Neno la Mungu: Jumapili VI ya Pasaka: Ujio wa Roho Mtakatifu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayatafakari Masomo ya dominika ya Sita ya kipindi cha Pasaka. Somo la kwanza (Mdo. 8:5-8, 14-17) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Kitabu hiki kinaendelea kutupatia ushuhuda wa ukuaji wa Kanisa na namna ulivyofanyika uinjilishaji wa mwanzo baada tu ya ufufuko wa Kristo. Somo la leo linafungua ukurasa mpya kwa kudokeza nafasi ya Roho Mtakatifu katika ukuaji wa Kanisa na katika uinjilishaji. Katika hatua ya kwanza, somo linaonesha kazi kubwa aliyoifanya Filipo katika mji wa Samaria. Filipo huyu alikuwa ni mmojawapo wa wale Mashemasi saba waliowekwa ili kuwasaidia mitume katika huduma. Utume ambao Shemasi Filipo aliufanya huko Samaria uliambatana na miujiza mbalimbali ambapo wagonjwa waliponywa na pepo wachafu waliondolewa. Somo linaendelea kuonesha kuwa utume alioufanya Shemasi Filipo ulikuwa ni kama maandalizi ya kumpokea Roho Mtakatifu. Tunaliona hilo kwa sababu walipofika baadaye Mitume Petro na Yohane, walikuta tayari watu wamekwisha lipokea Neno na wamekwisha batizwa ndipo wakawawekea mikono nao wakampokea Roho Mtakatifu.
Hata leo katika Kanisa, Sakramenti ya Kipaimara ambayo ndiyo Sakramenti inayomjaza mwamini ukamilifu wa Roho Mtakatifu, ni Sakramenti inayotanguliwa na mafundisho, Ubatizo na Ekaristi Takatifu. Nayo huja kama kilele cha Sakramenti zinazomuingiza mtu katika ukristo. Ni muhimu pia kuona katika somo hili uhusiano kati ya alichofanya Filipo - kuwatoa watu pepo wachafu na walichofanya Mitume - kuwajaza Roho Mtakatifu. Katika uhusiano huu tunaona kuwa kuiandaa roho ya mwamini kumpokea Roho Mtakatifu ni muhimu kwanza kuisafisha na kuondoa pepo wachafu wanaofanya maskani ndani yake. Hali kadhalika, huduma ya kuwawinga watu pepo wachafu ni muhimu ikakamilishwa kwa kumwalika Roho Mtakatifu na kuendelea kuitunza neema yake ya utakaso kwa njia ya Sakramenti.
Somo la pili (1Pet 3:15-18) ni kutoka katika waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa watu wote. Mtume Petro anaendelea kutoa mafundisho kwa wakristo wapya na kuwaandaa kwa maisha mapya wanayoyaanza baada ya kubatizwa. Katika mazingira ya wakati wa Mtume Petro, Ukristo haukuwa dini rasmi na wala haukutambuliwa na jamii kwa ujumla kuwa ni jambo halali katika kuyaishi mapenzi ya Mungu. Wakristo walionekana kama kikundi cha siri cha wanaharakati ambacho hakikuwa na nia nzuri wa watawala na kwa jamii yenyewe. Wakristo walionekana kama watu waliopumbazwa akili kwa mafundisho yao na mtindo wao wa maisha ulionekana na jamii kuwa ni mtindo usio na mantiki. Kwa jinsi hiyo, wakristo walitengwa na ilikuwa kawaida kwao kuteswa na kujikuta katika adha mbalimbali za kijamii. Mafundisho ya Petro tunayoyasikia katika somo hili, yanalenga kumbe kuwaandaa hawa wabatizwa wapya kukabiliana na hali hii. Hivyo, Mtume Petro anawaasa akiwaambia kuwa “wale wanaowashutumu kuwa mmepumbazwa akili, muwe tayari kuwajibu kuwa ndani yenu mnalo tumaini ambalo ndilo linawapa dira katika maisha”. Na hilo, Mtume Petro anawaomba walifanye kwa upole na kwa hofu, yaani kwa heshima na uungwana wa kibinadamu.
Kuhusu mateso mbalimbali wanayoteseka kwa sababu ya kuwa wakristo, Petro anawaasa kufanya mambo yote wakiongozwa na dhamiri njema. Yule anayefanya jambo kwa dhamiri njema halafu akashutumiwa na jamii au akawekwa katika wakati mgumu, kamwe asiogope wala kufadhaika, adumu katika kuishikilia dhamiri yake njema. Lakini pia Petro anatahadharisha kuwa mtu asiyeongozwa na dhamiri njema, akishutumiwa au akiwekwa katika mazingira magumu asiseme anateseka kwa sababu ya Kristo kwani “ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kuteswa kwa kutenda mabaya”. Mateso manyanyaso mbalimbali kwa kanisa na kwa wakristo hayajakoma hadi leo. Yapo yanayoendelezwa kimfumo na yapo yale yanayoendelea chini kwa chini ndani ya jamii zetu. Maneno ya Mtume Petro katika somo hili ni maneo ya kututia nguvu ya kuishi na kutenda kadiri ya dhamiri njema. Aidha, Mtume Petro anaonesha pia kuwa tangu mwanzo, Kanisa halijachukua njia ya kujibu mashambulizi kwa kutoa mashambulishi. Badala yake limeendelea kutoa majibu kwa yaani kwa heshima na uungwana wa kibinadamu likisisitiza uundaji wa dhamiri hai kama chemichemi ya ujenzi wa jamii ya watu wanaoheshimiana, wanaovumiliana na kushirikiana kuukuza ubinadamu.
Injili (Yoh 14:15-21) Katika Injili ya leo, Kristo anawaambia wanafunzi wake kuwa hatawaacha yatima bali atawaletea Msaidizi mwingine ili akae nao hata milele. Katika mpangilio wa Injili ya Yohane, Yesu anazungumza maneno haya akiwa katika karamu ya mwisho na wanafunzi wake. Ni maneno ya kuwaaga na kuwaimarisha kwa utume unaowasubiri. Msaidizi anayemzungumzia ni Roho Mtakatifu. Jina hilo Msaidizi, kutoka katika neno la Kiyunani parēkletos, humaanisha pia mtetezi na pia mfariji na maana zote hizi hutumika kumuelezea Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ambaye Yesu anawaahidia Mitume ni Msaidizi katika maana halisi ya neno kusaidia kwa maana ndiye atakayeambatana na mitume na kuwasaidia kutekeleza utume wao wote. Roho Mtakatifu ni mtetezi (advocatus), kama ambavyo wakili hutetea au huwakilisha madai ya mtu mbele ya hakimu, ndivyo na Roho Mtakatifu atakavyowatetea na kuwakilisha madai yao mbele ya Mungu. Roho Mtakatifu ni mfariji; ndiye atakayekuwa kitulizo na faraja yao katika mateso na magumu mbalimbali ya utume na ndiye atakayewapa ile faraja ya mwisho ya kupumzika katika amani ya Mungu Baba baada ya kumaliza vema maisha na utume wa kumshuhudia Kristo duniani. Huyu ndiye Roho wa kweli ambaye Yesu anasema ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu haumtambui. Anawaalika wanafunzi wake kumtambua na kumpokea kwa sababu anakaa kwao.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu katika dominika hii ya sita ya Pasaka yanadokeza nafasi ya Roho Mtakatifu katika ukuaji wa Kanisa na katika maisha ya wafuasi wa Kristo. Tunaona katika dominika hii, Liturujia inaanza kutuandaa kwa ufunuo wa Roho Mtakatifu. Mafundisho haya kuhusu Roho Mtakifu tutaendelea kuyapata na yatafikia kilele chake katika Sherehe ya Pentekoste ambapo tutaadhimisha tukio la Roho Mtakatifu kuwashukia wafuasi na Kanisa zima. Tafakari hii ya siku ya leo inatualika kumtambua Roho Mtakatifu kama zawadi itokayo kwa Baba na kwa Mwana, naye anakuja katika Kanisa ili kuthibisha yale aliyoyafundisha Kristo. Hili ni fundisho ambalo tunalikiri pia katika kanuni ya imani tunaposali “nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima atokaye kwa Baba na Mwana”. Kumbe, Roho Mtakatifu hawezi kutengwa na kuchukuliwa peke yake. Tena Yeye sio nguvu inayoweza kuwekwa katika mzani ikikinzana na nafasi ya Kristo. Yeye pamoja na Baba na Mwana ni kitu kimoja. Kumpokea Roho Mtakatifu ni kumpokea Baba na ni kumpokea pia Mwana.
Ni katika uhusiano huu, masomo ya leo yanatualika pia kuona kuwa Roho Mtakatifu ambaye Yesu anawaahidia Mitume, haji ili kutoa mafundisho mapya wala au labda kurekebisha sehemu fulani katika mafundisho ya Yesu. Mafundisho ya Yesu yalikamilika na ufunuo alioutoa ulikuwa kamili. Roho Mtakatifu anakuja kuwaimarisha Mitume na hivi kuliimarisha Kanisa katika kuyaelewa, kuyaishi na kuyashuhudia yale aliyoyafunua Kristo mwenyewe. Tafakari hii basi itusaidie na kutuelekeza kumuishi Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa na katika muunganiko na Kanisa. Huu ni muunganiko na Kanisa zima linalofundisha, yaani katika kuyapokea mafundisho yake yote; Kanisa linalotakasa, yaani kuishi ushirika katika sakramenti zake; na Kanisa linalochungwa kama kondoo wa Bwana, yaani utii kwa mamlaka na uongozi wake wa Hierakia.