Tafuta

Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema! Kwa Mwaka 2020 ni Siku ya 57 ya Kuombea Miito Mtakatifu Duniani. Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema! Kwa Mwaka 2020 ni Siku ya 57 ya Kuombea Miito Mtakatifu Duniani. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Mchungaji Mwema: Sifa zake!

Wazo kuu la Dominika ya IV ya Pasaka: Bwana Yesu Kristo Mfufuka ndiye Mchungaji wetu mwema. Mchungaji katika Agano la Kale na hasa katika mazingira ya Mashariki ya Kati alikuwa sio tu kiongozi wa kundi lake bali zaidi sana alikuwa ni msafiri pamoja nao maisha yao yote, alishiriki nao maji, machungo katika nyakati mbali mbali na hivyo alikuwa ni mmoja pamoja na kundi lake!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francis siku ya kuombea Miito: ‘’Jipeni moyo ni mimi msiogope:Maneno ya miito: Mateso, Shukrani, Ujasiri na Sifa’’ Mathayo 14:22-33. Dominika ya 4 ya Pasaka inajulikana pia kama Dominika ya Mchungaji Mwema, kwani kila mwaka wa kiliturjia Mama Kanisa anatualika kutafakari sura ile ya 10 ya Injili ya Yohane.  Na Mwaka huu kwa namna ya pekee anatualika kutafakari sehemu ile ya kwanza yaani aya zile 10 za mwanzo. Katika sehemu ile ya kwanza hatusikii sana juu ya wazo mama la Mchungaji Mwema ila tu kwa kugusiwa. Ni tunaposoma mbele zaidi ndipo Yesu anajitambulisha na kusema ‘’Mimi ni Mchungaji Mwema/mzuri. Lakini katika sehemu hii ya kwanza tunayoalikwa kuitafakari Mwaka huu wa Kiliturujia wazo kuu ni Yesu kama mlango wa kondoo. Tunasikia pia juu ya wezi na wanyang’anyi, zizi, mngoja mlango na mgeni. Labda katika tafakari yetu ya leo ninawaalika tuyatambue haya makundi pia anayoyaeleza Mwinjili ili tuweze kupata ujumbe kusudiwa.

Katika Liturujia ya Neno la Mungu tunaimba na kusikia Zaburi ile pendwa na labda inayojulikana sana na wengi ‘’Bwana ndiye mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu…’’Zaburi 23 Hivyo wazo kuu la Dominika ya leo ni Bwana Yesu Kristo Mfufuka ndiye Mchungaji wetu mwema. Mchungaji katika Agano la Kale na hasa katika mazingira ya Mashariki ya Kati alikuwa sio tu kiongozi wa kundi lake bali zaidi sana alikuwa ni msafiri pamoja nao maisha yao yote, alishiriki nao maji, machungo ya mbali juani, baridi nyakati za majira ya baridi na hivyo alikuwa ni mmoja pamoja na kundi lake daima. Yesu anajitambulisha katika Injili ya leo kama Mchungaji na zaidi sana kama mlango wa zizi. Yesu yupo hekaluni Yerusalemu na ametoka tu kumponya mtu aliyezaliwa kipofu. Ni katika mazingira ya sikukuu zile za vibanda, zilizojulikana pia kama sikukuu za mwanga kwani waliadhimisha na kukumbuka kukombolewa kwao kutoka utumwani Misri.

Ni katika muktadha huu na akiwa kati ya viongozi wa dini ya Kiyahudi Yesu anajitambulisha tena kama mchungaji mwema na mzuri. Pale hekaluni upande wa mashariki kulikuwa na mlango uliojulikana kama mlango wa kondoo. Yesu akiwa pale hekaluni aliwaona wayahudi wakiingia na kupitia mlango ule na kununua kondoo ili waingie nao hekaluni na kuwatolea sadaka. Ni katika muktadha huo Yesu anajitambulisha kuwa ni Yeye aliye mlango wa kweli wa kondoo. Ni karibu na kusema Yesu anakufuru kadiri ya mtazamo wao wa kidini waliokuwa nao. Si tu Yesu anajitambulisha kama mlango ila ni kuwaalika kubadili vichwa vyao na kuliona hekalu la kweli, kuwa ni Yesu mwenyewe. Yesu anatumia maneno ‘’Ego eimi’’, ‘’ Mimi ndiye au Mimi ndimi’’ kwa myahudi maneno hayo ni utambulisho wa Mungu mwenyewe, ndiyo kusema Yesu anajitambulisha na kuwaalika kwenda kwake aliye kweli Bwana na Mungu wao, kumwabudu Yeye aliye Mwanakondoo wa kweli. Hivyo sehemu ya Injili ya Mwinjili Yohana inatutambulisha pia Umungu wa Yesu. Yesu anawaalika wayahudi kumtambua kama Mungu wao, ndiye mlango wa kondoo na ni Mwanakondoo wa kweli.

Zizi kwa desturi za wachungaji wa Kiyahudi lilitengenezwa ama kwa kuta za mawe kwa chini na juu waliweka miiba ili kuwalinda na kuzuia mifugo yao kutoka au kuibiwa na kuvamiwa na wanyama wakali wa porini. Mazizi yaliweza kutengenezwa mbele ya nyumba za makazi yao kwa nje sehemu ya wazi, lakini hasa mazizi waliyatengeneza katika miteremko ya milima na humo kwa desturi waliweza kulaza mifugo ya wachungaji wengi kwa pamoja. Na hapo wachungaji waliweza kupeana zamu nyakati za usiku kulinda mifugo yao. Wakati mmoja alibaki mlangoni kulinda na wengine waliweza kulala na kupeana zamu mpaka asubuhi. Wachungaji pia walikuwa wa aina mbili, kuna wale waliokuwa wanachunga kundi lao na wengine walikuwa ni watu wa mshahara na labda katika kundi angeweza kuwa na kondoo mmoja au wawili ila wengine wote walikuwa ni wa mwajiri wake.

Tunaposoma kutoka Mwinjili Luka 2:8 ‘’Katika sehemu hizo, walikuwepo wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao’’. Na kwa desturi aliyekuwa zamu ndiye aliyebaki sehemu ile ya kuingilia kwani kwa hakika hakukuwa na mlango kama tunavyoweza kujenga picha leo ya mazizi ya kisasa, hivyo ni mchungaji mwenyewe kwa kubaki au kuketi au kulala pale sehemu ya kuingilia na kutokea ilitosha kutimiza wajibu wake kama mlinzi. Hivyo wezi na wanyang’anyi au hata wanyama wakali wasingeweza kirahisi kuingia au kusogelea zizi isipokuwa ni kwa wale tu alioweza kuwaruhusu kuingia zizini aliyekuwa zamu ya kulinda mlango. Hivyo kupata picha kamili, zizi moja ndani yake kulikuwa na mifugo yaani kondoo au mbuzi wa wachungaji mbali mbali kwa pamoja na asubuhi mapema kila mchungaji alifika ili kuswaga na kuwapeleka malishoni mifugo yake. Kondoo waliwatambua na kuwafahamu wachungaji wao kwa sauti zao, hivyo kila mchungaji ilitosha afike katika mlango na kutoa mlio au sauti fulani na mifugo yake ilimtambua na kumfuata.

Na walimtambua si kwa sauti bali walitambua zaidi wema na upendo na uzuri wa mchungaji wao wa kuwaongoza kwenye malisho mazuri na maji ya utulivu. Walimfuata kwani walionja kupendwa na kuhakikishiwa ulinzi na usalama wao. Kwa maneno rahisi walikuwa kwenye mikono salama. Ni kwa kutumia lugha ya picha inayoeleweka vema na wasikiliza wake, Yesu anatumia fursa hii kufikisha ujumbe kwa wasikilizaji wake na hata kwetu nasi leo. Lugha ya picha ya Yesu tunaweza kusema ni rahisi ila kwa kweli ni lugha iliyojaa mafumbo na ndio nawaalika tuweke kutafakari na kuona hasa maana kusudiwa ya Yesu kwetu hasa tunaoishi si nyakati tu tofauti bali hata mila na desturi na tamaduni tofauti. Na hata wasikiliza wa Yesu kama anavyotuambia Mwinjili kuwa aliwaambia mfano huo lakini bado hawakumuelewa. Yohane 10:6.  Yesu si tu anatumia lugha ya picha ila ni lugha ya mafumbo hivyo ili kupata ujumbe wake hatuna budi kuelewa maana ya ishara alizotumia.

Yesu anaanza sehemu ya kwanza ya Injili ya leo kwa lugha kali na ya mafumbo, anatuwambia yeyote asiyeingia zizini kwa kupitia mlangoni huyo ni mwizi na mnyang’anyi. Ila mchungaji wa kweli ni yule anayeingia kupitia mlangoni na mngoja mlango umfungulia, na kondoo uisikia sauti yake na anawaita kondoo wake kwa majina na kuwaongoza nje. Kwa Yesu kondoo wake sio tu kundi bali ana mahusiano nao kila mmoja binafsi na kujua na kutambua hali za kila mmoja wao. Isaya 40:11 ‘’Atalilisha kundi lake kama mchungaji, atawakusanya wanakondoo mikononi mwake, atawabeba kifuani pake, na kondoo wanyonyeshao atawaongoza polepole’’. Yesu kama mchungaji anafahamu kila kondoo wake kwa jina na hali zao hivyo kuwachukua na kuwaongoza kadiri ya hali zao. Mchungaji mwema anawaongoza nje kondoo zake kutoka zizini, anawaongoza nje kama Mwenyezi Mungu alivyowaongoza Taifa la Israeli kutoka utumwani Misri, ndio kusema anawaongoza katika sehemu ya wazi na yenye uhuru zaidi, sio tena katika msongamano ule wa zizini bali kwenye maisha ya uhuru wa kweli, kwenye malisho na maji ya utulivu. Anawaongoza kwa mfano kwa kuwatangulia mbele, si kuwaburuza na kutumia mabavu bali kwa kujali kondoo zake, si kwa masilahi yake bali masilahi ya kondoo zake. Yesu kama mchungaji anawaongoza nje kondoo zake kwa upendo na uvumilivu mkubwa.

Kinyume na Mchungaji wa kondoo tunasikia juu ya wezi na wanyang’anyi. Nyakati za Yesu kulikuwa na wakuu wa kidini na wa kisiasa ambao nao walijifanya kuwa viongozi wa watu lakini kimsingi hawakujali masilahi ya watu bali yao binafsi. Lengo lao kubwa ni kuwatawala watu, sifa na utukufu wao binafsi, faida na masilahi kwanza na walitumia mabavu na nguvu kuwatawala. Hivyo hawakuwa wachungaji wema na wazuri na ndio tunasoma siku moja Yesu anasukumwa kwa huruma na kusema, Marko 6:34-44. ‘’Aliposhuka pwani, Yesu aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji, Akaanza kuwafundisha mambo mengi…’’ Yesu anawaonea huruma si tu watu wa nyakati zile bali hata nasi leo na ndio anatualika nasi kuisikia sauti yake na kumfuata, na si kama wale wezi na wanyang’anyi wanaokuja sio kwa masilahi ya kondoo bali yao binafsi. Hapa tunaweza kuangalia ulimwengu wetu wa leo na kuona waziwazi juu ya wezi na wanyang’anyi wa nyakati zetu pia.

Sauti ya mchungaji ni muhimu hata kwetu nasi leo, kuijua na kuitambua kati ya sauti nyingi hasa katika nyakati zetu. Ni Yesu anayeongea nasi kupitia Neno lake, kupitia Kanisa lake na kupitia Masakramenti yake. Wanafunzi wa Yesu baada ya ufufuko wanamtambua Bwana na Mwalimu wao anapotoa sauti yake, hivyo nasi tunamtambua Yesu hasa anapoongea na kila mmoja wetu iwe katika dhamiri zetu lakini hasa kwa kulisikiliza Neno lake Takatifu. Luka 24:15,37 na Yohane 21:4 Leo kuna sauti nyingi sana ila kila mara hatuna budi kama wakristo kuisikia na kuitambua sauti ya Kristo Mfufuka ambayo tunakutana nayo kwa namna ya pekee katika Neno la Mungu, katika Injili. Yesu anajitambulisha kama mlango wa zizi, ndio kusema kama tulivyoona hapo juu ni Yeye mwenyewe anabaki pale mlangoni kulinda kundi lake. Ni Yesu anayebaki mlangoni kwa ajili ya usalama na ulinzi wa kundi lake, na ndiye asubuhi na mapema anatualika kuisikia sauti yake na kumfuata ili atuongoze kwenye malisho na maji. Yesu kama mlango anakazi mbili ndio kuruhusu kondoo wake kutoka na pia kuzuia wezi na wanyang’anyi na wanyama wakali kudhuru kondoo wake.

Yesu kama mlango anawatoa nje kondoo zake na kuwaongoza malishoni, ndio kutuongoza kwenye uhuru na maisha ya kweli. Ni Yeye mwenyewe pia anajitoa kuwa chakula chetu kwa kila siku za maisha yetu, Yesu mchungaji ndiye pia kondoo wa Pasaka anayejitoa kwenye meza ile ya Neno lake na katika meza ile ya Ekaristi Takatifu. Yesu anatualika kutoka katika zizi, kutoka mle ndani kunakokuwa na hewa na harufu na mazingira yasiyokuwa rafiki kwa afya yetu. Ni anatuaongoza kwenye hewa na malisho na maji safi. Anatuita ili tutoke katika yale yote yanayotufanya kukosa uhuru kamili. Labda yafaa tukumbuka uhuru kamili na anatuotualika Yesu sio ule wa kutii hisia na hulka zetu bali kukubali sasa kuishi kama wana wa Mungu wa kuisikiliza na kuitii sauti ya Yesu, ni kukubali kuwa wana pamoja na Mwana pekee wa Mungu. Uhuru wa kweli ni katika kuenenda kadiri ya maongozi ya Mungu na si kinyume chake. Ni kukubali kutoka na kubadili vichwa vyetu na hivyo kuwa na sura halisi ya Mungu, sio Mungu anayekuwa mbali nasi bali anayetujua kila mmoja wetu kwa majina na hali zetu, anayetupenda bila masharti na kutuongoza hata tunapokuwa katika hali duni na dhaifu, anayetualika kumfuata Yeye tu kwani daima ni mwema kwetu na anatuongoza kwenye malisho na maji safi ya utulivu.

Ni Mungu anayetupenda bila masharti na ndio kusema sio kwa masilahi yake bali yangu na yako, anatupenda bila kusubiri malipo au faida binafsi ila ni kwa ajili ya wokovu wetu wanadamu. Anatualika kututoa kutoka utumwa wa pesa, madaraka na ukubwa, chuki na magomvi, itikadi na hata vifungo vyetu vya ndani vya maisha. Anatutoe nje ili tuweze kuwa na uhuru kamili kwani Yeye anatupenda. Yeye anatuongoza kwenye njia iliyo salama. Kukubali kuisikia sauti yake na kuongozwa naye ni kuingia katika ulimwengu mpya, ulimwengu wa kuongozwa na mantiki ya Mungu mwenyewe na si tena ile ya kibinadamu inayotufanya kuwa watumwa. Kinyume chake ni wezi na wanyang’anyi wanaokuja ili kuiba, kuua na kuharibu. Yesu anakuja sio kuiba wala kuua au kuharibu bali ili tuweze kupata maisha ya kweli, uzima wa kweli, uzima wa milele.

Nawatakieni nyote tafakari njema na Dominika njema na tuzidi kusali na kuombea miito. Nawaalika kusali pia kwa ajili ya ulimwengu mzima na hasa nayakati hizi tunapopitia mazingira magumu ya janga hili la COVID-19. Tuwaguse na tuwabebe katika sala zetu wagonjwa, wauguzi wa ngazi mbalimbali, viongozi wa ngazi mbalimbali wanaojitoa kweli kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi na misaada ya kuokoa uhai wa mwanadamu, wanaojitolea pia kwa huduma mbali mbali popote ulimwenguni kusaidia wagonjwa na hata kuwazika wafu wetu na wanaokuwa wahitaji zaidi, maskini na wenye shida mbali mbali ambao wanakosa kimbilio na msaada na wote wanaokuwa katika uhitaji wa sala na maombi yetu.

01 May 2020, 08:28