Tafakari Jumapili 14 ya Mwaka A wa Kanisa: Yesu Mfalme wa Amani
Na Padre William Bahitwa, -Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 14 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (Zak 9:9-10) ni kutoka kitabu cha nabii Zakaria. Katika somo hili, Zakaria anatoa unabii wa kimasiha. Kipindi cha Zakaria ni kipindi kile ambacho Israeli imekwishatoka utumwani na imarudi sasa kuanza kujijenga upya kama taifa: inajenga upya hekalu na kujenga upya matumaini yake kwa Mungu. Ni kipindi ambacho Israeli haina tena mfalme kumbe nguvu yao na kitovu chao cha umoja na ustawi kilikuwa ni hekalu na katika matumaini kuwa siku zinakuja ambazo Mungu atamwinua masiha atakayewaongoza na kuwaunganisha kama tena kama taifa. Unabii wa Zakaria katika somo la leo ni kuwa masiha huyo atakayekuja atakuwa ni mfalme. Naye atakuwa ni mfalme mwenye haki, wa wokovu na mnyenyekevu. Kama alama ya unyenyekevu wake yeye atatumia punda.
Kwa kawaida wafalme walitumia magari ya farasi kuonesha nguvu zao za kivita na mamlaka. Mfalme masiha kutumia punda badala ya farasi ni alama kubwa sana ya unyenyekevu wake. Lakini pia kwa kuzingatia kuwa farasi walikuwa ni wanyama wa vita, uamuzi wake wa kutumia punda unaashiria kuwa masiha hatakuwa mfalme mwenye kuongoza kwa nguvu za kivita bali atakuwa ni mwenye kuongoza kwa upole na katika amani. Ni katika muungano na dhamira hiyo ya amani Zakaria anasema kuwa mfame masiha ataliondoa gari la vita liwe mbali na Efraimu na farasi awe mbali na Yerusalemu. Naye atawahubiria watu wake amani. Somo hili linatuonesha namna ambayo matumaini ya masiha yalisaidia kuihifadhi imani ya waisraeli hata walipokuwa katika nyakati ngumu za maisha yao. Linatuonesha pia kuwa amani ni mojawapo ya matamanio makubwa sana ya jamii tangu enzi na enzi. Utawala au uongozi unaojikita katika kulinda amani ya watu wake huacha alama njema ya kudumu kwani ni katika amani ambapo mafanikio mengine yote hujijenga.
Somo la pili (Rum 8:9, 11-13) ni kutoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika somo la leo, Mtume Paulo anazungumzia nafasi ya Roho Mtakatifu kwa wale ambao wamempokea Kristo. Anasema kuwa wale ambao wamekwisha mpokea Kristo hawapo tena chini ya utawala wa mwili kwa sababu Roho wa Mungu anakaa ndani yao. Anasisitiza kuonesha kuwa Roho huyu ana nguvu ya kuleta mabadiliko ndani yao kwa sababu ni Roho huyu huyu aliyemfufua Kristo kutoka mauti. Mtume Paulo anaelewa fika udhaifu wa ubinadamu pamoja na maelekeo ya mwili. Anachowaandikia Warumi katika somo hili ni kuwatia moyo wasiuangalie tu udhaifu wa mwili wala maelekeo yake bali wamkazie macho Roho wa Mungu aliye ndani yao ili wasiendelee kutawaliwa na matendo ya mwili bali yale ya Roho. Fundisho la Paulo kwa Warumi katika somo hili ni kuwa wasiyaangalie mambo hasi yanayoweza kuwakatisha tamaa au kuwarudisha nyuma katika maisha yao ya kumfuasa Kristo bali wajikite katika yale yaliyo chanya, yaani katika Roho Mtakatifu.
Injili (Mt 11:25-30) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Mathayo. Yesu Kristo ambaye ndiye ufunuo halisi wa Mungu baba. Ndiye aliyetoka kwa Baba na anashiriki umungu mmoja na Baba. Ni kwa jinsi hii anasema “hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana hupenda kumfunulia”. Yesu anaongeza kuwa ufunuo huu hauendi kwa wenye hekima na akili bali kwa watoto wachanga, yaani wale wanaojishusha na kujinyenyekeza mbele ya Mungu. Anapowageukia sasa hao walio watoto wachanga anawaalika akisema “njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kuelemewa na mizigo nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu mjifunze kutoka kwangu kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo. Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu mwepesi”. Yesu anapojitambulisha kuwa ni mpole na mnyenyekevu wa moyo anavuta taswira ya unabii wa Zakaria tuliousikia katika somo la kwanza. Zakaria alitabiri kuwa masiha ajaye hatatumia magari ya farasi bali atapanda punda na mwanapunda naye atawaongoza watu kwa upole. Kwa maneno hayo, Yesu anaukamilisha unabii wa Zakaria na ni kama anawatangazia watu kuwa yule masiha mlekuwa mkingoja sasa amefika. Na tazama kweli ni mpole na ni myenyekevu wa moyo naye atawaongoza watu wake kwa amani.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika hii ya 14 ya mwaka A wa Kanisa inatupatia nafasi nyingine ya kumfahamu Kristo ambaye tunamfuasa katika maisha yetu. Taswira ambayo masomo ya leo yanatupatia ni ya Kristo mpole, mnyenyekevu wa moyo na ambaye sheria yake ni upendo ili kuwapatia watu wake amani. Nabii Zakaria katika somo la kwanza amebeba matumaini ya waisraeli juu ya masiha. Kama tulivyoona katika ufafanuzi wa somo hilo, waisraeli walikuwa na matumaini makubwa juu ya ujio wa masiha, lakini hawakuwa na picha kamili kuwa huyo masiha atakuwa wa namna gani. Wapo waliotabiri kuwa masiha huyo atakuwa ni kuhani, wapo waliotabiri kuwa atakuwa ni nabii na wapo waliotabiri kuwa atakuwa mfalme au kiongozi wa kisiasa na ndiye atakayewaletea uhuru kamili wa kisiasa. Kwa namna fulani Zakaria anawaondoa polepole watu kutoka katika mategemeo ya kisiasa ya masiha anapowaambia kuwa masiha atakuwa ni mfalme wa amani na hatawaongoza kwa nguvu za kivita bali kwa upole.
Leo tunapata kusikia Kristo mwenyewe akithibitisha unabii wa Zakaria. Anajitambulisha kuwa ni mpole na mnyenyekevu wa moyo. Tena anapomshukuru Mungu kuwa mambo hayo amewaficha wenye hekima na akili akawafunulia watoto wachanga, anaonesha pia kwa mfano wa maisha yake kuwa yeye ndio wa kwanza kujifanya mdogo kama mtoto mchanga. Na amejifanya hivyo kwa unyenyekevu wake. Ndio maana amepata kumjua Baba fika kiasi kwamba hakuna amjuaye Baba ila Yeye. Mwisho anaalika wafuasi wake kujitiwisha nira yake. Nira ni lile jembe la kulimia ambalo kwa kawaida hukokokwa na ng’ombe wawili. Katika Biblia, nira inatumika pia kuwakilisha Torati, yaani zile sheria ambazo Mungu aliwapa Waisraeli kupitia Musa, sheria ambazo baadaye waisraeli waliziongeza zikawa nyingi kiasi cha kuwa mzigo kwao.
Yesu anatambua bado umuhimu wa Torati. Haiondoi bali anabadilisha kiini chake. Anawaambia wajitwishe nira yake ambayo ni laini. Haina uzito wa sheria bali ina uwepesi wa upendo. Nao wakikubali kuongozwa na nira ya upendo basi watapata raha nafsini kwani kama alivosema Mt. Augustino “palipo na upendo hakuna mzigo na hata kama ukiwepo basi na mzigo huo utapendwa”. Huyu ndiye Kristo tunayemwamini na kumfuasa. Kristo mpole na mnyenyekevu wa moyo, Kristo anayetualika tujitwishe nira yake ya upendo ili tuishi katika amani yake. Tuupokee basi mwaliko wake nasi tuziige na kuziishi tunu hizo katika maisha yetu.