Tafakari Jumapili 20 Mwaka A: Uadilifu, Wokovu na Imani Thabiti
Na Padre Nikas Kiuko, Mwanza, Tanzania.
Karibuni katika adhimisho la Misa Takatifu, leo tunalikwa kuwa na imani thabiti kwa Mungu. Mwaliko huu tunaupata katika masomo tutakayo yasikia. Katika imani tunaweza kuwa na hofu ya Mungu, tukatenda haki na kujijengea tabia ya uaminifu katika maisha ya kilasiku kama Nabii Isaya anavyo tuonya (56:1,6-7) Somo hili linatufundisha kuwa jinsi gani Mungu atawaongoza wanyenyekevu hata kama watakuwa watu wamataifa kama wana imani atawaongoza katika mlima mtakatifu wa Mungu, atawapa maisha ya furaha. Anawahidi watu wa mataifa kuingia hekauni na kutoa dhabiu, sadaka na maombi yao. Lengo kubomoa ukuta wa utengano kati ya Wayahudi na watu wa mataifa ili kumaliza tofauti zao. Utabiri huu tunapata ukamilifu wake katika Injili ya Mathayo 15:21-28) Mama Mkaanani anamwamini Yesu. Na hayo yote tuna pata ujumla wake katika somo la pili Mtakatifu Paulo kuwa Mtume wa Mataifa, anawahubiria Mataifa ujumbe wa Mungu.
Leo Yesu anakutana na mama mwenye mahitaji makubwa katika maisha yake. Huyu mama mmkaanani tuliye msikia kwenye Injili la Mathayo, Mwinjili Marko 7:24-28 anasema alikuwa mzaliwa wa Ugiriki, mwenyeji wa Sirofoinike au Uyunani. Alikua chotala kati ya damu ya Siria na Foinike, alikuwa analelewa na babu yake huko Siria na baadhi ya ndugu zake wa Foenike. Hivyo alikuwa hana malezi sahihi au uhusiano wa karibu sana na ndugu zake. Hiyo ikasababisha malezi yake kuyumba na akapata ujauzito pasipo kutegemea. Mchumba aliye mpa mimba baada ya kumwambia nina ujauzito wako akakimbia. Huyo mama akawa anaishi peke yake, ndugu zake wakamtenga, akakosa msaada kutoka kwa watu wake wakaribu. Aliondolewa katika familia yake. Mara baada ya kujifungua mototo wake akawa anadalili za kifafa, akamtunza, akampenda, akamhudumia lakini majirani zake wakasema ni haki yake anastahili kupatwa na mahangaiko kama hayo.
Hakua na uchaguzi, hakuwa na mtu wa karibu, hakuwa na rafiki wa kweli wa kumwambia mambo yake, hakuwa na pesa ya kujikimu, akaanza kujihangakia mwenyewe. Tukumbuke alikuwa mpagani lakini alikuwa na miungu ya tamaduni yao ikashindikana. Aliposikia utume na mafundisho ya Yesu akaona ni namna pekee ya kumpeleka mtoto wake. Alisikia Myahudi anafanya miujiza, anaponya wagonjwa na mwenye mamlaka juu ya pepo (Luka 11:14-38) ikawa kimbilio lake. Yesu anamwambia imani yako imekuponya. Mwinjili Mathayo 15:21-24 anamwita mama huyu Mkaanani. (Mama mmoja Mkaanani akapaza sauti “Bwana, Mwana wa Daudi nionee huruma” Binti yangu anasumbuliwa na pepo.” Huyu mama alikuwa na amani kubwa kwa Yesu, alikuwa na binti yake anaye umwa, na alihangaika kwa muda sehemu mbali mbali bila kupata nafuu kwa mtoto wake, anasikia mafundisho na matendo ya Yesu katika utume. Anamkimbilia Yesu.
Mama huyu anatukumbusha mambo mawili katika maisha yetu ya kila siku. Kwanza kujali maisha ya watoto wetu, tujali afya za watoto wetu. Cha pili tuombe uponyaji wa kweli ndani ya mioyo yetu. Kama wazazi kuamini nguvu ya Mungu, nguvu ya Sakramenti za uponyaji na Neno la Mungu. Waisraeli walimtaka Yesu ashuhudie kama kweli ni masia na aonyeshe ishara mbali mbali zihusuzo umasia wake, lakini kwa mama mkananayo, mtu wa Mataifa anashuhudia kuwa Yesu ni Masiha na anaamini atamponya mwanae mwili na roho. Uhusiano na Mungu haupo katika kuzaliwa katika kabila moja, kuwa Myahudi bali kwa kushika imani, kuwa na imani dhabiti kwa Mungu. Injili inatukumbusha mtazamo wetu juu ya wenzetu, makabila mengine, mataifa mengine, juu ya imani zao. Kama wanaparokia tuna mahusiano mazuri na madhehebu mengine? Tuna shirikiana nao katika kuwaombea, kuwatembelea wakiwa wagonjwa au wamefiwa au wamefungwa au wakiwa wananjaa? Tukumbuke Yesu mwenyewe anasema katika hali kama hizo yeye yupo pamoja nasi (Mathayo 25:35-40)
Yule mama Mkaanani aliendelea kumwambia Yesu nisaidie mwanagu ni mgonjwa. Yesu akamwambia Mama imani yako ni kubwa kwa Mungu. Injili inashangaza wengi kwa Yesu kumsifia mtu wa mataifa kuwa na imani kubwa kiasi hiki, Wayahudi wamuige Mkaanani katika maisha ya kiroho, waige mfano wa mama mpagani katika kumfasa kristo. Tunakumbushwa kuwa Mungu haangalii kama mwanadamu anavyo angalia, sisi tunaangalia kabila, matukio ya mtu, tabia ya mtu, vionjo na matukio yake katika jamii, lakini namna gani mtu katubu na namna alivyo tubu huwa inabaki ni mtu na Mungu, Mungu hupokea wa wote wanao mrudia na kutaka waokolewe, Mungu ni mwenye huruma na mapendo anaona jitihada za mtu za kujirekebisha hata kama sisi tuna ona mdhambi kwa matendo yake kama katubu, kaungama na kumwamini Mungu anakuwa wathamani. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo, maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo (1Samuel 16:7)
Tujifunze kutoka kwa mama Mkaanani, ni mama kutoka katika kipato cha chini, maskini, sio Myahudi, hakuwa na nafasi ya pekee katika jamii yake, anamshangaza Yesu. Mama huyu anamshangaza Yesu kwa kutambua utume na mafundisho ya Yesu. Anamtambua Yesu kama ni pekee anaye weza kumponya mgonjwa wake. Anaomba kwa imani kuu. Tujiulize mimi na wewe mahusiano yetu na Mungu ni nyakati gani, za furaha, magonjwa au mahangaiko? Tudumu katika kusali. Changamoto za huyu mama zilikuwa nyingi, kutengwa na ndugu, kukosa msaada, lakini bado kupada Baraka za Mungu alihangaika. Yesu alikataa kwa sababu ya kwamba alikuwa sio Myahudi. Kwani ni Yesu alimpitisha tena katika njia ngumu kama hii katika imani yake, na Yesu likuwa mkali? Sababu moja wapo ni kwamba maandiko matakatifu wengi walipitia njia ngumu kuthibitisha imani yao. Ibrahimu alijaribiwa kiasi cha kumtoa mwanae wa pekee Isaka, (Mwanzo 22:2) Yakabo alipata changamoto nyingi (Mwanzo 32:22-32) Daudi alipambana na Golihati (1Samuel 17:4-10) Katika Injili Yesu amewajaribu wafuasi wake mara nyingi. (1Petro 1:7).
Imani yetu ni ya thamani kuliko dhahabu. Baada ya majaribu mototo akapona na mama akawa mfano wa kuigwa katika imani. Tudumu katika kusali. Mwinjili anataka kutuonyesha kuwa Wayahudi na Watu wa Mataifa wanaweza kupata upendo wa Mungu kwa njia ya imani. Tudumu kuishi imani yetu, Imani katika kuwatendea watu wote matendo mema, kuhudumiana, na kupenda. Tumsifu Yesu Kristo.