Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya XXI inakazia ungamo la imani kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya XXI inakazia ungamo la imani kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. 

Tafakari Jumapili 21 ya Mwaka A: Ungamo la Imani Kwa Kristo Yesu!

Kiri ya Imani: ‘’Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai’’. Petro anamtambua Yesu kuwa ni Kristo, kuwa Masiha, kuwa ni mpakwa mafuta wa Mungu, kuwa ni Mwana wa Mungu, kuwa ni Mungu, ndio kusema anakiri imani, anamkiri Yesu kuwa kweli ni Mungu. Jibu lake ni kukiri imani, anaungama imani ya kweli kwa Yesu kuwa ndiye Kristo, ndiye Bwana na Mkombozi wetu. Jibu makini

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama!Kaisaria-Filipo kwa sasa ndio ule mji unaojulikana kama Banyas, ambao zamani ulijulikana kama Paneas, yaani mji wa mungu Pan. Pan ndio mungu wa kipagani, mungu wa maji, misitu na uzazi. Ni mji uliojengwa chini ya mlima Hermoni, na hapo kuna chanzo au chemuchemu ya mto Yordani, unaotiririsha maji yake katika ziwa Galilaya na baadaye kuishia katika bahari ile mfu. Ni katika mji huu wapagani wa Galilaya walifika ili kumwabudu mungu wa uoto wa asili, mungu wa maji, mungu wa uzazi na ndiye huyo mungu Pan. Miaka 20 kabla ya kuzaliwa Kristo, Kaisari Augusto aliutoa mji huu kama zawadi kwa Herode mkuu ambaye naye alishaanza kujenga hekalu kwa heshima ya mungu Pan. Na baadaye Herode mkuu alimpatia eneo la mji huu mwanae Filipo, na ni Filipo aliamua kufanya makao makuu yake katika mji ule, na ndio maana ukaitwa ‘’Kaisaria-Filipo’’, ni jina lenye kubeba wahusika wawili kwa heshima yao mji ule ukapata kujengwa yaani Kaisari Augusto aliyeutoa zawadi na baadaye kujengwa na Filipo, aliyekuwa mwana wa Herode mkuu. Ni katika muktadha huu, yaani katika mji wa kipagani, tunaona Yesu alifika kule pamoja na wanafunzi wake na wakiwa pale akawapa mtihani mdogo. Yesu anawauliza swali lile lile moja lakini anapenda kusikia majibu kutoka makundi mawili tofauti. ‘’Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?’’ Ndilo swali la kwanza. Lakini lililokuwa gumu zaidi ni lile la pili; ‘’Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?’’.  

Jibu la swali lile la kwanza halikuwa gumu kwa Mitume kwani si wao waliokuwa wahusika wakuu au walengwa wa swali lile na badala yake wao kuwa wawakilishi tu wa majibu na mitazamo ya watu wengine. Na jibu lao linaonesha jinsi walivyomuona Yesu kama mtu mashuhuri kama Yohane Mbatizaji, Eliya, Yeremia au mmojawapo wa manabii wa kale. Kama nyakati zile hata leo kuna wengi wanaoishia kumtambua Yesu kama mtu wa pekee tu, wanashindwa kumtambua Yesu katika uhalisia wake. Hivyo Yesu anabaki ni mtenda miujiza, ni mtu wa pekee mwenye sifa za kipekee tu tofauti na wanadamu wa kawaida, labda hata baadhi yetu wahubiri ni mara ngapi tunamuonesha Yesu kama mtenda miujiza na maajabu kati yetu? Yesu leo anatambulika kirahisi na wengi kwa bahati mbaya sana kama mtenda miujiza, kama mmoja mwenye uwezo wa kipekee na hivyo kumkimbilia nyakati za shida tu. Yesu pia leo si tu anawauliza mitume wake bali kila mmoja wetu, ni swali kwangu na kwako kama wafuasi na marafiki zake Kristo. Mtume Petro anajibu kwa niaba yake na wenzake kuwa ‘’Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai’’.

Mtume Petro anamtambua Yesu kuwa ni Kristo, kuwa Masiha, kuwa ni mpakwa mafuta wa Mungu, kuwa ni Mwana wa Mungu, kuwa ni Mungu, ndio kusema anakiri imani, anamkiri Yesu kuwa kweli ni Mungu. Jibu lake ni kukiri imani, anaungama imani ya kweli kwa Yesu kuwa ndiye Kristo, ndiye Bwana na Mkombozi wetu.  Mtume Petro ametoa jibu sahihi kabisa kumhusu Yesu, na tunasoma jinsi Yesu mara moja anavyomsifu na kumuonesha kuwa jibu lile halikutokana na akili au uwezo wake wa kibinadamu bali kwa kufunuliwa na Mungu Baba. Imani sio matunda au matokeo ya juhudi zetu bali kwa nafasi ya kwanza ni neema, ni zawadi ya Mungu kwa mwanadamu, kwa yeyote anayekuwa tayari kuongozwa na Mungu mwenyewe kwa njia hasa ya Neno lake. Ni mwaliko kuwa nasi tunaalikwa kukiri imani na kuishi imani yetu sio tu kwa nguvu zetu bali daima kwa nafasi ya kwanza, kwa msaada wa Mungu mwenyewe. Imani ni kukutana na Mungu na kumruhusu aongoze maisha yetu.

Pamoja na kutoa jibu sahihi lakini bado picha ya Masiha aliyokuwa nayo Mtume Petro ni tofauti na mantiki ya kimungu, ni tofauti na ile ya Kristo mwenyewe na ndio maana Yesu anatambua hilo na kuwaonya wasimwambie mtu. Wasiseme kwa kuwa bado hawajaiva na kumtambua katika uhalisia wake. Bado wana safari ya kuifanya ili kupata kumwelewa Kristo na ufalme wake kuwa ni wa namna gani.  ‘’Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu’’. Yesu anamtambulisha kama ‘’Πετρος’’, (Petros). Labda hapa naomba niiweke wazi kuwa tafsiri inayotumika kama ‘’mwamba’’ inapotosha na basi tuchukue nafasi kuona maana hasa kusudiwa. Katika Agano Jipya tunaona anayetambulishwa kama mwamba, kama msingi na juu yake Kanisa limejengeka ni Yesu Kristo pekee. ‘’Hakuna mtu awezaye kuweka msingi mwingine badala ya ule uliokwisha wekwa, yaani Yesu Kristo’’ (1Wakorintho 3:11). ‘’Basi, nyinyi si wageni tena, wala si watu wa nje. Nyinyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu wa jamaa ya Mungu. Mmejengwa juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi. Yeye ndiye mwenye kuliunganisha jengo lote na kulikuza liwe hekalu takatifu kwa ajili ya Bwana’’ (Waefeso 2:19-21).

Na hata Mtume Petro mwenyewe kwenye Waraka wake kwa watu wote anawaandikia na kuwausia waamini wale wachanga katika imani yaani waliotoka kubatizwa na kuwaambia; ‘’Basi mwendeeni Bwana! Yeye ndiye jiwe hai lililokataliwa na watu; lakini mbele ya Mungu ni jiwe teule na la thamani kubwa’’ lakini pia mbele anawatambua waamini wote kuwa ni mawe pia ‘’Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya kiroho ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea dhabihu za kiroho zenye kumpendeza Mungu kwa njia ya Yesu Kristo’’. (1 Petro 2:4-6). Jina Petro kwa lugha ya Kiaramayo, lugha aliyozungumza Yesu mwenyewe ni ‘’Kefa’’ na kwa kweli halina maana ya mwamba bali ni jiwe la msingi linalotumika wakati wa ujenzi. Hivyo, mwamba pekee ambao juu yake Kanisa limejengwa sio Petro bali ni Yesu Kristo mwenyewe. Kefa ni jiwe lile la msingi ambalo kwalo mawe mengine yote yanapata kuwa pamoja. Yesu anamtambua Simon Bar-yona kama Petro, kama Kefa, kama jiwe la msingi ndio kusema ni jiwe kwa maana ya imani ile aliyoikiri Petro. Ni katika imani ile aliyoikiri hapo Kanisa linajengeka katika msingi huo, jiwe linalotuunganisha sote kwa mwamba ambaye ni Kristo mwenyewe.

Na ni kwa njia hiyo nasi tunaalikwa kuwa mawe hai, kuwa wenye imani hai na kutokana na imani sisi sote tunalijenga jengo moja yaani Kanisa, chini ya mchungaji mmoja ambaye ni Kristo Yesu. Kefa ni jiwe kwa imani ile aliyoikiri na ndio tunaona mpaka leo Baba Mtakatifu anabaki kuwa kiongozi wetu katika mambo yote ya imani na maadili, ni yeye anayepaswa kuliongoza Kanisa la Kristo katika umoja wa kiimani na mambo ya maadili na utu wema. Yesu anamuweka rasmi Mtume Petro kuwa ishara ya umoja wa Kanisa, akimfanya naye ashiriki katika kuwa jiwe la msingi kwa maana ya kutuunganisha sisi wengine wote na kuwa kundi moja yaani Kanisa na chini ya Mchungaji mmoja ambaye ni Kristo mwenyewe. Yesu bado anaendelea kutumia lugha ya picha na zaidi ya kumtambua kama jiwe anampa funguo. Funguo ni ishara ya mamlaka ya kiutawala, kimahakama na hata katika nyanja za utaalamu. Na ndio tumesoma katika somo la kwanza la leo, Eliakimu mtumishi wa Mungu anakabidhiwa funguo za nyumba ya Daudi mabegani mwake, akiwa yeye anafungua hakuna wa kufunga na anapofunga hakuna wa kufungua. Ni ishara ya mamlaka anayokuwa nayo Eliakimu. (Isaya 22:22)

Mtume Petro kwa kukabidhiwa funguo anakuwa pia ishara wazi ya kuwa kwa njia yake Kristo anafundisha, kuliongoza na kulitakatifuza kundi lake yaani Kanisa. Ni kwa njia ya Mtume Petro kama Kefa, kama wakili wa Kristo ulimwenguni anakuwa mgawaji wa mambo matakatifu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, ni kwa njia yake Neno la Mungu linahubiriwa na hata kupewa tafsiri inayokuwa sahihi na ndio tunaona mamlaka ya kufundisha katika mambo yahusuyo imani na maadili. Ishara na mgawaji wa upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote. Ishara hii ya funguo inapelekea pia ishara ya tatu, nayo ndio uwezo wa kufunga na kufungua. ‘’Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni’’. Labda yafaa pia tutambue tangu awali kuwa uwezo wa kufunga na kufungua haujakabidhiwa kwa Petro peke yake bali kwa jumuiya nzima yaani Kanisa. ‘’Nawaambieni kweli, mtakachofunga duniani kitafungwa mbinguni, na mtakachofungua duniani kitafunguliwa mbinguni’’ (Mathayo 18:18). Tunasoma pia katika Pentekoste ile ya Yohana, iliyofanyika siku ile ile ya ufufuko; ‘’Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa; msipowasamehe, hawasamehewi’’ (Yohane 20:23).

Kufunga na kufungua ni lugha yenye asili yake katika muktadha wa kisheria na kimahakama. Ni lugha ya kisheria ikiwa na maana ya mambo yaliyoruhusiwa kisheria na yale yaliyokatazwa na sheria. Hivyo marabi waliamini kuwa ni wao ndio waliokuwa na funguo zenye kufunga na kufungua mintarafu tafsiri za Torah, sheria za Musa. Ni wao walikuwa na mamlaka ya kuwafundisha watu juu ya sheria zile, nini kiliruhusiwa na nini kilikatazwa na sheria ya Mungu, kwani ni wao wenye uwezo na mamlaka ya kutafsiri sheria zile. Ni wao walikuwa na haki hiyo na hata ya kusema ni nani yupo sahihi na nani amepotoka kwa kwenda kinyume na matakwa ya kisheria, ni wao waliweza kusema nani ni watu safi kwa maana watakatifu na wale waliokuwa najisi yaani wadhambi. ‘’Ole wenu nyinyi waalimu wa sheria, kwa sababu mmeuficha ule ufunguo wa mlango wa elimu; nyinyi wenyewe hamkuingia na mmewazuia waliokuwa wanaingia wasiingie’’ (Luka 11:52). Ndio kusema lugha ile ilikuwa inaeleweka vema kwa wasikilizaji wa nyakati za Yesu. Ndio kusema Yesu anaonesha jinsi gani walimu wa sheria walivyotumia vibaya madaraka yao kwa kushindwa kuwaruhusu watu kumwendea na kumkaribia Mungu kwani walikosa kupata sura halisi ya Mungu, upendo na huruma yake.

Kwa njia ya Mtume Petro na Mitume wengine wote tunaona Yesu anawapa jukumu la kuwa wajumbe wa upendo na huruma ya Mungu kwa watu wake. Ni kuwa vyombo vya huruma na upendo wa Mungu hata katika siku zetu. Kama tulivyoona hapa juu katika Pentekoste ile ya Yohana, iliyotukia siku ile ile ya ufufuko; ‘’Pokeeni Roho Mtakatifu. Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa; msipowasamehe, hawasamehewi’’ (Yohane 20:22-23). Ndio kusema mitume wanapokea utume wa kuwa wajumbe wa msamaha wa Mungu, upendo wa Mungu, faraja ya Mungu, wakionya na kufundisha na kuliongoza kundi lile moja yaani Kanisa. Na ndio tunaona mpaka leo katika nyakati zile mitume kwa nafasi ya kwanza yaani maaskofu wetu na makasisi wanakuwa ni wagawaji wa huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya sakramenti ile ya upatanisho, sakramenti ya huruma na upendo wa Mungu kwetu. Yesu anawanyang’anya funguo zile marabi na waalimu wa sheria na leo anauchukua yeye mwenyewe. ‘’Mimi niliye mtakatifu na wa kweli, ambaye nina ule ufunguo wa Daudi na ambaye hufungua na hakuna awezaye kufunga, hufunga na hakuna awezaye kufungua’’ (Ufunuo 3:7). Na ndio hata leo iwe ni mitume au wasaidizi wa mitume kwa maana ya makasisi, wanabaki kuwa ni wagawaji wa matakatifu yatokayo kwa Mungu mwenyewe, wanabaki kuwa ni vyombo tu vya kugawa kweli za mbinguni, mtoaji wa neema na baraka hizo ni Mungu mwenyewe.

Tunapoungama dhambi zetu ni Mungu mwenyewe anatusamehe kwa njia ya makasisi kama vyombo vya huruma na upendo wake. Mtume Petro kwa kukabidhiwa funguo hawi mlinzi au mlinda mlango wa Paradiso wala mmiliki wa kuamua nani aingie na nani hapana. Mtume Petro anatambua kuwa yeye ni wakili tu wa zawadi za Mungu, si mmiliki wala mtoaji wa zawadi hizo, yeye ni mtumishi tu wa Mungu, na hivyo anadaiwa daima kuliongoza kundi kwa kuwa mfano hai na mzuri. ‘’Msiwatawale kwa mabavu hao waliowekwa chini ya ulinzi wenu, bali muwe mfano kwa hilo kundi’’ (1 Petro 5:3). Katika somo la Injili ya Jumapili ya XXI kwa namna ya pekee tunaona wajibu wa pekee anaokabidhiwa mtume Petro kama kiongozi wa mitume na Kanisa la Kristo. Ni Petro anapaswa kuwa kielelezo cha umoja wa Kanisa kwa kukiri imani moja. Nasi sote tunaalikwa kumtambua wakili huyu wa Mtume Petro kama kiongozi wetu na kupokea mafundisho yake katika mambo ya imani na maadili. Jiwe, funguo na uwezo wa kufunga na kufungua ni ishara kubwa za Kanisa la Kristo. Ni kwa njia ya Mtume Petro leo tunaona Papa akiendelea kuwa ishara ya umoja wetu katika kukiri imani kwa Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wangu, ni Mwana wa Mungu.

Ni kwa njia ya Papa hata leo tunaona akifungua mlango na kuwaelekeza watu wote kuingia katika nyumba ile ya Kristo yaani Kanisa, kwa kuwa chombo na mgawaji wa upendo na huruma ya Mungu, hivyo kutuonesha wote njia ile ya kuelekea uzimani, kuelekea maisha ya umilele, maisha yasiyo na mwisho. Na ndio tunaweza kuona mpaka Papa anabaki kuwa ni kielelezo namba moja katika upendo, ni yeye anayekuwa kiongozi wetu, mfano wetu wa upendo wa Mungu kwa watu wake iwe katika nafasi ile kama mwalimu, kiongozi na mtakatifuzaji. Niwaalike leo kwa namna ya pekee kumuombea Baba Mtakatifu ili adumu daima kuwa kielelezo cha imani yetu, pamoja naye maaskofu wetu na wasaidizi wao makasisi na mashemasi kama vyombo na wagawaji wa zawadi zile zitokazo mbinguni. Tuzidi kuwaombea ili watambue kuufanya utume huo kwa unyenyekevu mkubwa bila kujikweza na kujichukulia nafasi ya Kristo mwenyewe ambaye ndiye kichwa cha Kanisa. Nawatakia tafakari na Dominika njema.

20 August 2020, 14:08