Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa: Wazo kuu: Ufunuo wa wema, ukarimu na upendo wa Mungu Baba kwa waja wake! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa: Wazo kuu: Ufunuo wa wema, ukarimu na upendo wa Mungu Baba kwa waja wake! 

Tafakari Jumapili 18 ya Mwaka A: Ukarimu na Upendo wa Mungu!

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya 18 ya Mwaka. Alama ya juu kabisa ya huruma, ukarimu na upendo wa Mungu kwa waja wake ni Ekaristi ambayo muujiza huu umekuwa daima unaashiria. Yesu anakuwa ni wa kwanza kuwapa umati huo mikate, ishara ambayo ataikamilisha siku ile ya Karamu ya Mwisho ambapo anajitoa kama mkate hai unaoshibisha miili na roho za waamini wake.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 18 ya mwaka A wa Kanisa. Katika dominika hii, Kanisa la Tanzania linaungana na Kanisa lote ulimwenguni kuadhimisha siku ya Upashanaji Habari inayofahamika pia kama siku ya Mawasiliano duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni iliyoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 24 Mei 2020 sanjari na Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, ulipambwa kwa kauli mbiu “Nawe upate kusema masikioni mwa wanao, na masikioni mwa mjukuu wako” Sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Kitabu cha Kutoka:10:2. Maisha yanakuwa ni historia. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anapembua kwa kina na mapana kuhusu mwingiliano wa hadithi na kwamba, si kila hadithi ni hadithi njema. Kuna hadithi ya hadithi; hadithi iliyopyaishwa na hatimaye kuna hadithi inayoendelea kumpyaisha mwanadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao ukweli wa historia ya Habari Njema ya Wokovu

Somo la kwanza (Isa 55:1-3) ni kutoka Kitabu cha Nabii Isaya. Unabii anaoutoa Isaya katika somo la leo, unafanana namna na wale wauzaji wa vitu kwenye minada au masokoni. Wale wauzaji ambao katika siku ya soko hupaza sauti kuita wanunuaji – “njooni mjipatie hiki na hiki kwa bei nafuu”. Nguvu yao ya kuita wateja huiweka katika kusifia ubora wa bidhaa au unafuu wa bei. Isaya naye leo anatangaza – kila anayeona kiu aje kwenye maji. Njooni mnunue divai na maziwa bila fedha na bila thamani, yaani bure. Unabii huu maana yake ni nini? Tukianza na divai na maziwa, vitu ambavyo Isaya anavitaja kama mchuuzi tunagundua kuwa ni vitu vinavyowakilisha rutuba katika ardhi na uzazi katika wanyama. Katika ujumla wake vinawakilisha matunda na furaha ya nchi ya ahadi ambayo Mungu aliwaahidia. Jambo la pili ni kuwa Nabii Isaya anatangaza kuwa vitu hivi vyote vinanunulika bure, bila fedha na bila thamani. Ni nani sasa mwingine anayeweza kuwajalia watu wake matunda ya nchi ya ahadi tena bure kama sio Mungu mwenyewe? Ni hapa tunaona kuwa kumbe huyu anayetangaza anamwakilisha Mungu ambaye anawaalika watu wake kufurahia matunda ya nchi ya ahadi anayowapa.

Tukiyaangalia pia mazingira ya kihistoria ambayo unabii huu ulitolewa tunaona kuwa unabii huu ulitolewa wakati Waisraeli wakiwa utumwani Babeli. Wako mbali na nchi yao ya ahadi. Ni hapa tunaona kuwa kumbe ujumbe wote huu ambao Isaya anautoa ni ujumbe wa kuwaambia watu kuwa ukombozi wao umekaribia. Watarudi katika nchi yao na watayafurahia matunda yake kama Bwana alivyokuwa amewaahidia. Na watarudi bure, yaani wao hawapaswi kufanya chochote isipokuwa kuutegemea mkono wa Mungu utakaotenda kwa badala yao. Watanunua divai na maziwa bila fedha na bila thamani. Somo hili basi linaawalika Waisraeli kumtumainia Mungu. Nasi pia linatupa ujumbe huo huo wa kumtumainia Mungu. Wao Waisraeli walipelekwa utumwani Babeli kwa sababu walikosa kuweka tumaini lao kwa Mungu, wakatumaini nguvu za wafalme wao na uwezo wao wenyewe. Sasa wokovu wao unarudi kupitia pale pale walipokosa. Kama mwanzo waliadhibiwa kwa kukosa kumtumainia Mungu basi sasa wanaalikwa kuupokea ukombozi kupitia kumtumainia Mungu.

Somo la pili (Rum 8: 35, 37-39) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika somo hili tunakutana na mojawapo ya maneno maarufu ya Mtume Paulo. Ni maneno ambayo Mtume Paulo anaanza kujiuliza, “ni kitu gani kitatutenga na upendo wa Kristo?” kisha hapo anataja msururu wa mateso, mahangaiko na mengine mengi. Lakini hata baada ya kutaja orodha hiyo ya vitu vinavyoonekana vingeweza kumtenga mtu na upendo wa Kristo anarudi kusema hakuna kinachoweza kututenga na upendo wa Kristo kwa sababu katika yeye daima tutashinda. Mtume Paulo anapoandika sehemu hii, anajiweka na yeye kati ya Wakristo wa Roma. Hawa ni wakristo ambao walikuwa tayari wamekwishapitia mateso mbalimbali chini ya utawala wa dola ya kirumi. Walikwishafukuzwa Roma, walikwishachomewa nyumba zao na wengi wao kuuwawa na hata wakati huo ukristo haukuwa unatambulika kama ni dini. Walikuwa wanasali kwa kujificha kwenye mahandaki au nyumbani kwa siri na yeyote ambaye angejitangaza kuwa mkristo basi adhabu yake ilikuwa ni kuuwawa. Kumbe Mtume Paulo anapowaandikia maneno haya anawaandikia ili kuwatia moyo, wasikate tamaa ya kuiishi imani yao hata katikati ya magumu yote hayo kwa maana upendo wa Kristo juu yao ni mkubwa na hata kama watalazimika kuuwawa kwa ajili ya Kristo wasihofu kukikabili kifo na kumtolea Kristo ushahidi huo wa juu kabisa.

Somo hili linazungumza vizuri sana hata kwetu leo. Mateso na madhulumu kwa Wakristo hayajawahi kukoma. Yalikuwapo, yapo na yataendelea kuwapo hadi mwisho wa dunia. Kinachobadilika ni sura tu ambayo mateso hayo huwajia wakristo kulingana na wakati na mazingira waliyopo. Ni mwaliko wa kujifunga kibwebwe cha imani tukijua kwamba, hakuna hata wakati mmoja ambapo tutakuwa na ukristo wa mtelemko. Huenda tukifikia wakati huo, hautakuwa ukristo tena ule aliouanzisha Kristo mwenyewe na hapo tutakuwa tumetengeneza dini yetu nyingine. Twende nayo yote kama sehemu ya kutoka ushahidi kwa imani yetu tukitiwa nguvu na upendo mkubwa wa Kristo unaotuunganisha naye.

Injili (Mt 14:13-21) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo.  Katika injili hii, Mathayo anatupatia simulizi la muujiza wa Yesu kuwalisha watu zaidi ya elfu tano kutoka vipande vitano vya mikate na samaki wawili. Tunapoisoma injili hii katika muungano na masomo mengine ya dominika ya leo tunaona kuwa inabeba msisitizo fulani wa pekee. Kabla ya muujiza kuna mazungumzo kati ya Yesu na wanafunzi wake. Wanafunzi wanamwambia Yesu awaage watu waende kujinunulia chakula wenyewe. Yesu lakini hakubaliani na wazo hilo. Anawaambia “wapeni ninyi chakula”. Dhana hii ni ile ile ambayo tumeisikia katika somo la kwanza kwenye unabii wa Isaya. Isaya amewatangazia watu waje awape bure chakula: divai na maziwa. Na kama tulivyoona kuwa Isaya alikuwa anatangaza ahadi ya  Mungu kuwajalia watu wake mema yake basi Yesu naye katika injili hii anawataka mitume wake waendeleze ishara hiyo ya kuwa wagawaji wa mema ya Mungu kwa watu wake.

Alama ya juu kabisa ya wema huo ni Ekaristi ambayo muujiza huu umekuwa daima unaashiria. Yesu anakuwa ni wa kwanza kuwapa umati huo mikate, ishara ambayo ataikamilisha siku ile ya Karamu ya Mwisho ambapo anajitoa kama mkate hai unaoshibisha miili na roho za waamini wake. Ni Injili basi ambayo inatoa mwaliko si kwa Mitume tu bali kwetu sote tunaomfuasa Kristo kuwa wagawaji wa mema ya Mungu. Kuwa wagawaji na sio wauzaji kwa maana yeye mwenyewe alishasema mmepewa bure, toeni bure. Tujitolee muda wetu, vipaji vyetu, nafasi zetu na hata rasilimali zetu ili kwa njia hizo mema yake Mungu na mafumbo makuu ya wokovu yaweze kuwafikia wote, yaweze kuadhimishwa kwa ajili ya wote na yaweze kuwanufaisha wote.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News,  Maandiko Matakatifu katika dominika hii yanatualika tuutafakari ukuu wa wema wa Mungu kwetu sisi viumbe vyake. Katika kuadhimisha siku hii ya Upashanaji Habari duniani, Baba Mtakatifu Francisko ametupatia ujumbe  unaongozwa na maneno ya kutoka katika kitabu cha Kut. 10:2 “Nawe upate kusema masikioni mwa mwanao na masikioni mwa mjukuu wako” – Maisha hutengeneza Historia. Kupashana habari ni kushirikisha matukio. Matukio hayo mbalimbali huunda maisha, si tu ya wale wahusika wa moja kwa moja bali huathiri pia maisha kwa namna moja au nyingine, ya wale wanaoshirikishwa habari. Ni katika mtazamo huu, Baba Mtakatifu anakumbusha kuwa ili upashanaji habari uwe ni tendo la kujenga maisha basi habari zenyewe tunazoshirikishana ziwe ni zile zinazojenga. Sote tu mashahidi juu ya namna ambavyo vyombo mbalimbali vya mawasiliano, viwe binafsi au vya taasisi, vimeshiriki mara kadhaa kubomoa maisha ya watu  na maadili kwa ujumla badala ya kuyajenga.

Maadhimisho ya siku hii ya leo yaziamshe basi dhamiri zetu katika upande huo wa upashanaji habari. Tutambue uzito wa matokeo ya kile kinachoshirikishwa na kuzingatia daima maadili yake.  Katika siku hii pia ni vema kurejea mwaliko aliokwishawahi kuutoa Papa Mstaafu Benedikto XVI kuwa Wakristo tusiogope kutumia njia mbalimbali za mawasiliano ya kiteknolojia ili kuieneza imani yetu na ili kumtangaza Kristo. Tusipofanya hivyo, kwa wale walio na uwezo, tutakuwa tunapoteza fursa kubwa ya kutoa ushuhuda kwa imani yetu na kuna hatari mitandao ya mawasiliano ikabaki kuwa ni mahala pasipoijua hofu ya Mungu. Wema wa Mungu kwetu utuvute pia kuutangaza na kuushirikisha kwa wengine.

Liturujia J18
01 August 2020, 07:08