Pentekoste: Pasaka: Kanisa, Umoja, Amani na Upatanisho!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Sherehe ya Pentekoste ni kilele cha maadhimisho ya siku 50 tangu Kristo Yesu alipofufuka kutoka kwa wafu. Huu ni utimilifu wa Pasaka ya Kristo kwa kummimina Roho Mtakatifu na Mapaji yake saba. Huyu ni Roho Mtakatifu ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kutoka utimilifu wake Kristo, Bwana anammimina Roho Mtakatifu kwa wingi. Sherehe ya Pentekoste ni utimilifu wa ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ufalme wa Mungu uliotangazwa na Kristo Yesu uko wazi kwa ajili ya hao wanaomsaidiki katika unyenyekevu wa mwili na katika imani, wanashiriki tayari ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Roho Mtakatifu anauingiza ulimwengu katika “nyakati za mwisho, nyakati za Kanisa”. Roho Mtakatifu ni Paji la Mungu ambaye ni upendo. Utume wa Kristo Yesu na Roho Mtakatifu unakamilika katika Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo na Hekalu la Roho Mtakatifu na kuwashirikisha waamini wa Kristo Yesu katika Fumbo la Roho Mtakatifu.
Roho Mtakatifu hutayarisha watu, akiwaendea kwa neema yake ili kuwapeleka kwa Kristo Yesu. Anamdhihirisha kwao Bwana Mfufuka, anawakumbusha neno lake, anawafumbua akili zao ili kulitambua Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Analifanya Fumbo la Kristo liwepo kwao, juu ya yote katika Ekaristi Takatifu na mwishowe, kuwapatanisha na kuwaweka katika umoja na Mungu ili wazae matunda mengi. Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu: linatumwa kutangaza na kushuhudia; kutekeleza na kueneza Fumbo la Ushirika wa Utatu Mtakatifu. Kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Kristo anavishirikisha viungo vya mwili wake Roho Mtakatifu, Mtakasaji na Mwalimu wa Sala. Rej. KKK namba 731-741. Roho Mtakatifu ndiye anayejenga na kudumisha umoja wa Kanisa unaojidhihirisha kwa utofauti wa karama na kutenda kazi ili kusaidiana na kukamilishana kama anavyosema Mtakatifu Paulo katika Somo la Pili. 1 Kor. 12:3-7; 12-13. Kwa njia ya Roho Mtakatifu wote wamebatizwa na kufanywa viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Huu ni umoja katika matumaini na imani; Ubatizo, Bwana, Roho Mtakatifu na Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote. Rej. Ef. 4:4. Sherehe ya Pentekoste inabeba umuhimu wa pekee, kwani Kanisa linaadhimisha pia Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Ut Unum Sint” yaani “Ili wawe wamoja: Dhamana ya Kiekumene”. Ujumbe huu ulichapishwa hapo tarehe 25 Mei 1995. Huu ni mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene yaliyoanzishwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hii ni njia ya Kanisa inayojikita katika upyaisho wa maisha na wongofu wa ndani. Ni mwaliko kwa waamini kufahamu Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake, anasema, viongozi wa Makanisa wanapaswa kuendelea kuimarisha na kudumisha mchakato wa uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, Wakristo washikamane ili kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, hatimaye, siku moja Wakristo wote waweze kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa! Uekumene wa damu unafumbatwa katika dhana ya: mauaji, nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaouwawa si kutokana na madhehebu yao, bali imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Uekumene na Ubatizo wa damu, tayari umekwisha waunganisha Wakristo huko mbinguni, mbele ya Mwana Kondoo wa Mungu. Sherehe ya Pentekoste ni Siku ya Kuzaliwa kwa Kanisa. Kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, Mitume waliokuwa wamejifungia ndani kwa woga wa Wayahudi, waliweza kutokea hadharani na kutangaza kwa ari na moyo mkuu Fumbo la Pasaka. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, Kanisa likaongezeka na kuenea sehemu mbali mbali za dunia kama inavyojidhihirisha kwenye Somo la Kwanza kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 2: 1-11.
Roho Mtakatifu aliwaonesha dira na kuwapatia mwongozo wa kuleta mageuzi katika historia ya maisha ya binadamu. Hata katika ulimwengu mamboleo, Kanisa linapaswa kumsikiliza Roho Mtakatifu pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati. Roho Mtakatifu ni alama na utambulisho wa Kanisa. Huyu ndiye Roho Mtakatifu Mfariji, Mtetezi, Shuhuda na Hakimu. Rej. Yn. 15:26.Katika Injili kama ilivyoandikwa na Yohane 20:19-23, Kristo Yesu anawapatia wanafunzi wake amani kama zawadi ya ufufuko wake, inayowakirimia utulivu wa ndani. Amani na utulivu wa ndani, viwasaidie waamini kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mtakatifu Yohane XXIII anasema, amani ya kweli inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru kamili! Amani kama zawadi kutoka kwa Kristo Mfufuka inawataka wafuasi wa Kristo kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kristo Yesu aliwaambia wafuasi wake “Wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa; na wowote watakaofungiwa dhambi, wamefungiwa.
Kristo Yesu ndiye mganga wa roho na miili yetu. Yeye ndiye mwenye uwezo wa kusamehe dhambi na kuponya magonjwa na hivyo, kumrejeshea tena mja wake afya ya roho na mwili. Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho, kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu linaendeleza kazi ya uponyaji na ya wokovu. Ningependa kuhitimisha tafakari hii kwa Sala ya Sherehe ya Pentekoste: Ee Mungu Baba Mwenyezi, wewe unalitakasa Kanisa lako lililo kati ya makabila na mataifa yote kwa Fumbo la Sherehe ya leo. Eneza mapaji ya Roho Mtakatifu popote duniani; na zile karama ulizozitoa tangu mwanzo wa kuhubiriwa Injili, hata sasa uzieneze kwa juhudi ya waamini wako. Ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili na wajenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani! Amina!
Wimbo wa Roho Mtakatifu kwa Lugha ya Kilatin
Veni, creator Spiritus, / mentes tuorum visita, / imple superna gratia / quae tu creasti pectora. Qui diceris Paraclitus, / donum Dei altissimi, / fons vivus, ignis, / caritas et spiritalis unctio. Tu semptiformis munere, / dextrae Dei tu digitus, /tu rite promissum Patris / sermone ditans guttura. Accende lumen sensibus, / infunde amorem cordibus, / infirma nostri corporis / virtute firmans perpeti. Hostem repellas longius / pacemque dones protinus; / ductore sic te praevio / vitemus omne noxium. Per te sciamus da Patrem, / noscamus atque Filium, / te utriusque Spiritum / credamus omni tempore. Amen.