Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu: Matatizo, changamoto na suluhu zilizotolewa na Wakristo wa Kanisa la Mwanzo: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti na Injili ya upendo kwa maskini! Tafakari ya Neno la Mungu: Matatizo, changamoto na suluhu zilizotolewa na Wakristo wa Kanisa la Mwanzo: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti na Injili ya upendo kwa maskini! 

Jumapili ya V ya Pasaka: Kanisa la Mwanzo: Matatizo, Changamoto na Ufumbuzi

Injili ya leo ni sehemu ya mafundisho hayo ambayo pia yanafahamika kama wosia kwa kuwa ndiyo yalikuwa ya mwisho mwisho kabla ya kukamatwa, kuteswa na kufa kwake Msalabani. Yesu anatambua yale yatakayowakabili wanafunzi wake baada ya Yeye kuondoka. Anatambua kuwa watakuwa wanaanza awamu mpya ya maisha ambayo hawakuwahi kuyaishi. Umoja wa Kanisa!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayatafakari Masomo ya dominika ya tano ya Pasaka.  Somo la kwanza (Mdo. 6:1-7) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Katika kipindi hiki cha Pasaka, kitabu cha Matendo ya Mitume kinaendelea kutupatia mafundisho kwa njia ya masimulizi yanayohusu hatua mbalimbali ya ukuaji wa kanisa la mwanzo. Ni kitabu hiki kinachoonesha  kwa namna iliyo wazi zaidi kuwa ufufuko wa Kristo ndio ulioashiria mwanzo wa kanisa. Katika dominika zilizopita, masimulizi ya kitabu hiki yamekuwa yanatoa zaidi picha chanya ya ukuaji wa Kanisa: mahubiri ya Petro, ujasiri wa mitume, wongofu na ubatizo wa watu wengi hadi hatua ya uundwaji wa Jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Somo la leo linaonesha kuwa pamoja na mambo yake yote mazuri, Kanisa hilo la mwanzo halikukosa changamoto. Kundi moja katika jumuiya lilianza kunung’unika kuwa linabaguliwa katika kupata huduma na mahitaji ya kila siku. Tatizo hili lilikuwa kubwa na lilihatarisha umoja na mafungamano ya jumuiya nzima.

Mitume waliguswa na tatizo hili. Walilikusanya kundi zima na kuzungumza pamoja. Wakaona si vema wao kuendelea kushugulika na mambo yote mawili yaani huduma ya Neno na huduma ya kijamii. Hivyo wakachagua mashemasi 7, wakawakabidhi huduma ya jamii na wao wakabaki na huduma ya Neno. Huduma zote hizi mbili zinawakilisha kazi nzima ya uchungaji ambayo kanisa inalitekeleza kama wajibu wake wa msingi. Si huduma zinazopingana bali zina mlengo mmoja wa kumkomboa mwanadamu katika ukamilifu wa ubinadamu wake yaani roho na mwili. Ni katika mtazamo huu pia somo linatoa chimbuko la Huduma ya Ushemasi ambayo imeunganishwa katika Sakramenti moja ya Daraja Takatifu na huduma ya kikuhani. Somo hili linatupatia tafakari kuhusu utatuzi wa changamoto mbalimbali katika jumuiya zetu. Hakuna jumuiya isiyokutana na changamoto. Na changamoto hizi, ziwe ndogo au kubwa, kama zisiposhughulikiwa vizuri na kwa wakati zinaweza kuhatarisha uhai wa jumuiya yenyewe. Jumuiya kamili siyo ile isiyo na changamoto bali ni ile inayojitahidi katika hatua zake mbalimbali kutafuta ufumbuzi wa changamoto zake, ili kulinda uhai wa jumuiya yenyewe.

Somo la pili (1Pet 2:4-9) ni kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote. Katika somo hili, Mtume Petro anazungumzia hali na hadhi mpya ya wakristo baada ya ubatizo. Anaeleza kuwa kwa ubatizo mkristo anafanywa kuwa jiwe hai linalojenga mwili wa kiroho wa Kristo, yaani Kanisa. Tunafahamu Kanisa kama jengo linalojengwa kwa mawe au matofali. Petro analiona jengo hilo la Kanisa kama alama ya mwili wa kiroho wa Kristo na hivyo yale mawe au matofali ambayo kwayo kanisa zima linasimama, ndio wakristo wenyewe.  Mtume Petro anaongeza kuwa kwa Ubatizo, mkristo anafanywa kuwa kuhani, yaani Padre. Ukuhani huu wa mbatizwa ndio ule ukuhani ambao Kanisa linauita ukuhani wa jumla ukitofautishwa na ule ukuhani wa daraja. Kwa ukuhani huu wa jumla, kila mbatizwa anashirikishwa kazi zile zile za Kristo kuhani, nabii na mfalme. Mkristo hushiriki ukuhani wa Kristo  kwa kuutakatifuza ulimwengu kwa sala;  hushiriki unabii wa Kristo kwa kufundisha, kutetea na kushuhudia ukweli kama ulivyofunuliwa na Mungu na kuendelezwa na mafundisho ya kanisa;  na hushiriki ufalme wa Kristo kwa kujibidiisha kuujenga ufalme wa Mungu katika mazingira ya jamii anamoishi na kufanya kazi.

Injili (Yoh 10:1-10) Katika Injili ya leo, Kristo anasema kuwa Yeye ndiye Njia, Ukweli na Uzima. Tupo katika sura ya 14 ya Injili kama ilivyoandikwa na Yohane. Kadiri ya mpangilio wa Injili ya Yohane, sura ya 13 hadi ya 17 zinaeleza tukio la Karamu ya mwisho ambayo Yesu alikula na wanafunzi wake. Baada ya Yesu kuwaosha wanafunzi miguu na baada ya Yuda kuwa ameondoka ndipo Yesu akaanza kuwapa mafundisho mbalimbali. Injili ya leo ni sehemu ya mafundisho hayo ambayo pia yanafahamika kama wosia kwa kuwa ndiyo yalikuwa ya mwisho mwisho kabla ya kukamatwa, kuteswa na kufa kwake Msalabani. Yesu anatambua yale yatakayowakabili wanafunzi wake baada ya Yeye kuondoka. Anatambua kuwa watakuwa wanaanza awamu mpya ya maisha ambayo hawakuwahi kuyaishi. Utume anaokwenda kuwaachia sio mdogo; una madai mengi na utawahitaji vingi, na hayo yote yanaweza kuwa sababu ya kuwahangaisha na hata kuwakatisha tamaa. Ni kwa sababu hii anaanza kwa kuwatia moyo akisema msifadhaike mioyoni mwenu – msiwe na wasiwasi – tulieni. Anaongeza kusema muaminini Mungu na niaminini mimi pia. Hapo anawahakikishia kuwa imani anayowaachia inayo nguvu ya kuwavusha katika yote hayo na kuwafikisha kule ambako Yeye anatangulia kuwaandalia makao. Anawaalika wayasimike maisha yao na utume wao wote katika msingi ambao ni Yeye mwenyewe.

Ni katika mazingira haya anasema Yeye ni njia, ukweli na uzima. Kwanza; Njia anayokwenda kuipitia yeye ndiyo njia anayowaalika na wao wajiandae kuipitia, nayo ni njia ya Msalaba. Wajiandae kuupokea msalaba kama yeye anavyoupokea lakini pia waupokee msalaba kama kumpokea Kristo mwenyewe. Pili, utume anaowaachia utakuwa ni wa kufundisha, kuuishi na kuushuhudia ukweli. Hapo anawakumbusha kuwa Yeye ndio huo ukweli. Wamfundishe yeye, wamuishi Yeye na wamshuhudie Yeye daima. Tatu, Yeye ndiye uzima. Ndiye kitulizo wawapo duniani na tuzo lao mbinguni. Uzima huu ndio watakaoupokea watakapokuwa wanapokea wao wenyewe sakramenti anazowaachia na ndio uzima wataowajalia watu kwa  njia ya sakramenti hizo hizo watakazokuwa wanaadhimisha. Sio kwa bahati mbaya kwamba Yesu anatoa fundisho hili akiwa katika karamu ya mwisho na akiwa punde tu amemaliza kuianzisha sakramenti ya daraja Takatifu na ya Ekaristi.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu katika dominika ya leo yanatualika tuyasimike maisha yetu katika Kristo; njia, ukweli na uzima ili tuweze kuzikabili changamoto mbalimbali katika maisha na utume wetu kama wabatizwa. Baba Mtakatifu Francisko ametukumbusha mara nyingi kuwa ukristo sio mkusanyiko wa kanuni, mawazo au nadharia bali ni maisha yaliyojengwa juu ya nafsi ya Kristo. Kuwa mkristo maana yake ni kumfuasa Kristo. Yesu anapojitambulisha leo kuwa yeye ndiye njia, ukweli na uzima analithibitisha fundisho hili na kutuhakikishia kuwa maisha yetu kama wakristo yanapata maana pale yanapokuwa na msingi katika yeye.

Ni jambo la pekee kuona pia namna ambayo Liturujia ya leo inaweka sambamba fundisho hili la Yesu pamoja na lile la Mtume Petro katika somo la pili. Mtume Petro amefundisha kuwa kwa ubatizo mkristo ni jiwe hai linalojenga mwili wa fumbo wa Kristo. Naye analijenga kanisa kwa kushiriki katika kazi za Kristo kuhani, nabii na mfalme. Hapa tunauona Ukuhani, Unabii na Ufalme katika maisha ya mbatizwa vikiakisi njia, ukweli na uzima katika Kristo. Liturujia ya leo inapotuonesha uhusiano huu inatualika kutambua kuwa kuuishi vema ubatizo wetu na kutekeleza kikamilifu wajibu wetu wa kikuhani, kinabii na ufalme yaani kujitakatifuza na kuutakatifuza ulimwengu kwa sala, kuushuhudia ukweli na kuusimika duniani ufalme wa Mungu ndiyo kuishika Njia, kuufuata Ukweli na kuishi katika Uzima kama anavyotualika Kristo mwenyewe. Amina.

Neno la Mungu J5 Pasaka
08 May 2020, 14:40