pande kuu mbili. Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi. Mwinjili Luka anawaandikia Jumuiya ile ya waamini wa uzao wa tatu baada ya ufufuko wake Bwana wetu Kristo ambao baadhi walianza kupoteza imani na hata kutaka Kristo Mfufuka awatokee kama alivyofanya kwa wanafunzi wale wa mwanzo. Mwinjili Luka anaona anao wajibu wa kuwaandikia na kuwaimarisha katika imani na hasa kukumbusha kuwa katika kila Adhimisho la Ekaristi Takatifu hapo tunakutana na anakaa katikati yetu Kristo Mfufuka katika Neno lake na katika maumbo yale ya mkate na divai. Na ndio tunaona pia Mwinjili Luka anamtaja kwa jina mmoja wa wale wafuasi wa Emau kuwa alikuwa ni Kleopa na mwingine hamtaji jina. Ndio kusema ni mimi na weye tunaalikwa kuwa yule mwanafunzi mwingine, kila mmoja mwenye njaa na kiu ya kukutana na Kristo Mfufuka katika maisha yake. Tunaalikwa kufanya safari ile pamoja na Kleopa ili kwa msaada wa Adhimisho la Ekaristi nasi tuweze kukutana na kumtambua Kristo Mfufuka.

Mwinjili anasema walikuwa njiani kurejea kijijini. Katika Maandiko Matakatifu kila mara neno kijiji linaamisha kurejea katika mapokeo, namna za awali za kufikiri na kutenda. Ni kubaki na mtazamo wa kale. Na ndio tunaona wakiwa njiani walijawa na huzuni, walisimama wamekunja nyuso zao Wanajawa na huzuni baada ya kuona matarajio yao yote yamefikia ukomo kwani kwao Kifo cha Yesu walichoshuhudia pale Yerusalemu wakaona ndio mwamuzi wa mwisho, ndio neno la mwisho. Kwani kwao Masiha asingetarajiwa kufa tena kifo cha aibu namna ile. Matarajio yao ni kumuona Masiha mwenye nguvu na mabavu, anayekuja kuwakomboa watu wake kwa manguvu kutoka utawala wa kikoloni wa Kirumi. Na ndio pia jumuiya ile ya Luka, ilikuwa inapitia kipindi kigumu cha mateso na madhulumu. Hata nao kama wale wafuasi wa Emau wanapoteza matumaini yote na kugubikwa na huzuni. Hata nasi mara kadhaa leo hii tunajikuta wenye huzuni na fadhaha kubwa. Kila mmoja wetu itoshe kuingia na kuangalia maisha yake binafsi, maisha ya jumuiya ya wanakanisa na hata kiulimwengu kiujumla na hasa siku hizi tunapokuwa katika maisha ya mashaka makubwa ya janga la maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kila mmoja wetu anaweza kuona nyakati ambazo tunakunja nyuso zetu, tunakuwa wenye huzuni na hata kupoteza imani.

Jumuiya inayosimama katika imani kwa Kristo Mfufuka haipaswi kubaki na huzuni na mashaka makubwa. Ni jumuiya inayosimama kichwa juu na kwa matumaini kwani si ugonjwa, dhiki au kifo chenye neno la mwisho.  Ni jumuiya inayoongozwa na mbiu ya ushindi wa Kristo Mfufuka hata kama inapitia nyakati ngumu za mateso. Wafuasi wawili wa Emau walifahamu vema maisha ya Yesu na hata kuweza kuelezea vema isipokuwa kwao yote yalikamilika pale juu msalabani kwa kifo na hivyo kushindwa kufika hasa pale tunapopaswa sote kufika kama wafuasi wa Kristo Mfufuka. Ni mawazo ya wengi hata leo kuwa Yesu ametenda mema mengi na kufundisha, ni mtu mwenye hekima na busara ya pekee, ujumbe wake daima ni juu ya amani na upendo na hivyo kuweza kugusa na kubadili mioyo ya watu wengi… lakini mwishoni akakusanywa na wakuu wa makuhani na kumuua. Ni kumuona Yesu kama mtu mwema na wa kustaabisha kwa mengi. Kuwa na mtazamo huo wa Yesu hakika lazima kubaki daima mwenye huzuni. Ni kwa kufika katika imani ya kweli kwa Kristo Mfufuka hapo tutaepuka kubeba sura zenye huzuni hata kama tunapitia magumu kwenye maisha yetu ya siku kwa siku.  Bila kuwa na imani katika Ufufuko basi maisha kwetu yana mwisho katika saa ile ya kifo. Ili nasi tuweze kuwa daima wajumbe wa Habari Njema hatuna budi kujifunza na kuepuka makosa ya wanafunzi wale wa Emau.

Kosa lao la kwanza ni kujitenga kutoka katika jumuiya. Kwao baada ya kifo cha Yesu wakaona kila kitu kimefika mwisho na hivyo wanarejea kijijini kwao kuendelea na maisha yao ya awali. Wanajitenga na jumuiya ila ya wanafunzi wengine, wanaanza safari ya kurejea maisha ya zamani. Kristo Mfufuka kila mara kwa msaada wa Neno lake na Meza ile ya Ekaristi Takatifu anatualika kurejea na kubaki na jumuiya, ni katika jumuiya nasi tunakuwa na hakika ya kubaki na Kristo Mfufuka. Kaa nasi Bwana, “Mane Nobiscum Domine” anakaa kweli nasi katika maisha ya jumuiya ya wanakanisa na zaidi katika Neno lake na Sakramenti zake. Wafuasi wale wawili walipaswa nao kushiriki na zaidi sana kuwa na hakika juu ya ujumbe ule uliowafikia kutoka kwa wanawake kuwa Kristo kweli amefufuka na hilo lingewezekana tu kwa kubaki pamoja na jumuiya. Nasi tunaalikwa daima kubaki pamoja na jumuiya ya wanakanisa kama kweli tunataka kushuhudia kweli ya Ufufuko wake Kristo. Na wengi wa waamini katika jumuiya ile ya Mwinjili Luka walijikuta wanarudia kosa lile lile kwani kila mara walipopatwa na shida na mateso walitoka na kujitenga na jumuiya. Hawakutaka kutafuta suluhu ya magumu au matatizo yao pamoja na jumuiya ya wanakanisa bali waliona wachukue njia yao na ndio kurejea kijijini, kurejea katika mtindo na namna ile ya zamani. Walirejea katika mapokeo na ukale.

Na kosa la tatu kwa wale wanafunzi wa Emau ni kutokukubali kubadili vichwa vyao kuhusiana na sura ya Masiha waliyokuwa nayo. Walibaki na sura ile ya kumuona Masiya anayekuja na enzi kama ya ulimwengu huu. Masiya asiyepitia njia ile ya kukataliwa, kuteswa na hata kufa bali anayekuja na majeshi na nguvu ili kuwarejeshea wana Waisraeli ufalme, Yesu daima aliwahubiria kuwa amekuja kuutangaza Ufalme wa Mungu na sio Ufalme wa Israeli, ni wachache waliokubali kubadili vichwa vyao yaani namna zao za kufikiri waliweza kukubaliana na namna na mantiki mpya ya kufikiri. Tunaona hata Mitume bado walikuwa kichwani mwao wanafikiri Kristo amekuja kwa ajili ya kuwarejeshea Wanawaisraeli ufalme na ndio wanauliza swali hili hata kabla ya Bwana kupaa mbinguni. Hata hivyo tunaona Yesu hawaachi kamwe hata wale wanaochagua njiia isiyo sahihi, njia ya kurejea kijijini na ndio tunaona leo anasafiri nao kuelekea kijijini. Kama tulivyoona kwa wafuasi wengine hata kwao pia hawakumtambua Kristo Mfufuka wakiwa njiani. Si kwamba Kristo Mfufuka anawatokea katika sura nyingine na tofauti bali sasa anawatokea katika sura ya utukufu, ni maisha mengine kabisa tofauti na yale ya awali, lakini anatualika nasi kuanza safari mpya ya maisha ya utukufu, maisha ya ufufuko pamoja naye, maisha ya muungano wa utakatifu na Mungu mwenyewe, ni maisha ya mantiki mpya sio ile ya dunia hii, siyo tena ya kijijini bali mantiki ya Mungu mwenyewe.

Maisha baada ya ufufuko sio uboreshwaji wa maisha yetu ya hapa duniani, ni maisha mapya kabisa, ni tofauti kabisa na maisha yetu ya hapa duniani, ni maisha ya utukufu na muunganiko kamili na Mungu. Na ndio maana tunaona Wainjili kila mara wanatuonesha ugumu walioupata wafuasi kumtambua Kristo Mfufuka. Kristo Mfufuka anawaalika kumwangalia mikono na ubavu wake, anawaalika nao kushiriki katika huduma ya upendo na ndio ushuhuda wa maisha mapya ya utukufu, Ulimwengu na watu watatutambua kuwa tu wafuasi na wanafunzi wa Kristo Mfufuka kwa namna zetu za kufikiri na kutenda, kwa maisha yetu watu wanapaswa kututambua kuwa sisi ni wafuasi na rafiki zake Kristo Mfufuka. Kinyume chake tunabaki na kurudia kosa lile lile la wafuasi wanaorejea kijijini na kuendelea na maisha yao ya kimapokeo ya awali. Yesu anakutana nao katika mahangaiko yao na anawasaidia kufanya safari ya imani, sio ile ya kurejea katika ukale bali katika kumtambua na kukutana na Kristo mfufuka, ndio anawafafanulia Maandiko. Hakika walijua Maandiko ila bila kujua maana yake na ndio leo Mama Kanisa anatualika sio tu kusoma Neno la Mungu bali kufafanua na ili kupata ujumbe kusudiwa kutoka kwa Mungu mwenyewe.

Pamoja na kuwa walijua Maandiko bado walimhitaji Yesu awafafanulie.  Na ndio leo tunajikuta tuna sayansi ya ufafanuzi ya Maandiko kwani hata kitenzi kinachotumika kwa lugha ya Kigiriki ni ‘’διερμηνευσεν’’ (diermeneusen). Likiwa na maana sisisi aliwafafanulia wao wawili, na ndio leo tunapata neno ‘’Hermeneutics’’. Ni Mwaliko wa Mama Kanisa kukumbuka Mwalimu wa kwanza wa Maandiko ni Roho Mtakatifu hivyo kila mara tunaposoma hatuna budi kumwomba Roho wa Mungu atuangazie na atufafanulie Neno la Mungu. Wafuasi wale walikuwa hawasomi Maandiko kwa kuongozwa na mantiki ya Mungu mwenyewe bali ile ya kibinadamu na ndio tunaona Yesu akiwaonya juu ya ugumu wa mioyo yao. Njia ile ya msalaba anayotumia Mungu kumkomboa mwanadamu si rahisi kuielewa na hata kuifafanua leo kwa akili zetu. Na ndio tunaona Maandiko haitoshi tu kuyasoma bali tunaalikwa pia kuyaelewa na kwa msaada wa kufafanuliwa. Na tunaona si tu Yesu anawafafanulia na kushibisha akili zao bali anagusa mioyo yao na ndio wanaulizana mioyo yetu haikuwa imewaka njiani. Neno la Mungu linapaswa daima kutupa joto mioyoni mwetu, kutugusa na kuturejeshea maana ya maisha yetu. Linapaswa kuwa kila siku linaleta ujumbe mpya na mahususi katika maisha ya kila mmoja wetu.

Jioni ya Siku ile ya Kwanza ya Juma wanafika mwisho wa safari yao na Mwinjili hatutajii kuwa nyumba ile walikuwa wanaishi wao wawili tu, Je, hakukuwa na wanafamilia wengine? Na ndio leo wataalamu wengi wa Maandiko wanakubaliana na kusema watu wale yawezekana kabisa walikuwa ni mume na mke, lakini hata hivyo Mwinjili Luka hataji jina la yule wa pili na na kweli si kwa ajali anaacha kutaja jina la mfuasi yule wa pili. Itoshe kama nilivyosema hapo juu yule mfuasi wa pili asiyetajwa jina ni mimi na wewe. Mwinjili Luka anatuonesha waziwazi kuwa mahali pekee tunapoweza kumtambua Kristo Mfufuka ni katika Adhimisho lile la Ekaristi Takatifu, katika Neno lake na katika maumbo yale ya mkate na divai. Na ndio mwaliko na msisitizo si tu kwa jumuiya yake bali hata kwetu leo. Daima na kwa namna ya pekee kabisa na juu kabisa tunakutana na Kristo Mfufuka katika Maadhimisho ya Kumega Neno na Mwili wake. Na Adhimisho hili daima linatualika kudumu na kubaki katika jumuiya ya waamini. Ni katika Ekaristi Takatifu pekee Kristo Mfufuka anakuwa na Kanisa lake kwa namna ya pekee kabisa, ni Yeye mwenyewe mzima katika maumbo yale na ndio katekesi anayotupa leo Mwinjili Luka kuwa mara akatoweka na si kusema kuwa Yesu alitoweka bali anawakumbusha kuwa anaendelea kuwepo pamoja nasi katika maumbo yale ya Mkate na Divai, kwani ni Mwili na Damu yake Azizi.

Ni Kristo Mfufuka mwenyewe mzima si tena kama alivyotembea na kuambatana nao miaka 2000 iliyopita bali sasa katika maumbo haya mapya ya Mkate na Divai kwani baada ya mageuzi si tena Mkate, si tena Divai bali vinakuwa ni Mwili na Damu yake Azizi. Ekaristi ni kutaniko na Kristo Mfufuka katika Neno lake na katika maumbo ya mkate na divai, yaani Mwili na Damu yake Azizi. Tunaona ni kwa msaada wa Neno la Mungu wanapofika mezani wakati wa kuumega mkate wanaweza kumtambua Kristo Mfufuka. Nasi leo tunaalikwa kuona umuhimu na msaada wa Neno la Mungu katika kufikia mwisho mwema wa safari yetu ya imani, kamwe tutabaki kuona ni mkate tu au ni divai tu kama hatutakaa tuongozwe na Maandiko Matakatifu. Mwinjili Luka pekee anatuonesha kuwa Yesu anawaalika wanafunzi wake kufanya na kurudia tendo lile la Ekaristia kwa kumkumbuka Yeye, si tendo la kukumbuka historia na mambo ya kale bali ndio kilele na chemuchemu ya maisha ya kila muumini, ndio wakati pekee ambapo Yesu Kristo Mfufuka anakuja na kuweka makazi yake pamoja nasi, kaa nasi, ndio ‘’Μεινον μεθ ημων’’, ni ombi ni sala inayopaswa kuwa ya kila mmoja katika safari yetu ya imani ya kusafiri na hasa kubaki pia na Kristo Mfufuka katika Neno lake na katika Maumbo yale ya Mkate na Divai, ndio mwili na damu yake takatifu.

Hatumwoni kwa macho ya nyama tena bali anatualika kumuona kwa macho ya imani katika maumbo yale ya mkate na divai kwani ni Yeye mzima. Ni mwaliko wa kuwa na imani baada ya kukutana na Kristo Mfufuka. Na ndio baada ya kumtambua katika kuumega mkate wanarudi kwa kukimbia ili kuwapasha habari wale wengine kuwa wamemwona Bwana Mfufuka. Hiyo ni ari na shauku ya kila mmoja anayekutana na Bwana mfufuka, kutoweza kuzuia furaha na shauku ile ya kuwashirikisha wengine. Hata nasi hatuna budi kukutana na Kristo Mfufuka na hapo tutajawa na shauku na ari si ya kubaki kijijini au kuenenda katika namna zetu za zamani, bali kutoka na kumshuhudia kwa wengine. Ni Furaha isiyoelezeka ya kukutana na Kristo Mfufuka! Kristo Mfufuka kila mara anapokutana nasi anatuonesha mikono na ubavu wake, anatualika nasi kumshuhudia kwa kuwahudumia wengine kwa upendo usio na masharti. Niwatakie tafakari njema na Dominika yenye furaha tele za kukutana na Kristo Mfufuka katika Neno na katika kuumega mkate.

27 April 2020, 07:21