Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 16 ya Mwaka A. Wema na huruma ya Mungu kama kichocheo cha toba na wongofu wa ndani. Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 16 ya Mwaka A. Wema na huruma ya Mungu kama kichocheo cha toba na wongofu wa ndani. 

Tafakari Jumapili 16 ya Mwaka A: Wema: Toba na Wongofu wa ndani!

Mama Kanisa yanatualika kuutafakari wema wa Mungu kama kichocheo cha wongofu kwetu. Mungu ni mwema, mwenye huruma na haki na tena mwenye uvumilivu mwingi. Kwa kinywa cha Nabii Ezekieli yeye mwenyewe alitamka “sifurahii kifo cha mtu mwenye dhambi bali aaiche njia yake mbaya apate kuishi” (Zak 33:11). Wongofu ni mwaliko huo wa kudumu wa kuiacha njia mbaya ili kuishi.

Na Padre William Bahitwa, -Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 16 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (Hek 12:13, 16-19) ni kutoka Kitabu cha Hekima ya Sulemani. Mwandishi wa kitabu hiki anatafuta kuyapa mang’amuzi matukio mbalimbali ya kimaisha ambayo watu wa taifa lake wameyapitia. Kama ilivyokuwa katika mataifa yaliyowazunguka, Israeli ilikuwa pa na mfumo wake wa mafundisho ya Hekima. Haya yalikuwa ni mafundisho mbalimbali kuhusu maisha ambayo wazee kutokana na uzoefu wao waliwarithisha vijana. Hekima hii pia wakati mwingine ilitafuta namna ya kujibu baadhi ya maswali magumu kuhusu maisha yenyewe. Hapa ilitafuta kutoa majibu kwa mfano kuhusu fumbo la kifo, kuhusu mateso, magonjwa au hali mbalimbali za maisha ambazo zilionekana kuwa si za kawaida.

Katika somo la leo, mwandishi huyu anayapatia tafsiri matukio magumu ambayo taifa lake liliyapitia hapo nyuma. Tukiangalia aya zilizotangulia somo hili tunaona kuwa mojawapo ya matukio hayo ni upinzani mkali ambao waisraeli waliupata kutoka kwa wakanaani wakati walipokuwa wakitakata kuingia katika nchi hiyo ya ahadi. Mwandishi anaitafsiri hiyo kama ni adhabu ambayo walipewa kwa sababu ya makosa yao mbalimbali waliyokuwa wamemfanyia Mungu. Hata hivyo mwandishi huyu anakiri kuwa Mungu alifanya hivyo kwa haki. Hakuwaonea kitu chochote. Yeye ndiye Mungu aliye na uwezo wote na uwezo huo aliutumia kwa haki. Na anakiri kabisa kuwa pamoja na kuwahukumu kwa haki, Mungu alikuwa bado na huruma nyingi kwao kwa sababu aliwapa adhabu hiyo kwa uangalifu mkubwa sana ili wasikate tamaa na mwishoni aliwajalia kufanya toba ili wasiangamie.

Katika nafasi ya kwanza, somo hili linaonesha ule upekee wa Hekima ya Israeli dhidi ya Hekima ya mataifa mengine. Na upekee huu ni kuwa Hekima ya Israeli ilikuwa na kiini chake katika kuwavuta watu kumcha Mungu. Kwao “kumcha Bwana ndio mwanzo wa Hekima”. Hekima ya mataifa mengine haikuwa na fikra yoyote kuhusu Mungu. Pili, somo hili ni mojawapo ya vifungu katika Biblia vinavyoonesha kuwa kwa Mungu haki na huruma huenda pamoja. Mungu mwenye huruma ni Mungu pia mwenye haki anayemlipa mtu kadiri ya matendo yake. Vivyo hivyo Mungu mwenye haki anayemlipa mtu kadiri ya matendo yake ni Mungu pia mwenye huruma.

Somo la pili (Rum 8: 26-27) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika waraka huu, Paulo amesisitiza kwa kirefu sana juu ya nafasi ya Kristo katika wokovu. Ameonesha kuwa kwa Wayahudi na hata watu wa mataifa, wokovu hupatikana kwa njia ya Kristo pekee. Hivyo alialika wote kumpokea Kristo na kujenga imani yao kwake. Katika somo la leo, Paulo anaongeza kwa kuonehs msaada wa Roho Mtakatifu katika kuufanikisha wokovu huo. Anasema, kwa udhaifu wetu wa kibinadamu hatujui kwa kweli kusali katika namna inayotupaswa kusali. Katika mantiki kuwa sala ni mawasiliano au mahusiano kati ya mtu na Mungu, Paulo anaonesha kuwa hatuwezi kuwa na mahusiano yale tunayopaswa kuwa nayo na Mungu kwa sababu ya udhaifu wetu. Hivyo ni Roho Mtakatifu ndiye huingilia kati na kuja kutusaidia katika udhaifu wetu huo. Ni Roho anayetuombea kwa mlio usioweza kutamkwa. Ni Roho anayetusaidia na kutuinua kutoka udhaifu wetu. Somo hili linatujaza nguvu ya kusonga mbele kuuekea ukamilifu wetu kwa matumaini makubwa kuwa tunaye Roho anayetusaidia.

Injili (Mt 13:24-43) injili ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Mathayo.  Yesu anaendelea kufundisha kwa njia ya mifano. Leo anatoa mifano mitatu anayoitumia kuelezea ufalme wa Mungu. Katika mfano wa kwanza anaufananisha ufalme wa Mungu na mtu alipanda mbegu njema ya ngano shambani mwake, lakini usiku akaja adui yake akapanda magugu. Mwenye shamba lakini hakutaka kuyang’oa yote pamoja, akayaacha yakue yote na wakati wa mavuno ndio akatenganisha magugu na ngano. Katika mfano wa pili aliufananisha ufalme wa Mungu na mbegu ya haradali. Mbegu ambayo ni ndogo sana lakini ikikua inatengeneza mmea mkubwa na ndege wa angani wanakuja kutengeneza viota katika majani yake. Katika mfano wa tatu anaufananisha ufalme wa Mungu na hamira ambayo ni kiasi kidogo tu kinatosha kabisa kuumua donge kubwa la unga wa ngano unaokandwa. Mifano hii, pamoja na mingine mingi, Yesu aliitumia kuelezea uhalisia ambao watu walikuwa hawaufahamu. Yaani anatumia lugha ya vitu ambavyo watu tayari wanavifahamu na anavifananisha na vile wasivyovifahamu ili kuwafanya wapate picha ya kile anachowaelezea.

Katika mifano hii anatumia picha ya vitu vya kawaida vinavyofahamika ili watu wapate picha juu ya ufalme wa Mungu. Katika mifano hii tunaona kuwa ufalme wa Mungu ni kitu kinachokua. Unakua kama vile mbegu inavyokuwa kufikia hatua ya kuwa mmea kamili. Ufalme nao tangu mtu anapoupokea unakua na kuzidi kujifunua ndani yake kuelelekea ukamilifu wake siku ya mwisho. Pili, ukuaji wa ufalme huo ndani ya mtu ni siri na ni kazi ya Mungu. Mwanadamu katika hilo si mtendaji bali ni mpokeaji. Tunaona katika mifano hiyo Yesu aliyoitoa, mpanzi alikwenda kulala na katika namna na muda asiojua, mbegu ziliendelea kukua. Ndiyo maana hata katika sala ya Baba yetu tunasali “ufalme wako ufike”.  Sisi tunajiweka tu katika hali ya kupokea ukuaji wa ufalme huo lakini mtendaji ni Mungu.

Tatu katika ukuaji wa ufalme huo, ipo pia jitihada ya adui, yaani shetani, akiuzuia ufalme huo kukua ndani yetu. Ndiyo maana hapa na pale mwanadamu anaanguka katika mitego na mivuto ya adui na anajikuta anakuza ngano njema ya ufalme pamoja na magugu katika moyo wake. Hata hivyo Yesu anaonesha uvumilivu mkubwa wa Mungu mwenyewe katika ukuaji wa ufalme pale anaposema “acheni magugu na ngano vimee pamoja hadi mwisho wa mavuno”. Huu ni uvumilivu wa fumbo la ufalme ambao haupendi kumwangamiza mara moja mtu mwovu bali hata katika uovu na ulegevu wake bado Mungu humwacha akitumaini kuwa siku moja mtu huyo atabadilika. Ni uvumilivu ambao kamwe hauhalalishi uovu bali humpa mtu nafasi ya kugeuza njia zake mbaya arudi katika kuwa mwana wa ufalme.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii ya 16 ya mwaka A wa Kanisa yanatualika kuutafakari wema wa Mungu kama kichocheo cha wongofu kwetu. Mungu ni mwema, mwenye huruma na haki na tena mwenye uvumilivu mwingi kwetu sisi viumbe wake. Kwa kinywa cha Nabii Ezekieli yeye mwenyewe alitamka “sifurahii kifo cha mtu mwenye dhambi bali aaiche njia yake mbaya apate kuishi” (Zak 33:11). Wongofu ni mwaliko huo wa kudumu wa kuiacha njia mbaya ili kuishi. Kanisa linatufundisha kuwa zipo hatua mbili za kumwongokea Kristo. Hatua ya kwanza ni pale mtu anapozaliwa mara ya pili kwa ubatizo. Hii hufanyika mara moja tu basi. (Rej. KKK 1426). Hatua ya pili ni ile kazi ya kudumu ya mapambano kwa ajili ya utakatifu na uzima wa milele ambayo mkristo huifanya kila siku ya maisha yake. Huu ni mwaliko wa kudumu kwa sababu ubatizo pamoja na sakramenti za mwanzo havikomeshi udhaifu na maelekeo ya dhambi kwa mwanadamu. Na hii huifanya safari nzima ya mkristo kuwa ni safari ya toba na ya kuutafuta wongofu wa ndani kila siku. Maandiko matakatifu siku ya leo yanatualika pia tuitegemee nguvu ya Roho Mtakatifu ambaye huja kutuimarisha na kutusaidia katika udhaifu wetu ili siku kwa siku tuzidi kuuishi wongofu utupasao na kwa wema wake Mungu tustahili kuuingia ufame wa Mungu.

Liturujia Jumapili 16

 

17 July 2020, 13:02