Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 25 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Haki ya Wafanyakazi! Huruma na Upendo wa Mungu kwa watu wote! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 25 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Haki ya Wafanyakazi! Huruma na Upendo wa Mungu kwa watu wote! 

Tafakari Jumapili 25 ya Mwaka A: Haki, Huruma Na Upendo wa Mungu

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya XXV ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, inafafanua kuhusu haki za wafanyakazi zinazopaswa kwenda sanjari na huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake wote. Malalamiko dhidi ya huruma na wema wa Mungu ni kielelezo cha kukosa imani. Haki ya Mungu inafumbatwa katika neema, huruma na upendo usiokuwa na masharti kwa watu wote!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Haki za wafanyakazi leo ni kilio cha ulimwengu mzima. Na hata mataifa maskini zaidi duniani pia nao wanalia kwa kuwa mikataba mingi ni ya kinyonyaji na kandamizi.  Mtume Yakobo analia pamoja na wafanyakazi wanaonyonywa na kugandamizwa katika kipato chao: ‘’Hamkuwalipa mishahara watumishi waliofanya kazi katika mashamba yenu. Sikilizeni malalamiko yao! Kilio cha hao wanaovuna mashamba yenu kimefika masikioni mwa Bwana wa majeshi’’ (Yakobo 5:4). Mfano wa kwenye somo la Injili la leo, tunaona linatupa ugumu kuona haki ya Mungu ya kumlipa mmoja aliyefanya kazi kwa lisaa limoja tu sawa na yule aliyeshinda na kutumika siku nzima. Mfano tunaousikia leo ni vigumu kuweza kuuelezea kwa kutumia mantiki zetu za kibinadamu na ndio maana katika somo la kwanza la leo tunasoma: ‘’Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu, asema Bwana’’ Ni kutoka kitabu cha Nabii Isaya. Na bado maneno ya mwisho ya somo la Injili ya leo nayo yanatualika kutafakari zaidi ili kupata ujumbe kusudiwa na Bwana wetu Yesu Kristo. ‘’Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho’’. Kwa kweli ni katika maneno haya tunapata japo picha ya ujumbe wa somo la Injili ya leo.

Mfano wa somo la Injili la leo unajikita katika sehemu kuu mbili. Ya kwanza ni wakulima wanaoajiriwa katika mida tofauti ya siku lakini wote wakikubaliana ujira mmoja, na sehemu ya pili ni malalamiko kwa wale walioshinda siku nzima wakiwa kazini na kuona wanapokea ujira sawa na wale waliofanya kazi kwa lisaa limoja tu. Mara nyingi Yesu anapotumia lugha ya mifano au lugha ya picha tunaalikwa kutafakari na hasa kurejelea maana ya lugha ile wakati walipokuwa wanaandika Injili, yaani kurejelea nyakati na muktadha ule wa nyakati za Yesu mwenyewe. Nyakati za Yesu, Mafarisayo ambao walijihesabu kuwa ni watu wenye haki, walikwazika kumwona Yesu aliyetambulika kama Masiha, anawatangazia pia wokovu wadhambi, wale waliohesabika kuwa ni watu wa mwisho, watu wasio na haki, maana ni watu waovu na watenda maovu na hivyo kustahili adhabu ya milele. Kundi la wenye haki walilalamika, kulalamika katika Maandiko Matakatifu ni ishara ya watu wasio na imani.

Somo la Injili ya leo pia linaakisi uhalisia wa Kanisa lile la mwanzo, Kanisa lililokuwa wazi kuwapokea watu wa mataifa yote bila kujali tofauti zao. Yesu anawaalika kuwa wafuasi wake si tu Wayahudi bali hata watu wa mataifa waliohesabika kama wapagani, wadhambi kwa wenye haki. Agano la Kale lilijikita katika haki, wakati Agano Jipya limejikita katika, upendo, neema na huruma isiyo na masharti, zawadi kutoka Mungu na si haki au mastahili yatokanayo na matendo yetu mema. Ufalme wa Mungu sio tuzo ambayo mmoja anatunukiwa kwa kuwa ametenda matendo mema, sio malipo ya mastahili yetu bali ni zawadi itokayo kwa Mungu kwa yeyote anayekuwa tayari kuipokea. Ni Mungu anayetujalia wanadamu wote, ni zawadi itokanayo na upendo wa Mungu usio na mipaka wala masharti yoyote. Ni ukarimu wa Mungu kwetu bila kuangalia mastahili yetu. Ni wema wa Mungu unaomjali hata yule anayeanza kuingia shambani na kutumia saa ile ya jioni kabisa, karibu na mwisho wa saa ya kazi.

Kwa mantiki za kiuchumi na za kiulimwengu huu waliostahili ujira na hata malipo ya ziada ni wale waliotumikia siku nzima shambani wakivumilia jua na shuruba ya siku nzima, hivyo haikuwa sawa kuwalipa wale wa lisaa limoja sawa na wale waliotumikia siku nzima. Na ndio mikataba yetu tunayoingia na kuifanya: inaongozwa na kanuni ya haki na sio upendo. Leo Yesu anatualika kubadili vichwa vyetu, kuanza kuangalia mambo si kwa kutumia kanuni za dunia hii bali kwa kuongozwa na mantiki ya Kimungu, nayo ndio ile ya upendo juu ya kanuni nyingine zozote zile. Simulizi la Yesu katika somo la Injili ya leo, jinsi linavyotushangaza na ndio hapo nasi tunaweza kuchota ujumbe kusudiwa kama nilivyoanza kuonesha hapo juu. Juu ya haki ya Mungu kwetu wanadamu, juu ya mantiki ya Mungu inavyokuwa tofauti sana na ile yetu ya kibinadamu, vipimo na njia zetu ni tofauti kabisa na zake kama somo letu la kwanza la leo linavyosema, kutoka kitabu cha Nabii Isaya.

Ni wakati wa mavuno ya zabibu kutoka katika shamba la mizabibu. Ni wakati ambapo mwenye shamba alipaswa kufanya kila linalowezekana kutafuta vibarua au wakulima ili waweze kuvuna zabibu ili kuziepusha kuharibika, ni mavuno yanayofanyika kwa haraka na kwa wakati mmoja kwani zabibu zinakomaa kwa pamoja. Ni majira haya wamiliki wa mashamba waliwasaka wakulima wa msimu na kukubaliana nao ujira wa siku tu, au leo tungezungumzia wafanyakazi wanaolipwa ujira kwa masaa katika mashamba ya wakulima matajiri wakubwa au ndio wanaojulikana kama vibarua! Vibarua walipaswa kukusanyika katika sehemu za wazi mapema alfajiri na hapo wenye mashamba walifika na kuchagua aina ya wafanyakazi waliowahitaji katika mashamba yao kwa ajili ya kazi za kuvuna zabibu. Mwenye shamba naye alipaswa mapema kabisa kuanza kufanya maandalizi, mfano kuandaa vifaa vya kuwekea mavuno, kuandaa japo mikate ya kutosha na matunda ya mizeituni kwa ajili ya vibarua wake ili wale wakati wa mlo wa mchana. Hata walipofika kwa kufanya makubaliano ya masaa ya kazi na malipo, ilitosha maneno machache sana kwani malipo yalijulikana na karibu yalifanana kwa sehemu kubwa ya matajiri wenye mashamba. Vibarua walijua ujira wa siku, kwani ni ujira uliotosha na kukidhi mahitaji yao japo ya msingi kwa ajili yao na familia zao.

Kwa kuwa mwenye shamba alisukumwa na uharaka wa kumaliza kazi ile mapema, tunaona si tu anatoka mara nne kwa siku ili kusaka vibarua au wakulima ili kuweza kumsaidia kuvuna matunda kwa wakati kabla ya kuruhusu kuharibika. Alitoka mapema alfajiri, saa tatu, saa sita, saa tisa na hata saa kumi na moja ya jioni, wakati lilibakia lisaa limoja tu kabla ya kumaliza siku ya kazi hapo saa kumi na mbili jioni.

Mtu mwenye nyumba tunaweza kumfananisha na Mungu au Kristo; wakulima ni wafuasi, ambao kila mmoja anaitwa kwa wakati wake katika safari ya maisha ya kila mmoja wetu. Shamba ndio jumuiya ya waamini, yaani Kanisa (Ekklesia), ambamo daima kazi hazikosekani na sote tunaalikwa na kuitwa katika saa tofauti katika siku kwenda na kukusanya mavuno. Daima sote tunaalikwa na kuitwa kwenda kwa haraka, utume wa Kanisa daima ni wa haraka na kamwe sio wa kusuasua au wa kupoteza muda, kila mmoja wetu anaalikwa kwenda kwa haraka na kuunganika na jumuiya ya waamini ili kutangaza na kushuhudia makuu ya Mungu, kuwa mashahidi wa Habari Njema duniani kote, ili kukusanya mavuno ndio kuwaalika na kuwaambukiza wengine ufuasi na ndio imani yetu. ‘’Msichukue mfuko wa fedha, mkoba, wala viatu; msimsalimie mtu yeyote njiani’’ (Luka 10:4). Siku ndio safari ya maisha ya kila mmoja wetu na jioni ndio saa ile ya malipo, saa ile ya kukutana na hakimu mwenye haki.

“Usimdhulumu kibarua maskini na mhitaji, awe Mwisraeli au mmoja wa wageni wanaoishi katika miji yenu. Kila siku, kabla jua halijakuchwa, mlipe ujira wake wa siku hiyo, maana yeye ni maskini na huo ujira ni tegemeo la moyo wake; ili asije akamlilia Mwenyezi Mungu, nawe ukawa na hatia’’ (Kumbukumbu la Torati 24:14-15). Na ndio hapa tunaona Yesu katika mfano wakulima wanaitwa ili wapate ujira wao wa siku, kila mmoja dinari kuanzia na yule wa mwisho. Ni hapa labda hata tunapata maswali mengi, kama mwenye nyumba alitaka kuwalipa wote ujira sawa kwa nini basi hakuwalipa kwa siri, na tena kwa nini ameanza kuwalipa wale wa mwisho na hakuanza na wale walioshinda kazini siku nzima? Kwa nini mwenye nyumba anaanza kuwalipa wale waliofanya kazi kwa lisaa limoja tu na hivyo kuamsha hasira za wale waliochomwa jua siku nzima na kuvumilia kutumikia masaa karibu kumi na mawili kwa kuwapa ujira sawa tena kwa kuwafanya wasubiri kwanza kuwalipa wale wa lisaa limoja? Kwa nini anawafanya hawa wahuzinike kwa kuona waliofanya kazi kwa lisaa limoja wanapokea sawa na wao na tena anawatanguliza katika malipo wakati walifika mwishoni kazini?

Mwenye shamba alikubaliana na wale vibarua wa mapema alfajiri ujira wa dinari moja, na wengine ile itakayokuwa haki na wale wa saa ya mwisho hawakubaliani lolote zaidi ya kuwaalika nao kwenda na kufanya kazi katika shamba lake. Ni hapa matata na malalamiko yanazaliwa. Malalamiko yanazaliwa kwa kushindwa kumuelewa hasa nini haki kwa mwenye shamba. Vibarua wale walikuwa wanatumia mantiki na vipimo vya haki vya dunia hii wakati mwenye shamba anatumia vipimo na njia tofauti kabisa na zile zao, au zetu za ulimwengu huu. ‘’Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami dinari? Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe’’. Ndio jibu la Yesu kwa mmoja aliyekuwa analalamika baada ya kuona amepokea ujira sawa na yule aliyefanya kazi kwa lisaa limoja tu. Hii ndio namna ya Mungu ya kutenda ni namna inayotushangaza kwani haki ya Mungu ni kupenda bila masharti, kupenda bila mastahili, wokovu ni zawadi na sio malipo ya mastahili yetu, kwetu ni kufungua mikono na kuipokea zawadi hiyo.

Dini ya mastahili ni tofauti na mantiki ya Injili ya Yesu Kristo, na ndio maana nasi leo tunaalikwa kubadili vichwa vyetu, namna zetu za kufikiri na kuhusiana na Mungu. Hatutendi mema ili twende mbinguni kwani bado huko ni kujitafuta na kutenda kibinafsi, sisi tunaalikwa kutenda yote sio kwa ajili yetu bali kwa kuwa nasi tunapenda kama Mungu, tunampenda Mungu na jirani bila masharti, ni upendo pekee unaotufanya sisi kuwa wana wa Mungu na si kitu kingine chochote, hatutendi kwa sababu fulani fulani binafsi bali kwa kupenda bila sababu, ndio kupenda bila masharti. Mungu anamwita Abrahamu hata kabla hajawa na imani, anamuita angali bado mpagani, angali bado mtu wa mataifa. Wito wa Abrahamu sio kwa mastahili yake bali yote ni neema, ni zawadi itokayo kwa Mungu na Mungu anatuita na kutualika hata leo tuwe wafuasi na rafiki zake sio kwa sababu mimi na wewe ni watu wema, la hasha bali imani ni neema, ni zawadi itokayo kwa Mungu, ni Mungu anajitoa ili akutane nasi, ili liwe tukio la kubadili vichwa na namna zetu za kuenenda katika safari ya maisha yetu hapa duniani.

Upendo wa Mungu kwetu hautokani na wema au kazi zetu njema, ni neema, ni zawadi itokayo kwa Mungu bila masharti yoyote. Ni wenye njaa yeye anawashibisha na matajiri anawaacha waende mikono mitupu (Luka 1:53). Mungu hachoki kamwe kujitoa kwa mwanadamu, kuja na kukutana na kila mmoja wetu, ni sisi ndio tunamkataa na kujiweka mbali naye, tunakana mwaliko na upendo wa kukutana naye, mwaliko wa kutujalia neema zake, kwani imani ni neema, imani ni zawadi, ni Mungu anakuja kukutana na nafsi ya kila mmoja wetu. Dini ya mastahili ndio ile leo Yesu anatuonya kukaa nayo mbali, kubadili na kukata vichwa vyetu, kwani ndio ile iliwafanya wakulima na vibarua wale kuanza kulalamika. Kulalamika kama nilivyotangulia kusema ni ishara wazi ya kukosa imani, hivyo wakulima na vibarua wale walioshinda siku nzima wakifanya kazi walikosa imani, imani ya kweli inaonekana katika upendo, katika kumtakia mema mwingine bila kuangalia mafao au masilahi au faida binafsi. Imani ya kweli ni kupenda kweli kweli, ni kupenda bila masharti.

Na ndio ulikuwa mtazamo wa kifarisayo, mtazamo wa dini ya mastahili kwa wale tu waliokuwa wanashika amri za Mungu kiaminifu siku zote za maisha yao. Wenye imani ni wale wanaopenda kweli, ni wale wasioona wivu kuona na wengine nao wanajaliwa neema ya Mungu, kila mara kama moyoni mwangu nawaka wivu kwa kuona mwingine naye anapokea wokovu, anapokea neema dakika ya mwisho, ni ishara kuwa ndani mwangu bado nipo mbali na Mungu. Kila aliye mfuasi kweli wa Kristo ni yule anayejifunza kupenda kama Kristo mwenyewe, ndiko kupenda bila masharti, ni kwa kukubali tukue tu katika upendo hapo kweli tunakuwa wafuasi na rafiki zake Kristo. Tuwake moto wa upendo na kuona tunaalikwa nasi kuwaalika wengine wawe karibu na Kristo, washiriki furaha ya kuwa na Kristo bila kuanza kujihesabia haki wala mastahili. Kuitwa mapema sio kupata ujira mdogo bali kufurahia kukaa na Yesu pamoja naye kwa safari nzima ya maisha yetu, hivyo hatuna budi baada ya kukutana na Yesu nasi tusukumwe na hamu na shauku ya kuwashirikisha wengine furaha hiyo.

Mwinjili Mathayo leo anatualika hata nasi waamini wakristo kuwa macho na mtazamo wa dini ya mastahili, dini ya mafarisayo, dini ya kuishi kwa mashindano kati yetu, dini ya kuoneana wivu na hata kuchukiana na kutokutakiana mema. Hata mmoja wetu asijione kuwa bora kuliko wengine, mwenye mastahili kuliko wengine, mwenye haki kuliko wengine, kwani hicho ni kishawishi ambacho kinaweza kuwepo hata katika maisha yetu ya kuwa wafuasi wa Yesu Kristo. Sisi sote hatuna budi kujitambua kuwa hakuna hata mmoja wetu ambaye ni mwenye nyumba bali sote ni wakulima, ni vibarua tunaoitwa masaa tofauti katika mwendo wa siku nzima ya kazi. Mfano wa Yesu wa leo unakosa hitimisho kama mfano wa yule Baba Mwenye huruma. Luka 15:11-32. Mwana mkubwa aliporejea hakuona kwa nini baba yake amefanya sherehe kubwa kwa ajili ya ndugu yake ambaye kwake alimuona ni mzinzi na mpenda starehe, aliyetapanya mali za urithi kwa kwenda na kuzitumia hovyo, hakuona kama ndugu yake mdogo alipaswa kutendewa yale kwa kuwa hakuwa anastahili.

Leo tunaona jinsi anavyotupenda na kututhamini sio kwa mastahili yetu, bali kwa kuwa Yeye anatupenda bila masharti, anatupenda na kutuhurumia bila masharti, na ndio upendo wa Mungu unaotushangaza na kutuacha na bumbuwazi. Mfano unakosa hitimisho kwani hatusikii zaidi nini kilijiri baada ya malalamiko yao, Je, walimrudishia mwenye nyumba dinari ile, au walimtupia usoni, au walimtusi au walimalizana vipi vibarua wale na mwenye nyumba? Ni maswali ambayo labda majibu yake sio ya muhimu sana kwani ujumbe ni mwaliko wa kuona haki ya Mungu ni katika kupenda bila masharti. Nawatakia tafakari na Dominika njema.

19 September 2020, 08:00