Tafakari Jumapili 24 ya Mwaka A: Msamaha Ni Mlango wa Uponyaji
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 24 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Katika maisha yetu ya kila siku kama wanadamu tunakoseana na kuwakosea wenzetu kwa namna moja au nyingine na hivyo tunaharibu uhusiano mwema na watu na na Mungu pia. Dawa pekee ya kurudisha tena hali ile njema katika nafsi zetu na kati yetu na watu na kati yetu na Mungu ni toba na msamaha. Ni kwa njia ya toba na msamaha wa kweli ndipo twaweza kufungua njia ya kumwendea Mungu. Huu ndio ujumbe wa masomo ya domenika hii unaotukumbusha wajibu wa kuwasamehe waliotukosea. Lengo ni kukamilisha ujumbe wa masomo ya domenika iliyopita yaliyotukumbusha wajibu na namna ya kuwasahihisha waliokosea ili waweze kumrudia Mungu. Leo tunakumbushwa wajibu wa kuwasamehe na sio tu kuwasahihisha bali pia kuwasamehe, na msamaha huu hauna kipimo. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira latueleza kuwa tunapaswa kuwasamehe wengine kwa kuwa hata sisi tunahitaji kusamehewa maana hatuko wakamilifu, tu wadhambi.
Yoshua bin Sira anauliza, mtu mwenye dhambi anawezaje kutumaini kusamehewa makosa yake na Mungu iwapo anatunza hasira, ghadhabu na kisirani moyoni mwake? Kwanza yampasa amsamehe jirani yake ili naye apate kusamehewa. Kumbe mwenye kujilimbikizia kisasi ataona kisasi kutoka kwa Bwana; hakika Yeye atamfungia dhambi zake. Kumsamehe jirahi makosa aliyokufanyia ni sharti la kusamehewa dhambi zako wakati utakaposali na kuomba msamaha kwa Mungu. Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Warumi anatueleza kuwa vile sisi sote tumekombolewa kwa kifo na ufufuko wa Kristo, basi sote tu mali ya Mungu. Yeye peke yake ni Bwana wetu. Hivi lengo la matendo yetu yote liwe katika kumpendeza Mungu. Na ili kumpendeza Mungu lazima kuwa na upendo kwa wenzetu kama Mungu anawapenda na kuwasamehe pale wanapokosea. Mtume Paulo anasisitiza kuwa sisi sote tunadaiwa na Mungu. Deni letu ni kubwa sana kiasi kwamba hakuna mtu mwenye matumaini ya kuweza kulilipa. Tunadaiwa na Mungu kwa kuwa vyote tulivyonacho katika maisha yetu ni vyake hata maisha yetu ni yake.
Na tukija katika ulimwengu wa roho, akili zetu ni zake, utashi wetu ni wake na karama tulizonazo ni zake. Kumbe hakuna tunacho na haki mbele za Mungu isipokuwa dhambi zetu tu. Lakini Mungu kwa upendo na huruma yake anatusamehe dhambi zetu kila tunapomuomba msamaha. Kumbe nasi tunapaswa kuwasamehe ndugu zetu waliotukosea kwa sababu Bwana ametusamehe makosa yetu. Huu siyo ushauri kutoka kwa Mungu bali ni amri na anatupa amri hii kama sharti la kutusamehe tena. Mtume Petro katika injili anamwuliza Yesu ni mara ngapi tunapaswa kuwasamehe ndugu zetu au jirani zetu wanapotukosea. Jibu la Yesu ni kuwa tuwasamehe daima bila kipimo. Sababu gani ni lazima sisi tuwasamehe jirani zetu? Kwa sababu sisi pia tunategemea daima msamaha wa Mungu. Maadamu sisi tu watoto wa Mungu, hatuna budi kuiga mfano wa Baba. Kusamehe ni sharti la sisi kusamhewa na Mungu kama yatuambiavyo maandiko matakatifu: Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehi, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu (Mk. 11:25, 26).
Lakini licha ya kuwa kuwasamehewe wengine ni sharti la sisi kusamehewa, lakini pia kusamehe kuna faida zaidi katika maisha yetu ya kila siku kuliko kutokusamehe. Msamaha na upatanisho huleta mahusiano mema na kukata mzunguko wa chuki, hasira na kisasi. Msamaha humnyang’anya adui silaha. Lakini tutambue kuwa sisi ni washiriki tu katika kutoa msamaha kwani mwenye uwezo wa kusamehe dhambi ni Mungu peke yake. Mafundisho na mang’amuzi ya mababa wa Kanisa na watakatifu na wasomi mbalimbali wanatufundisha faida nyingi zinazopatikana pale msamaha unapotolewa kutoka katika undani wa nafsi ya mtu. Msamaha ni afya, kusamehe ni utu, kusamehe ni uungwana, kusamehe ni upendo, kusamehe ni ukomavu kwani ni kufanya maamuzi, ukisamehe, unajiweka huru, ukisamehe unajiponya mwenyewe, ukisamehe, unajitakia mema, kusamehe ni kujipenda, kusamahe huimarisha roho ya kujitolea katika jamii, kusahamehe hupunguza uadui, kusamahe ni njia nzuri ya kujilinda na hasira, kusamehe hukufanya ujisikie vizuri mbele za Mungu, kusamahe huimarisha saikolojia yako, kusamehe hupunguza maumivu sugu, kusamehe ni kukaribisha uponyaji wa mwili na roho.
Kusamehe ni mlango wa uponyaji wa ndani na wa nje, kusamehe kunakufanya uwe na mwelekeo mzuri na mipangilio mizuri katika maisha yako, kusamehe kunaongeza siku za kuishi, kusamehe kunafanya chachu za mwili zifanye kazi vizuri na hivyo kupunguza magonjwa mbalimbali kama magonjwa ya moyo, tumbo na akili. Kusamehe ni kujifariji mwenyewe, kusamehe kunadumisha heshima, kusamehe ni njia nzuri ya kujua kinachofuatia, kusamehe ni namna ya kujisamehe mwenyewe katika mambo uliyowahi kuyafanya yakakuaibisha katika jamii yako. Kumbe tunaweza kusema kuwa msamaha maana yake ni kurudisha tena hali njema kati ya mtu na mtu kati ya mtu na Mungu kati ya mtu na jamii kurudisha upendo kurudisha amani kurudisha urafiki uliopotea. Kuna kuna faida zaidi kusamehe kuliko kutokusamehe. Lakini mara nyingi inakuwa ngumu kusamehe pengine ni kwasababu ya kutokomaa katika imani kukosa moyo wa sala au kuacha kabisa sala ya kweli itokayo moyoni, na moyo wa kutenda haki. Tukumbuke kuwa Yesu ni msamaha wa kweli. Tunachota kwake neema za kuweza kusamehe na kuiga mfano wake wa kusamehe. Yeye alikubali kutusamehe sisi dhambi zetu kwa kufa msalabani akisema: Baba uwasamehe kwa kuwa hawajjui watendalo.
Hivyo basi, sisi kama wakristo tunapaswa kuwa watu wa msamaha tukikumbuka kwamba msahama wa kweli hujengwa katika amri ya Mapendo. Ndiyo maana tunaweza kusema kuwa mtu akisema naomba unisamehe ni sawa na kusema naomba unipende. Mtoto akikosea na akamwambia mama yake, mama naomba unisamehe ni sawa na kumwambia mama yake, mama naomba unipende. Na mama akijibu nimekusamehe mwanangu ni sawa na kusema nakupenda mwanangu. Hii ndiyo dhana ya kusamehe inayoleta furaha ya kweli katika maisha yetu. Tukumbuke kuwa msamaha ni zawadi ambayo ikitolewa inakumbukwa na vizazi vyote. Ni zawadi ambayo Yesu aliwapa waliomtesa na kumtundika msalabani. Ni zawadi ambayo Stefano katika kitabu cha matendo ya mitume, aliwapa waliomua. Ni zawadi ambayo Papa Yohane Paulo II alimpa Ali Agca ambaye alimpiga risasi. Ni zawadi ambayo Mtakatifu Josephina Bakhita wa Sudani aliwapa waliomuuza utumwani. Basi nasi tujifunze kutoa msamaha ili tuweke kumbukumbu duniani na mbinguni.