Tafuta

Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, ambamo Kanisa linatafakari kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, ambamo Kanisa linatafakari kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! 

Tafakari Neno la Mungu: Jumapili ya Matawi: Mateso ya Kristo Yesu!

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Matawi inawaingiza na kuwazamisha waamini katika tafakari ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kama utmilifu wa Maandiko Matakatifu. Kristo Yesu amekubali kuteswa na hatimaye kufa Msalabani ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Hiki ni kipindi cha imani, matumaini na mapendo.

Na Padre Gaston George Mkude, -Roma.

Amani na Salama! Wainjili wote wanatenga nafasi ya kutosha kutuelezea masimulizi juu ya mateso na kifo chake Bwana wetu Yesu Kristo. Kimsingi kweli za imani zinabaki kuwa ni zilezile ingawa zinawakilishwa kila mmoja kwa mtindo wake. Kila mwinjili kwa namna yake kwa kutegemea aina ya uandishi, lakini pia aina ya jumuiya aliyokuwa anaiandikia, na lengo au makusudi yake ya kufikisha katekesi kusudiwa. Mwaka huu, Mama Kanisa anatualika katika Dominika ya Matawi kutafakari sehemu ya Injili ya Mathayo, hivyo katika tafakari yetu tutajitahidi kuwa waaminifu ili tupate ujumbe kusudiwa na Mwinjili. Dominika ya matawi inatuingiza katika lile Juma Kuu, Juma Takatifu, Juma la Wokovu wetu, ndilo Juma la kutafakari wokovu wetu yaani mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Mwinjili Mathayo, katika masimulizi yake anatumia maneno “…Ili litimie andiko’’. Tunasoma Mathayo 25:24 “Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yasemavyo’’. Tunasoma pia Mathayo 26:56: “Lakini haya yote yametendeka ili maandiko na manabii yatimie…’’. Ndio kusema tunaposoma sehemu kubwa ya Injili ya Mathayo hatuna budi kukumbuka kuwa alikuwa anawaandikia Jumuiya ya Wakristo wenye asili ya Kiyahudi, hivyo daima kwa kuwaonesha na kuwakumbusha kuwa Yesu ndiye Kristo, ndiye Masiha aliyetabiriwa na Manabii na Agano la Kale kwa ujumla.

Hadhira yake ilielewa mara moja na kupata ujumbe kwani walikuwa tayari wanajua Maandiko Matakatifu hasa Agano la Kale. Yesu Kristo ndio ukamilifu wa Maandiko Matakatifu, unabii wote unakamilika na kutimia katika nafsi ya Yesu Kristo. Mwinjili Mathayo pia anatupa hata kiasi gani cha pesa alichopewa Yuda Iskariote ili amsaliti Yesu na pia anatuonesha jinsi hatima na mwisho wake ulivyokuwa wa kusikitisha na kuhuzunisha. Mathayo 27:9-10 Si kwa ajali anatupa kila taarifu kumhusu ili kila mmoja wetu kama mfuasi wa Yesu ajichunguze na kuangalia maisha yake na hasa mahusiano yetu na Yesu Kristo. Katika kutualika kumuona Yesu, tayari akiwa anazungumziwa katika Agano la Kale, tunaona jinsi simulizi lake linavyoendana na Zaburi 22 juu ya mateso ya mtu mwenye haki. Yesu ni ukamilifu wa ufunuo wote, ndio ukamilifu wa kile kilichonenwa na kutabiriwa katika Agano la Kale. Hapa chini nitajaribu kuonesha mfanano wa karibu kabisa wa Zaburi 22 na Yesu Kristo katika masimulizi ya Mateso na Kifo chake kadiri ya Mwinjili Mathayo.

Kadiri ya Mwinjili Mathayo, mtu huyu mwenye haki anayezungumziwa katika Zaburi ya 22 ni Yesu Kristo. Kama Yesu alipokuwa pale juu msalabani alivyolia, Matayo 27:46 ndivyo pia anavyoanza mtu mwenye haki. “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?’’ Mtu mwenye haki tunasoma Zaburi 22:8-9 “Husema: Alimtegemea Mwenyezi-Mungu, basi, Mungu na amkomboe! Lakini ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu…’’ Ndio maneno na kashfa alizozipata Yesu kwa wale waliomwona akiwa pale juu msalabani. Matayo 27:39,41-43. Zaburi 22:16 “Koo langu limekauka kama kigae…’’ Ndivyo na Yesu anaona kiu akiwa pale juu msalabani. Mtu wa haki akiwa amezungukwa na watesi wake, Zaburi 22:17 “Nimebaki mifupa mitupu; adui zangu waniangalia na kunisimanga. Wanagawana nguo zangu, na kulipigia kura vazi langu.’’ Ndicho ambacho wanafanya pia wale maaskari wa kirumi waliomsulubisha Yesu wakiwa chini ya msalaba. Matayo 27:35. Kama Yesu alivyolia kwa sauti kubwa na kuisalimu roho yake Matayo 27:50 ndivyo pia Mtu wa haki afanyavyo Zaburi 22:25.

Mwinjili Mathayo anatumia Zaburi hiyo ya 22 ili kutuelezea masimulizi ya mateso yake Yesu Kristo, kuwa ndiye mtu wa haki, mtu wa Mungu aliyeteseka bila kuwa na kosa wala dhambi yeyote ile. Ni lengo lake kutualika nasi kutafakari kwa kina mateso na kifo chake Bwana wetu Yesu Kristo ili tusiishie tu kuona kama ni kweli ya kihistoria bali nyuma yake kuna ujumbe mkubwa na mzito. Ingawa hata Wainjili wengine nao wanafanya marejeo kwa Maandiko Matakatifu ila sio kwa kiasi kile anachofanya Mwinjili Mathayo. Na sababu kubwa kama nilivyosema hapo juu kuwa alikuwa anawaandikia jumuiya ya waamini wenye asili ya kiyahudi, hivyo walikuwa ni watu waliokuwa na kulelewa wakisoma Maandiko Matakatifu. Wayahudi walikuwa daima wanamtarajia Masiha anayekuja kama mshindi, mtawala mwenye nguvu na mabavu. Ni katika hatima ya Yesu anaonekana kuwa dhaifu na mnyonge na aliyeshindwa, ni katika mazingira haya Wayahudi wanakwazika na kushindwa kumwona Yesu kama Masiha.

Ni pale chini Msalabani tunaona makuhani, waandishi na wazee wa Kiyahudi wakimrushia maneno ya kejeli Yesu msalubiwa: Mathayo 27:40 “Wewe! Si ulijidai kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi, shuka Msalabani!’’ Huo ndio ulikuwa mtazamo wao wa Masiha anayeshinda na sio anayeshindwa na kuishia kufa kifo cha aibu pale Msalabani. Mtazamo huu labda sio tu wa Wayahudi nyakati za kale bali hata baadhi yetu leo na hasa katika kipindi hiki kigumu na mateso na mahangaiko ulimwenguni kote juu ya janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ni sala na maombi yetu kuona mkono wa Mungu na Bwana wetu Yesu Kristo ukitenda miujiza na kuonesha ukuu na enzi na mamlaka yake. Ni katika wakati huu tunapojiuliza nini maana na kwa nini mateso na magonjwa na kifo katika maisha yetu? Ni wakati huu nasi tunalia na kujiuliza Mungu wangu, Mungu wangu mbona umetuacha.

Ni katika mazingira haya tunaona Mwinjili Mathayo anamzungumzia Yesu kama Masiha yule anayezungumziwa kutoka Kitabu cha Zaburi 22, juu ya mtu wa haki anayeteseka na kutaabika bila hatia, anamfananisha huyu na Yesu. Mungu hakumuokoa Yesu kutoka pale juu Msalabani kwani angeweza kufanya hilo katika uwezo wake wa Kimungu. Mungu hakuzuia Mwana wake wa pekee asipitie hukumu ile na hata mateso yake bila kustahili. Mzaburi na pia Yesu anapokuwa pale Msalabani anasali na kulia; “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha’’, labda ndio kishawishi kikubwa na sala ya wengi wetu leo ulimwenguni kote. Ni haki kabisa kumlilia na kumwomba Mungu awe nasi daima kila nyakati katika maisha yetu. Kama vile Kristo anavyosali daima awe na Baba yake nasi tunaalikwa pia kutambua kuwa bila Mungu hatuwezi kumshinda yule mwovu na hila zake. Mungu alibadili kushindwa kwake na kuwa ushindi, kifo chake kuwa ni kuzaliwa katika maisha mapya, kaburi lake kuwa ni tumbo kutoka kwake sisi sote tumepata uzima wa milele. Ni mwaliko wangu leo kuwa na jicho jipya na hasa tukumbuke kuwa maisha ya duniani ni ya muda tu kwani sisi ni raia wa maisha ya umilele, maisha yasio na mwisho, maisha pamoja na Mungu.

Dominika ya Matawi inapoadhimishwa kwa baadhi ya nchi kushindwa hata kupata fursa na nafasi ya kusali katika makanisa yetu, itupe nafasi ya kutambua na kutafakari udogo wetu lakini zaidi sana kuona kuwa yote ya hapa duniani ni maandilizi ya maisha ya umilele, makao yetu ya kudumu si hapa duniani bali mbinguni milele yote pamoja na Mungu mwenyezi. Ni kwa njia ya Yesu nasi tunaalikwa kuwa na muono mpya au kuongozwa na mantiki mpya. Mwenyezi Mungu leo anatuonesha kuwa kamwe hatuokoi kutoka kwa yule mwovu kwa muujiza bali kwa kutupitisha katika mateso na dhiki kuu ili tuweze kupata uzima wa kweli, maji ya uzima wa milele. Tubaki tukiongozwa sio kwa akili zetu bali kwa Neno lake. Tunaona leo kila fani kama vile wanafalsafa wanahoji juu ya COVID-19, wanasayansi wetu, wanasiasa wetu na labda kila mmoja wetu, lakini sote tunakiri kuwa pamoja na CORONA kirusi kuwa ni kiumbe kidogo sana tena kisicho hai hatuna bado majibu ya kuridhisha kwa mwanadamu anayetafuta majibu. Ni Mungu pekee anayekuwa ni jibu kwani yeye ndio ukweli wote, mungu ndiye sayansi yote, ndiye falsafa yote, ni kwa kumkimbilia na kukubali kuongozwa na Neno lake tunapata majibu ya maswali na hasa juu ya maana ya maisha yetu hapa duniani na hasa maisha ya umilele.  

Ni ngumu wakati fulani kukubali kuongozwa na mantiki ya Mungu ila ni kwa unyenyekevu mkuu tunaweza kupata ujumbe wa Mungu na kuongozwa nao. Naomba tutafakari pamoja na tuongozwe na maneno ya Yesu mwenyewe katika kipindi hiki kigumu na chenye mateso na mahangaiko mengi. Mathayo 11:28-30 “Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyeyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.’’ Wapendwa mwaliko wa Yesu hauna ubaguzi ni kwetu sote, hata kwa wale wasiomwamini na wadhambi. Yesu anatualika na hasa Juma hili Kuu tunalolianza leo na kualikwa kutafakari mateso, kifo na ufufuko wake, si tu kwetu sisi wakristo tunaomwamini bali kila mwanadamu leo hii anayeona kulemewa na mizigo. Mizigo ipo ya kila aina. Leo hii dunia ina hofu, mashaka, uoga, mahangaiko dhidi ya janga ya hili gonjwa, lakini zaidi sana kila mmoja wetu ana mizigo yake mingi inayomsumbua na kumlemea. Ni mwaliko twendeni sote kwa Yesu ili tupumzike.

Yesu si tu anatualika bali anatuhakikishia kupumzika, kila mmoja wetu leo anasongwa na mizigo yake na hivyo sote tunahitaji kupumzika, kupata maana ya maisha yetu, kwa hakika sio kwa waganga, sio kwa wataalamu au wanasayansi, sio kwa wanasiasa au nguvu na akili zetu bali Yesu anatuhakikishia pumziko kwake.  Yesu anatualika kujifunza kutoka kwake, leo tunapotafakari masimulizi ya mateso yake, Yesu anatualika nasi kupata maana ya mateso na magonjwa na shida katika maisha yetu kwa kujifunza kwake. Leo kuna wengi hata wanafikia kukufuru kwa kudhani na kusema, Mungu anatuadhibu, nawasihi tuepuke mtazamo na fikra za namna hiyo kwani ni kumkosea Mungu, Mungu daima ni huyu anatualika bila ubaguzi wowote ule ila anasubiri kutoka kwetu ni ndiyo yetu kwa upendo wake usio na masharti wala mipaka. Kusema Mungu anatuadhibu ni sawa na kusema Mungu alimwadhibu kwanza Yesu kwa kufa pale juu msalabani bila kuwa na dhambi yeyote. Leo wanakufa si tu wale wenye dhambi na labda wengi ni watu wanyofu na wenye kumpenda Mungu, je tutaeleza vipi kwa kifo cha watu wenye haki. Nimewaalika hapo juu kuwa lazima kubadili mtazamo wetu kwani sisi tunaalikwa kuwa watu wa umilele, makazi yetu ya kudumu sio hapa duniani bali ni mbinguni kwa baba na Mungu wetu.

Hatuna budi kukutana na Yesu na kuongea naye kama Mwanamke msamaria alivyofanya pale kisimani, pamoja na dhambi zake tunaona Yesu hakuanza kumshutuma na kumpa majina ya kumkashifu na kumuhukumu bali anamwalika kubadili mtazamano na maisha yake, asiye anayehangaika na maji ya kunywa leo na kesho anaona kiu tena, anamwalika kufika kuutafuta uzima wa milele. Na hata hotuba yake juu ya kuwa mkate wa uzima, makutano walimfuata sio ili wapata mkate wa uzima wa milele bali kwa kuwa walikula mikate wakashiba. Na labda hata nasi leo wengi wetu tunaposali na kumlilia Mungu hatuna budi kutoishia kuomba uponyaji wa miili yetu bali kumuomba nasi atujalie uzima wa milele. Mtume Petro anatambua kuwa hatuna pengine kwa kwenda zaidi ya kwake hata kama wengine wanakwazika na kuondoka. Hata leo wanaosaka miujiza kwa Yesu na kuikosa wanakwazika na hata kuondoka zao wakiwa wamekata tamaa, sisi hatuna budi kumlilia na kubaki naye kwani ni kwake tu kuna maneno yenye uzima wa milele.

Mafundisho potofu katika nyakati zetu ndiyo ile ya ‘’secularization’’ nikiri kukosa neno la kufaa kwa Kiswahili lakini mzizi wa neno hilo ni ‘’saeculum’’, neno la Kilatini lenye kumaanisha, ya ulimwengu huu, ni kuishi kwa kuongozwa na kuona kila kitu kinaanza na kuishia hapa ulimwenguni, kuona sasa na kusahau kuwa kuna umilele. Sisi hata kama tunapitia nyakati ngumu kiasi gani hatuna budi kuongozwa na ukweli kuwa sisi ni wa milele, sisi maisha yetu hayaishi kwa kuwa tunakufa leo hata kwa wingi, kwa maradhi, ajali, njaa, kiu au kuuawa kama anavyouawa Yesu pale juu msalabani. Na mafundisho potofu haya ndiyo yanayotufanya nasi kurudia kosa lilelile la Yuda Iskariote, badala ya kumgeukia na kumfuasa Kristo tunajikuta mara nyingi tunakuwa watumwa wa fedha na mali. Maisha yetu yanapokosa kuelekea umilele na kuona kana kwamba hapa duniani tunabaki milele. Yuda Iskariote ni mimi na wewe kila mara tunamfuasa Yesu Kristo huku tukisukumwa na tamaa zetu nyingine za kibinadamu. Yuda Iskariote anakosa kuona thamani kwa Yesu Kristo aliye Bwana na rafiki yake wa kweli na kugeukia vipande vile vya fedha, anaona thamani katika kubaki na kuongozwa na maisha ya kale, kadiri ya mafundisho ya makuu wa makuhani.

Yuda Iskariote anapotambua kosa lake anakwenda kwa makuhani wakuu na huko kwa kweli anakosa huruma na msamaha ambao kwa hakika alipaswa kuupata kwa Bwana wake tu, Yesu Kristo. Yuda Iskariote anakosea njia, anakosa mwelekeo sahihi, kila mara hatuna budi kutambua kuwa ni kwa kumkimbilia Yesu tu pale msalabani hapo kwa hakika tunapokea huruma yake ya milele, huruma isiyo na mipaka. Yuda Iskariote alikosea njia pale mwanzoni na kujikuta anamsaliti Bwana na Mwalimu wake na hata baada ya kutambua kosa lake bado anakosea tena njia. Yuda Iskariote anabaki kutualika nasi kujitafakari maisha yetu iwe kabla ya kutenda makosa na baada ya kutenda, ni wapi nakimbilia mimi na weye? Mwinjili Mathayo pia leo anatualika kuwa sisi wanafunzi wa Yesu hatunabudi kuepuka kila aina ya dhulma na utumiaji wa mabavu. Petro anaalikwa na Yesu kurudisha upanga wake alani, sisi wakristo hatuna hata nafasi moja inayohalalisha kutumia upanga bali daima sisi tunaalikwa kuwa wajumbe wa amani, iwe katika familia zetu, katika jamii zetu, katika nafasi zetu za kazi na popote pale.

Leo Baba Mtakatifu Francisko anaualika ulimwengu mzima kujitafakari tena hasa nyakati hizi za janga la COVID-19, mataifa makubwa leo wanatumia sehemu kubwa ya bajeti zao kwa silaha za kila aina na za kisasa na za bei ghali lakini hakuna uwekezaji mkubwa katika elimu, afya, na hata wengi wanakufa leo kwa kukosa chakula na maji safi na salama na makazi bora ya kuishi. Labda mimi na weye tunaweza kusema tupo mbali na mfano huo, itoshe tu kuona mara ngapi tumekuwa na mambo mengi hata tusiyoyahitaji na pembeni yangu kuna mtu anakosa chakula, dawa au hata elimu? Tunaweza kila mmoja wetu ajiangalie ndani mwake. Yesu amekufa pale Msalabani ili kuukomboa ulimwengu mzima, hatuna budi nasi kutambua kuwa wokovu sio mali ya watu au kikundi cha watu fulani bali ni kwa ulimwengu mzima.  Nawatakia tafakari njema na Maadhimisho mema ya Mateso, Kifo na Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Juma Kuu lirejeshe tena: imani, matumaini na amani ulimwenguni kote. Kristo ameshinda mateso na kifo kwa ufufuko wake nasi tu watu wa ufufuko, daima tumkimbilie Yesu Kristo aliye Bwana na Mwokozi wetu.

04 April 2020, 08:53