Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu: Jumapili VI ya Kipindi cha Pasaka: Roho Mtakatifu Mfariji, Roho wa kweli na Msaidizi mwingine! Liturujia ya Neno la Mungu: Jumapili VI ya Kipindi cha Pasaka: Roho Mtakatifu Mfariji, Roho wa kweli na Msaidizi mwingine! 

Jumapili VI ya Pasaka: Roho Mtakatifu: Msaidizi Mwingine!

Yesu anawahakikishia kumtuma kwao Msaidizi mwingine ndiye pia Roho wa kweli, atakayebaki nao siku zote. Ni uwepo wa Yesu mwenyewe katika namna na mtindo mwingine. Huyu ni Msaidizi mwingine anayeitwa pia Roho wa kweli. Ni ahadi ya ujio wa Roho huyo ambaye Yesu katika Injili ya Luka anatuambia kuwa Roho wa Bwana yu juu yake, kuwa ni Roho wa Yesu, ni Roho wa Mungu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Sehemu ya Injili ya Dominika ya leo, kama ile ya Dominika iliyopita ni moja ya hotuba za wosia wa Yesu kwa wanafunzi na wafuasi wake wakiwa katika karamu ya mwisho. Wafuasi wanajawa na mahangaiko na huzuni kubwa si tu akilini bali hata kimwili na kisaikolojia, wanakuwa na mashaka makubwa kusikia kuwa siku itafika ambapo hawatakuwa tena na Bwana na Mwalimu wao katikati yao kama umbo la mwili. Ni wakati wa mashaka ya hatima na maisha yao na hasa kwa kuwa bado hawakuwa wameuelewa ufalme wake Kristo. Kwao bado walimwona Yesu kama Masiha anayekuja kuwapigania na kuwakomboa kutoka utawala wa Kirumi na si vinginevyo. Lakini Yesu anawahakikishia kumtuma kwao Msaidizi mwingine ndiye pia Roho wa kweli, atakayebaki nao siku zote, atakayekaa kwao na ndani yao. Ni uwepo wa Yesu mwenyewe katika namna na mtindo mwingine. Na ndio uwepo wake kwa huyu Msaidizi mwingine anayeitwa pia Roho wa kweli, ingawa hataonekana kwa macho ya nyama bali kwa yale ya imani. Ni ahadi ya ujio wa Roho huyo ambaye Yesu katika Injili ya Luka anatuambia kuwa Roho wa Bwana yu juu yake, kuwa ni Roho wa Yesu, ni Roho wa Mungu, ndiye huyo anayebaki na wafuasi wa Kristo siku zote mpaka ukamilifu wa dunia. Luka 4:1,14,18.

Ni wale tu wanaokubali na kuzishika amri za Kristo hao Roho Mtakatifu mfariji atakaa kwao na ndani yao. Ulimwengu hauwezi kumuona wala kumtambua kwani hawajaweza kuzipokea amri zake Kristo. Ulimwengu hapa haina maana ya wapagani au wasio wakristo bali wale wote wasiokuwa na nafasi ya kulipokea na kuishi kadiri ya Neno lake, kadiri ya amri yake mpya yaani upendo. Ni wale wasiopenda, hao kwa kweli wanakwenda kinyume na misheni na maisha mapya ya wafuasi wa Kristo. Ni katika upendo tu wafuasi wa Kristo watatambulika kuwa ni wafuasi wake na si kwa kitu kingine chochote. Amri za Yesu pamoja hapa anazitamka katika uwingi ila ni ile ile moja ya upendo inayochukua sura mbali mbali. Labda katika lugha yetu ya Kiswahili kwa bahati mbaya hatuna namna mbali mbali za kusema neno kupenda, ila katika lugha ya Kigiriki kuna namna takribani nne za kusema upendo. Na leo Mwinjili Yohane anatumia neno la ‘’αγαπατε’’ ‘’agapate’’ ni kitenzi katika uwingi likimaanisha mkipenda, upendo wa agape ni upendo usio na masharti, ni kupenda kama Mungu anavyotupenda sisi bila kutegemea chochote wala kujitafuta kwa upande wake, kwani Mungu ni Upendo.

Kupenda kwa ajili ya kupenda tu na si kusubiria lolote au chochote kwa upande wangu au wako. Ndio Yesu leo anatualika kupenda kwa namna hiyo hiyo iwe kwa Mungu au kwa jirani. Kupenda kwa sababu tumeumbwa kupenda, na ndio wito wetu wa msingi. Neno Agape katika Agano Jipya linatumika mara 259 na Mwinjili Yohane analitumia mara 26 ndio kusema umuhimu na ulazima wa kupenda kwa mtindo wa agape kwetu sisi rafiki na wafuasi wa Kristo Mfufuka, ulimwengu utatutambua kuwa sisi ni wakristo si kwa wingi wa sala au ibada mbalimbali tunazokuwa nazo bali kwa Injili ya maisha yetu ndio upendo. Roho Mtakatifu leo anatambulishwa kwa majina mawili nayo ni ‘’Msaidizi mwingine’’ na ‘’Roho wa kweli’’. Neno sahihi lililotumika la Kigiriki ni ‘’παρακλητον’’ (paracleton’’ likimaanisha hasa mfariji au anayekupa moyo, mtetezi ila maana halisi ni wakili, anayesimama mahali pako unapokuwa mahakami, ni mtetezi anayejua sheria na mtu wa haki anayefika ili kukusaidia mahakamani.  ‘’Paracleton’’ ni neno lililokuwa linatumika katika mahakama za Kigiriki, likimaanisha yule anayesimama pembeni au karibu au nyuma yako.

Mwanzoni katika mahakama za Kigiriki hakukuwa na utaratibu wa mawakili. Hivyo aliyehukumiwa alipaswa ajitetee mwenyewe, hivyo ingeweza kutokea kuwa mshtakiwa hana hatia, na wakati huo hana uwezo wa kujitetea mahakamani, hivyo tumaini pekee lilibaki ni kutokea mmoja wa kumtetea, wa kumsemea ili aweze kupata haki yake. Ilitosha uwepo wa mtu aliyeheshimika na wote, mtu asiye na hila wala hatia, huyo angeweza kusimama na kwenda kusimama kando au pembeni ya mtuhumiwa bila kusema neno, hiyo ilihesabika na kuonekana kama ishara kuwa mtuhumiwa huyo hana hatia yoyote na hivyo hapaswi kuadhibiwa. Ndiye huyo wakili mtetezi au ‘’paracleton’’. Anayekuja na kusimama pembeni yangu wakati ule sina jinsi yoyote ya kujitetea na kujiokoa. Kwa lugha ya Kilatini alijulikana kama ‘’advocatus’’ ni yule aliyeitwa kwa utetezi, anayefika na kusimama pembeni au nyuma yako kama mtetezi, kama msaidizi wakati wa hukumu na mashitaka. Mwinjili Yohane anamtambulisha Roho Mtakatifu kama ‘’paracleton’’ au ‘’advocatus’’ kwa kuwa tayari anatuonesha Yesu, ingawa ni mtu mwenye haki anasimama akihukumiwa na kuteswa pale msalabani. Mwinjili anaiona pia jumuiya ya Kanisa linaloteswa na kushitakiwa bila kuwa na hatia yeyote.

Kama vile Kristo alivyohitaji wakili mtetezi pale juu msalabani vivyo hivyo na Kanisa lake linahitaji wakili msaidizi na mtetezi dhidi ya yule mwovu, mshitaki na msingiziaji. Kanisa litapitia magumu na mateso na madhulumu mengi yatokayo kwa yule mshitaki ndiye mwovu, hivyo daima litabaki salama kwa kubaki pamoja na Wakili msaidizi, ndiye Roho Mtakatifu. Mathayo 10:19-20 ‘’Basi, watakapowapeleka nyinyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema. Maana si nyinyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu’’. Kristo pia anajulikana kama Msaidizi na ndio maana leo anasema nitawatumia Msaidizi mwingine. Ni Msaidizi kwa maana ya wakili wetu mbele ya yule mwovu na uovu. 1Yohane 2:1 ‘’Watoto wangu, ninawaandikieni mambo haya, kusudi msitende dhambi. Lakini, ikijatokea mtu akatenda dhambi, tunaye mmoja ambaye hutuombea kwa Baba, ndiye Yesu Kristo aliye mwadilifu kabisa’’.  Ni msaidizi wetu au wakili wetu dhidi ya uongo na baba wa uongo yaani Ibilisi. Yohane 8:44 Roho Mtakatifu ni wakili msaidizi wetu kwa maana ile ile ya Yesu kwani ni uwepo wa Kristo Mfufuka pamoja na Kanisa lake kwa namna isiyoonekana tena kama awali kabla ya mateso na kifo na ufufuko wake. Anabaki na Kanisa kulisaidia na kulitetea dhidi ya nguvu za yule muovu na uovu.

Pia anajulikana kama ‘’Roho wa kweli’’, kama mwalimu wa ukweli sote tunaweza kujua jinsi ujumbe unavyoweza kupotea pale unapotoka kwa mtu au kizazi kimoja kwenda kwa mwingine au kizazi kingine. Neno la Yesu na ujumbe wake ni kwa ajili ya watu wote na wa vizazi vyote, mpaka ukamilifu wa dunia. Kwa akili na uwezo wetu wa kibinadamu ni wazi ingekuwa ni juu ya uwezo wetu kuhakikisha ujumbe na Neno lake halipotezi uasili wake. Injili na ujumbe wake unabaki kuwa ni ule ule kwa kuwa Kanisa linasambaza ujumbe huo kwa msaada wa Roho Mtakatifu anayebaki kuwa Mwalimu wetu wa daima. Tunaposoma Neno lake na kuwashirikisha wengine daima hatuna budi kumsikiliza Roho Mtakatifu ndiye Mwalimu wetu. Si tu Roho Mtakatifu anatusaidia katika kuubakisha na kuutunza ujumbe na Injili yake Kristo bali pia kutufundisha kweli yote. Na ndio utaona Kanisa kila siku linatualika kulitafakari Neno lake na hata kutambua kweli za Injili zinazojibu maswali ya nyakati zote kiaminifu. Hata wanafunzi wa Yesu wa mwanzo hawakuwa na uwezo kama ambavyo hatuna hata nasi leo kuweza kuujua ukweli wote hivyo daima Roho Mtakatifu anabaki kuwa Mwalimu anayetufundisha kweli yote.

Si kwamba anatufundisha kweli nyingine bali ni Kweli yote kwani ukweli ni mmoja na ndiye Yesu mwenyewe kama tulivyotafakari Dominika iiyopita. ‘’Mimi ni njia, kweli na uzima’’ Yohane 14:6. Na ndio maana Kanisa mpaka leo linatualika sote kuwa wazi kwa msaada wa Roho Mtakatifu katika kuufikia ukweli wote, kila siku tunajifunza kweli hiyo hivyo hatuwezi kusema kuwa tayari tumekamilisha kuujua ukweli wote, hapana kwani hatuwezi pia kimsingi kuujua ukweli wote vinginevyo itakuwa ni kukufuru, ni Yesu tu, ni Mungu tu aliye kweli yote, bali kwa msaada wa Roho Mtakatifu anatusaidia katika kuufikia ukweli wote kila siku katika maisha ya Kanisa. Ni Yesu aliye kweli ndiye anayemfunua Mungu Baba katika ukamilifu wake. Mwinjili Yohana tayari anamtambua yule muovu kuwa ni baba wa uongo kwani kweli haimo ndani mwake. Yohane 8:44 ‘’Nyinyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutelekeza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo’’. Sisi ni wana wa Mungu aliye kweli hivyo hatuna budi kuishi kweli na kweli tunayoalikwa kuishi ndio upendo kwa Mungu na kwa jirani. Aliye wa kweli na kuongozwa na Roho wa kweli huyo ataishi katika kweli hiyo na ndio kushika maagizo yake, kupenda bila masharti. Kinyume chake ni kuwa wafuasi wa baba wa uongo ndiye muovu au Ibilisi. Niwatakie tafakari na Dominika njema.

15 May 2020, 07:39