Tafuta

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Chemchemi ya haki, amani, upendo, huruma na mshikamano wa kweli. Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Chemchemi ya haki, amani, upendo, huruma na mshikamano wa kweli. 

Moyo Mtakatifu wa Yesu: Kisima cha: Faraja, Amani na Upendo!

Leo ni siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre. Mapadre waendelee kukesha kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Upatanisho kama nyenzo za kujitakatifuza na kujipatia wongofu; kujipatia utakatifu. Ni mwaliko wa kujichotea fadhila za Moyo wa Yesu ili tuweze kuishi maisha mapya: Maisha ya kujitoa, maisha ya kujisadaka.

Na Padre Liston Lukoo, Dar es Salaam.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican "Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake"(1Yoh 4:16). Mama Kanisa leo anaadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ni sherehe ya upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Upendo huu umedhihirika pale Mungu alipomtuma mwanaye kwetu. Na Bwana Yesu amedhihirisha upendo huu kwa kumwaga damu yake Msalabani pale "askari mmojawapo alipomchoma ubavu kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji"(Yoh 19:34). Alama ya upendo huu wa Yesu kwetu ni moyo wake mtakatifu. Moyo mtakatifu wa Yesu ni kitulizo chetu. Yeye mwenyewe anasema "Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha"(Mt 11:25). Mwanadamu ana mizigo mingi na mizito. Wapo ambao ndoa zao zimekuwa mizigo isiyobebeka tena. Tupo ambao maisha ya upadre na utawa yamekuwa mizigo inayotuelemea. Wapo ambao ajira zao zimekuwa mizigo isiyovumilika.

Wapo ambao maisha kwao ni usumbufu na yamekuwa mzigo. Katika hali hiyo tunahitaji kitulizo na faraja. Je!  Tunaipata wapi?  Zipo sehemu na namna mbalimbali za kupata kitulizo na faraja. Lakini zote hizo ni za muda mfupi na si za kweli. Faraja ya kweli na ya kudumu inapatikana katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ndani ya moyo wa Yesu kuna amani. "Nawaachieni amani, nawapeni amani yangu"(Yoh 14:27). Moyo wa Yesu ni shule ya upole na unyenyekevu. "Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo"(Mt 11:29). Moyo Mtakatifu wa Yesu ni shule ya msamaha na huruma ya Mungu. Alipokuwa msalabani Yesu alionyesha moyo wa huruma na msamaha aliposema "Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya"(Lk 23:34). Leo pia ni siku ya kuwatakatifuza Mapadre.

Akieleza juu ya siku hii, Baba Mtakatifu Francisko akirejea mafundisho ya Mtangulizi wake Mtakatifu Papa Yohane Paul II, anahimiza kwamba leo ni siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Mapadre kuendelea kukesha kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Upatanisho kama nyenzo za kujitakatifuza na kujipatia wongofu; kujipatia utakatifu. Sherehe hii ya Moyo Mtakatifu wa Yesu inatualika sisi sote kujichotea fadhila za Moyo wa Yesu ili tuweze kuziishi kwa mfano wa Yeye mwenyewe. Sherehe hii inatualika kuishi maisha mapya: Maisha ya kujitoa, maisha ya kujisadaka. Tunaalikwa kuifungua mioyo yetu ili kuruhusu fadhila za Moyo Mtakatifu wa Yesu kupenya ndani yetu; lakini wakati huohuo kuruhusu fadhila hizo zitoke ndani yetu na ziwafikie wengine. Hayo yote yatawezekana iwapo tu tutasukumwa na upendo kwa kiasi kilekile alichotupenda Kristu aliyesema "Pendaneni, pendaneni kama nilivyowapenda ninyi" (Yoh 13:34). Moyo Mtakatifu wa Yesu ufalme wako ufike. Ninawatakia nyote sikukuu njema. Mungu atubariki sote.

19 June 2020, 13:39