Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XII ya Mwaka A wa Kanisa: Msiogope kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XII ya Mwaka A wa Kanisa: Msiogope kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu! 

Tafakari Jumapili 12 ya Mwaka A: Msiogope Kutangaza Neno la Mungu

Utume ambao Mungu anatuita tuutekeleze ndani ya Kanisa na kwa njia ya Kanisa unao ugumu wake. Kanisa nalo kwa kuangalia historia yake nzima, linakiri kuwa magumu na mateso havikosekani kamwe. Na magumu haya hayabagui kati ya wakleri au walei, kati ya viongozi wa juu au wa chini au hata kati ya wale waliopiga hatua zaidi katika maisha ya kiroho na wale walio bado nyuma.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 12 ya mwaka A wa Kanisa. Katika ujumla wake, masomo haya yanatuzungumzia leo juu ya mateso ya watumishi wa Bwana. Yanatuonesha kuwa kazi na utume wa watumishi wa Bwana imeambatana na mateso pamoja na magumu mengi tangu mwanzo, sasa na hata katika wakati ujao. Kwa namna hii yanalenga kuwakumbusha uhalisia huu katika utume na kuwatia moyo katika kuukabili. Somo la kwanza (Yer 20:10-13) ni kutoka Kitabu cha Nabii Yeremia. Yeremia ni nabii aliyeteseka sana katika kutekeleza utume wake wa unabii. Tunaweza kabisa kusema huenda ndiye nabii aliyeteseka kuliko manabii wote wa Agano la Kale. Aliitwa katika kipindi ambacho utawala wa Yuda, yaani ufalme wa Israeli ya kusini, unakaribia kuanguka chini ya utawala wa Babeli. Ni maanguko haya ambayo baadae yalipelekea Israeli kupelekwa utumwani Babeli. Wito wake kumbe ulikuwa ni kuamsha dhamiri za watawala na za waisraeli wote kwa ujumla juu ya hatari iliyokuwa inawakabili. Kwa jinsi ambavyo uasi wa Israeli kwa Torati ulivyokuwa mkubwa, Yeremia alitabiri kuwa Yuda itaanguka na wanawe kuchukuliwa mateka.

Utabiri huu haukuwafurahisha watu na hasa ikizingatiwa kuwa katika kipindi hicho hicho, ambacho Yeremia alikuwa akitoa unabii, walikuwapo pia manabii wa uwongo ambao kazi yao ilikuwa ni kuwapa watu matumaini hewa kuwa hakuna hatari yoyote itakayokuja. Kwa sababu hii Yeremia alitupiliwa mbali, akawekwa katika mateso makali hata ikabidi kujificha ili kuokoa maisha yake. Somo letu la leo linaleta mawazo aliyokuwa nayo Yeremia katika kipindi hiki kigumu cha utume wake. Anasema hofu zimemzunguka pande zote, rafiki zake wote wamemkimbia na watu wanamvizia wamshitaki na kujilipizia kwake kisasi. Ni kama anataka kukata tamaa. Lakini hapo hapo anatambua kuwa unabii alionao sio wito wake yeye kama Yeremia bali ni wito alioitiwa na Mungu. Naye Mungu aliyemwita hajamwacha, bado yuko naye. Hilo linakuwa ni jambo linalompa nguvu Yeremia kwani anaamini kuwa pamoja na magumu anayopitia bado ana kila sababu ya kumtumaini yule aliyemwitia kazi ya unabii na ni kwa nguvu zake ataiponya roho yake na kuifikisha mwisho kazi aliyomuitia. Ni somo linalomwalika kila mtumishi wa Bwana kuiweka hatima ya utumishi wake mikononi mwa Bwana.

Somo la pili (Rum 5:12-15) ni kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Warumi. Ni sehemu ya kifungu cha Waraka ambapo Mtume Paulo anamlinganisha katika upande mmoja Adamu na katika upande mwingine Kristo. Na hapo hapo analinganisha katika upande wa Adamu dhambi na katika upande wa Kristo, neema. Hivyo anasema kwa mtu mmoja, Adamu dhambi iliingia ulimwenguni na kwa mtu mmoja, Kristo neema imepatikana. Mwanzoni mwa waraka huu, Paulo alikwisha tamka kuwa ulimwengu wote upo katika hali ya dhambi na hakuna anayeweza kujihesabia haki iwe ni myahudi au mtu wa mataifa. Paulo alitoa fundisho hilo kama sehemu ya kuwaalika wote kuupokea ukombozi unaopatikana kwa njia ya Kristo. Katika somo la leo, anapolinganisha hali hizo mbili yaani Adamu na Kristo  na pia dhambi na neema, anasema “lakini karama ile haikuwa kama lile kosa”.

Maana yake ni kwamba hatuwezi tukaweka katika uwiano sawa matokeo ya dhambi ya Adamu na matokeo ya karama ipatikanyo kwa neema ya Kristo. Matokeo ya neema ya Kristo inayoenea ulimwenguni ni makubwa na yanazidi matokeo ya kuenea kwa dhambi ya Adamu ulimwenguni. Somo hili la leo linatoa mwono chanya juu ya ulimwengu. Linaonesha uwepo wa dhambi na matokeo yake yanayoendelea kuujaza ulimwengu na kila aina ya uovu lakini hapo hapo linaonesha kuwa ipo pia ulimwenguni karama ipatikanayo kwa neema ya Kristo. Na karama hii ni kubwa mno kushinda nguvu ya uovu iliyopo ulimwenguni. Ni mwaliko basi kwa wote wanaomwamini Kristo kutokukubali kulemewa na nguvu ya uovu bali kujishikamanisha na Kristo ili kwa neema yake kusambaza karama njema ulimwenguni.

Injili (Mt 10:26-33) katika Injili ya dominika hii, inajitokeza waziwazi dhamira ya mateso ya watumishi wa Bwana. Yesu mwenyewe anawaambia Mitume: “msiwaogope wauao mwili wasiweze kuiua na roho. Afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanamu”. Maneno haya Yesu anawatamkia mitume alipokuwa akiwaandaa katika utume uliokuwa ukiwasubiri. Na tayari tunaona kuwa tangu mwanzo Yesu anaonesha kuwa katika utume huo watakabiliana na mateso yatakayohatarisha hata maisha yao. Hapo anawaimarisha wasiogope. Katika hali yoyote ile wasikubali kuuweka hatarini utume wao kwa sababu ya kujinusuru wao kwani aliyewapa utume ana nguvu za kuangamiza mwili hapa duniani pamoja na roho huko jehanam. Kama lilivyo somo la kwanza, injili hii pia inalenga kuwatia moyo na kuwaimarisha watumishi wa Bwana katika kuzikabili changamoto zinazoambatana na utumishi wao.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Dominika ya leo inatualika tutafakari kuhusu mateso yanayoambatana na utumishi ambao Mungu anamwitia kila mmoja wetu katika Kanisa. Mwanzoni kabisa mwa tafakari hii tunayakumbuka maneno ya Yoshua bin Sira “mwanangu ukija kumtumikia Bwana, weka tayari roho yako kwa kujaribiwa” (Sir 2:1). Utume ambao Mungu anatuita tuutekeleze ndani ya Kanisa na kwa njia ya Kanisa unao ugumu wake. Kanisa nalo kwa kuangalia historia yake nzima, linakiri kuwa magumu na mateso havikosekani kamwe (Rej. Lumen Gentium n 42). Na magumu haya hayabagui kati ya wakleri au walei, kati ya viongozi wa juu au wa chini au hata kati ya wale waliopiga hatua zaidi katika maisha ya kiroho na wale walio bado nyuma. Tafakari ya masomo ya dominika hii inatuonesha kuwa ni Mungu mwenyewe alikusudia hivyo, kuwa utume unaofanyika kwa jina lake utwae sura hiyo. Kwa mfano wa nabii Yeremia tunaona mateso ya watumishi wa Agano la Kale. Mateso hayo yalifikia kilele kwa Kristo mwenyewe pale alipochagua kuukomboa ulimwengu kwa njia ya mateso na kifo Msalabani. Tena ni Kristo huyo huyo ambaye aliyetahadharisha mitume wake akiwaambia “ikiwa wameutendea hivi mti mbichi, itakuwaje kwa mti mkavu? (Lk 23:31).

Tunapoyatafakari haya, hatulengi kurudi nyuma na kuogopa. Hatulengi pia kutafuta kila liwezalo kubadili taswira hii ya utume kwa kuepuka kwa gharama yoyote adha na magumu yanayoambatana na utume wenyewe hata kuufanya kuwa kama “kazi” au huduma nyingine yoyote ya kijamii. Tafakari hii ina lengo la kututia nguvu ya kuendelea kuutekeleza utume na kuushuhudia hata katika magumu yake tukiitumainia nguvu yake aliyetuita na kutupatia utume huo. Ni tafakari inayotualika kuzidi kuomba fadhila ya nguvu kutoka kwake aliyesema “msiogope”. Hii ndiyo fadhila inayotuwezesha kushinda hofu, hata hofu ya kifo, na kukabiliana na majaribu na madhulumu mbalimbali (Rej. KKK 1808). Tunafanya hivyo tukiamini katika nguvu ya ushuhuda wa imani kwa ajili ya wokovu wetu na wa wale ambao kwa ajili yao tumeupokea utume.

Liturujia J12 ya Mwaka A wa Kanisa

 

20 June 2020, 07:51