Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 18 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Yesu anatendsa muujiza kwa kuulisha umati wa watu! Leo hii baa ya njaa ni changamoto pevu duniani! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 18 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Yesu anatendsa muujiza kwa kuulisha umati wa watu! Leo hii baa ya njaa ni changamoto pevu duniani! 

Tafakari Jumapili 18 Mwaka A: Chakula Cha Kila Siku! Baa la Njaa

Muujiza unaofanyika leo ni ule wa kukubali kubadili vichwa vyetu na kukumbatia mantiki ya Injili, ambayo ndio ya Mungu mwenyewe. Ni kwa njia hiyo ya kumpenda kweli Mungu na jirani basi kila mmoja wetu hatatindikiwa na chakula wala kinywaji, kila mmoja anaweza kutosheka na kuridhika kwani hatutaweka hazina yetu katika mali na vitu bali kwa Mungu mwenyewe. Tuwe wakarimu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Yesu leo anatenda muujiza wa kulisha umati mkubwa wa watu kwa mikate mitano na samaki wawili. Tukibaki kuuangalia kama muujiza tu hakika tunabaki na maswali mengi na magumu kuyapatia majibu ya kuridhisha.  Mwinjili anatuambia kuwa Yesu alikuwa faraghani na hivyo umati ule mkubwa ulimfuata, kufikiria umati wa watu tena wanatajwa kwa idadi kuwa wanaume walikuwa elfu tano bila kuhesabu wanawake na watoto, ni kwa jinsi gani umati mkubwa kiasi hicho wangeweza kusafiri kwa pamoja kutoka mijini kwao na kumfuata Yesu? Tunaambiwa kuwa ilikuwa jioni, saa ya giza, Je, iliwezekana vipi kuwaketisha umati mkubwa na kuweza kuwagawia mikate na samaki wale katika saa ile na mahali ambapo hakukuwa na taa wala mwanga wa kutosha? Mwinjili anatuambia walikusanya masazo vikapu kumi na viwili, tunajiuliza vilitoka wapi vikapu vile au vilikuwepo tangu awali bila kitu? Lakini zaidi sana hata nasi leo tunapoishia kuuona huu kama muujiza bado tunakuwa na swali la haki na msingi kabisa na hasa tunapoona watu wengi duniani leo wanakufa kwa baa la njaa.

Kama Yesu aliweza kutenda muujiza ule miaka elfu mbili iliyopita, kwa nini basi Mungu anaruhusu leo watu kufa kutokana na kukosa chakula? Kwa nini leo Mungu hasikii kilio cha watu wake wanaosali na kumlilia kila siku ‘’Utupe leo mkate wetu wa kila siku’’? Je, Mungu amewasahau wanae wanaomlilia na kumuomba kila siku? Leo tunaposhuhudia watu wengi wakifa kwa kukosa chakula, tunashuhudia pia hata wale wenye chakula cha kutosha na kusaza wanajikuta na njaa ya upweke, kukosa furaha na amani ya kweli. Njaa ya kuwa na vingi zaidi na kujilimbikizia ndio mantiki ya ulimwengu wa leo ambayo kila mara inazaa njaa na kiu ya kuwa na zaidi na zaidi. Mwanadamu leo anajikuta katika mahangaiko ya kujilimbikizia akidhani kuwa kwa kumiliki vitu basi hapo atapata furaha na utulivu wa nafsi, lakini kinyume chake tunaona mwanadamu anajikuta bado katika mtego wa kujawa na wasiwasi na utupu wa nafsi. Mwanadamu hajawahi kutimiza njaa na kiu katika vitu na mali.

Ni katika muktadha huu nasi leo tunaalikwa kutafakari vema somo la Injili. Ni kwa kuangalia maisha yetu jinsi kila mmoja alivyo na njaa na kiu si tu ya mkate na maji bali na mali na vitu. Muujiza unaofanyika leo ni ule wa kukubali kubadili vichwa vyetu na kukumbatia mantiki ya Injili, ambayo ndio ya Mungu mwenyewe. Ni kwa njia hiyo ya kumpenda kweli Mungu na jirani basi kila mmoja wetu hatatindikiwa na chakula wala kinywaji, kila mmoja anaweza kutosheka na kuridhika kwani hatutaweka hazina yetu katika mali na vitu bali kwa Mungu mwenyewe. Yawezekana isiwe rahisi kwetu kusema kwa hakika kile kilichojiri kandokando ya ziwa Galilaya miaka elfu mbili iliyopita. Yafaa leo kuchota katika simulizi la muujiza huu wa kulisha watu wengi ujumbe kusudiwa kutoka kwa Mwinjili Mathayo. Makutano wanatoka katika miji na kumfuata Yesu aliyekuwa faragha nyikani, ndio kusema Yesu ndiye Musa mpya, ndiye kiongozi mpya ambaye sote tunaalikwa kutoka katika miji na vijiji vyetu ili kumfuata. Kuacha maisha yetu ya kale na mazoea yetu ili Kristo atuoneshe maisha mapya, atupe mantiki mpya ya kuenenda katika maisha yetu, ili atuponye magonjwa yetu na kutushibisha kwa chakula na kinywaji cha kweli.

Wanawaisraeli walitoka katika nchi ile ya utumwa na kwenda jangwani kuanza safari kwenda katika nchi ile ya uhuru, nchi ya maziwa na asali. Mwinjili Mathayo anatupa simulizi la muujiza wa leo baada ya kifo cha Yohane Mbatizaji. Yohane Mbatizaji anauawa baada ya Herode kufanya karamu ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa (Mathayo 14:3-12). Sherehe ile ya Herode inawakilisha jamii iliyopotoka na kukengeuka, jamii isiyo na haki wala kujali walio wanyonge na wanaosimamia ukweli wa maadili. Jamii ambayo kwa kiasi kikubwa inaakisi hata jamii zetu nyingi leo, jamii zinazotawaliwa na ukosefu wa maadili, kweli, upendo na haki, jamii ya kulipiza kisasi, yenye ukatili na tamaduni ya kifo. Ni kwa njia ya kutoka katika miji na vijiji vyetu ili tuweze nasi kukutana na Yesu jangwani ili kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda. Yesu anapowaona makutano anawahurumia. Neno la lugha ya Kigiriki linalotumika hapa ni ‘’splagknizomai’’ likiwa na maana sio tu hisia za kimuhemuko bali ni hisia za ndani kabisa. Ni hisia itokanayo na upendo wa kweli na wa dhati, ndio kusema ni sawa na hisia kali anayokuwa nayo mama mzazi anapomuona mwana wake katika mateso na mahangaiko, ni hisia za tumbo la uzazi, ni hisia kali zitokanazo na upendo.

Ndivyo Yesu anakuwa na hisia hizi za kutuhurumia kwa upendo kwa kutuona katika mateso na mahangaiko kwa kutawaliwa na mantiki za ulimwengu huu wa mali na vitu. Utamaduni wa kutoridhika kwani tumeweka mioyo yetu katika mali na vitu. Kila mara Yesu anapowaona makutano anasukumwa na huruma kwao. ‘’Basi, alipowaona watu, makundi kwa makundi, aliwaonea huruma kwa sababu walikuwa ni wenye wasiwasi kama kondoo wasio na mchungaji’’ (Mathayo 9:36) Hivyo Yesu kila mara anapotuona na kukutana nasi katika hali mbaya anaguswa na kutuhurumia. Yesu haishii tu kutuonea huruma na kutufariji kwa maneno matupu bali anashuka chomboni na kufanya kitu. Tunaona Yesu akatoka na kuwaponya wagonjwa wao. Yesu hata leo anapokutana nasi anatoka na kutuponya magonjwa yetu yanayotusonga na kutusumbua katika maisha yetu. Si tu Yesu anapokutana na makutano anawaonea huruma na kufanya kitu, bali leo anatualika nasi wafuasi wake kutenda kama anavyotenda yeye, ndio kuwa na huruma lakini zaidi sana kuiweka huruma hiyo katika matendo. ‘’Muwe na msimamo uleule aliokuwa nao Kristo Yesu’’ (Wafilipi 2:5). Mtume Paulo anatusihi nasi leo kuenenda kama Kristo, kuwa na huruma na upendo uleule wa Kristo mwenyewe. Yesu anaguswa sio tu na maradhi na magonjwa yanayowasumbua bali hata na mahitaji yao ya lazima na ya msingi kama ukosefu wa chakula. Je, ni upi mwitikio wa Yesu kwa wahitaji wa ulimwengu wetu wa leo?

Kwa hakika kama jibu la Yesu ni kutenda muujiza kama ule alioufanya yeye miaka elfu mbili iliyopita tutajikuta katika ugumu na hata kukata tamaa kwani hakuna hata mmoja wetu mwenye uwezo wa kutenda muujiza au kuomba ili muujiza wa aina ile ufanyike hata leo kwa wale wahitaji na hasa wanaokuja kutokana na kukosa chakula. Lakini kwa muujiza ule Yesu leo anatualika kuona nini kila mmoja wetu kama mfuasi na rafiki yake anapaswa kutenda ili asiwepo hata mwanadamu mmoja katika uhitaji wa chakula na mahitaji ya lazima. Yesu leo hatendi muujiza ule wa kulisha makutano bila kuwashirikisha wanafunzi wake wa karibu, na ndio anavyotulika nasi leo kushirikiana naye kwa kuwahurumia na kutenda kitu ili asitokee mmoja wa kutindikiwa. Mara nyingi changamoto kubwa iliyopo ni ile hali ya kujiona sihusiki na sina la kufanya katika kusaidia wanaokuwa katika uhitaji mkubwa au mdogo. Mitume nao walikuwa na hisia hiyo hasi ya kumshauri Yesu awaage makutano ili wakajitafutie wenyewe chakula. Ni njia rahisi kwani badala ya kufanya kitu mimi, kila mmoja ajifikirie na kujihangaikia mwenyewe, na ndio mantiki ya ulimwengu wa leo, kila mmoja apambane na hali yake, kila mmoja ajihangaikie kwa bidii na juhudi ili kupata mahitaji yake ya lazima. Ni ulimwengu wa kila mmoja kujali yake.

Ni changamoto hata kwa Kanisa letu, ni mara ngapi jumuiya zetu, vigango vyetu, parokia zetu na hata familia zetu zimekuwa ni sehemu ya kukimbiliwa na wahitaji wa kila aina, si tu wa chakula, wale wa upweke na wanaokosa kupendwa, wanaosetwa na kutengwa kutokana na hali zao, ni mara ngapi mimi na wewe tumewaonea huruma wahitaji hao na kufanya kitu ili nao wasibaki katika hali duni ya uhitaji?  Yesu leo anatuambia, ‘’Hawana haja ya kwenda zao, wapeni ninyi kula’’, ni amri na maagizo kutoka kwa Bwana na Mwalimu wetu kwa kila mmoja wetu. Ni mara chache Yesu anatumia lugha ya amri ila leo anatumia kwangu na kwako, kwa kila mmoja wetu kujiona kuwa tuna wajibu wa kufanya kitu kwa ajili ya ndugu zetu wanaokuwa katika hali ya kuhurumiwa kwa mahitaji mbali mbali kwani yaweza kuwa ya kimwili na hata kiroho.

‘’Hatuna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili’’, ndio jibu la mitume, ndilo jibu letu nasi leo kila mara Yesu anapotualika kuhurumia na kufanya kitu kwa ajili ya wahitaji. Kila mmoja anajiona alicho nacho ni kwa ajili yangu peke yangu na labda wale tu wanaokuwa karibu na mimi. Ni jibu bado lenye ubinafsi, la kutokuwa tayari kushirikiana na wengine kwa kisingizio kuwa nilicho nacho ni kidogo. Hakuna mmoja maskini hivi kwamba hana cha kutoa na vile hakuna mmoja mwenye kila kitu hivyo asiye na uhitaji wa chochote. Mwenyezi Mungu ametuumba hivyo kila mmoja wetu anamuhitaji mwingine, ni kwa kuwa tayari kuachana na ubinafsi hakika hapo muujiza utatendeka kwani kila mmoja ataondoka ametosheka na kushiba, ni kwa njia ya kukubali kufungua moyo wangu kwa ajili ya wengine wanaonizunguka. Leo watu wanakufa njaa duniani wakati wachache wanajilimbikizia utajiri na mali zisizokuwa na kifani. Watu wanakufa njaa kwa kuwa wachache tumekuwa wabinafsi na wachoyo, tumeona kila tulicho nacho ni kwa ajili yetu na familia zetu tu.

‘’Nileteeni hapa’’ ni agizo na amri nyingine ya Yesu katika somo la Injili ya leo. Ni agizo kwa kila mmoja wetu kumpelekea Yesu kila nilichonacho, ndio kusema ni katika mikono ya Yesu pekee hapo kidogo kinaweza kugawanywa kwa wengine wanaokuwa wahitaji na muujiza mkubwa ukatendeka. Ni kwa kukubali kutoa yote, kukubali kuongozwa na mantiki ya Injili peke yake hapo muujiza mkubwa unatendeka kwani kile kidogo naweza kuwashirikisha wengine kwa ukarimu. Duniani leo kungekuwa mahali pazuri pa kuishi ikiwa tu mwanadamu ataachana na ubinafsi na uchoyo, ataachana na moyo ule wa kuona kila alichonacho ni kidogo na kwa ajili yake peke yake. Mikate mitano na samaki wawili, na hapo jumla inakuwa ni saba. Namba saba katika Maandiko ni namba ya ukamilifu, ndio kusema mitume wanaalikwa kuweka mikononi mwa Yesu sio tu sehemu ya walichokuwa nacho bali chote bila kubakisha chochote. Ndio mwaliko anaotupa Yesu leo kupeleka mikononi mwake sio sehemu tu ya kile anachokuwa nacho kila mmoja wetu bali vyote bila kubakiza chochote nyuma. Ndio kusema naalikwa leo kupeleka mikononi mwa Yesu sio tu pesa au chakula au mavazi bali hata vipawa na karama zangu, muda na ujuzi wangu, kila kitu nilichonacho napaswa kutambua kuwa ni mali yake Mungu na hivyo lazima kuvitumia kwa upendo na ukarimu mkubwa.

Mkate katika Biblia ni chakula cha kila siku kama vile ugali na wali au ndizi kwa baadhi ya jamii zetu. Kusema mkate ni sawa na kusema ‘’chakula’’ na ndio maana kwa Wayahudi mkate hairuhusiwi kupewa wanyama, wala unapokanyaga mkate njiani ulipaswa kuuokota kwani kuutupa mkate ni sawa na kumkosea heshima Mungu, mkate ni zawadi kutoka kwa Mungu hivyo lazima kutumika pia kwa heshima na shukrani. Katika mazingira ya Yesu mkate haukatwi hata mara moja kwa kisu bali kumegwa kwa mikono. Mkate unaheshimika na hata kuonekana kama kiumbe hai na ndio maana marufuku kukata mkate kwa kisu. Mkate ni kitu kitakatifu hivyo hakina budi kuchukuliwa kwa heshima kubwa, ni zawadi ya Mungu kwa mwanadamu, hivyo Yesu leo anatukumbusha nasi kuwa vyote tulivyo navyo ni mali ya Mungu na hivyo hatuna budi kuyatumia yote kwa moyo wa shukrani na ukarimu kama mkate, kuwa tayari kuwashirikisha na wengine wanaokuwa wahitaji kwani vyote ni mali ya Mungu, sisi tumewekwa kuwa waangalizi tu na kamwe sio wamiliki wa yale tunayokuwa nayo katika maisha.

‘’Akawaagiza makutano waketi katika majani’’ Labda pia tunaona picha ya mahali inabadilika mara moja kutoka sehemu ya jangwa na kuwa mahali penye majani, ndio kusema kila mara Yesu anatualika kutoka jangwani na kwenda kwake na hapo anatuketisha katika majani. Majani ni ishara ya uhai na matumaini. Kuketi ni mkao wa wale wanaokuwa huru na sio watumwa. Katika mazingira ya Yesu mtumwa wakati wa milo hakuruhusiwa kuketi na badala yake kusimama na kuwa tayari kutumikia, ila leo Yesu anawaalika makutano kuketi ndio kusema anawapa uhuru, anatupa uhuru kila mmoja anayekuwa tayari kumkimbilia, na pia anatualika nasi kuwafanya wengine waketi, kusaidia wengine kutembea katika uhuru wa wana wa Mungu. Kuwafanya wengine waongozwe sio kwa mantiki za ulimwengu huu bali zile za Injili, za Neno la Mungu. ‘’Akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano’’. Yesu anatazama mbinguni ndio kusema mikate ile na samaki wale ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kila kitu ninachokuwa nacho katika maisha yangu ni mali ya Mungu na hivyo sina budi kutazama mbinguni ili kumshukuru Mungu na kutolea yote kwa wengine wanaokuwa wahitaji.

Mkate wa kweli ni Yesu mwenyewe anayejitoa kwetu katika maumbo yale ya mkate na divai, katika Ekaristi Takatifu. Ni Yesu anayejitoa kwetu pia kwa njia ya Neno lake, ili lifanyike mwili na kukaa kati yetu. Yesu anakuja kwetu kwa namna ya pekee kabisa katika kila maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu katika Meza ya Neno na pili katika uhalisia na ukamilifu wote katika Meza ya Ekaristi Takatifu. Ni kupokea Neno lake na Mwili na Damu yake hapo njaa na kiu yetu inakamilika. Ni kukubali kuongozwa na mantiki ya Injili hapo dunia inakuwa mahali pazuri kwani kila mmoja anatambua hana budi kuwashirikisha wengine kwa huruma na upendo mema yote aliyopokea kutoka kwa Mungu. ‘’Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. Nao waliokuwepo walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto’’. Idadi ya wanaume elfu tano inawakilisha taifa lile la wanawaisraeli ambalo Yesu anafanyika mwili na kukaa kati yao na vikapu vile kumi na viwili ndio idadi ya mitume wale wanaotumwa na kutoka kueneza Habari Njema kwa watu wote, yaani jumuiya mpya ya waamini wakristo, ndio Kanisa la Kristo.

Kujaa kule kwa vikapu kumi na viwili ndio kusema daima Kanisa la Kristo halitakaa kutindikiwa na uwepo wa Kristo kwa njia ya Neno lake, Sakramenti na hasa ile ya Ekaristi Takatifu, na ndio maana Yesu mzima na kamili tunakutana naye katika maumbo yale duni kabisa ya mkate na divai katika Ekaristi Takatifu. Leo kama Kristo anavyotualika na kututaka sisi wanafunzi na wafuasi wake kuendeleza kuutenda muujiza ule wa kulisha makutano chakula kwa njia ya ukarimu wa kila mmoja, kila mmoja wetu leo anaalikwa kuwa na nafasi kwa ajili ya muhitaji iwe katika ngazi ya familia, jumuiya, vigango, parokia na majimbo yetu na Kanisa kiujumla. Ni kwa njia hiyo pekee hapo Yesu anaendelea kutenda muujiza ule wa kuona kila mmoja anakula na kushiba na hata kusaza. Yesu wa Ekaristi anayekuja na kuingia ndani mwetu atujalie nasi neema tunazohitaji ili kila mara kutambua kuwa ni wajibu wetu wa kuwaketisha watu na kuwapa chakula. Ni wajibu wetu kuiishi Injili na hapa matokeo yake ni muujiza mkubwa kama ule alioutenda Yesu miaka elfu mbili iliyopita. Nawatakia tafakari na Dominika njema.

31 July 2020, 13:48