Tafakari Jumapili 25 ya Mwaka A: Udumifu, Toba na Wongofu!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na kuyatafakari masomo ya dominika ya 25 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (Is 55:6-9) ni kutoka kitabu cha Nabii Isaya. Somo hili linatujia kutoka katika sehemu ya tatu ya mpangilio wa kitabu cha Nabii Isaya. Sehemu hii ya tatu inahusu unabii uliotolewa katika kipindi ambacho Waisraeli wamerejeshwa kutoka utumwani Babeli na wanaanza kuijenga upya Israeli. Katika kuijenga upya Israeli na katika kuanza upya kujiimarisha kama taifa, nabii Isaya anawakumbusha umuhimu wa kuanza upya na Bwana. Anasema “mtafuteni Bwana kwa maana anapatikana, mwiteni kwa maana yeye yu karibu”. Kwa maneno haya, nabii Isaya anarejea ujumbe ule wa mzaburi kuwa kama Mungu asipoijenga nyumba basi mwanadamu anajisumbua bure. Yote yaanze na Mungu, na kwa baraka zake yatafikia utimilifu wake.
Katika somo hili Nabii Isaya anawaalika Waisraeli kuisahau historia yao mbaya na upotevu wao wa kiimani uliosababisha wakapelekwa utumwani na hivyo anawaalika wamrudie Mungu. Wamrudie kwa matumaini na toba kwa maana njia zake Mungu sio sawa na za binadamu, Yeye atawapokea na kuwasamehe na kuendelea kuwafungulia baraka zake katika maisha mapya wanayoyaanza. Kwetu sisi leo, somo hili linatukumbusha mojawapo ya sifa kuu ya Mungu nayo ni ile ya kumpa daima mwanadamu nafasi nyingine ya kuanza upya, nafasi ya kurekebisha mapungufu katika maisha na kumpa tumaini jipya la kumrudia kwa toba na wongofu. Njia zake sio sawa na zetu, mawazo yake sio sawa na yetu, tumtafute na tumrudie Bwana Mungu wetu, Mungu yupo na anapatikana kwa wote wanaomtafuta. Ni Mungu wa huruma na haki.
Somo la pili (Waf. 1:20-24,27) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi. Mtume Paulo anauandika Waraka huu akiwa kifungoni Roma. Mtume Paulo anajua wazi kuwa kifungo chake kinaweza kuwakwaza waamini wa Filippi aliowahubiria Injili. Alijua kuwa wangeweza kuwaza na kusema “kama injili aliyotuhubiria huyu mtu ni ya kweli, kwa nini sasa amefungwa na yuko gerezani? Na Kama huyo Kristo anayemhubiri ana nguvu, kwa nini hakumpigania asifungwe?” Ni katika muktadha huu anawaandikia katika somo la leo kuwa Kristo anaendelea kuadhimishwa iwe ni kwa kifungo, au kwa uzima au hata kwa mauti. Kristo hawezi kuadhimishwa katika sehemu au nyakati fulani fulani tu za maisha ya watumishi wake. Maisha yote ya waamini wake yanamwadhimisha na kumtukuza Kristo iwe ni katika hali njema au hali ngumu za maisha. Mtume Paulo anatualika nasi tuutwae msimamo wake “Kwangu mimi kuishi ni Kristo na kufa ni faida kwake” Tuziondoe hofu za maisha, hasa zile hofu zinazotuzuia kujitoa kikamilifu kwa Kristo.
Injili (Mt 20:1-16) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo. Inahusu bwana mwenye shamba la mizabibu ambaye alitoka katika nyakati mbalimbali za siku kwenda kualika watendakazi katika shamba lake la mizabibu. Simulizi lenyewe lipo katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ndiyo hiyo ya kuajiri watendakazi na sehemu ya pili ni ya malipo kwa watendakazi hao. Awali ya yote ni muhimu kuzingatia kuwa katika Agano la Kale, shamba la mizabibu ni lugha ya picha inayomaanisha taifa la Israeli (Rej. Is 5, 1-7 na Yer 12:10). Yesu anapozungumzia shamba la mizabibu anarejea na yeye kuzungumzia taifa hilo hilo lakini anaenda mbali zaidi kuzungumzia taifa pana zaidi la waana wote wa Mungu wanaoitwa kuunda Israeli mpya.
Mmiliki wa shamba ni Mungu mwenyewe ambaye anawatafuta wote kuingia katika taifa lake. Wale wanaoajiriwa alfajiri ni wale ambao wanaupokea mwaliko huo wa Mungu mapema na bila kusitasita. Baadaye wakafuata wale wa saa 3, saa 6 saa 9 na hata saa 11 jioni. Hawa ni wale ambao ama hawakupewa mwaliko mapema au walipopewa hawakuwa tayari kuupokea hadi hapo ulipofika wakati wao. Ulipofika wakati wa kupokea ujira, kila mmoja alipewa dinari moja. Hiki kilikuwa ni kiwango sahihi kwa wafanyakazi wa kutwa. Wale waliofanya kazi kutwa nzima hawakupunjwa na wale waliofanya kazi saa moja hawakupendelewa. Wote waliupokea ukarimu ule ule wa bwana mwenye shamba.
Mfano huu unatukumbusha kuwa katika maisha kila mmoja wetu anao wakati wake wa kuupokea na kuuitikia mwaliko wa kimungu. Na tukiangalia vizuri, hakuna anayewahi na hakuna anayechelewa. Hii ndiyo maana wote walipewa ujira mmoja. Mfano huu unakazia kuonesha kuwa tangu wakati ule ambao mtu anapokea mwaliko huo wa imani basi ajitahidi adumu hadi mwisho. Kati ya wale waliopewa ujira hakuna aliyefanya kazi kidogo halafu akakomea njiani. Wote walifika hadi muda wa mwisho wa kazi wakastahili kupewa ujira wa kazi waliyofanya.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika ya XXV ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa yanatupatia tafakari kuhusu mwaliko ambao Mwenyezi Mungu anampatia kila mmoja wetu kuingia katika ufalme wake. Na tunapozungumzia ufalme wa Mungu hatumaanishi tu lile tuzo la utakatifu ambalo tunategemea kulipata baada ya maisha ya hapa duniani. Yesu mwenyewe ameonesha kuwa ufalme wa Mungu huanzia hapa duniani kwa kuitikia mwaliko wa kuishi katika neema ya utakaso tukiyafuata mashauri ya Injili. Tunaalikwa katika dominika ya leo kutambua kuwa ili kuingia katika ufalme huo ni wajibu wetu kumtafuta Bwana.
Tumtafute kwa toba na wongofu wa ndani maana yeye anapatikana. Yupo kwa ajili yetu, hajifichi uso wake mbele ya nafsi inayomtafuta kwa moyo mnyofu. Yesu anatuonesha pia kuwa ni Mungu hasa anayewatafuta watu wake. Kumbe kumtafuta Mungu ni kujiweka katika hali ya kuwa tayari kupatikana pale ambapo Mungu anatutafuta. Kumtafuta Mungu ni kuwa tayari kuupokea kwa ukarimu mwito wake na kumtafuta Mungu ni kuwa tayari kudumu katika imani na wito hadi kustahili kupokea tuzo ya kuingia katika ufalme wake. Yesu anasisizita fadhila hiyo ya kudumu pale anaposema wapo walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza na wapo walio wa kwanza watakaokuwa wa mwisho. Haitoshi tu kuupokea mwaliko wa Mungu, kuipokea imani na wito, bali kuuishi mwaliko huo hadi ile jioni ya maisha yetu.