Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Somo la Injili ya Dominika ya leo tunasoma sehemu ya mwisho ya mazungumzo marefu ya Yesu juu ya Mkate wa uzima, ambayo Yesu aliyatoa akiwa katika Sinagogi la Kapernaumu baada ya kutenda ishara ile ya kulisha watu wengi kwa mikate mitano na samaki wawili. Ni mazungumzo yanayobeba katekesi yenye Taalimungu makini kumhusu Yesu mwenyewe kama Mkate ulioshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Ishara au muujiza ule ukaamsha mshangao mkubwa kati ya makutano na hata wakataka kumkamata Yesu kwa nguvu na kumfanya kuwa mfalme wao (Yohane 6:14-15). Makutano wametambua na kuona nguvu za Mungu zikifanya kazi ndani ya Yesu na hivyo kumwamini. Ila mara moja tunaweza kusema bado walikuwa na imani changa, isiyokomaa bado. Kwao Yesu ni mtenda miujiza, ni mmoja anayeweza kutimiza mahitaji yao ya msingi kama chakula na labda kuwaponya na magonjwa na maradhi mbali mbali. Ni kishawishi kwa wengi wanaokosa imani iliyokomaa kumkimbilia Yesu kwa ajili ya mahitaji na shida za kimwili. Si kosa kumkimbilia Yesu wakati wa shida na dhiki ila mahusiano yetu na Yesu hayapaswi kujengwa katika hayo bali katika upendo wa dhati, usio na masharti kwake. Yesu sio mtenda miujiza kwa nafasi ya kwanza bali ni Bwana na Mwokozi wetu.
Imani iliyokomaa kinyume chake ni tofauti na hiyo ya kusaka miujiza na kutimiziwa mahitaji au shida zetu mbali mbali. Kwa mwenye imani thabiti ya kweli ishara ya miujiza sio lengo la kwanza bali katika ishara na miujiza tunaalikwa kupata ujumbe ulio mkubwa zaidi. Hivyo hatupaswi kuishia katika kustaajabia na kuvutwa na miujiza au ishara kama anayoiita mwinjili Yohana. Katika muujiza wa uponyaji wa yule mtu aliyezaliwa kipofu tunaalikwa kumuona Yesu kama taa na mwanga wa maisha yetu; Ishara ya pale Kana ambapo Yesu anageuza maji kuwa divai hapo tunaalikwa kuona zawadi ya Roho ambaye ndiye chemuchemu ya furaha, divai ni ishara ya upendo na furaha; Yesu anapomfufua Lazaro tunaalikwa kumtambua Yesu kama Bwana wa uzima; Katika muujiza wa kulisha watu mikate na samaki hapo tunaalikwa kumtambua Yesu kama chakula chetu cha kweli na cha uzima wa milele sio wa mwili tu. Ishara au miujiza zina lengo na nia ya kuufunua ukuu na uweza wa Mungu na sio kwa ajili ya kututimizia mahitaji yetu kwa nafasi ya kwanza.
Pale Kapernaumu makutano walibaki kuwa na imani changa iliyokosa ukomavu kwa kumuona Yesu kama mtenda miujiza na mambo ya kustaajabisha machoni pao. Yesu anatumia fursa hii kuwafundisha ili imani yao ipate kukomaa na kuwa imani ya kweli. Na ndio Katekesi tunayopata siku ya leo tunapotafakari somo la Injili. Yesu anajitambulisha kuwa Yeye ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni (Yohane 6:33-35). Maneno haya yanakuwa ni kikwazo kwa wasikilizaji wake na hasa wayahudi. Kwa wayahudi mkate kutoka mbinguni ni mana waliyokula babu zao wakiwa safarini jangwani kuelekea nchi ile ya ahadi (Zaburi 78:24) na chakula ni Neno la Mungu (Isaya 55:1-3). Kwao inakuwa ngumu na hata kujiuliza inawezekanaje mwana wa mseremala akajitambulisha kama chakula cha uzima kilichoshuka kutoka mbinguni, na kuwaalika kula mwili wake na kunywa damu yake? Ni swali lenye kuleta sio tu sintofahamu bali makwazo kwao.
Mkate nitakaowapatia ni mwili wangu, ni maneno ya Yesu yanayowaacha si tu kinywa wazi bali wakiwa na mshangao na hata kukosa kuelewa maana yake. Katika Maandiko Matakatifu mwili unalinganishwa na mtu (Mwanzo 6:3). Neno mwili halimaanishi tu nyama bali inakuwa lina maana kubwa zaidi ndio kusema unyonge na udhaifu wetu wa kibinadamu, hali ya kuteseka na kuugua na hata kufa. Mwili unamtambulisha mwanadamu lakini hasa udhaifu wake (Zaburi 78:39). Katika Mwinjiili Yohane 1:14 tunasoma: Neno alifanyika mwili, ndio kuonesha jinsi Mwana wa Mungu alivyokubali kujishusha na kutwaa hali yetu duni na nyonge, kuwa na mwili ule unaoweza kuteseka na hata kufa. Umwilisho kumbe ni kutwaa hali duni ili sisi tulio duni tuweze kupata rehema na neema, kushiriki maisha ya kimungu. Na kutokana na ukweli huo wa umwilisho wa Mwana wa Mungu, leo Yesu anatualika kula mwili wake ili tupate uzima wa milele. Kula ndio kukubali kumpokea Yesu afanyike mwili katika mwili wako na wangu, awe pamoja nawe, nami katika yote, ndio kukubali kubadili maisha yetu ili yafanane na yake. Huyu aliyekubali kumwilika kwa kutwaa mwili wetu ulio duni na dhaifu anatualika nasi kuula mwili wake na kuinywa damu yake ili tupata uzima wa milele. Mwili na Damu ya Kristo sio kwa ajili ya uhai au maisha ya kibaiolojia bali kwa uzima wa roho zetu, kwa uzima wa milele.
Makutano bado waliona shida na kujawa na mashaka kuwa itawezekanaje mtu huyu kuwapa mwili wake? Ndio kusema walimwelewa Yesu kuwa si tu alimaanisha kufananisha maisha yao na yake bali pia wale mwili wake. Kitenzi kula kinasikika leo mara 11 na mara nne kwa kweli Yesu anawaalika kula sio kwa namna ile ya kawaida ya kula bali kumla kama vile simba mwenye njaa anavyokula mzoga wa nyama. Kula huko kwa kusukumwa na njaa na kiu isiyokuwa ya kawaida, na ndio kila mkristo anapaswa kuwa na njaa na kiu ya kula Mwili na kunywa Damu yake Bwana wetu Yesu Kristo. Hatuna budi kuwa na njaa kubwa kabisa katika maisha yetu sio ya kitu kingine chochote bali ya Mwili na Damu yake Kristo. Yesu haishii tu kuwaalika kuula mwili wake kama mkate ulioshuka kutoka mbinguni bali pia kunywa damu yake kama kinywaji cha uzima wa milele. Katika Agano la Kale kitabu cha Mambo ya Walawi 17:10-11, tunaona jinsi Mungu anavyokataza kunywa damu kwani ni katika damu kuna uhai na maisha. Uhai sio mali yetu bali ni ya Mungu. Hivyo ni kwa kunywa damu yake nasi tunajaliwa uhai na uzima wa Kimungu ndani mwetu. Ndio kusema tunashiriki maisha ya Kimungu kwa kushiriki fumbo hilo takatifu la kula Mwili wake na kunywa Damu yake.
Ni katika Sakramenti hii ya Ekaristi Takatifu Kanisa linapata chemchemi na kilele cha maisha yake. Leo Yesu anarudiarudia kutualika kula na kunywa, naomba nasi tutilie mkazo maneno haya ya Yesu. Ni wazi Mama Kanisa leo anatupa nafasi ya kuweza kukaa na Yesu wa Ekaristi aidha anapokuwa katika tabernakulo au wakati wa uonesho na ibada za kuabudu. Yafaa ikumbukwe na hata tukumbuke Yesu wa Ekaristi kwa nafasi ya kwanza kabisa anatualika kula Mwili wake na kunywa Damu yake na kamwe tusiiishie kutosheka na kumwabudu akiwa katika Tabernakulo au pale altareni wakati wa Ibada zetu za kuabudu. Neno la Mungu tunalolisikia kabla ya kujongea Meza ile ya Ekaristi linatuandaa kabla kukubali aingie ndani mwako na kwangu. Mwili na Damu yake tunapopokea ni kukubali kufananisha maisha yetu na yake, kulishika Neno lake katika maisha yetu ya siku kwa siku. Kumpokea Yesu wa Ekaristi ndio kusema tunataka mawazo yetu yalandane na yake, maisha yetu katika kila hali yafanane na ya Yesu aliye kweli chakula chetu cha uzima.
Adhmisho la Ekaristi Takatifu ni adhimisho la Agano kati ya mwanadamu na Mungu, na ndio maana daima kabla ya kujongea meza ya Mwili na Damu yake Azizi daima tunatangulia kwa kulisikiliza Neno lake. Kumpokea Yesu wa Ekaristi ndio kusema kukubali kuingia naye mahusiano ya ndani kabisa, na ndio maana kila anayekula Mwili wake na kunywa Damu yake, Yesu anakuja na kufanya makao yake ndani mwake. Kristo ni kwa Njia ya Meza ya Neno na Meza ya Ekaristia anaingia kwa namna ya pekee kabisa katika maisha ya kila mwumini. Hatuna budi kuwa na kiu ya Neno la Mungu na pia Meza ya Ekaristi Takatifu. Neno la Mungu si tu kwa kulisoma na kulisikia bali kulishika na kuliweka katika maisha yetu ya siku kwa siku, Mwili na Damu yake Azizi inatupa nguvu ya kuweza kulishika Neno la Mungu katika maisha yetu. Ekaristi sio chakula cha kimwili bali cha kiroho na hivyo kutujalia uzima wa milele. Nawatakia tafakari na Dominika njema!