Tafakari Jumapili 21 ya Mwaka: Msingi wa Kitume wa Kanisa
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 21 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (Isa 22:19-23) ni kutoka kitabu cha Isaya. Katika somo hili, Isaya anatoa unabii kwa mtu aliyeitwa Shebna. Huyu alikuwa ni mkuu wa nyumba ya mfalme. Somo hili linatuletea sehemu pekee ambapo Isaya anatoa unabii kwa mtu binafsi. Mara zote ametoa unabii wake au kwa Israeli nzima au kwa mataifa mengine ya kigeni. Katika unabii huu, Isaya anatabiri kuwa Shebna ataondolewa katika nafasi yake na nafasi hiyo atapewa mtu mwingine. Anapotoa utabiri huo, Isaya anatumia lugha ya picha ya ufunguo pamoja na maneno ya kufunga na kufungua. Lugha hii ya picha ya ufunguo inamaanisha mamlaka ya kutawala na maneno “kufunga na kufungua” humaanisha mamlaka ya kuhukumu au kutoa hukumu. Na Mungu mwenyewe anapotamka kwa kinywa cha nabii Isaya akisema nitaweka mabegani mwako funguo – au nitakupatia funguo – anajitambulisha kuwa ni yeye anayetoa mamlaka hayo katika himaya ya mfalme. Tendo hili linakuwa ni kielekezo cha Mungu mwenyewe kuamua kuamua kumpa mwanadamu mamlaka na uwezo wa kutenda kazi juu ya ndugu zake.Tendo hili Kristo atalifanya kwa Petro anapomweka juu ya Kanisa lake. Naye atampa mamlaka ya kutawala na ya kutoa hukumu akimwambia anampatia funguo za kufunga na kufungua.
Somo la pili (Rum 11: 33-36) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika somo hili, Paulo ahahitimisha mafundisho yake kwa warumi, mafundisho ambayo yalijikita kuelezea wokovu upatikanao kwa njia ya Kristo kwa ajili ya wayahudi na kwa wasio wayahudi. Kwa kweli fundisho hilo ambalo Paulo amekuwa analitoa lilikuwa ni gumu. Lilikuwa ni gumu kueleweka wa watu kwa sababu ni kama lililenga kubomoa msingi wa mapokeo yaliyokuwapo lakini pia lilikuwa ni gumu kwake yeye mwenyewe Mtume Paulo kulielezea kwa ufasaha na hapa na pale ilimbidi kutumia namna nyingi na tofauti tofauti kuelezea kitu kile kile kimoja. Hapa sasa anapohitimisha akakiri kuwa pamoja na jitihada zake zote kufafanua fundisho hilo bado ufahamu wa kibinadamu unafika mahala unakwama katika kuyapambanua mawazo na makusudi ya Mungu. Anasema maarifa ya Mungu ni makuu mno, hukumu zake hazichunguziki na wala njia zake hazieleweki. Kwa maneno hayo Paulo anakiri ufinyu wa ufahamu wa kibinadamu mbele ya mafumbo ya kimungu. Ni kwa sababu hii mafumbo ya kimungu mtu hapaswi kuyaendea kwa kutanguliza maarifa pekee au kwa kutafuta hoja kwa vipimo vya elimu zetu au ufahamu. Mafumbo ya kimungu, pamoja na akili na ufahamu, mtu hualikwa kuyaendea kwa imani. Ni imani inayoweza kufika pale ambapo akili na ufahamu wa kibinadamu haiwezi kufika. Tena ni imani inayoweza kuiangazia akili kupata hoja ya kuyapokea. Imani na ufahamu vinapaswa kwenda pamoja.
Injili (Mt 16:13-20) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo. Katika Injili ya leo Mtume Petro anamkiri Yesu kuwa ndiye “Kristo mwana wa Mungu aliye hai”. Petro anafanya ungamo hili la imani pale Yesu anapowageukia wanafunzi na kuwauliza “na ninyi mwanisema mimi kuwa ni nani”? Ilikuwa ni muhimu kabisa kuwa baada ya kumwelezea Yesu mwono wa watu juu yake, wao nao waoneshe mwono wao juu yake. Ungamo hili la imani ambalo Petro analifanya, Yesu anamwambia si matokeo ya ubinadamu wake bali ni matokeo ya ufunuo kutoka kwa Mungu. Hili linatuonesha kuwa imani ni zawadi kutoka kwa Mungu. Ni paji linalotoka juu ambalo ni Mungu pekee anaweza kuwajalia watu wake kwa ufunuo. Mwanadamu yeye huipokea tu zawadi hii pale anapofungua moyo wake na kuifungua akili yake kuangazwa na ufunuo huu. Yesu katika mafundisho yake yote hakuwahi kuwaambia wafuasi wake “itafuteni imani au jitahidini kujipatia imani” bali daima alisema “mwombeni Baba awaongezee imani – Mwombeni Baba awajalie imani” kwa maana imani ni fadhila ya kimungu, ni paji linalotoka kwa Mungu.
Katika nafasi ya pili Yesu anamwambia “wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu”. Kisha anamwambia atampa funguo za kufunga na kufungua. Chochote atakachofunga duniani kitakuwa kimefungwa na mbinguni na chochote atakachofungua duniani kitakuwa kimefunguliwa na mbinguni. Tunafahamu kuwa Petro halikuwa jina la huyu mtume. Aliitwa Simoni. Ni baada ya ungamo lake hili la imani, Yesu anambadilisha jina na kumwita Petro. Jina lenyewe Petro linamaanisha “jiwe dogo” kwa Kiswahili cha kawaida tungeweza kusema ni “kokoto”. Lakini jiwe hili dogo ambalo Yesu ameliona ni imani, analifananisha na jiwe kubwa kabisa, yaani mwamba ambao juu yake atalijenga Kanisa lake. Kumbe Yesu hajengi kanisa juu ya Petro kama mtume tu bali anajenga Kanisa juu ya Petro kama imani ambayo mtume huyu anaitoa. Kitendo cha kumbadilishia Mtume Petro jina kinakuwa tena ni kielelezo cha utu mpya ambao Petro anautwaa kwa ungamo lake la imani. Utu mpya unaoonesha pia hali yake mpya ya kuwa kiongozi wa imani. Yanarejea sasa yale Isaya aliyoyatabiri kuwa Mungu anamjalia mwanadamu mamlaka kwa kumpa funguo za kufunga na kufungua. Ndivyo Petro anavyopewa mamlaka ya kuwa halifa wa Kristo duniani kwa ajili ya kuiimarisha na kulinda imani ya kanisa.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya leo yanatualika tutafakari juu ya msingi wa kitume wa Kanisa. Katika ungamo letu la imani tunasali na kusadiki kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Kanisa ni la kitume kwa sababu limejengwa juu ya mitume na hii ni kwa maana tatu: kwanza, limejengwa na linabaki limejengwa juu ya msingi wa mitume, mashahidi waliochaguliwa na kupelekwa katika utume na Kristo mwenyewe. Pili linahifadhi na kuendeleza kwa msaada wa Roho Mtakatifu, mafundisho, na ile “amana nzuri” yaani mapokeo ya maneno ya wokovu liliyoyasikia kutoka kwa mitume. Na tatu kanisa ni la kitume kwa sababu linaendelea kufundishwa, kutakatifuzwa na kuongozwa na mitume mpaka hapo atakaporudi Kristo. Hili linaendela kufanyika kwa njia ya mahalifa katika utume wa kichungaji ambao ni maaskofu wakisaidiwa na mapadre katika umoja na halifa wa mtume Petro ambaye ni Baba Mtakatifu.
Tunapotayatakari haya tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya zawadi hii ambayo inaendelea kudhihirishwa katika uongozi hiarakia wa Kanisa. Kwa nafasi moja tuuombee uongozi huu katika ngazi zake zote ili usilegee katika imani. Tumeona katika Injili kuwa muungano wa ndani kabisa kati ya hierakia na Kristo mwenyewe ni imani aliyoikiri Petro. Hiarakia iliyothabiti na inayoshikilia imani itaendelea kulisimika kanisa katika mwamba imara usiotetereka. Katika nafasi ya pili sisi sote waamini ambao pamoja na hiarakia tunaunda kanisa moja na ambao chini yao tunaongozwa katika imani, tuombe kudumu katika upendo, ushirikiano na utii ili utume ule ambao Kristo ameliachia kanisa lake uweze kuendelea. Rej. KKK. 857.