Sherehe ya Pentekoste: Ni Sikukuu ya Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume. Ni Siku ya Kuzaliwa kwa Kanisa! Ni Siku ya Waamini Walei kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa njia ya maisha yao. Sherehe ya Pentekoste: Ni Sikukuu ya Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume. Ni Siku ya Kuzaliwa kwa Kanisa! Ni Siku ya Waamini Walei kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa njia ya maisha yao. 

Sherehe ya Pentekoste: Waamini Walei: Karama! Umoja na Upendo

Sherehe ya Pentekoste inafumbata utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni siku Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume; mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa, changamoto na mwaliko kwa waamini walei kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya karama na mapaji ya Roho Mtakatifu. Ni sikukuu ya Upendo!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Neno la Mungu, katika Domenika ya Pentekoste, siku ya hamsini tangu tulipo sherehekea ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, siku ya domenika ya Pasaka. Ni sikukuu ya ujio wa Roho Mtakatifu na vitu “kuumbwa” upya. Ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa Kanisa na mwanzo wa utume wa Kanisa la mwanzo la mitume. Ni sherehe ya waamini walei wote. Sherehe hii inakamilisha fumbo la Pasaka kwa kuhitimisha kipindi cha Pasaka, tunaacha kusali sala ya Malkia wa Mbingu na kuanza kusali sala ya Malaika wa Bwana. Mwanzo na asili ya sherehe ya Pentekoste. Katika Agano la kale kwa asili sherehe hii ilikuwa ni sikukuu ya wakulima wakaanani. Ilikuwa sikukuu ya kumshukuru Mungu baada ya kuvuna mazao yao ya kwanza na papo hapo kumwomba Mungu awajalie tena mavuno mema msimu ufuatao. Ndiyo maana iliitwa sikukuu ya mavuno (Kut. 23:16), au “Sikukuu ya Mavuno ya kwanza” Hes 23:26 kwa sababu muda huo Waisraeli walimshukuru Mungu kwa mazao ya ngano waliyomaliza kuvuna au “Sikukuu ya Majuma,” kwa sababu iliadhimishwa majuma saba baada ya Pasaka (Kut 34:22).

Licha ya kuwa sherehe hii ilikuwa ni ya wenyeji wa Wakaanani katika kumshukuru Mungu kwa mavuno mapya  na Waisraeli walipotoka Misri walikuwa ni ufugaji na sio wakulima, sikukuu hii ya shukrani ni agizo la Mungu kama Kitabu cha Kumbukumbu la Torati kinatuambia: “Na itakuwa, ukiisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi, na kuimiliki, na kukaa ndani yake; twaa malimbuko ya ardhi, utakayoyavuna katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako; ukayatie katika kikapu, ukaende hata mahali pale atakapopachagua Bwana, Mungu wako, ili alikalishe jina lake huko. Ukamwendee kuhani atakayekuwapo siku zile, ukamwambie, “Ninakiri leo kwa Bwana, Mungu wako, ya kuwa nimeingia katika nchi Bwana aliyowaapia baba zetu ya kwamba atatupa.” Naye kuhani atakipokea kikapu mkononi mwako, akiweke chini mbele ya madhabahu ya Bwana, Mungu wako… (Kumb 26:1–13). Mwanzoni, Sikukuu hii haikuwa na tarehe ya kusheherekea. Baada ya uhamisho wa Babiloni, Sherehe ya Pentekoste ikaanza kuchukua maana mpya. Wayahudi wakaanza kukumbuka Agano la Sinai, jinsi Mungu alivyowapa amri kumi na kuzaliwa kwa Taifa lao.

Sherehe ya Pentekoste iliadhimishwa siku ya 50 baada ya Pasaka, kwa sababu tangu kutoka Misri (Pasaka) mpaka kufika Mlima wa Sinai zilipita siku 50 (Kut 19:1). Sherehe hii ikahusianishwa na historia ya Wokovu wao yaani Pasaka na kupokelewa kwa amri kumi za Mungu mlimani Sinai ikapewa jina la sikukuu ya majuma kwa vile ilisherehekewa majuma saba baada ya Pasaka ya Wayahudi ambayo yanafanya siku hamsini ndiyo maana ikaitwa Pentekoste neno la kigiriki likimaanisha siku ya hamsini baada ya Pasaka, (2Mak 12:31ff; Tob 2:1). Kitabu cha Mambo ya Walawi 23:15–22 kinasema; “Nanyi mtajihesabu tangu siku ya pili baada ya sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia sabato saba; hata siku ya pili ya hiyo sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsongezea Bwana sadaka ya unga mpya. Mtatoa katika makao yenu mikate miwili ya kutikiswa, itakuwa sehemu za kumi mbili za efa; itakuwa ya unga mwembamba, itaokwa na chachu, iwe malimbuko kwa Bwana...” Ndipo sasa sherehe ya Pentekoste ikapewa maana mpya ya kidini ikawa sio tena sikukuu ya wakulima kama mwanzo. Sherehe hii ya Pentekoste ikawa ni siku ya kumbukumbuka ya siku Musa alipopewa amri kumi za Mungu mlimani Sinai ambapo ni siku ya kuzaliwa Taifa jipya la Israeli na kupewa katiba au kanuni za kuliongoza, yaani Amri kumi za Mungu. Ni katika siku hii walikula mikate iliyotiwa chachu.

Namna ilivyosherekewa: Pentekoste ikiwa ni mojawapo ya sikukuu kubwa za kuhiji Yerusalemu katika mwaka, zingine zikiwa ni sikukuu ya Mikate isiyotiwa chachu (yaani Pasaka), Sikukuu ya Majuma na Sikukuu ya Vibanda (yaani Pentekoste ilikuwa ni sikukuu ya shukrani kwa Mungu na “hakuna mtu atakayejitokeza mbele ya Bwana mikono mitupu: Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi ambavyo Bwana Mungu wenu alivyowabariki” (Kum 16:16-17) ambapo, wakulima wa Kiyahudi na waongofu toka sehemu mbalimbali walimiminika mjini Yerusalemu wakiwa wamechukua makapu yaliyojaa mazao yao ya kwanza kuja kutoa shukurani kwa musimu huo na kuomba baraka kwa musimu ujao. Baada ya kufika hekaluni walijipanga katika mtindo wa maandamano. Hapo waliwakuta Walawi na makuhani ambao waliwapokea na maandamano kuelekea hekaluni, kwa vifijo, vigelegele na nderemo huku wakiimba nyimbo za kumshukuru na kumsifu Mungu. Hatimaye, Kuhani wa zamu alichukua mikate miwili na kuitolea sadaka ya shukurani kwa Mungu. Mikate hii miwili ilitokana na ngano mpya iliyo na chachu.

Kuonesha upekee na umuhimu wake, ni sikukuu hii tu ndio Waisraeli walitumia mikate iliyotiwa chachu katika maadhimisho yao. Desturi hii ya kutoa shukrani ya mazao ilienea katika nchi nyingi kuzunguka bahari ya kati, na watu kutoka nchi mbalimbali pande zote za dunia hata Afrika, wote walikuja Yerusalemu kutoa shukrani kwa Mungu kwa neema na baraka za mavuno mapya ndiyo maana siku ya pentekoste kulikuwa na watu wengi wa kila taifa. Katika hali hiyo ya sherehe na kusanyiko la watu toka mataifa mbalimbali siku ya Pentekoste ya Kiyahudi, na Yesu akiwa ameshapaa mbinguni, Mitume kwa hofu ya Wayahudi wakiwa wamejifungia katika chumba cha juu, wakidumu katika kusali, wakisubiri ahadi ya Kristo, yaani ujio wa Roho Mtakatifu, humo ndani ghafla kukaja upepo toka mbinguni, ukakijaza chumba kile walikokuwamo, zikatokea ndimi za moto zilizogawanyika zikiwakalia kila mmoja. Wote wakajawa Roho Mtakatifu, wakapata ujasiri wakatoka nje, wakaenda hekaluni ambapo walikuwapo watu wa kila lugha, kila jamaa na kila taifa waliokuja kuhiji na kumtolea Mungu shukrani za mazao yao mapya na majina yao yanatajwa katika somo la kwanza la kitabu cha matendo ya mitume 2:1-11. Mitume wakaanza kuwahubiria kwa nguvu habari za Yesu Kristo mfufuka na wote wakasikia na kuelewa kila mmoja kwa lugha yake ya kuzaliwa na wakabatizwa.

Huu ujio wa Roho Mtakatifu ndiyo Siku ya kuzaliwa kwa Kanisa ndiyo maana tunasherehekea Pentekoste ya Kikristo, yaani siku hamsini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo na sio siku hamisini baada ya Pasaka ya Wayahudi, na ni siku chache tu baada ya Bwana wetu Yesu Kristo kupaa mbinguni. Kama vile Wayahudi walivyomshukuru Mungu kwa baraka za mavuno mapya huku wakikumbuka kuzaliwa upya kwa taifa lao la Israeli na kupewa amri kumi za Mungu, sisi siku hii tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya wakristo wapya waliobatizwa kwanza siku ile ya Pentekoste kanisa lilipozaliwa, watu wapatao elfu tatu na waliobatizwa katika mkesha wa Pasaka nyakati zetu ambapo mbiu ilipigwa tukisherekea usiku ule Mtakatifu tulipokombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Tunasherehekea ujio wa Mungu Roho Mtakatifu, nafsi ya tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, asiye na mwanzo wala mwisho, yeye ndiye mfariji, mtakatifuzaji, kiongozi na mwalimu wetu. Ndiye anayewajalia watu anaowashukia vipaji mbalimbali kama; hekima, akili, shauri, nguvu, elimu, ibada na uchaji kwa Mungu na karama mbalimbali kama; unabii, uponyaji, ualimu na kunena kwa lugha, kila mmoja kadiri atakavyo yeye kusudi tuvitumie kwa kufaana.

Hivyo basi, yatupasa kutambua karama hizo zote kuwa ni zawadi kutoka kwa Mungu zinazotufikia kwa njia ya Roho Mtakatifu, kumbe, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Roho Mtakatifu kwa kuzitumia vyema kwa manufaa ya yote maana tusipozitumia vyema tutadaiwa siku ya mwisho kama anavyouambia Paulo katika somo la pili la Waraka wa kwanza kwa Wakorinto 1kor. 12:3b-7,12-13. Tutambue kuwa vipaji hivi ni zawadi kwa ajili ya kuhudumiana, kujengana na kufaidiana sisi kwa sisi tukiongozwa na karama iliyo kubwa kuliko zote yaani upendo. Tujihadhari na dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu kwa kujifanya kila tulichonacho ni chetu kwani Yesu anasema; “kwa sababu hiyo nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu” (Mt.12:31). Kwa Ubatizo wetu na Kipaimara sote tumejazwa Roho Mtakatifu yatupasa kuongea lugha moja tu, lugha ya upendo kwa wote, lugha ambayo hakuna asiyeielewa. Upendo daima huvumilia, ni mpole, hauna wivu, haujidai, haujivuni, una adabu, tena hautafuti faida yake binafsi, haufurahii maovu, bali ukweli. (1Kor. 4-6).

Tumruhusu Roho Mtakatifu aingie ndani ya mioyo yetu, ndani ya nafsi zetu, akae nasi, akae ndani ya familia zetu na jumuiya zetu atufundishe kuishi kwa upendo, achome mioyo yetu atufanye tuwe safi, aondoe tabia zote ambazo zinaendana na hila za shetani, achome uovu wetu, achome Roho ya kisasi. Awashe ndani mwetu moto wa mapendo, atupe Roho ya hekima na elimu, atufundishe kusali vizuri, Roho huyu atushushie kipaji cha ukweli na mapendo ya kweli. Aondoe vilema vyote ambavyo vinatuvuruga, ambavyo vinatuletea maafa, atutie nguvu ya kuweza kufahamu madhaifu yetu, ili sote tuungane na kuwa mwili mmoja katika Kristo na tuione sura ya Mungu katika wenzetu kwa kuwapenda kama Kristo alivyoagiza. Mwisho tukumbuke kuwa baada ya Jumapili ya Pentekoste, Mshumaa wa Pasaka unatunzwa kwa heshima karibu na kisima cha ubatizo na unawashwa wakati wa kubatiza, ili mishumaa ya wabatizwa iwashwe kutokea mshumaa huu. Katika mazishi mshumaa wa Pasaka unawekwa kando ya jeneza kuwa ishara ya kifo cha mkristo ni Pasaka halisi. Nje ya kipindi cha Pasaka Mshumaa wa Pasaka hauwekwi patakatifuni na wala hauwashwi. Kuanzia Jumatatu baada ya Jumapili ya Pentekoste, husemwa “Malaika wa Bwana alimpasha Habari Maria …”

29 May 2020, 07:30