Tafakari Jumapili 15 ya Mwaka A: Matumaini, Nguvu na Wokovu!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 15 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (Is 55, 10-11) ni kutoka kitabu cha nabii Isaya. Katika somo hili, Isaya anawahakikishia Waisraeli kuwa Neno la Mungu ni la kuaminika daima. Ni Neno la kweli na lina nguvu ya kutekeleza kile linachotangaza. Kihistoria, somo hili linarejea unabii ambao Isaya alikuwa anautoa wakati ambapo waisraeli walikuwa utumwani Babeli. Katika kipindi hicho Isaya aliandika kuwatia watu moyo na kuwaalika waitumainie nguvu ya Mungu inayookoa. Aliwatabiria mwisho wa utumwa na kurudi tena katika nchi yao. Mwisho wa unabii huo ndipo Nabii Isaya anatamka maneno haya tunayoyasikia katika somo hili la kwanza. Analifananisha Neno la Mungu na mvua ambayo ikishatoka mawinguni hairudi bure mpaka imeinyeshea ardhi na imechipusha vyote vimeavyo ndani yake. Na kama vile ambavyo mvua ikishatoka ni lazima idondoke chini, vivyo hivo na Neno la Bwana likishatoka kinywani mwake lazima litekeleze kile lilichoadhidi. Amawahakikishia kuwa unabii wa Bwana ambao ameutoa kwa hakika utatimia kwa sababu Neno la Mungu ni la kuaminika. Kwetu sisi tunaolikiliza Neno la Mungu leo tunavutwa kuwa na imani. Kuliamini Neno la Mungu na kuzitumainia ahadi zake kwetu kwani yeye ni mwaminifu na Neno lake lina nguvu ya kutekeleza kile anachoahidi.
Somo la pili (Rum 8: 18-23) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika somo la leo, Paulo anazungumzia hali ijayo ya wana wa Mungu. Kila anayempokea Kristo kwa ubatizo hufanyika mwana wa Mungu akishiriki pamoja na Kristo urithi wa ahadi za wana. Hili ni mojawapo ya malengo ya Paulo kuandika waraka huu kwa warumi. Kanisa la Rumi lilikuwa ni mchanganyiko wa wayahudi pamoja na wasio wayahudi ambao waliitwa watu wa mataifa. Wayahudi walijihesabu tayari kuwa wamekwishafanyika wana wa Mungu kwa sababu ya Torati ambayo Mungu mwenyewe aliwapa alipoingia nao Agano. Tutakumbuka kuwa Mungu alimpa Abrahamu ahadi tatu: uzao mwingi, kuimiliki nchi ya Kanaani na kuwa Yeye atakuwa Mungu wao na uzao wa Abrahamu watakuwa watu wake, yaani watakuwa watoto wake. Kumbe, ni katika Torati wayahudi waliona ukamilifu wa ahadi hiyo ya kufanyika wana wa Mungu. Paulo katika waraka huu anawaandikia watu wa mataifa kuwa wao hawahitaji kwanza kuishika Torati ili wafanyike wana wa Mungu. Wanachohitaji ni kumpokea Kristo tu.
Katika somo hili sasa anayajumlisha makundi yote mawili: Wayahudi na watu wa mataifa na kuwaonesha kuwa japokuwa kwa kumpokea Kristo wamefanyia kuwa wana, bado wanasubiri ukamilifu wa ufufunuo watakapokuwa wana kamili wa Mungu siku ya mwisho. Na wakati wakingojea hilo, viumbe vyote katika ulimwengu mzima unangoja kwa matumaini na shauku kubwa ukamilifu huo. Ni katika somo hili Paulo anaeleza waziwazi kuwa ukamilifu wa ufunuo uko mwishoni. Tukiwa hapa duniani bado tuko safarini. Hata tukiisha mpokea Kristo hatuwezi kujitapa kuwa tayari tumekwisha okoka. Bado tupo safarini kuuelekea wokovu mkamilifu siku ya mwisho. Ni mwaliko wa kuzidi kujitahidi katika njia tuliyokwishaianza na ni mwaliko pia wa kukoleza matumaini na shauku ya kuifikia siku hiyo kwa kutunza neema ya Kristo maishani.
Injili (Mt 13:1-23) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Mathayo. Ni kifungu ambacho kinafahamika kama Injili ya mpanzi. Tofauti na mifano mingine ambayo Yesu amekuwa anaitoa, huu anautolea ufafanuzi yeye mwenyewe. Anafafanua mbegu ni kitu gani, zie zilizoanguka kwenye njia maana yake ni nini hali kadhalika zilizoanguka kwenye miamba, kwenye miiba na hatimaye kwenye udongo mzuri. Ufafanuzi wa Yesu unaonesha wazi kuwa mfano huu unazungumzia Neno la Mungu ambalo kuhubiriwa kwake au kutangazwa kwake kunafananishwa na namna ambavyo mbegu zilikuwa zikidondoka kutoka kwa mpanzi. Uwezo wa mbegu kuchipua na kuzaa matunda ni ule ule kwa mbegu zote. Kinacholeta utofauti ni mahala ambapo mbegu hizo zinaangukia. Kwa mfano huo, Yesu anataka kuonesha kuwa Neno lake ambalo tangu kipindi cha Mitume hadi mwisho wa nyakati litakuwa likihubiriwa, lina nguvu ile ile ya kuleta mabadiliko katika mioyo ya watu. Utofauti unakuja tu kulingana na namna ambavyo mtu analipokea Neno hilo moyoni mwake. Yeye anayelipokea Neno na kulihifadhi katika moyo ulioandaliwa vema atapata matunda yake. Lakini yeye ambaye kwa kusongwa na mambo mengine au kwa kukosa msingi wa imani analipokea Neno, atachoka mapema, atakatishwa tamaa mapema, atakosa uvumilivu na ustahimilivu na mwishoni Neno hilo halitazaa matunda ndani yake.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika hii ya 15 ya mwaka A wa Kanisa inatupatia nafasi ya kutafakari kuhusu Neno la Mungu. Waraka kwa Waebrania unatufundisha kuwa “Neno la Mungu li hai, tenda lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga wenye makali kuwili ... tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo” (Ebr 4:12). Neno la Mungu ni nguvu yenyewe ya Mungu inayotekeleza kile inachotangaza. Ufunuo wa Neno hili la Mungu unapatikana katika Maandiko Matakatifu. Kumbe, anayesoma na kuyatafakari Maandiko Matakatifu hujiweka katika nafasi ya kushibishwa na Neno la Mungu. Kanisa linafundisha kuwa Mungu mwenyewe anazungumza kupitia Neno lake. Kila mara yanaposomwa Maandiko Matakatifu ni Mungu mwenyewe anayezungumza. Anaweza mtu kujiuliza, Maandiko Matakatifu yamejaa historia ya kale ya watu wa Israeli, Maandiko hayo yamejaa masimulizi ya yale aliyofanya Yesu na barua za mitume wake kwa mazingira hayo hayo ya kale, yote hayo yananizungumzia nini mimi katika wakati huu na katika mazingira haya niliyonayo?
Kujibu maswali hayo yafaa kukumbuka kuwa ni kwa njia ya masimulizi hayo tunapata kuona namna Mungu alivyohusiana na watu wake tangu alipoamua kujenga nao uhusiano wa pekee. Na mahusiano hayo aliyafanya katika mazingira ya kawada kabisa, mazingira ambayo watu hao aliowachagua walikuwa wakiyaishi. Ni kutoka hapo aliwaunda kuwa taifa lake na kupitia kwao akaufanya ulimwengu mzima kuwa watu wake. Ni hapo tunaona kuwa lengo la Maandiko Matakatifu sio kutoa masimulizi ya kihistoria bali ni kutoa ushuhuda wa ufunuo wa Mungu katika kuwaunda watu wake. Na hili halijakoma kwa watu wa kale tu bali linaendelea hadi nyakati zote kwa kuwa ni Mungu mwenyewe aliamua hivyo. Kwamba kama vile alivyohusiana na watu wa kale vivyo hivyo anaendelea kuhusiana na watu wa vizazi vyote kupitia Neno lake. Ndiyo maana Neno hilo limeendelea kutenda maajabu ulimwenguni vizazi hata vizazi; limekuza imani ya watu, limewafariji, limewaongoza, limewatuliza na limewapa mwelekeo wa maisha na limewaokoa wote walioliweka kama dira na mwongozo wa maisha yao. Tuzidi basi kulipokea Neno la Mungu. Tulisome kwa furaha na tulipende, tulitafakari na kulisali ili Mungu mwenyewe anayezungumza na kutenda kupitia Neno lake azidi kutuunda kuwa wanawe.