Tafakari Jumapili 20 ya Mwaka A: Wokovu wa Mungu Ni Zawadi!
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 20 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya domenika hii yanatufundisha kuwa wokovu ni kwa watu wote, lakini kwa sharti la kuzishika amri na maagizo ya Mungu na kumwamini Kristo aliyetumwa ili kutukomboa. Kumbe hakuna atakayeokoka kwa nguvu zake mwenyewe; ni Mungu tu anayeweza kutuokoa. Wokovu umefunuliwa kwa watu wote kwa njia ya Kristo; yeye aliyekusudia kweli kuupata, ataokolewa. Hakuna anayeweza kudai haki ya kuokoka; tunapata wokovu kwa njia ya upendo na huruma ya Mungu. Kusudio la Mungu ni kumwokoa kila mtu kama anavyosema Mtume Petro, Mungu hapendi mtu yeyote apotee, anataka kila mtu aongoke na kuokolewa (2Pet 3:9). Na matendo ya mitume yanaweka wazi Mungu hana upendeleo; mtu yeyote kutoka taifa lolote anayemcha na kutenda kwa haki anakubaliwa naye (Mdo 10:35).
Katika somo la kwanza Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya anawaonya waisraeli wakiwa utumwani kuwa kuwa wasipoongoka na kumrudia Mungu hawataokolewa. Waisraeli wakiwa ni Taifa teuli la Mungu walijua kuwa ni wao tu ndio wanaomjua na umfahamu Mungu wa kweli na Mungu ni wao tu na ndiye atakayewaokoa na adui zao wote. Ni kweli kuwa Israeli ni Taifa teule, lakini uteule wake haukuwa kwa ajili yake tu bali lilichaguliwa na kuandaliwa ili kumpokea Masiha mkombozi wa ulimwengu. Kumbe, wokovu ni kwa ajili ya watu wote ndiyo maana Mungu anasema; na wageni nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote. Hapa Kanisa kumbakumba linatabiriwa, Kanisa alilolianzisha Yesu, Kanisa linalowakumbatia wote wema na wabaya ili liweze kuwasaidia katika kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu ili nao wapate kuokolewa. Waisraeli pamoja na kuwa Taifa teule nao ili waokolewe wanapaswa kushika amri na maagizo ya Mungu ndiyo maana Mungu anawaonya akisema: shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. Kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu.
Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Warumi naye anasisitiza kuwa, ni mapenzi ya Mungu kwamba watu wote waokoke. Paulo pia anasisitiza ukweli kuwa Israeli kuwa Taifa teule la Mungu haikuwa tiketi ya wokuvu, bali walipaswa kushika amri na maagizo ya Mungu ili wapate kuokolewa. Lakini wokovu ni tendo la hiari kwa kuwa kila manadamu aliyeumbwa na kwa sura na mfano wa Mungu amejaliwa uhuru kamili na utashi. Ndiyo maana wayahudi walipokataa kuipokea habari njema habari njema ya wokovu, mlango ulifunguliwa kwa wapagani na kudhihirisha kuwa wokovu ni kwa wote wanashika amri na maagizo ya Mungu. Kumbe, ilikuwa mpango wa Mungu kwamba wokovu uwafikie wapagani yaani watu wa mataifa yote kwa njia ya taifa teule la Israeli. Kwa kuwa kwa uhuru wao waliikataa hii neema, vema siku itakuja wakati kinyume chake kitafanyika; wokovu utakuja kwa wayahudi kupitia wapagani yaani watu wa mataifa waliokubali kuwa wakristo. Jambo hili litakuwa la ajabu na kubwa kuliko kumfufua mtu aliyekufa kutoka wafu. Watu wa Israeli sasa wamekufa kiroho na siku moja watafufuliwa. Paulo anamalizia ujumbe wake kwa sentensi inayoeleza huruma na upendo wa Mungu; Mungu haondoi zawadi zake wala hatupilii mbali chaguo lake. Sisi sote tumekuwa mfano wa majaabu haya. Tutakapofika mbinguni kila mmoja wetu atafurahi kukiri; Bwana kama siyo huruma yako kuu nisingekuwa hapa.
Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo inakamilisha uaguzi wa nabii Isaya ya kuokolewa kwa watu wote. Yesu alipofika kando za pande za Tiro na Sidoni mahali ambapo walikaa wapagani watu wasio wa Taifa teule la Israeli anakutana na mwanamke mkananayo ambaye ni mpagani. Maneno ya Yesu kuwa si vyema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa katika sehemu ya injili hayana kusudi la kumdhalilisha huyu mwanamke wala hayaonyeshi ubaguzi wa Yesu bali kusisitiza nguvu ya imani katika wokovu wa mwanadamu na kuwafundisha mitume kuwa sio uteule wa Taifa la Israeli ndio utakaowaokoa bali ni imani. Ni imani ya mwanamke Mkananayo kwa Yesu iliyomfanya binti yake aponywe. Baada ya majibizano na huyu mwanamke Yesu anakiri wazi na kusema, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile. Huyu mwanamke Mkananayo alipaza sauti akisema, unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi bila kukoma, kwa msisitizo. Licha ya kuwa hakuwa Myahudi lakini alimtambua Yesu, kuwa Bwana na mwana wa Daudi. Kilio na kelele zake alizozitoa kwa msisitizo bila kuchoka wala kukata tamaa akiwa na imani kwa Yesu ziligeuka kuwa sala naye Yesu akamsikiliza na kumrehemu.
Kumbe, tunakumbushwa kuwa hata kama kwa ubatizo tuliteuliwa na kuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa tusiposhika maagano ya ubatizo wetu na kuyaishi, tuko sawa na Waisraeli na ukombozi utatupita pembeni. Ubatizo tu hautoshi, kuitwa mkristo tu haitoshi, tunapaswa kuuishi ukristo wetu, tunapaswa kuiishi imani yetu, tunapaswa kuzishika na kuziishi ahadi zetu kwa ubatizo. Wakati mwingine tunafikiria kuwa Mungu hasikilizi sala zetu na kukata tamaa na kuacha kusali na kuomba. Mfano wa mwanamke huyu mkananayo ni wa kuigwa kusali kwa kusisitiza bila kuchoka na wala bila kukata tamaa. Basi tumwombe Mungu ayatie nuru macho ya mioyo yetu, ili tumjue, tumpende na tumtumikie, atie mioyoni mwetu hamu ya kumpenda ili katika kumpenda katika mambo yote na kuliko yote, tupate ahadi zake tunazotamani kuzipata. Tumsifu Yesu Kristo.