Jumapili ya IV ya Kipindi Cha Pasaka: Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2020: Maneno ya Miito! Jumapili ya IV ya Kipindi Cha Pasaka: Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2020: Maneno ya Miito! 

Yesu Mchungaji Mwema! Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani, 2020

Kristo Yesu ndiye Mchungaji Mwema na Mlango wa kondoo! Yeye ni njia ya kufika kwa Mungu. Ni Yesu aliyekuja kufungua na kuonesha njia mpya ya mahusiano kati ya mwanadamu na Mungu na njia salama ya mwanadamu kufika katika patakatifu pa patakatifu. Kristo Yesu anawalika watu wampokee Yeye kama njia salama na ya uhakika ya kuwadumisha katika mahusiano mema na Mungu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayatafakari Masomo ya dominika ya nne ya Pasaka, dominika ambayo huitwa pia dominika ya Kristo Mchungaji mwema na ni Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2020. Masomo ya dominika hii yanatualika kupokea mwaliko wa Kristo ili kuingia katika wokovu wake. Tunautafakari ujumbe huu sambamba na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa siku hii ya kuombea miito tukiongozwa na yale ambayo Baba Mtakatifu mwenyewe anayaita “Maneno ya Wito” yaani shukrani kwa wito, ujasiri wa kuupokea, kukabiliana na magumu yake na mwisho kuutolea wito kama wimbo wa sifa na utukufu kwa Mungu kwa kuwa kwa njia yake Mungu mwenyewe anawakomboa wanadamu na ulimwengu mzima.

Somo la kwanza (Mdo. 2:14a, 36-41) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Linaelezea mwitikio wa watu kwa mahubiri ambayo Mtume Petro aliyatoa siku ya Pentekoste. Itakumbukwa kwamba ni katika siku hii ambapo Petro alijitokeza nje kwa mara ya kwanza akiwa na mitume wanzake na kuanza kuhubiri kuwa Kristo aliyeteswa, akasulubiwa na kufa sasa amefufuka kama alivyosema. Mahubiri haya ya Mtume Petro yaliwachoma watu mioyo kwa maana yaliwaonesha kuwa Kristo alikuja kwa ajili ya wokovu wao lakini wao hawakumpokea na badala yake walimuua kwa kumtundika Msalabani. Mtume Petro aliwaonesha kuwa mlango wa kumpokea Kristo haujafungwa kwa kifo chake, badala yake uko wazi na wote wanaalikwa kuuingia kwa kuupokea ubatizo kwa jina lake kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Umati mkubwa ulilipokea Neno na wakabatizwa siku hiyo watu wapatao elfu tatu.

Katika nafasi ya kwanza, somo hili linaonesha ule uliokuwa muundo na ukuaji wa Kanisa la mwanzo baada ya ufufuko wa Kristo. Kama tunavyoona katika mahubiri ya Petro, kiini cha utendaji wa kanisa la mwanzo kilikuwa ni kutangaza Habari Njema na kuwaalika watu kumwongokea Kristo na kubatizwa. Hata hivyo, hata kwetu leo somo hili linatuonesha kuwa Neno la Mungu tunalolisikia ni lazima liyachokoze maisha yetu ili nguvu yake ya kuokoa idhihirike ndani yetu. Bila kuliruhusu Neno la Mungu kuyachokoza na kuyachokonoa maisha yetu tutakuwa tunalisoma na kulisikiliza kama tunavyosikiliza “michapo” na kuiachia hapo hapo. Ni somo linalotualika tuikubali changamoto ya wongovu ambayo Neno la Mungu linaweka daima mbele yetu.

Somo la pili (1Pet 2:20b-25) ni kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa watu wote. Katika somo hili, Mtume Petro anaelekeza mafundisho kuhusu mateso, kifo na ufufko wa Kristo kwa watu wa tabaka la chini katika mazingira ya wakati wake. Kwa kiasi kikubwa kundi hili la tabaka la chini lilikuwa ni kundi la watumwa na watumishi wa ndani ambao licha ya kuwa na kazi ngumu, walipokea pia manyanyaso mengi kutoka kwa waajiri na bwana zao. Tofauti kabisa na ambavyo huenda tungetegemea kwamba Petro awahamasishe kupindua hali mara moja au na wao kuonesha ukaidi, yeye anawafundisha kudumu katika kutenda mema na kujifunza kutoka katika kielelezo cha Kristo. Anawaonesha kuwa Kristo aliteseka bila kuwa na hatia yoyote, allipotukanwa hakujibu kwa tukano bali aliyaweka maisha yake yote mikononi mwa Mungu, hakimu mwenye haki. Mtume Petro anapotoa mafundisho ya mateso ya Kristo kwa kundi la watu ambao kwa wakati huo wanateseka, anawafanya watu hao kupata picha halisi juu ya kile ambacho Kristo mwenyewe alikipitia katika mateso yake. Lakini pia kurejea mateso haya ya Kristo kwa kundi hili la watu ni kuendeleza ufunuo wa kibiblia na mafundisho ya kanisa kuhusu jamii kuwa kutafuta amani kwa njia ya mapambano au vita ni kuongeza matatizo kuliko yale yaliyokuwapo.

Injili (Yoh 10:1-10) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Yohane. Kristo anajitambulisha kuwa ndiye Mchungaji Mwema, kondoo wake huisikia sauti yake nao humfuata. Kwa kutumia lugha iliyozoeleka kwa wafugaji wa kipindi chake, Yesu analizungumzia taifa la Israeli kama kondoo wa malisho ya Mungu. Naye ndiye mchungaji mwema kwa sababu yuko tofauti na wengine waliowekwa kulisimamia kundi hilo kwa sababu yeye hatafuti maslahi yake wala hatafuti kuwapoteza kondoo bali kuwafikisha katika malisho bora. Yeye pia ndio mlango wa zizi, yaani uhakika wa uzima na usalama wa kondoo wake. Maneno haya haya ya Yesu tunaweza pia kuyatafsiri katika muktadha wa hekalu la Yerusalemu. Katika kipindi cha Nabii Nehemia kulikuwapo katika kuta za Yerusalemu, mlango uliokuwa ukiitwa mlango wa kondoo. Mlango huu ulitumika kupitishia kondoo waliokuwa wanakwenda kutolewa sadaka hekaluni. Huu ulikuwa ni mlango ulioelekeza kuingia moja kwa moja katika sehemu ya hekalu iliyoitwa patakatifu pa patakatifu, yaani alipo Mungu. Kumbe Yesu anapojitambulisha leo kuwa ndiye mlango wa kondoo, anajitambulisha kwa taifa zima la Mungu kuwa ni yeye aliye njia ya kufika kwa Mungu. Ni Yesu aliyekuja kufungua na kuonesha njia mpya ya mahusiano kati ya mwanadamu na Mungu na njia salama ya mwanadamu kufika katika patakatifu pa patakatifu. Kwa maneno haya basi Yesu alilenga kuwaalika watu wampokee yeye kama njia salama na ya uhakika ya kuwadumisha katika mahusiano mema na Mungu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika hii ya nne ya Pasaka tunautafakari ujumbe wa kuupokea mwaliko wa Kristo mchungaji mwema na mlango wa kutufikisha kwa baba sambamba na maadhimisho ya Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani. Katika mwanga wa masomo ya leo, tunauona wito kama namna ifaayo ya kuuitikia na kuupokea mwaliko wa Kristo. Dominika hii ni ya kuombea miito ya aina zote katika kanisa: wito wa ndoa, wito wa upadre na wito wa maisha ya utawa yaani ubruda na usista. Baba Mtakatifu Francisko ametualika tuiadhimishe siku hii ya sala kwa kuyatafakari yale anayoyaita “Maneno ya wito” ambayo ni Shukrani, Ujasiri, kukabiliana na magumu ya wito pamoja na Kutolea Sifa. Kwa maneno haya, Baba Mtakatifu Francisko anatukumbusha kuwa wito wowote ule ni zawadi kutoka kwa Mungu. Sio sisi tunaomchagua Mungu bali ni Yeye anayetuita ili tumfuate kupitia wito huo. Hivyo ni muhimu kuupokea kwa shukrani kama kutimiza yale ambayo si mapenzi yetu bali mapenzi yake Mungu.

Tunapoupokea wito kwa shukrani Baba Mtakatifu anatukumbusha kuwa katika safari ya kuuishi hatuko peke yetu. Mungu mwenyewe anasafiri pamoja nasi. Hivyo ni muhimu katika kuuishi wito kujiaminisha kwa Mungu anayeongoza mapito yetu yote. Kama safari yoyote ile, safari ya wito inayo pia magumu yake, inayo majukumu ya kutimiza ambayo si wakati wote yanakuwa rahisi. Katika hali hii, Baba Mtakatifu anatualika kujikita kikamilifu katika wito na kumkazia macho yeye aliyetuita bila kupepesa macho upande huu wala upande ule ili kutafuta ahueni. Kwa jinsi hii maisha yetu yote yatakuwa ni wimbo wa sifa na utukufu kwa Mungu mwenyewe ambaye kwa wito alioutuitia anakusudia kutuokoa sisi wenyewe, kuwaokoa wenzi wetu na kuuokoa ulimwengu mzima.

Liturujia J4 ya Pasaka

 

 

01 May 2020, 12:38