Tafakari Jumapili 25 ya Mwaka A: Wema Wa Mungu Hauna Mipaka!
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 25 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya domenika hii ni kuwa Mungu yu karibu na watu wake siku zote na nyakati zote na kila amwitaye humsikiliza na kumwomba humpatia mahitaji yanayomtosha bila upendeleo. Somo la kwanza kutoka Kitabu cha Nabii Isaya linatufundisha kuwa Waisraeli, walipelekwa utumwani Babeli kama adhabu kwao kwa kukosa uaminifu kwa Mungu. Baada ya kutambua ukubwa wa dhambi yao iliyowapeleka utumwani walikata tamaa na kufikiri kuwa Mungu hawezi kuwasamehe na hivyo wakakosa kabisa matumaini ya kurudi tena nyumbani katika nchi yao. Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya anabatilisha mtazamo wao kwamba mawazo yao ya kibinadamu sio sawa na yake akisema; mawazo yangu si mawazo yenu na njia zangu si njia zenu. Kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
Nabii Isaya anawaambia Waisraeli na anatuambia sisi pia; mtafuteni Bwana maadamu anapatikana, mwiteni maadamu yu karibu, mtu asiye haki aache uovu wake, amrudie Bwana, naye Bwana atamrehemu na kumsamehe kabisa uovu wake na kumhesabia haki ya kupata wokovu. Kwani daima Mungu yu karibu nao wanaotubu na kumrudia Yeye kwa moyo wote, kwa maana Mungu hatendi kama binadamu atendavyo. Kumbe katika shida na mahangaiko yetu hatupaswi kukata tamaa na kusema kuwa Mungu yu mbali nasi hatusikilizi bali tumtafute naye anapatikana, tumwite maadamu yu karibu atatusikiliza, lakini kwa sharti kuwa kama tutaziacha njia zetu mbaya na mawazo yetu maovu tukamrudia, Yeye ataturehemu na kutusamehe. Katika somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi, Mtume Paulo anatufundisha kwamba tunaposongwa na matatizo, tufanye lile tuwezalo huku tukijiweka chini ya maongozi yake Mungu na si kukaa na kulalamika tu. Yeye Mtume Paulo alipokuwa gerezani aliyaacha yote mikononi mwa Mungu akisema kuwa iwe ni kuishi au kufa yote ni sawa kwake maadamu Kristo atukuzwe. Huku ni kuonyesha ukomavu wa hali ya juu ya imani ya Mtume Paulo kwa Kristo ambayo nasi pia tunaalikwa kuwa nayo tukijikabidhi waziwazima kwa Mungu hakuna litakalotushinda.
Katika Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 20: 1-16, Yesu anafundisha kuwa wema wa Mungu upo kwa watu wote hata kwa wakosefu wanaotubu, kinyume kabisa na mafundisho ya Mafarisayo waliofikiri wokovu ni kwa ajili ya taifa teule la Israeli tena kwa wale wanaoshika amri tu. Hii inatufanya tufahamu kwamba namna ya kufikiri na kutenda kadiri ya ubinadamu wetu ni tofauti kabisa na Mungu. Yesu anamfananisha Mungu na mmiliki wa shamba la mizabibu anayewaajiri watu kufanya kazi katika shamba lake kwa muda tofauti tofauti, lakini mwishowe anawalipa wote kwa ujira sawa. Hii ni tofauti kabisa na uelewa wetu sisi wanadamu ambapo malipo anayolipwa mfanyakazi ni lazima yalinganishwe na uzoefu wake wa kazi, kiasi cha kazi na muda aliotumia kufanya kazi. Kadiri ya desturi ya Kiyahudi, ilipofika jioni ilikuwa ni lazima mtu alipwe kwa kazi aliyoifanya.Tunasoma hivi katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 24:14-15: Usimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni nduguyo Mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu. Mlipe ujira wake kila siku kabla ya jua kutua, kwa sababu yeye ni maskini na anautegemea ujira huo. La sivyo, anaweza kumlilia Bwana dhidi yako, nawe ukapata hatia ya dhambi.
Na kiwango ambacho mtu alilipwa ilipaswa walau kimsaidie mtu kupata mahitaji muhimu ya kutwa na denari moja ndiyo iliweza kutumiwa na kukidhi mahitaji ya siku. Ndiyo maana mmiliki wa shamba la mizabibu alipatana na wale waliokubali kufanya kazi katika shamba lake kwa kuwalipa denari moja kwa kila mmoja wao. Lakini katika simulizi la Yesu, walioajiriwa mapema walimnung’unikia mwajiri wao kwa kuwalipa kiwango sawa na wale waliofanya kazi kwa mda mfupi, ambapo kimsingi wanaolalamika hawana sababu kwa kuwa haki yao wameipata kadiri ya makubaliano kwamba watapokea dinari moja. Fundisho tunalopata katika mfano huu ni wema wa Mungu hauna mipaka. Mungu yu karibu na watu wake na anawatendea wote kadiri ya mapenzi yake. Mfano huu unatuonyesha pia ubaya wa dhambi ya unafiki. Mtu mnafiki ni yule ambaye anachosema ni kinyume na anachotenda. Ni mtu anayejiona kuwa mkamilifu. Haoni makosa yake, anaangalia tu makosa ya wenzake. Kwa vile anajiona mkamilifu haoni makosa yake, hatubu, hasamehewi na mwisho hawezi kupata wokovu. Dhambi hii ni kikwazo kwa ukombozi wa mwanadamu.
Mfano huu pia unatuonesha kuwa kuingia katika ufalme wa Mungu kunategemea huruma ya Mungu na si jitihada ya mtu binafsi tu. Kwa maneno mengine, mtu hawezi kudai haki ya kuurithi ufalme wa Mungu kwa kushika sheria tu. Kuingia katika ufalme wa Mungu ni zaidi ya kushika sheria. Ndiyo maana kijana tajiri alipomwendea Yesu na kumwuliza nifanye nini niweze kupata uzima wa milele, Yesu alimjibu shika amri. Naye akijibu nimezishika tangu ujana wangu. Yesu akamwambia nenda ukauze vyote ulivyo nanyo uwape maskini nawe utakuwa na hazina mbinguni kisha njoo unifuate. Yule kijana akaondoka kwa huzuni. Kumbe kushirika sheria tu haitoshi. Mwanadamu hawezi kudai haki ya kuupata uzima wa milele kwa kushika sheria tu kwani hana mastahili hayo. Mastahili ya kuurithi ufalme wa Mungu yanatokana na huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika kutimiza waji wa kila mbatizwa kuzishika amri na maagizo ya Mungu na kuiishi amri ya mapendo kwa maneno na matendo.
Tutambue kuwa lengo kuu la Mwenyezi Mungu la kutuumba ni kutushirikisha kheri yake na kazi kubwa tuliyo nayo ni kufanya kazi kiaminifu katika kuueneza ufalme wake hapa duniani kwa njia ya kumtumikia na pia kuwatumikia wenzetu. Baada ya pilikapilika za hapa duniani kila mtu atapewa tuzo kadiri ya kazi zake na upendo wa Mungu ambaye sisi ni mali yake na mbingu ni mali yake. Hatuna budi kufurahi tunapoona watu wanaongezeka katika shamba la Bwana na hatuna ruhusa ya kuwahukumu wenzetu kwamba wamechelewa kumurudia Mungu na hivyo hawana mastahili ya kupata Sakramenti mbalimbali katika Kanisa kwa kuwa vyote hivi ni mali yake Mungu. Sambamba na hilo, tunakumbushwa sisi tuliotangulia kubatizwa kutokuona kwamba, wenzetu waliotufuata ni wadogo au hawana ruhusa ya kumwita Mungu Baba. Fundisho lingine ni kwamba yule mwenye shamba hakupenda kuona watu ambao hawana kazi na hivyo nasi pia tunaalikwa kufanya jitihada ya kuwasaidia wengine wasio na fursa za ajira ili nao wapate kazi kwa ajili ya kupata mahitaji yao msingi.