Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili 20 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Kristo Yesu ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu wote. Wokovu ni zawadi ya Mungu kwa wote. Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili 20 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Kristo Yesu ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu wote. Wokovu ni zawadi ya Mungu kwa wote. 

Tafakari Jumapili 20 ya Mwaka A: Yesu Ni Njia, Ukweli Na Uzima!

Mwenyezi Mungu anataka kuwajumuisha wageni katika mpango wa kulijenga upya hekalu na tena wamwabudu na kumtolea sadaka. Katika Injili Yesu anaikosoa tabia na mwenendo wa Wayahudi wa kuwasukumia mbali wageni ili wasitumaini chochote toka kwa Masiha. Mtume Paulo anaonesha kuwa watu wa mataifa ni washiriki kwa imani yao katika ahadi za ukombozi. Wokovu na Imani!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 20 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (Isa 56:1, 6-7) ni kutoka kitabu cha Isaya. Somo hili linazungumzia kipindi cha kihistoria ambapo waisraeli walikuwa ndio tu wametolewa utumwani na wamerudi katika nchi yao ya ahadi. Wakati wa vita iliyowapeleka utumwani hekalu lao lilivunjwa na miji yao kuharibiwa vibaya sana. Kumbe sasa wanaporudi kazi yao kubwa ni kulijenga upya hekalu, kuijenga upya miji yao na pia wao wenyewe kujiunda upya kama taifa. Tangu mwanzo waisraeli walikuwa ni taifa ambalo halikutaka kabisa mwingiliano na watu wa mataifa mengine. Hao waliwaita wageni au watu wa mataifa. Hali hii ya kutokuruhusu kujichanganya na wageni ilikuwa katika ngazi ya kijamii lakini pia hata katika ngazi ya kidini. Unabii anaoutoa Isaya katika somo la leo unagusa kipengele hicho.

Mungu anatangaza kwa kinywa cha nabii Isaya kuwa katika kazi ya ujenzi upya wa taifa wageni nao watakuwa na nafasi. Anasema wageni ambao wanalicha jina la Bwana, wanaompenda na kumtumikia, Bwana atawaleta nao wawe sehemu ya taifa lake. Wao pia watashiriki kumtolea ibada hekaluni na sadaka watakazozitoa atazipokea. Hekalu linalojengwa ambalo ndio nyumba ya Bwana itakuwa kweli ni nyumba ya Bwana kwa ajili ya wote. Somo hili la leo linatuonesha namna ambayo Mungu amewafungulia milango watu wa mataifa ili washiriki nao kumtolea ibada hekaluni pake. Hii ni alama kuwa nao wanaitwa kuzishiriki ahadi zilezile za ukombozi ambazo Mungu alikuwa ameliahidia taifa lake teule. Ni katika taalimungu hii ya Nabii Isaya tunaona kuwa kitendo cha Mungu kuitwaa Israeli kama taifa lake teule hakikuwa ni kitendo mahsusi kwa ajli yao tu. Mungu aliichagua Israeli akaiunda kuwa taifa lake ili kwa njia yake aweze kuwakusanya watu wa mataifa yote, watu wa ulimwengu mzima katika kupokea ahadi zake za ukombozi.

Somo la pili (Rum 11: 13-15, 29-32) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika somo hili Paulo anarejea tena suala la ukombozi kwa waisraeli ambao walimkataa Kristo na hawakumpokea kama njia pekee ya wokovu wao. Kuna mambo mawili ambayo Paulo anayafafanua kutokana na hili. Jambo la kwanza ni kuhusu Agano ambalo Mungu alikuwa amefanya na Waisraeli. Agano hilo lilikuwa ni njia ya wokovu. Swali linakuja, waisraeli hawajampokea Kristo hawataokolewa, Je, hili halioneshi kuwa Mungu atakuwa ametengua ahadi ambazo alikuwa amewapa? Je, hapa Mungu hataonekana kuwa amekuwa kigeugeu? Paulo analijibu hili kwa kusema kuwa Mungu haoneshi kuwa kigeugeu na wala hawezi kutengua ahadi alizokuwa amewapa watu wake. Badala yake Mtume Paulo anawaonesha Waisraeli kuwa kutokumpokea Kristo ni kutokulishika Agano lile ambalo Mungu alikuwa amewapa. Anayelishika Agano hilo tunaloliita la Kale, hawezi kukosa kumpokea Kristo kwani Kristo ndiye ukamilifu wa Agano hilo. Wasiompokea Kristo hawawezi kuokolewa kwa sababu hawatakuwa pia wamelishika Agano. Suala la pili analolionesha Mtume Paulo ni kuwa Waisraeli sasa kwa kutokulishika Agano, ahadi za Mungu zimendelea kuwaokoa watu wa mataifa. Na kwa ufundi wa maneno ambayo pia ni tabia ya uandishi wa Mtume Paulo anasema kwa kuasi wa wayahudi ahadi zimehamia kwa watu wa mataifa, pale watakaporudi na kumkiri Kristo ulimwengu wote utakuwa umehama kutoka kwenye uasi kwenda kwenye rehema. Hapa pia Mtume Paulo anaonesha jinsi ahadi zake Mungu zilivyo kwa ajili ya wote.

Injili (Mt 15:21-28) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo.  Katika injili ya leo tunaona Yesu anafuatwa na mwanamke Mkananayo asiye Myahudi. Mwanamke huyu anamwomba Yesu kwa ajili ya binti yake aliyepagawa na pepo. Yesu anajibu “sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli”. Jibu hili ambalo Yesu analitoa linawakilisha ile iliyokuwa tabia ya asili ya Myahudi, kutokuruhusu mchanganyiko wa aina yoyote na asiye Myahudi. Na kutokana na asili hii wayahudi walijua kuwa hata masiha ajaye hatawapa nafasi wale wasiokuwa Wayahudi na atakuwa ni Masiha wa manufaa yao peke yao. Mwanamke huyo lakini anazidi kusisitiza na Yesu anaona huko kusisitiza kwake kuwa ni matokeo ya imani yake kubwa. Ni hapa kwenye imani ndipo Yesu anaonesha kutofautiana na pia kuirekebisha hiyo tabia ya asili ya Wayahudi. Anaonesha kuwa wote wana nafasi sawa mbele ya Mungu, Myahudi na asiye Wayahudi. Wote wanakubaliwa na Mungu na wote ni washiriki wa ahadi zake za ukombozi. Kigezo cha kuyapokea hayo yote si kuwa Myahudi wala kutokuwa Myahudi bali ni kigezo cha imani.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya leo yanatualika tutafakari juu ya “ukatoliki” wa Kanisa. Neno Katoliki linamaanisha kitu kilichoenea pote, kitu kilichokamilika na tena kinachowajumuisha wote. Kanisa, kama sakramenti ya wokovu, ni katoliki: limeenea pote ili kuwafikia wote, limekamilika kwa maana ya kuwa na uwezo wa kutenda kadiri ya asili yake na linawajumuisha wote bila ubaguzi wa aina yoyote na kuweka mbele yao wokovu ili kila mmoja aweze kuupokea kwa imani. Katekisimu ya Kanisa Katoliki (Rej. KKK 830-831) inatufundisha kuwa mantiki ya ukatoliki wa Kanisa ni Kristo. Kanisa ni Katoliki kwa sababu Kristo yumo ndani yake. Na kwa sababu hiyo Kanisa lina ukamilifu wa uwepo wa Kristo na uwezo wake. Hii ina maana kuwa linapokea toka kwake ukamilifu wa njia za wokovu kama alivyotaka Kristo mwenyewe.

Katika masomo ya leo tunaona pia msingi wa Kimaandiko wa ukatoliki wa Kanisa. Kwa kinywa cha Nabii Isaya Mungu anatamka kuwa kuwajumuisha wageni wasio wayahudi katika mpango wa kulijenga upya hekalu na tena atawafanya nao wapande hekaluni kumwabudu na kumtolea sadaka. Katika Injili Yesu anaikosoa tabia na mwenendo wa Wayahudi wa kuwasukumia mbali wale wasio wayahudi wasitumaini chochote toka kwa Masiha. Na Mtume Paulo katika waraka kwa warumi ambao ndio somo la pili katika dominika hii anaonesha kuwa watu wa mataifa ni washiriki kwa imani yao katika ahadi za ukombozi. Kuuishi mwaliko huu tunaopewa leo inatupasa kushuka chini. Kuliangalia kanisa si zaidi kama taasisi ya kiulimwengu bali kuliangalia kanisa mahalia tunapoishi na kuhusiana na wakristo wenzetu. Inaweza kuwa ni katika jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, katika vyama vya kitume, katika parokia au hata katika jimbo. Tunaweza kwenda mbele zaidi kuangalia pia hali katika mashirika ya kitawa na kati ya makleri:- tunauishi ukatoliki? Tunaujenga ukatoliki? Tunaudhihirisha ukatoliki? Tuiombe neema hiyo katika siku ya leo.

Liturujia Jumapili 20 Mwaka A

 

15 August 2020, 09:18