Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Kutukuka kwa Ubinadamu Mbinguni
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Katika dominika hii ya leo, Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana. Sherehe hii ni adhimisho la mojawapo ya mafumbo makuu ya imani yetu kuwa siku 40 baada ya kufufuka, Kristo alipaa mbinguni na huko amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi. Katika dominika hii pia Kanisa linaadhimisha Siku ya 54 ya Upashanaji Ulimwengu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika siku hii unaongozwa na maneno ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Kitabu cha Kutoka: Kut. 10:2 “Nawe upate kusema masikioni mwa mwanao na masikioni mwa mjukuu wako” – Maisha hutengeneza Historia.
Somo la kwanza (Mdo. 1:1-11) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Mwandishi wa kitabu hiki ni yule yule aliyeandika Injili ya Luka. Injili aliiandika kwa Teofilo na hata hapa anaeleza kuwa kitabu hiki pia amekiandika wa huyo huyo Teofilo. Inawezekana Teofilo huyu alikuwa ni afisa fulani aliyehitaji kujua Habari Njema lakini pia kwa kuzingatia maana ya jina lenyewe Teofilo, yaani mpendwa wa Mungu, Luka alimaanisha kuandika kwa ajli ya wapendwa wote wa Mungu. Katika somo hili, Luka anaeleza namna Yesu alivyopaa mbinguni. Yesu akiwa katikati ya wanafunzi wake, aliinuliwa na wingu likampokea kutoka machoni pao. Tukio hili la kupaa Bwana ambalo Luka amelielezea mwishoni mwa injili yake na pia mwanzoni kabisa mwa kitabu hiki cha Matendo ya Mitume lina maana ya pekee. Ni tukio linalohitimisha kazi nzima aliyokuja kuifanya Kristo duniani. Kazi hiyo ambayo ilianza kwa umwilisho wake na kufikia kilele chake pale alipokufa msalabani na kufufuka, sasa inahitimishwa kwa tukio hili la kupaa kwake mbinguni. Tukio hili linamaanisha kuanza kwa awamu mpya ya kuuishi ukombozi aliouleta Kristo na kuyaendeleza matunda yake kwa njia ya ushuhuda. Kristo mwenyewe analitamka hili anapowaambia wanafunzi wake kuwa “akiisha wajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu na katika Uyahudi wote na Samaria na hata miisho ya dunia”.
Somo la pili (Ef 1:17-23) ni kutoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso. Katika somo hili Paulo anaelezea kupaa mbinguni kama tendo la kutukuzwa kwa Kristo. Ni tendo la Kristo kuvikwa taji kwa ushindi mkubwa aliouleta duniani; kumkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi na kumrudisha kwenye nuru ya kuwa mwana wa Mungu. Mtume Paulo anaelezea kutukuzwa huku kwa Kristo anaposema kuwa Kristo amewekwa mkono wa kuume wa Mungu, amewekwa juu sana kuliko ufalme wote na nguvu na usultani na kila jina litajwalo. Mtume Paulo anatumia pia maneno ya Zaburi ya 110 isemayo “neno la Bwana kwa Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume hata niwafanyapo adui zako kuwa chini ya miguu yako”. Anaonesha kuwa ni maneno yanayotimia katika tendo hili la Kristo kupaa mbinguni kwa sababu ni Kristo ambaye akishapaa mbinguni amewekewa vitu vyote kuwa chini ya miguu yake. Mtume Paulo haachi kuonesha uhusiano uliopo kati ya tendo hili na manufaa kwa wote wanaomwamini Kristo. Anaeleza kuwa kanisa ni mwili wa fumbo wa Kristo ambapo Kristo mwenyewe ndiye kichwa na waamini wake wote ndio mwili wake. Kwa lugha hii ya picha, Paulo anaonesha kuwa kutukuzwa kwa Kristo ni ishara na uhakika kuwa mwili wake wote, yaani kanisa zima nalo litatukuzwa, na kule ambako Yeye ametangulia ndipo watakapokuwapo wote wanaomwamini.
Injili (Mt 28:16-20) Katika injili ya leo, Kristo anawaagiza wanafunzi wake akisema “enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu”. Agizo hiili ndilo la mwisho kadiri ya mwinjili Mathayo na ndilo agizo linalotangaza kiini cha utume wa kimisionari wa Kanisa, yaani kutoka – kufundisha na kubatiza. Kwa jinsi hii, Kristo hatoi agizo hili kwa wanafunzi wale waliokuwa wakimsikiliza tu bali ni agizo la kudumu litakaloambatana na Kanisa lake lote hadi hapo atakaporudi. Kwa agizo hili ni kanisa zima linatumwa kutoka kwenda kumtangaza Kristo na kuwajalia watu wote uzima kwa maadhimisho ya Sakramenti. Katika maadhimisho ya Sherehe ya leo ya kupaa Bwana, agizo hili linaendeleza fundisho la somo la kwanza. Linaonesha kuanza kwa awamu mpya baada ya ile ya uwepo wa Kristo duniani kwa jinsi ya mwili. Awamu hii mpya ni awamu ya Kanisa ambayo waamini na Kanisa zima wataiishi kwa kuwa mashahidi wa yale aliyoyafundisha na kuyatenda Kristo ili kuendeleza kazi ya ukombozi aliyokuja kuifanya. Kristo amepaa lakini utume wake unaendelea kwa njia ya Kanisa na ndani ya Kanisa. Naye ameahidi kuendelea kuwa na Kanisa lake siku zote hadi mwisho wa dunia.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Sherehe hii ya kupaa Bwana ni adhimisho la mojawapo ya mafumbo makuu ya imani yetu kumhusu Kristo. Katika kanuni ya Imani tunasali na kusadiki kuwa Kristo alifufuka na akapaa mbinguni. Huko ameketi kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi na kutoka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Kutoka katika kiri hii ya imani na hasa baada ya kupata ufafanuzi wa masomo ya sherehe hii, tunayachota maneno mawili ya kutuongoza katika tafakari yetu ya leo. Maneno hayo ni “amepaa mbinguni” na “ameketi kuume kwa Baba”. “Amepaa mbinguni” humaanisha kuwa sasa Kristo amerudi kule alikokuwa mwanzo. Anaurudia utukufu wa umungu wake ambao ulikuwa umefichwa na mwili wa ubinadamu alioutwaa akiwa hapa duniani. Mbingu ndilo neno linalomaanisha yalipo “makao” ya Mungu au unapokaa umungu. Kumbe Yesu kupaa mbinguni ni kumaamisha kuwa anaurudia umungu wake kwa namna iliyo wazi zaidi. Yeye mwenyewe anasema “Hakuna mtu aliyepaa mbinguni ila Yeye aliyeshuka kutoka mbinguni yaani Mwana wa Mungu” (Rej. Yon 16:28) kumaanisha kuwa ni Yule tu ambaye alikuwa Mungu anaweza kuurudia umungu wake.
“Ameketi kuume kwa Baba” humaanisha nguvu na mamlaka ambazo sasa Kristo amezitwaa. Katika lugha ya kibiblia iliyoenea sana katika Agano la Kale, “mkono wa kuume” humaanisha nguvu au mamlaka. Zaburi hutumia mara nyingi sana maneno “mkono wa kuume wa Bwana” kumaanisha nguvu ya Bwana. Hutumia kuisifu nguvu ya Bwana inayookoa, inayotenda makuu n.k. Kumbe Kristo kuketi mkono wa kuume wa Bwana humaanisha Kristo kuishiriki nguvu ile ile ya Mungu. KKK huongeza kuwa “kukeki kuume kwa Baba huonesha kuanzishwa kwa utawala wa Masiha na ni utimilifu wa manono ya Nabii Danieli kuhusu Mwana wa Mtu: ‘naye akapewa mamlaka na utukufu na ufalme ili watu wa kabila zote na mataifa yote na lugha zote wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele ambayo haitapita kamwe na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa” (Rej. KKK 664). Kristo anapourudia waziwazi umungu wake na kutwaa nguvu na utawala anautukuza ubinadamu wote na kuuelekeza kufika uwinguni yaliko makao yake ya umilele. Anatualika tuendeleze kazi yake ya ukombozi kwa kuwa mashahidi wake naye atakuwa pamoja nasi hadi mwisho wa nyakati.