Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa: Ufalme wa Mungu ni sawa na hazina iliyositirika, lulu nzuri na juya linalotupwa baharini. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa: Ufalme wa Mungu ni sawa na hazina iliyositirika, lulu nzuri na juya linalotupwa baharini. 

Tafakari Jumapili 17 ya Mwaka: Ufalme wa Mungu: Ni Hazina!

Tafakari ya Neno la Mungu: Kristo Yesu leo anaufananisha ufalme wa mbinguni na hazina iliyositirika, lulu nzuri na juya lililotupwa baharini. Mifano ile miwili ya kwanza ni mifano pacha kwa maana kuwa inatoa ujumbe unaofanana kuhusu ufalme wa mbinguni. Ufalme wa mbinguni ni kitu cha thamani kubwa kiasi kwamba kila anayetambua hilo lazima auze vyote alivyonavyo ili kuupata.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Kwa Dominika tatu mfululizo sasa, Mama Kanisa anatualika kutafakari mifano ya Yesu inayozungumzia juu ya Ufalme wa mbinguni katika sura ya 13 ya Injili ya Mathayo. Hata leo kama Dominika iliyopita Yesu anatumia tena lugha ya mifano mitatu na hitimisho fupi zote ni juu ya ufalme wa mbinguni. Kristo Yesu leo anaufananisha ufalme wa mbinguni na hazina iliyositirika, lulu nzuri na juya lililotupwa baharini. Mifano ile miwili ya kwanza ni mifano pacha kwa maana kuwa inatoa ujumbe unaofanana kuhusu ufalme wa mbinguni. Ufalme wa mbinguni ni kitu cha thamani kubwa kiasi kwamba kila anayetambua hilo lazima auze vyote alivyonavyo ili kuupata. Kila anayeutaka ufalme wa mbinguni anaalikwa kuwa tayari pia kufanya maamuzi magumu hata ya kutoa sadaka ya yote mengine yasiyokuwa na umuhimu ili kuupata. Ni vema kuelewa mazingira ya nyakati za Yesu ili kuelewa lugha ya mifano anayotupa katika somo la Injili ya leo. Kwa watafiti wa mambo ya kale hata nyakati zetu ni kawaida wanapochimba kukuta ardhini au katika majengo ya kale baadhi ya vitu vya thamani kubwa vikiwa vimefichwa au kuachwa katika majumba hayo. Ilikuwa hasa katika mazingira hatarishi ya kutokea kwa vita, watu walificha pesa na vitu vyao vya thamani ili wanaporejea kutoka vitani au uhamishoni waweze kuvipata tena vitu hivyo.

Iliweza kutokea kuwa baadhi ya wamiliki wa mali zile kufariki au kushindwa kurejea tena katika makazi yao. Hapo wale walioyachukua majumba au hata mashamba yao waliweza kwa bahati nasibu kuzipata mali zile zilizofichwa kabla. Ilikuwa pia ni katika mazingira haya hata vibarua katika mashamba walipoajiriwa kulima mashamba walilima kwa uangalifu mkubwa wakiwa na matumaini ya kukuta au kupata mali zilizofichwa ardhini, ilikuwa karibu na bahati nasibu za nyakati zetu au leo wengi tunazitambua kama ‘’betting’’. Mfano wa hazina iliyositirika, inapatikana kwa bahati nasibu bila juhudi za pekee kutoka kwa yule anayeigundua. Mtu yule alipoiona akaificha tena na hapo akaenda kuuza vyote alivyonavyo tena kwa furaha na kurudi kuja kununua shamba lote.  Tunaposikia mara ya kwanza simulizi la mtu huyu tunabaki na maswali mengi na hasa namna yake ya kutenda. Kwa nini alipoiona ile hazina ya kwanza hakuichukua na kwenda nayo kwa siri bila ya mwenye shamba kujua?

Ni mantiki nzuri kuiiba kwa siri ili anufaike nayo, ila kwa nini anaificha tena na kwenda na kuuza alivyo navyo tena kwa furaha?  Maswali haya yanatusaidia leo kuweza kupata ujumbe wa somo la Injili ya leo. Mkulima au kibarua yule kwa kitendo cha kuificha tena na kwenda na kuuza vyote alivyo navyo ili kulipata shamba lote ndio hasa mantiki inayopaswa kukumbatiwa nasi katika maisha yetu kila mara tunapogundua hazina. Ni baada ya kuona kipande kile cha hazina anagundua kuwa si tu kipande kile bali ni shamba lote chini yake kuna mali nyingi na yenye thamani kubwa zaidi kuliko kuondoka na kipande kile tu tena kwa wizi, anafanya maamuzi ya haki ya kuuza yote aliyonayo ili anunue shamba lile kwa haki, shamba lile kwake ni la thamani kubwa kuliko yote aliyonayo na ndio maana anauza kwa furaha yote ili anunue shamba lile.

Kibarua anatambua thamani kubwa iliyopo kwa kununua shamba lile lote, anabaki na uhakika sio wa kuwa na utajiri kwa kipande kile tu bali hazina yote inayoweza kupatikana chini ardhini katika shamba lile. Ufalme wa mbinguni unatualika nasi kuuona kuwa ni wa thamani isiyosemekana na hivyo lazima kuuza mengine yote ili kuweza kuupata, kuwa na hakika nao lazima kuacha mengine yote yanayokuwa kinzani na ufalme wa Mungu. Mkulima yule anaiona hazina ile sio kwa juhudi zake bali kwa bahati nasibu, ndio kusema sio kwa bidii na juhudi zetu bali ni zawadi kutoka kwa Mungu mwenyewe. Siyo kwa mastahili yetu kila mara hatuna budi kutambua Ufalme wa mbinguni ni neema ya Mungu kwetu, ni zawadi inayotolewa kwetu kama mmoja anayepata kushinda ‘’bingo’’ au ‘’betting’’, ni Mungu anajitoa zawadi kwa mwanadamu hivyo itoshe kwetu kutambua thamani kubwa isiyopimika inayotutaka kuuza mengine yote ili kuupata. Kwa kila anayeugundua anapaswa kutoka kwa haraka na kwenda kuuza yote ili kununua shamba lile.

Hakuna muda wa kupoteza ila kutoka na kwenda kuuza ili tununue, kutoka na kukubali kuuza ndio kuachana kwa haraka na yale yote tunayojua kwa hakika kuwa yanakuwa ni kikwazo cha kuimiliki hazina ile ya thamani kubwa, yaani ufalme wa Mungu. Ni kuuza yote sio tu baadhi ya yale tunayoona tunapenda kuuza bali yote. Kuuza mawazo yetu, malengo yetu na mipango yetu, mambo yote tunayoyapenda sisi ili kuweza kuupokea mpango wa Mungu katika maisha yetu. Kuwaza na kutenda yote tukiongozwa na Neno lake kwa msaada wa Mungu Roho Mtakatifu aliye mwalimu wetu wa daima. Hivyo kila mara ili kuenenda kadiri ya ufalme wa mbinguni hatuna budi kuongozwa na Mungu mwenyewe. Mkulima yule hauzi yote ili anunue hazina na mwishoni arejee kununua tena yale ya mwanzoni bali anabaki na furaha kubwa kwa kuwa mmiliki wa shamba lenye hazina. Maisha ya ufuasi ni kukubali kufanya mabadiliko makubwa sio tu ya maisha yetu bali hasa namna zetu za kufiriki, ndio mwaliko wa kubadili vichwa vyetu ili tukubali kuongozwa na mantiki sio ya dunia hii bali ile ya mbinguni, ya Mungu mwenyewe.

Mtume Paulo baada ya kukutana na Kristo Mfufuka akiwa njiani kwenda Damasko kutesa wakristo anafanya naye maamuzi magumu ya kubadili mtazamo na maisha yake kwani amekutana na hazina, amekutana na lulu ya thamani kubwa. ‘’Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.  Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo’’ (Wafilipi 3:7-8). Mabadiliko makubwa anayofanya Mtume Paulo kwa hakika yanatuacha na mshangao na vinywa wazi ila kwa yule anayetambua thamani isiyopimika wala kuelezeka ya ufalme wa mbinguni. Ni hivyo pia kwa wale wasiokuwa na imani katika Kristo wanashindwa kuona thamani kubwa ya kukutana na Kristo mfufuka, anayetualika nasi kubadili namna zetu za kufikiri na hata kuenenda, kwa kukubali daima kuongozwa na Neno lake kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Kila aliyemwona mkulima yule akiuza yote aliyonayo kwa hakika kwa haraka haraka ni rahisi kuona kuwa ni mtu aliyechanganyikiwa na kupoteza mwelekeo wa maisha yake. Na hasa ukizingatia aina ya ardhi ya nchi ile takatifu ya jangwa na yenye mawe mengi. Ni yeye mkulima pekee aliyetambua kuwa anafanya hilo ili kulipata lenye thamani kubwa zaidi kuliko jambo au kitu kingine kile. Ni hivyo hivyo hata kwa Mtume Paulo, mtu aliyejulikana kuwa mfarisayo kweli kweli na zaidi sana mbobezi katika Torati na hasa Sheria za Musa. ‘’Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo alisema kwa sauti kubwa, Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia wazimu! Lakini Paulo akasema, sina wazimu mheshimiwa Festo. Ninachosema ni ukweli mtupu’’. (Matendo 26:24-25) Mtume Paulo anabaki kuwashangaza si tu watesi wake bali hata watawala wa Kirumi kwa jinsi alivyokuwa mtu mpya na mwenye ujasiri mkubwa katika imani yake kwa Kristo Mfufuka. Haogopi minyonyoro, gereza wala kifo, yupo tayari kuweka rehani maisha yake ili aupate ufalme wa mbinguni, ili aipate hazina na lulu ya thamani kubwa.

Kila anayegundua na kuitambua hazina na lulu ya thamani anabaki na furaha kubwa, kama ilivyokuwa kwa mkulima yule na hata mtume Paulo.  ‘’Basi furahini daima katika kuungana na Bwana’’. (Wafilipi 4:4) na pia pale anaposema ‘’Katika kuungana na Bwana nimepata furaha kubwa kwamba mwishoni mlipata tena fursa ya kuonesha kwamba mnanikumbuka’’ (Wafilipi 4:10) Mfano wa pili au mfano pacha kwa kuwa unatoa pia ujumbe unaokaribiana sana na huu wa hazina ndio ule wa lulu ya thamani.  Kwenye mfano wa hazina mhusika mkuu ni mkulima yule maskini au kibarua aliyelipwa ujira wake wa siku tu; hapa tunakutana na mfanyabiashara tajiri anayezunguka duniani kote ili kuisaka lulu ya thamani. Lulu ni madini ya thamani, hivyo wafanyabiashara matajiri tu waliweza kuzisaka na kuzinunua kwa gharama kubwa kama ilivyo hata leo kwa vito vya thamani kubwa. Tofauti na mfano wa hazina, mkulima alipata hazina ile kwa bahati nasibu na sio kwa juhudi wala bidii zake binafsi, haikuwa mastahili yake bali ni zawadi tu iliyogundulika kwa nasibu akiwa analima. Hapa mfanyabiashara anaisaka kwa juhudi na bidii kubwa kwa kuzunguka duniani. Hivyo hazina na lulu ni matunda ya bahati kama zawadi na pia ni matunda ya juhudi na bidii kubwa.

Mfanyabiashara ni ishara ya wale wote wanaosaka na kutafuta kwa bidi maana ya Maisha yao, ni wale wanaousaka wokovu na ufalme wa Mungu kwa juhudi zao. Ndio kusema mifano hii miwili inakamilishana ili kuweza kuuelewa ufalme wa mbinguni. Ufalme wa mbinguni kwa nafasi ya kwanza ni zawadi lakini pia kwa nafasi ya pili kila mmoja wetu lazima ajibidishe ili kuupata. Ni Mungu anajitoa kama zawadi, kama neema lakini nasi kwa upande wetu hatuna budi kukubali kujibidisha ili uweze kukua na hatimaye kutoa matunda katika maisha yetu. Neema bila juhudi zetu haiwezi kuzaa matunda, hivyo ni mwaliko kila mara kuipokea hiyo neema na kuifanyia kazi kwa kuiweka katika maisha yetu ya siku kwa siku. Mfano wa tatu ndio ule wa juya lililotupwa baharini na kukusanya samaki wa kila aina. Mfano huu unaendana na ule tuliousikia Dominika iliyopita wa ngano pamoja na magugu. Mfano wa juya unaakisi mazingira ya ziwa lile la Galilaya ambapo wavuvi walitumia wavu kuvua samaki na daima walipata samaki wa kila aina wanaoweza kuliwa na hata wale waliotambulika kama najisi kadiri ya mapokeo yao. (Mambo ya Walawi 11:10-11) Baada ya kuwavua wavuvi walipaswa wakiwa ufukweni kuwachambua ili kuwatenganisha samaki wasafi au wanaoweza kuliwa na wale waliojulikana kama najisi ili kutupwa.

Kadiri ya nyakati zile bahari ilikuwa ni ishara ya nguvu za yule mwovu, adui wa maisha na uzima wa kweli. Wanafunzi wa Yesu wanatumwa kuwa wavuvi wa watu, maana yake kuwatoa katika utawala wa yule mwovu, kutoka nguvu zake za kifo, ndio tamaa zetu mbaya, ubinafsi, na yote mabaya ambayo yanatuondoa katika mpango wa Mungu wa kuishi kama wana wake kweli, kwa kuongozwa na Neno lake kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Ufalme wa Mungu unatuvua kwa kututoa chini ya yale yote maovu na kutuleta kwenye mwanga, karibu na Mungu na jirani. Mazungumzo haya kati ya Yesu na wanafunzi wake yanahitimishwa kwa swali kutoka kwa Yesu mwenyewe: ‘’Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam.’’ (Mathayo 13:51-52). Ni swali analolifanya Yesu leo kwangu na kwako, kwa kila mmoja wetu. Ni swali kwa kila mmoja anayekutana na hazina, lulu ya thamani, yaani kwa kila anayekutana na Yesu Kristo Mfufuka na hasa kwetu tunaoshiriki kila Dominika na labda kila siku katika Meza ile ya Neno lake na katika maumbo yale duni ya mkate na divai, yaani katika Ekaristi Takatifu.

Je, tunatambua hazina na lulu tunayokutana nayo katika Neno na katika sakramenti takatifu ya altare? Katika jumuiya ya Kanisa na katika masakramenti? Ni wakati ambapo tunaalikwa kugundua hazina na lulu na kwa kwa hatua hiyo tu muhimu tutaona umuhimu wa kufanya maamuzi magumu kwa kuuza mengine yote na kununua kile kilicho na thamani ya kweli, thamani ya milele isiyokuwa na mwisho iwe katika maisha ya sasa na hata ya milele. Nawatakia takafuri na Dominika njema.

23 July 2020, 13:12