Tafakari Jumapili 22 ya Mwaka A: Utukufu Umetundikwa Msalabani
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na kuyatafakari masomo ya dominika ya 22 ya Mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (Yer 20:7-9) ni kutoka kitabu cha Nabii Yeremia. Katika somo hili, Nabii Yeremia anamtolea Mwenyezi Mungu manung’uniko na uchungu ambao kazi yake ya unabii imemletea. Anamwambia Mwenyezi Mungu “umenihadaa nami nikahadaika” yaani umenidanganya nami nikadanganyika. Nabii Yeremia anaona amedanganyika kwa sababu ahadi ambazo Mungu alimpa alipomwita kuwa nabii zimegeuka kuwa kinyume. Sasa kila anayemwona anamcheka, neno analotangaza haoni kama linapenya katika maisha ya watu. Na hata yeye badala ya kupokelewa kama mjumbe wa Mungu anaonekana kituko machoni pao. Pamoja na manung’uniko hayo yote, pamoja na kukata tamaa, Nabii Yeremia bado anashangazwa na kitu kimoja. Anapoamua kuiacha kazi ya unabii na kupanga kutokuhubiri tena Neno la Mungu, anashindwa. Hawezi kujinasua kutoka katika utume wa unabii aliokwisha upokea na aliokwisha uanza. Kimwili amekata tamaa lakini bado kwa ndani Neno la Mungu linawaka na linamsukuma aendelee kulitangaza na kulishuhudia.
Somo la pili (Rum 12: 1-2) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika mpangilio wa Waraka kwa Warumi, sura hii ya 12 ambayo tunaisoma leo inafungua sehemu ya pili ya waraka, sehemu ambayo Mtume Paulo anajielekeza kutoa maonyo na maelekezo mbalimbali kuhusu maisha ya kila siku ya Wakristo wa Rumi. Leo anawaambia “itoleeni miili yenu kama sadaka hai na takatifu impendezayo Mungu”. Na tena anawaonya wasishawishike kuiga mitindo ya watu wa ulimwengu bali wao kama wakristo wazigeuze fikra zao, wamwelekee Mungu ili walitambue na kulitenda lililo jema, lililo kamilifu na lile linalofaa. Mtume Paulo anawaandikia maonyo haya akiyatambua fika mazingira ya Roma ya wakati huo. Huu ulikuwa ni mji mkubwa yalipokuwa makao makuu ya dola ya Kirumi. Ni mji ambao ulikusanya kila aina ya watu hivi kwamba, pamoja na maendeleo uliokuwa nayo, ulijikuta kuwa pia na mmong’onyoko mkubwa wa utu wema, maadili na uchaji. Mausia ya Mtume Paulo yalilenga basi kuwatahadharisha wakristo walioishi katika mji huu ili wasipoteze utambulisho wao wa kuwa wakristo na wasimezwe na mitindo ya wakazi wa mji huo. Somo hili linazungumza nasi pia ambao mazingira ya ulimwengu tunaoishi hayatofautiani sana na ya Roma ya wakati wa Mtume Paulo. Mwaliko ni uleule wa kutunza utambulisho wetu ili tusimezwe na mitindo ya sasa ya ulimwengu, tusimezwe na malimwengu
Injili (Mt 16:21-27) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo. Mtume Petro ambaye ni kitambo kidogo tu amekiri Yesu kuwa ndiye Kristo na ambaye Kristo mwenyewe amemwita mwamba ambao juu yake atalijenga Kanisa lake, sasa anageuka kuitwa Shetani. Tunasikia katika Injili ya leo Yesu anamwambia “rudi nyuma yangu Shetani maana wewe huyawazi yaliyo ya Mungu bali yaliyo ya wanadamu”. Karibu katika Israeli yote kulikuwa na mambo makubwa mawili yaliyowatatiza watu kumhusu Yesu. La kwanza lilikuwa ni kukubali kuwa Yesu ndiye Kristo, yaani Yesu ndiye Masiha yule aliyetabiriwa na ndiye Masiha aliyekuwa akingojewa kwa miaka mingi. La pili lilikuwa ni kukubali kuwa huyu Yesu ni Masiha atakayeteswa, yaani ataudhihirisha Umasiha wake na kuwaokoa watu kwa njia ya mateso na kifo Msalabani. Kwa Myahudi ilikuwa haiingii akilini kuchora picha ya Masiha mteswa. Ilikuwa ni fedheha na kashfa kubwa.
Mtume Petro alipomkiri Yesu kuwa ndiye Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, alivuka kizingiti cha kwanza. Lakini alishindwa kuvuka kizingiti cha pili cha kukubali kuwa itampasa Yesu kuingia katika mateso hadi kuuwawa na siku ya tatu kufufuka kwa wafu. Yesu anamkaripia na kutumia maneno makali hadi kumwita Shetani ili kurekebisha kasoro hiyo waliyokuwa nayo watu kumhusu. Ni hapa tunaona kuwa karipio hili la Yesu kumwita Mtume Petro Shetani sio lake peke yake. Ni karipio la wote ambao wanamwamini Yesu kuwa ndiye Kristo lakini bado hawataki au hawako tayari kumfuata katika njia ya mateso Kristo huyo wanayemwamini.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tafakari ya masomo ya dominika ya leo inachota ujumbe wake kutoka kwa maneno ya Yesu mwenyewe kama tulivyoyasikia katika Injili: “mtu akitaka kunifuata ajikane mwenyewe, ajitwike Msalaba wake na anifuate”. Yesu anatoa vigezo hivi vitatu kama muhtasari wa namna anavyopaswa kuwa na jinsi anavyopaswa kutenda kila aliye mfuasi wake. Nabii Yeremia, katika somo la kwanza, analetwa kwetu leo kama mfano wa namna ya kujikana mwenyewe. Manung’uniko yake, kukata kwake tamaa na hata kufikia hatua ya kutaka kuuacha utume wa unabii ni matokeo ya kutokujitambua kama mfuasi na mtumishi anayepaswa kujikana. Mtumishi hapaswi kujiweka katika ngazi moja na utume ambao Mungu amemwitia. Utume ambao Mungu anamwita mtu na kumpatia unazo njia zake na unayo malengo yake ambayo si mara zote yataendana na malengo ya yule aliyeitwa kuufanya. Na tena ni mtumishi anayebeba gharama za utume aliopewa. Gharama hizo anazibeba kwa kujikana, yaani kujisadaka na kwa kukubali atumike ili utume usonge mbele. Nabii Yeremia anatuonesha kuwa hata pale sadaka inapokuwa kubwa, mtumishi hapaswi kuukimbia utume alioupokea. Kama usemavyo msemo maarufu “bora punda afe lakini mzigo ufike”, ni muhimu kutambua kuwa ni utume ulio na kipaumbele kupita maslahi binafsi ya mtumishi.
Mtume Petro katika Injili analetwa kwetu kama mfano mintarafu kigezo cha kujitwika Msalaba. Petro kwa kumzuia Yesu asiingie katika mateso na kifo Msalabani ni kushindwa kukipokea kigezo cha pili cha ufuasi, yaani kujitwika Msalaba. Njia ya msalaba ni njia ngumu na tena yenye mateso na uchungu mwingi. Hakuna ambaye katika hali ya kawaida angaliichagua kama kungalikuwa na njia nyingine mbadala. Yesu anatudhihirishia kwa mara nyingine tena leo, kuwa mfuasi hawezi kuikwepa Njia ya Msalaba bila kugeuka yeye mwenyewe kuwa kikwazo kwa wokovu. Ni katika njia ya Msalaba ndipo unapolala wokovu. Yesu anatualika tuibebe misalaba yetu tumfuate akijua fika kwamba, ni misalaba hiyo hiyo ambayo kwa uhalisia ndiyo inayotubeba sisi kutufikisha katika wokovu anaotuitia. Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi na mafundisho yake juu ya maisha ya kila siku yampasayo mkristo ndiyo ufuasi wenyewe. Kisha kujikana na kisha kujitwika Msalaba, mfuasi anaalikwa kuyaweka katika maisha yake ya kawaida ya siku kwa siku yale anayoyaamini na kuyachuchumalia kwa sadaka na matumaini makubwa. Mwenyezi Mungu na atujalie neema katika juma hili na siku zote za maisha yetu ili tuweze kujikana na kujitwika misalaba yetu ili tumfuate mwanae Yesu Kristo kila siku ya maisha yetu bila kusitasita na bila kizuio.