Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Uwepo, Neno na Roho Mtakatifu
Na Padre William Bahitwa, Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Katika dominika hii, Kanisa linaadhimisha sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, inayoitwa pia sherehe ya Ekaristi Takatifu. Katika sherehe hii Kanisa linakiri, linatangaza na kuadhimisha uwepo halisi na hai wa Bwana wetu Yesu Kristo katika Ekaristi Takatifu. Somo la kwanza (Kum 8:2-3, 14b-16a) kutoka kitabu cha Kumbukumbu la Torati. Katika ujumla wake, kitabu hiki kinabeba hotuba na mafundisho ya Musa kwa waisraeli wanapojiandaa kuingia katika nchi ya ahadi. Katika hotuba hizi, Musa anawakumbusha waisraeli thamani ya Torati na maana yake katika maisha yao yote. Kimsingi anawaalika waisraeli kutambua kuwa katika nchi ya ahadi ambayo sasa wanajiandaa kuiingia, usalama wao upo katika kuishika Torati. Watakapoishika Torati kisawasawa, maisha yao yatakuwa mazuri la endapo wataipuuzia maisha yao yatajaa shida na taabu. Katika somo la leo, Musa anawakumbusha waisraeli namna ambavyo Mungu alihifadhi maisha yao walipokuwa jangwani kwa kuwayeshea chakula kutoka mbinguni.
Anasema Bwana “akakulisha kwa mana usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua, apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu hataishi kwa mkate tu bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana”. Mapokeo ya Kanisa yameona katika somo hili kidokezo cha Ekaristi Takatifu. Chakula ambacho Mungu aliwashushia Waisraeli jangwani kilikuwa kweli ni chakula, lakini hapo hapo kilikuwa ni kielelezo cha kile chakula halisi kwa ajili ya uzima wa roho ambacho Kristo angekuja kukitoa katika Agano Jipya. Ni uzima huu wa roho ambao haupatikani kwa kula mkate tu bali hupatikana kwa mwanadamu kuishi kwa kutegemea kila litokalo katika kile kinywa cha Mungu. Yesu alinukuu andiko hili pale alipokuwa akimjibu ibilisi (Rej. Mt. 4:4). Akafafanua kuwa linalotoka katika kinywa cha Mungu ni Neno lake. Neno la Mungu ni nani? Ni Kristo, ndiye yeye Neno aliyetwaa mwili akakaa kwetu. Ndiye Neno aliyejitoa sadaka msalabani akatuachia ukumbusho wa sadaka yake katika Ekaristi.
Somo la pili (1 Kor 10:16-17) ni kutoka katika waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorinto. Katika somo hili Paulo anawaandikia wakorintho akiwaonya juu ya kufuru walizokuwa wakizifanya wakati wa adhimisho la Ekaristi. Anawakumbusha mapokeo kuwa kikombe kile cha baraka tukibarikicho ni ushirika na damu ya Kristo. Tena mkate ule tuumegao ni ushirika na Mwili wa Kristo. Anapotaja kikombe cha baraka anarejea kikombe kile ambacho Kristo alikitwaa akakibariki wakati wa Karamu ya mwisho na wanafunzi wake. Katika utamaduni wa kiyahudi, mlo wa Pasaka ulisindikizwa na vikombe vinne vya divai. Kikombe cha kwanza kilinywewa kabla ya mlo, cha pili wakati wa mlo, cha tatu baada ya mlo na cha nne mda mfupi kabla ya kuagana. Kikombe alichokitwaa Yesu akakibariki ni kile cha tatu, baada ya kula. Hiki ndicho kikombe pekee ambacho wakristo wa mwanzo walikibakiza. Japokuwa hawakuendeleza utamaduni wa kuwa na vikombe vinne, waliendelea kukiita kikombe cha Baraka. Msingi wa mafundisho ya Paulo anaponukuu mapokeo haya ni kuonesha kuwa adhimisho la Ekaristi linaendeleza tendo lile lile alilolifanya Kristo katika karamu ya mwisho. Na kwa adhimisho hilo, Kristo mwenyewe yupo: Ni ushirika na mwili wake na ni ushirika na damu yake. Na huu ni mwaliko wa kulishiriki kwa uchaji na utakatifu unaostahili.
Injili (Yoh 6:51-58) somo la injili ni kutoka kwa mwinjili Yohane. Yesu anajitangaza kuwa ndiye chakula cha uzima kilichoshuka kutoka mbinguni. Mtu akila chakula hicho ataishi milele. Tena akaongeza kufafanua kuwa chakula anachotoa Yeye ni mwili wake kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Yesu anapojitaja kuwa ndiye chakula cha uzima, anarejea mana ambayo katika Agano la Kale Mungu aliwalisha waisraeli jangwani. Ni hapa ambapo Yesu anakamilisha tendo hilo ambalo Mungu alilifanya zamani kama ishara. Kile kilichofanyika kama ishara, sasa kinapata ukamilifu wake na kile ambacho kilifanywa kama kielelezo, sasa kinapata uhalisia. Yesu amejitoa kama chakula halisi na kubaki kwa njia ya Ekaristi Takatifu kwa ajili ya uzima wa roho wa wote wanaompokea. Ni uzima huu wa roho ambao Yesu anasisitiza kuwa hautakufa bali utaishi milele. Huu ndio uzima ambao Ekaristi inatukumbusha tuushugulikie kwa kuishi tumeungana na Kristo kisakramenti.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Ekaristi Takatifu ni adhimisho la uwepo hai wa Bwana Wetu Yesu Kristo katika mwili na damu yake chini ya maumbo ya mkate na divai. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha kuwa Ekaristi ndiyo jumla na muhtasari wa imani yetu nzima (KKK 1327). Imani yetu na fumbo zima la wokovu wa mwanadamu vimelala juu ya Ekaristi Takatifu. Ndiyo ishara thabiti ya ushirika katika uzima wa kimungu na adhimisho lake ni ishara ya muunganiko na liturujia ya mbinguni. Ekaristi ndio chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo. Kumbukumbu rasmi ya kuwekwa kwa Ekaristi ni siku ya Alhamisi Kuu. Lakini kama tunavyofahamu ilivyo nidhamu ya maadhimisho ya Juma Kuu hasa zile siku tatu kuu za Pasaka, hatuwezi kuadhimisha siku hiyo kwa shangwe kuu pamoja na maandamano ya kutangaza ukuu wa fumbo hili ambalo Kristo ameliachia Kanisa. Ndiyo maana ikatengwa siku nyingine baada ya sherehe za Pasaka kwa ajili ya adhimisho hili kubwa la Ekaristi pamoja na maandamano ya hadharani ili kukiri wazi na kutangaza ufahari wa imani yetu hii kubwa kuwa katika Ekaristi Takatifu yume kweli na mzima Bwana wetu Yesu Kristo.
Mtakatifu Toma wa Akwino anafundisha kuwa sherehe hii ya Ekaristi Takatifu inatukumbusha yaliyotendeka hapo mwanzo, inatusaidia kuishi vema maisha yetu ya sasa na inatuandaa kwa yale yajayo. Kwa kurejea yaliyokwisha tukia mwanzo, Ekaristi inatukumbusha sadaka ile isiyo na doa aliyoitoa Kristo kwa ajili ya wokovu wetu. Katika maisha yetu ya sasa, Ekaristi inatualika kuishi tumeungana na Kristo na katika maisha yajayo Ekaristi inatufanya tuushi umungu tukingali bado hapa duniani. Tuimbe kwa furaha, tuisifu Ekaristi alimo Yesu Kristo, alimo mzima. Amina.