Tafuta

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu ni kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu! Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu ni kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu! 

Utatu Mtakatifu: Huruma ya Mungu na Wokovu wa Mwanadamu

Katika mpango wa ukombozi kila Nafsi ya Mungu inatekeleza kazi yake ya pamoja kufuatana na hali yake kama nafsi. Ndiyo maana tunamtaja Baba kama muumbaji, Mwana kama mkombozi na Roho Mtakatifu kama mfariji anayetakatifuza. Yote hii ni kazi ya pamoja ya Nafsi tatu za Mungu mmoja kwa sababu hizi ni nafsi zenye asili moja na kwa sababu hiyo zina utendaji mmoja ulio sawa.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Katika dominika hii, Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu, sherehe ambayo kwa njia yake Kanisa linamkiri na kumtukuza Mungu mmoja aliyejifunua katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Somo la kwanza (Kut. 34:4b-6, 8-9) kutoka kitabu cha Kutoka. Linaelezea tukio ambalo Mungu alimwita Musa katika mlima Sinai ili ampe kwa mara ya pili amri kumi zilizokuwa kielelezo cha agano kati yake na waisraeli. Tutakumbuka kuwa mbao za kwanza za amri kumi ambazo Mungu alimpa Musa, Musa mwenyewe alizivunja kwa hasira mbele ya waisraeli pale aliposhuka kutoka mlimani Sinai akakuta wametengeneza ndama ya dhahabu wakiiabudu kama mungu wao. Lilikuwa ni tukio baya linaloonesha uasi wa hali ya juu kabisa wa waisraeli kwa Mungu wao. Ni baada ya uasi huu, Mungu anamwita tena Musa ili ampe kwa mara ya pili mbao za Torati, yaani mbao za amri kumi zikionesha nia ya Mungu kuendelea kufunga agano na watu wake.

Maneno tunayosikia katika somo hili ni maneno anayotamka Mungu mwenyewe kabla ya kuzitoa tena mbao za Torati. Ni maneno ambayo kwayo Mungu anajitambulisha Yeye ni nani, ili waisraeli wanapoingia agano nao wajue huyu waliyeingia naye agano ni nani hasa. Na anapojitambulisha anasema “mimi ni Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli”. Kabla ya hapa, Mungu alikwisha jifunua mara nyingi kwa waisraeli kwa njia ya matendo makuu aliyowafanyia hasa lile la kuwatoa utumwani Misri. Pamoja na hayo, ni katika ufunuo huu wa leo Waisraeli walipata kwa mara ya kwanza ufunuo wa asili ya Mungu. Ni hapa Mungu alipofunua katika asili (nature) yake na si katika utendaji wake wala yale anayoyafanya kwa watu wake. Asili aliyoifunua ndiyo hiyo: huruma, fadhili, rehema na kweli. Sifa hizi kwa kiebrania zinabebwa na neno moja tu hesed ambalo teolojia imetafsiri katika neno huruma. Kumbe katika adhimisho la Utatu Mtakatifu, somo hili linaleta ufunuo wa Mungu katika asili yake. Asili ya Mungu ni huruma na ni asili hii inayomtambulisha katika utendaji wake wote na katika mahusiano yake na mwanadamu na ulimwengu aliouumba.

Somo la pili (2 Kor 13:11-13) ni kutoka katika waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorinto. Tunachokisoma katika somo hili ni maneno ambayo Paulo anayatumia kuhitimisha mausia na mafundisho mbalimbali aliyokuwa amewaandikia. Anasema “Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na pendo la Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote”. Ni maneno haya haya ambayo liturujia ya Misa inayatumia kama fomula au kanuni ambayo Padre anayatumia kuwasalimu na kuwakaribisha waamini katika adhimisho takatifu. Ni maneno yanayozitaja kwa pamoja nafsi zote za Utatu Mtakatifu mintarafu matunda ya wokovu wa mwanadamu: Neema, Upendo na Ushirika. Kwa upande mmoja, maneno haya yanaonesha imani ambayo tayari Kanisa la mwanzo lilikuwa nayo kuhusu Utatu Mtakatifu. Wachambuzi wa Maandiko Matakatifu wanaonesha kuwa maneno haya hayakuwa ya Paulo mwenyewe. Yalikuwa ni maneno ambayo tayari jumuiya ya wakristo wa mwanzo waliyatumia katika kusalimiana na kutakiana baraka. Kumbe adhimisho la Utatu Mtakatifu lililokuja kuwekwa na Kanisa miaka mingi sana baadaye lina msingi pia katika imani ya Kanisa la mwanzo. Kwa upande mwingine, fomula hii ya Utatu Mtakatifu ni mwaliko wa kuyasimika maisha katika ufunuo wa Utatu Mtakatifu ambamo ndani yake yanaanza, yanakombolewa na yanakuzwa hadi kuufikia uzima wa milele.

Injili (Yoh 3:16-18) somo la Injili ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Yohane. Ni somo linaloufunua upendo mkubwa alionao Mungu kwa wanadamu. Kipimo cha upendo huo ni tendo la Mungu kumtoa mwanae wa pekee ulimwenguni ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele. Kuna uhusiano wa pekee ambao liturujia ya leo inataka kutuonesha kati ya somo la kwanza na somo hili la Injili. Katika somo la kwanza Mungu aliufunua upendo wake alipojitambulisha kuwa ni Mungu wa huruma, fadhili,wema na kweli. Ni upendo huo huo wa Mungu ambao sasa katika Injili unaelezwa kuwa maelekeo yake makuu ni wokovu wa mwanadamu. Upendo ni sifa na asili ya Mungu. Lakini sifa hii siyo kwa ajili ya yenyewe, yaani kama sifa iliyopo kwa ajili tu ya kumtambulisha yule aliyenaye. La, ni sifa ya Mungu ambayo inajionesha katika ukombozi. Ndiyo maana Mungu kwa kusukumwa na upendo huo aliamua Yeye mwenyewe kuchukua jukumu na nafasi ya kwanza katika kumkomboa mwanadamu pale alipoamua kumtuma duniani Mwanaye wa pekee.

Maneno hayo tunayoyasikia ni sehemu ya mazungumzo ya Yesu na Nikodemo. Nikodemo huyu alikuwa ni mkuu wa Wayahudi na tena alikuwa ni mmoja wa Mafarisayo. Ndiye aliyemfata Yesu usiku ili amsikilize kwa kuwa alikuwa na kiu na mafundisho yake. Alimfuata Yesu usiku kwa sababu aliogopa kuonwa na wenzake ambao walikuwa kinyume na mafundisho ya Yesu. Katika Injili ya Yohane, Nikodemo anawakilisha wote walio na kiu ya kumtafuta Yesu lakini kwa kutokana na mazingira fulani fulani ya maisha yao au kwa kulingana na hali walizonazo hawaoni kama wanastahili kuupokea upendo unaookoa wa Mungu. Ni kwa watu kama hawa mwinjili Yohane anawaandikia kuwa “Mungu hakumtuma ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu bali ili ulimwengu uokolewe katika Yeye. Amwaminiye Yeye hahukumiwi bali asiyeamini amekwisha hukumiwa”.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, sherehe tunayoadhimisha leo ni sherehe inayogusa fundisho kuu juu ya Mungu mwenyewe. Ni fundisho la imani na hapohapo ni Fumbo, kwamba Mungu wa kweli na wa pekee ni mmoja katika nafsi tatu ambazo ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Tunaamini juu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa sababu Mungu mwenyewe amelifunua. Amelifunua  hatua kwa hatua katika historia ya wokovu; katika fumbo la uumbaji, katika fumbo la ukombozi wa mwanadamu na katika fumbo la kumtuma Roho Mtakatifu. Katika mpango huu wa ukombozi kila Nafsi ya Mungu inatekeleza kazi yake ya pamoja kufuatana na hali yake kama nafsi. Ndiyo maana tunamtaja Baba kama muumbaji, Mwana kama mkombozi na Roho Mtakatifu kama mfariji anayetakatifuza. Hata hivyo hii yote ni kazi ya pamoja ya Nafsi tatu za Mungu mmoja kwa sababu hizi ni nafsi zenye asili moja na kwa sababu hiyo zina utendaji mmoja ulio sawa. Na maisha yote ya kikristo ni ushirika wa kila nafsi ya Mungu bila kuzitenganisha kwa namna yoyote. Anayemtukuza Baba hufanya hivyo kwa njia ya Mwana katika Roho Mtakatifu; anayemfuata Kristo anafanya hivyo kwa sababu Baba anamvuta na kwa sababu Roho Mtakatifu anamwongoza.

Kristo mwenyewe katika mafundisho yake ameuzungumzia Utatu Mtakatifu kama makao, makao ambayo Yeye yumo ndani ya Baba na Baba yumo ndani yake katika ushirika wa Roho Mtakatifu. Haya ni makao ambayo ni kilele cha wafuasi wake na kila anayemwamini anaalikwa kuyaingia na kuyashiriki. Naye anasema “mtu akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake na kufanya makao kwake” (Yoh 17:21-23). Nasi tunapata matumaini ya kuyaingia kwa njia ya Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, ndani ya upendo wa Mungu Baba na katika ushirika wa Roho Mtakatifu. Makao haya ya Mungu katika utatu Mtakatifu, yanaakisi pia makao yetu hapa duniani katika familia, jumuiya na taasisi zetu. Neema, upendo na ushirika ndani ya Utatu Mtakatifu na kwa njia ya Utatu Mtakatifu ni mwaliko wa kwetu kuziishi tunu hizi katika familia zetu, jumuiya zetu na katika taasisi zetu. Maadhimisho ya leo yawe kichocheo kwetu cha kujenga familia na jumuiya zinazojitahidi kutunza neema zilizopata kwa njia Kristo, familia na jumuiya zinazoiga siku kwa siku upendo wa Baba na kwa mfano wa upendo huo kupendana wao kwa wao: familia na jumuiya zinazoishi kwa kushirikiana na kusaidiana hasa katika nyakati ngumu ambapo mmoja wa wanafamilia au wanafamilia wote wanapokuwa wanapita katika kipindi kigumu cha maisha. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu uwe nasi katika familia na jumuiya zetu zote. Amina.

Liturujia: Utatu Mtakatifu
06 June 2020, 09:48