Tafakari Jumapili 16 ya Mwaka A: Mhusika Mkuu ni Mungu!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Tulianza Dominika ya XV kwa kutafakari sura ile ya 13 ya Injili ya Mathayo, sura ya mifano, Yesu ananena nasi kwa lugha ya mifano. Lugha tafakarishi kwa kila msikilizaji wake ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa wa Bwana na Mwalimu wetu Yesu Kristo. Kama vile katika sehemu ya Injili ya Dominika iliyopita tulialikwa kutafakari mfano wa mpanzi, leo Mama Kanisa anatualika tena kutafakari mfano wa magugu yaliyopandwa katika shamba la ngano. Wazo la msingi ni ‘’Ufalme wa Mbinguni’’, hivyo Yesu anatumia lugha ya mifano kujaribu kuuelezea ufalme wa Mungu kati yetu. Ufalme ambao Mungu mwenyewe anataka kusafiri na kutembea na mwanadamu katika historia yetu, katika maisha yetu ya siku kwa siku, ili abaki kuwa kiongozi wetu katika yote. Ili kuuelezea Ufalme wa Mbinguni, Yesu leo anatumia mifano mitatu ndio ile ya magugu katika shamba la ngano, punje ya haradali inayopandwa na kuwa mti mkubwa na chachu aliyoitwaa mwanamke na kuisitiri ndani ya pishi tatu za unga na hatimaye ukachachwa wote.
Yesu ananena nasi kwa mifano ili kuendelea kutusaidia kupata jibu kwa nini uovu duniani, umetoka wapi uovu katika ulimwengu kwani kila alichoumba Mungu ni chema na kizuri. Ni swali tafakarishi si tu kati yetu tunaoamini bali hata kwa wale wasioamini katika historia ya mwanadamu. Jumuiya ile ya waamini ya Mwinjili Mathayo, nayo pia ilikumbwa na swali hili gumu na tafakarishi juu ya uwepo wa uovu kati yao. Ni jumuiya karibu miaka 50 baada ya kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo, ni waamini wakiangalia jumuiya yao wanaona bado kuna uovu na ubaya kati kati yao, na hivyo wanajiuliza kwa nini wokovu, ufalme wa Mungu haujabadili maisha yao na kuyafanya mapya bila uwepo wa uovu kati kati yao. Katika lugha ya mifano ya Yesu tunaona mara moja anatuonesha kuwa muhusika mkuu na wa kwanza ni Mungu mwenyewe. Ni Mungu anayetambulishwa kama mpanzi, anayetoka na mbegu nzuri na kuzipanda katika konde lake.
Mbegu iliyopandwa ni njema, ndio kusema kila kitu kitokacho kwa Mungu kama vile tunavyosoma sura mbili za kwanza za uumbaji wa ulimwengu kuwa kila kitu kilichoumbwa na kitokacho kwa Mungu ni chema na kizuri. Naomba hapa tuelewe kwa kusema kila alichoumba Mungu ni chema na kizuri haina maana ya kusema hakutakuwa na maafa na majanga ya asili, magonjwa na kifo, ila yote ni mema kwa kuwa yanaakisi na hayapingani na mpango mzima wa Mungu. Kila kiumbe ni chema na kizuri kama ilivyo njema kila mbegu anayoipanda Mungu mwenyewe katika konde lake, katika mioyo ya kila mmoja wetu. Muhusika wa pili ndiye yule aliye muovu, aliye adui wa mpango na madhumuni ya Mungu aliye muumbaji wetu. Adui huyo ndio mantiki ya ulimwengu huu, mtindo wa maisha unaokinzana na Injili. Inayopandwa usiku, saa ile ya giza, saa ile ambayo sote tunakuwa usingizini. Magugu haya yanayopandwa usiku yanakua na hata kuisonga ngano, kuisonga mbegu njema iliyopandwa na Mungu na hata kuinyonya kwa kutumia rutuba iliyokusudiwa kwa ajili ya ngano kumea na kukua vema.
Adui amekuja na kupanda magugu katikati ya ngano saa ile ya usiku. Usiku ndio kusema saa ile ambapo tunakuwa usingizi na hivyo kukosa kuwa waangalifu kwa kuwa tupo usingizini, ndio saa ile tunayojisahau katika maisha yetu na hivyo kujikuta tunaruhusu mantiki na mitindo ya dunia hii kuingia katika maisha yetu na kuanza kuweka mizizi na kukua. Hivyo ni mwaliko kuwa hatuna budi kuwa macho na wenye kukesha kila mara ili kutoruhusu adui kupanda mbegu ya magugu, mbegu ile inayokinzana na Injili katika maisha yetu. Magugu hupandwa ndani mwetu saa ile tunapoacha kuwa walinzi wa maisha yetu, tunapojisahau na kuruhusu mantiki na mitindo ya kidunia kuingia na kuisonga mbegu njema katika maisha yetu. Wahusika wa tatu katika mfano wa magugu na ngano ndio watumwa au watumishi. Watumwa wale tunawaona wakivaa sura ile ya kushangaa na kushtushwa na uwepo wa magugu katika konde lile la Bwana wao. Kwa kweli labda mwitikio wao ndio unaokuwa wa wengi wetu kila mara tunapoangalia jamii na jumuiya zetu za waamini na hasa juu ya uwepo wa uovu kati yetu tena wakati mwingine wa kushangaza na tusioutarajia.
Majivuno na majigambo kati yetu, chuki na fitina za kila aina kati yetu tunaojiita wakristo, kuharibiana majina ndio kuua nafsi ya mwingine kwa uongo na roho mbaya, hapa tunaweza kutaja kila aina ya ubaya na uovu unaokuwepo katika jumuiya zetu waamini na tunaotambulika kama rafiki na wafuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo. Na hapo tunapokutana na watumishi wale wanaofanya mdahalo wa haki na Bwana wao, mazungumzo yanayoonesha juu ya shauku na hamu yao kuona kuwa shamba lile linabaki kuwa safi na salama kwa kuondoa kila aina ya magugu yanayozisonga ngano. Ni shauku yao kuona ngano inastawi na kutoa matunda mengi na mazuri, hivyo watumishi hawa sio tu watu wa mshahara bali hapa wanaonekana kuwa ni sehemu kabisa ya familia ya mwenye shamba. Ni shauku na hamu yao hiyo ya kutaka kuona ngano ile inastawi vema na vizuri, tunaalikwa kupata ujumbe wa Injili ya leo. Ili kutimiza hilo basi wanaomba ruhusa ya kwenda kutoa magugu shambani, ni hamu na shauku ya haki kabisa kwani shamba lilitayarishwa kwa ajili ya ngano na sio magugu, lakini mwenye shamba anawakumbusha hatari inayokuwepo mbele yao.
Shauku na hamu yao inawafumba macho kutoona hatari nyingine inayokuwepo mbele yao katika zoezi zima la kuangamiza magugu. Mwenye shamba kwa kuwa alibaki na kichwa kitulivu hivyo haanguki katika mtego ule, kwani haongozwi kwa hisia kali na jazba bali anaongozwa na moyo wa utulivu na uvumilivu, ndio moyo unaokuwa wazi, unaoangalia mambo kwa mapana na kwa umakini mkubwa bila kuacha eneo lolote linalopaswa kuangaliwa vema na vizuri. Jibu la mwenye konde linaonesha pia jinsi Mungu anavyoacha uovu ukue pamoja na wema katika nafsi ya kila mmoja wetu, mbegu njema inayosongwa na ile mbaya katika nafsi na maisha ya kila mmoja wetu. Labda hapa tunaweza kuwa na swali ikiwa Mungu ni Mwenye uwezo wote kwa nini basi asitoe magugu ya uovu katika nafsi na maisha yetu? Kwa nini asinifanye mimi kuwa mtenda mema tu na kamwe ubaya na uovu usisikike wala kuonekana katika maisha yangu? Labda ni swali la haki na tamanio linalokuwa jema, na hivyo niwaalike kutafakari zaidi juu ya hili.
Mungu sio mwenye uwezo wote kadiri ya tunavyofikiri sisi mara nyingi, nitajaribu kueleza japo kifupi ili nisije eleweka vibaya hapa. Kwa kweli Maandiko Matakatifu hakuna hata sehemu moja Mungu anayopewa sifa hiyo ya kuwa muweza wa yote, ila anaitwa ‘’muweza au mwenye nguvu’’ (Luka 1:49) au kwa kigiriki ‘’pantokràtor’’ (Ufunuo 1:8), ‘’...asema Bwana Mungu mwenye nguvu, aliyeko, aliyekuwako ma anayekuja’’. Mwenye nguvu haimaanishi kuwa anaweza kufanya lolote au chochote anachotaka. Ila Mungu wetu ni mwenye nguvu ndio kusema hakuna kitu kinachoshindikana mbele yake. Mungu anamuumba mwanadamu na kumpa utashi, ni Mungu anamuumba mwanadamu akisukumwa na upendo na kutaka kubaki katika mahusiano ya upendo na mwanadamu na sio kama yale ambayo mara nyingi tunayatamani yaani kuishi bila utashi. Mahusiano yetu na Mungu mwenye nguvu ni mahusiano yanayojengeka juu ya upendo. Daima hatuna budi kuishi huku tukitambua kuwa Mungu wetu ni mwenye nguvu na hivyo mwisho ni Yeye atakayeshinda uovu na muovu, bali katika maisha ya sasa hatuna budi kukubali kupatwa na changamoto za kuishi katika ulimwengu huu wenye magugu.
Kila anayetambua kuwa Mungu ni “pantokràtor”, ndiye yule anayetambua udogo na uduni wake na hivyo kumtegemea na kumkimbilia Mungu. Ni kutokana na uduni na unyenyekevu hu,o hapo tunaalikwa kuona kuwa Mungu anatualika kwake kwani Yeye ni muumba wetu asiyetaka hata mmoja wetu apotee bali sote tufikie uzima wa milele. Tunaangamiza maisha yetu na kupotea kwa kiburi chetu cha kugoma na kuukataa uwezo na nguvu za Mungu. Mungu daima ni mwenye nguvu na uwezo kwa kila anayemkimbilia na kusafiri naye. Hakuna mmoja atakayemkimbilia Mungu na kuruhusu kuongozwa naye atakayepotea, ila bado Mungu anaheshimu utashi wetu, hivyo kutuacha huru katika kuchagua hatima yetu. Uwepo wa magugu ambao tumeshaona kuwa ndio uovu na ubaya unaokuwepo kati yetu, kwa hakika unatusumbua sisi sote iwe unapokuwa ndani mwetu na hata pale tunapoushuhudia kwa wengine. Hekima 7:20 tunaona jinsi mwandishi yule anavyojiuliza kuwa hakuna hata mmoja wetu asiyekuwa na magugu au uovu ndani mwake, na kwa kweli itoshe sisi wenyewe kuwa wakweli na kuingia ndani mwetu na kujichunguza na hapo tunatambua kuwa kila mmoja wetu ana magugu yake moyoni, magugu katika maisha yake. Magugu ambayo hata nyakati nyingine hutukatisha tamaa na kuturudisha nyuma, kwani yanasonga mbegu ile njema iliyopandwa na Mungu ndani mwetu.
Pamoja na kuwa hatuwezi kuhalalisha uwepo wa magugu na uovu katika maisha yetu, ila leo Yesu anatualika kuwa na mtazamo mpya, mtazamo ule wa Mungu mwenyewe, mtazamo wa mwenye shamba, kubaki watulivu na kutenda kwa hekima kuu itokanayo na Mungu mwenyewe, mmiliki wa konde la ngano. Mungu daima anatuhurumia, anatusamehe, anatupa nafasi nyingine kila mara tunapoanguka, hivyo hivyo nasi hatuna budi kwenda katika shule yake ya huruma na kujifunza kutoka kwake. Leo tunaalikwa kwenda shule ya Mungu mwenyewe ikiwa kweli tunahitaji kukua katika utakatifu. Kukimbilia kwake na kuruhusu kuongozwa naye kama kweli tunahitaji kukua katika mahusiano yetu na Mungu na wengine. Magugu yake kwa Lugha ya Kigiriki yanajulikana kama ‘’zizania’’ na kwa Kilatini ‘’Ebriacum’’ na katika lugha ya mimea kitaalamu yanajulikana kama ‘’lolium temulentum’’, majira ya mimea kuchipua basi magugu haya yanakua na kuisonga ngano na hata kuepelea hapa na pale kuua kabisa ngano.
Na jinsi magugu haya yalivyo yana mfanano mkubwa sana na ngano na hivyo kuwa ni vigumu kutofautishwa kutoka ngano. Ndio kusema magugu yanafanana sana na ngano, ni kama baadhi ya matendo yetu maovu jinsi yanavyovaa sura ya wema hata kuwafanya wengine na hata sisi wenyewe kushindwa kutofautisha. Na ndio hata mantiki za ulimwengu na mitindo yake mara nyingi inakuja ikiwa na mavazi ya wema na uzuri kiasi kwamba tukikosa kuwa makini tunajikuta tayari tumekaribisha na kupanda ndani mwetu magugu yanayosonga na kuua mbegu njema ya ngano. Nimejaribu kuweka na majina yake katika lugha hizo mbali mbali sio kwa lengo la kuwasumbua bali kutusaidia kuona ni mmea wa aina gani na hasa mfanano wake na ngano. Zaidi ya mfano wa magugu yaliyopandwa na adui katika konde lile la ngano, leo pia Yesu ananena nasi kwa mifano mingine mifupi miwili, inayojulikana kama mifano pacha kwani inafanana sana na ina ujumbe unaofanana pia.
Ni mifano inayoonesha mwanzo duni lakini matokeo yake ni makubwa na ya kustaajabisha. Punje ndogo sana ya haradali, jinsi inavyomea na kukua na hatimaye kuwa mti mkubwa sana. Hivyo hivyo chachu kidogo inavyoweza kufanya maajabu ya kuchachusha kiasi kikubwa cha unga. Mifano hii pacha ya mbegu ya haradali na chachu inaonesha nguvu ya Roho wa Mungu na Neno la Mungu pamoja inaweza kutoonekana kwa macho ya nyama na katika mantiki ya dunia hii lakini daima yenye matunda makubwa. Mfano wa haradali katika Maandiko Matakatifu ni Yesu pekee anautumia tena mara mbili, zaidi ya Injili ya leo tunasikia tena juu ya mbegu ya haradali katika msemo ule maarufu wa Yesu katika Mathayo 17:20 ‘’…kama tu mkiwa na imani, iwe ndogo hata kama mbegu ya haradali, mtaweza kuumbia mlima huu: Toka hapa uende pale, nao utakwenda…’’ Ni punje ile ndogo inakua na kuwa mti mkubwa karibu mita 3 mpaka 4 na hivyo kuwa makazi ya ndege. Ndio kusema Ufalme wa Mbinguni daima unaanza na hata kuonekana kuwa ni kitu kidogo lakini matokeo yake daima ni makubwa na yenye kustaajabisha.
Sehemu ya mwisho ya Injili ya leo, Mwinjli anaonesha nia na shabaha ya Yesu kwa kutupa ufafanuzi wa mfano wa magugu katika shamba la ngano. Yesu hayupo tena katika chombo bali nyumbani, na pia haongei tena na makutano bali na jumuiya ndogo ya wafuasi wake wa karibu yaani mitume. Hata wahusika hapa tunaweza kuona wanakuwa tofauti na vile tulivyoona mapema katika tafakari yetu hii. Sasa lugha ile ya mifano inaonekana kuwa katika mtindo wa kufananishwa, ‘’allegory’’. Hata lugha inayotumika hapa inatofautiana na ile ya mwanzo ambapo tunaona Mungu mwenye huruma na mvumilivu bali anayetaka kuangamiza mara moja. Hivyo tunajiuliza kwa nini tofauti ya ghafla ya uandishi tena katika sura moja na ile ile na Mwinjili yule yule. Mwinjili kwa kweli anahitimisha katika mtindo huu, ilikuwa ni katika wakati ambapo Mwinjili akiwa anaandika wale waamini walikuwa katika maisha ya kujisahau na kuanza kuishi maisha yasiyoakisi Injili na imani yao.
Mwinjili anaona anayo kila sababu ya kuwaonya na kuwatahadharisha. Hivyo anatumia mtindo na hata lugha ya wahubiri wengi wa nyakati zake. Mwandishi ni Myahudi, ni mmoja wa Marabi na alikuwa anaongea na jumuiya ya waamini wenye asili ya kiyahudi hivyo ili kupata ujumbe alipaswa kutumia lugha inayoeleweka kwao. Ndio lugha inayokuwa ya kutisha na kuogofya. Moja la hakika na lazima tutambue kuwa anayetuangamiza sio Mungu bali ni sisi wenyewe tunayaangamiza maisha yetu kwa kutotumia vema akili na utashi wetu aliotuumba nao Mungu kwa kuacha kuchagua mema na kuchagua uovu. Mungu ni mwenye nguvu kwa kila anayemkimbilia na kumlilia na kukubali kuongozwa naye katika maisha. Ikiwa tunakubali kuongozwa naye na kuisikiliza sauti yake yaani Neno lake, hakika hapo tunakuwa na maisha ya uzima wa milele. Nawatakia Dominika na tafakari njema.