Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 18 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 18 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. 

Tafakari Jumapili 18 ya Mwaka A: Huruma na Upendo wa Mungu!

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa. Wazo kuu ni: Huruma ya Mungu ambayo imefumbatwa katika upendo wake kwa maisha ya mwanadamu kiasi cha kumtoa mwanae wa pekee ili kila amwaminiye na kumfuata apate uzima wa milele. Kristo amejitoa kama chakula chetu cha kiroho katika safari yetu kuelekea mbinguni.. Ni chakula kwa wote wanaomwamini.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 18 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Dhamira kuu ya masomo ya domenika hii ni huruma ya Mungu katika kuwalisha watu wake imefumbatwa katika upendo wake kwa maisha ya mwanadamu kiasi cha kumtoa mwanae wa pekee ili kila amwaminiye na kumfuata apate uzima wa milele. Kristo amejitoa kwetu bila kujibakiza kama chakula chetu cha kiroho katika safari yetu kuelekea mbinguni. Chakula hiki ni cha wote wale wanaomwamini na kumsaidiki. Mwanadamu anahitaji chakula na kinywaji ili aweze kuishi. Mahangaiko yote ya hapa duniani ni kutafuta chakula kuzima njaa yake na kinywaji kukata kiu yake. Mapambano yote ni kushibisha tumbo ili apate furha ambayo kimsingi hawezi kuipata kwani utimilifu wa furaha ya mwanadamu ni kuuna uso wa Mungu kwani furaha ya kweli haipo katika mwili bali katika roho kwani roho ndiyo itiayo uzima mwili haufai kitu.

Kumbe, ili kupata furha ya kweli tunahitaji kuilisha miili yetu, akili zetu na roho zetu. Mara nyingi tunajitahidi kuishibisha miili yetu na akili zetu tunasahau roho zetu ndio maana hatupati furaha ya kweli hivyo hatujisikiii kuridhika. Moyo wa mwanadamu unatatufuta furaha na hakuna kitu chochote hapa duniani kinachoweza kutuliza njaa hii. Familia, mali, upendo wa kibinadamu vinatuliza njaa ya moyo wetu ya kutafuta furaha lakini kwa kidogo tu. Mtakatifu Augostino alisoma sana, akapata maarifa mengi, akawa na kazi nzuri, fedha, na kutafuta anasa zote lakini bado hakuridhika. Baada ya wongofu wake, akaandika kitabu kuhusu maisha yake kijulikanacho kama maungamo ya Mtakatifu Agustino. Moja ya maneno mazito aliyoandika ni haya: umetuumbwa kwa ajili yake ee Bwana na mioyo yetu haiwezi kutulia mpaka itakapotulia ndani yako.

Hii njaa ya kiroho iliwaakumba pia wana wa Israeli ambao nabii Isaya anaongea nao katika somo la kwanza. Kwa sababu ya kutokuwa na uaminifu kwa Mungu, watu wa Israeli walichukuliwa utumwani. Lakini hata kule uhamishoni Mungu hakuwasahau watu wake, aliendelea kuwapelekea ujumbe kwa njia ya manabii. Miaka ya mwanzo wakiwa uhamishoni, watu walipata njaa ya mahitaji ya mwili lakini pole pole mahitaji yao ya mwili yalitoshelezwa kiasi. Lakini njaa yao ya kiroho iliongezeka siku baada ya siku kwa kuiacha dini yao na kuishi maisha ya kipagani. Katika somo la kwanza Nabii Isaya anawafariji watu wake. Ni sauti ya baba au mama anayemhangaikia mtoto wake anayekaribia kufa kwa kukataa kula chakula. Anawaalika watu wake katika karamu ambayo kuna vyakula na vinywaji tele vimeandaliwa kwa ajili yao akisema: kila aonaye kiu, njoni majini, naye asiye na fedha; nunueni mle; naam, njoni, nunueni divai na maziwa bila fedha na bila thamani. Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema. Na kujifurahisha nafsi zenu, kwa unono, tegeni masikio yenu, na kunijia. Sikieni, na nafsi zenu zitaishi nami nitafanya nanyi agano la milele, naam, rehema za Daudi zilizo imara.

Baadaye tena Wayahudi waliruhusiwa kurudi Yerusalemu na utabiri wa nabii Isaya ulitimia kiasi fulani wakati hekalu lilipojengwa, ibada za kumwabudu Mungu zikafanywa tena na watu wakahudumiwa tena kiroho na viongozi wa kidini. Wakafundishwa tena sheria ya Musa na kupata tiba ya kiroho katika maandiko matakatifu na sala. Faraja hii anayowapa Isaya ni ya kiroho zaidi ambapo utabiri huu wa kununua bila gharama unatimizwa kwa mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu ambaye kwa upendo wake wa pekee kwetu anatoa maisha yake kulipia gharama ya adhabu tuliyostahili kwa dhambi zetu na kujitoa mwenyewe kuwa chakula chetu cha kiroho yaana Ekaristi Takatifu. Yesu mwenyewe anaseama yeye ni mkate wa uzima ulioshuka kutoka mbinguni. Yoh 6:51 na maji yenye uzima ambayo yeyote ayanywae hatasikia kiu tena Yoh 4:10,14. Hili kwa hakika ni pendo la ajabu. Mtume Paulo katika Somo la Pili la Waraka wake kwa Warumi analisisitiza hili pendo la Mungu kwetu kuwa limedhihirishwa katika Kristo Yesu.

Tukikubali kushikwa na hilo pendo, hakuna hatari wala matatizo yawezayo kututenganisha na Kristo, wala dhiki, wala shida, wala adha, wala njaa, wala uchi, wala hatari, wala upanga, wala mauti, wala uzima wala malaika, wala wenye mamlaka wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu. Lakini kinyume chake ni kweli, kwa wale ambao wanaukataa upendo wa Kristo na kuutupilia mbali, dhiki, shida, adha, njaa, uchi, hatari, upanga na mauti ndio chakula chao .Injili ilivyoandikwa na Mathayo inadokeza matayarisho ya Karamu ya Ekaristi Takatifu na upendo wa Mungu anayetualika wote kwenye karamu ya mbinguni kwa kuibariki, kuimega mikate mitano na samaki wawili na watu wote wakala wakashiba. Yesu anayafanya haya yote kwa kusukumwa na huruma yake kwa watu iliyofumbatwa katika upendo hata kuyatoa maisha yake kwa watu walio kama kondoo wasio na mchungaji hivyo akawaponya wagonjwa, akawafundisha, akawapa chakula.

Katika muujiza huu wa kuongezeka kwa mikate ulikuwa ni mwangwi tu wa kuwekwa kwa Ekaristi Takatifu katika karamu ya mwisho kwani matendo haya mawili yanafanana: kisha atachukua mikate mitano na samaki wawili, akainua macho yake mbinguni na kubariki, akaimega na kuwapa wafuasi wake nao wakawapa makutano (Mt. 14:19). Wakati walipokuwa wanakula, Yesu alichukua mkate na baada ya kuubariki, aliumega na kuwapa wanafunzi wake akisema; twaeni, mle, huu ni mwili wangu. (Mt. 26:26) .Nasi kila mara tunapokusanyika katika adhimisho la Ekaristi Takatifu muujiza huu unafanyika, kwanza Yesu anatuponya magonjwa yetu kwa kutusamehe dhambi zetu ndiyo maana tunaanza maadhimisho ya Ekaristi Takatifu kwa kumwomba msamaha Mungu na wenzetu, pili tunatulisha kwa Neno lake kwani Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu vinakwenda pamoja, tunahitaji aina zote mbili za vyakula, tukipokea kimoja na kuacha kingine hatutatosheleza mahitaji yetu ya kiroho. Yesu angeweza kuandaa chakula kwa ajili ya mkutano bila kuwa na kitu chochote kwanza. Badala yake alichagua kutumia mikate mitano na samaki wawili alivyokuwanavyo mtoto. Hii inatuonyesha wa majitoleo yetu wakati wa Sadaka ya Misa Takatifu ambapo sala na majitoleo yetu ya vipaji mbalimbali vinageuzwa kuwa hazina yenye thamani inayotusaidia kupata uzima wa milele baada ya maisha haya.

Katika sehemu hii ya Injili, mwinjili Matayo ametumia lugha ya picha katika mfumo wa namba. Kwanza ni namba saba: Mikate mitano na samaki wawili  wanafanya idadi ya jumla ya namba saba ambayo inawakilisha ukamilifu kama zilivyo sakramenti saba za Kanisa. Kile ambacho mitume walikiona kidogo na hakitoshi kikiwekwa pamoja kinakuwa cha kutosha kwa wote. Kidogo kikichangiwa na kugawiwa hakipungua kinawatosha wote. Muujiza huu unaonyesha mpango wa Mungu ulivyo mkamilifu. Mungu aliandaa vyote vinavyowatosha binadamu wote duniani mpaka kusaza kwa nyakati zote na huko mbinguni mioyo yetu itashiba na kuridhika. Lakini kwa uchoyo wetu wapo wanajilimbikizia vitu ambavyo hata kama wakivitumia kila siku hawawezi kuvimaliza na vingine yawezakuwa hawavitumii wakati wapo wengine wanaokufa kwa njaa na kiu. Ni katika hili tutahukumiwa siku ya mwisho na hatukashibishwa kamwe. Baada ya kula walikusanya vikapu kumi na viwili, idadi ya mitume na idadi ya makabila kumi na mawili ya Israeli (Mw. 49 :28) ambapo maana yake taifa jipya la Mungu lazima liwe la kushirikiana na sio la kutengana. Waliokula wapata watu elfu tano. Idadi hii ya watu elfu tano inaashiria kazi ya roho Mtakatifu siku ya Pentekoste ambapo waliobatizwa ni yapata watu elfu tano.

Hii ni kumaanisha kuwa watu hawa elfu tano hawakulishwa tu chakula cha kimwili bali pia chakula cha kiroho kinachowapa maana mpya ya maisha. Kumbe tunaalikwa sote tunapopokea Ekaristi Takatifu tusiwe wachoyo. Kama Kristo alivyojitoa yeye mwenyewe kwa ajili yetu sisi nasi tunaompokea tunawajibu wa kujitoa sisi wenyewe kuwahudumia wengine kwa maisha yetu. Haitoshi kutoa vitu kwa ajili ya wengine bali kujitoa wenyewe kwenda kuwahudumia kwa vile tulivyonavyo huko ndio kwa maana zaidi. Ukarimu wa Mungu ni mkuu hivi kwamba hakuna kiumbe hapa duniani kinachopaswa kuona njaa; anavilisha viumbe vyote kama mwenyewe anavyosema katika Injili (Mt. 6:26). Watu duniani kupatwa na njaa, ni kosa la mwanadamu anayepindua mipango ya Mungu katika maisha yake kwa dhambi. Mungu ni mkarimu, anatupa chakula cha roho zetu. Wakati wote kuna meza iliyoandaliwa kwa ajili ya watoto wa ufalme wake; neno la Mungu na Ekaristi vipo wakati wote mbele yetu.

Tunapaswa kuhakikisha kuwa tunajongea meza hii na kushiriki chakula hiki cha kiroho, vinginevyo tutakuwa wadhaifu na hatimaye kufa njaa wakati chakula kipo. Mungu anatualika kila jumapili kushiriki karamu yake. Wale wanaokataa kuja, wale wanaokuja lakini hawashiriki hawawezi kumlaumu Mungu; wanapaswa kujilaumu wenyewe kwa kuugua kwashakoo ya kiroho. Haijalishi tunampenda Mungu namna gani, haijalishi upendo wetu kwake ni wa namna gani, siku zote tutatambua kuwa anatupenda sisi kwanza na kwamba upendo wake kwetu unapita upendo wetu kwake. Tuombe neema za roho Mtakatifu ili tuweze kuwa na moyo wa kutokuchoka kuwahudumia ndugu zetu walio wanyonge kama Yesu hata kama alikuwa amechoka alipowaona watu wahitaji aliwaonea huruma na kuwahudumia.

29 July 2020, 14:01