Tafakari Jumapili 26 ya Mwaka A: Zingatia: Ukweli Na Uaminifu!
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 26 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Jumapili hii, Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, inayoongozwa na kauli mbiu “Kama Kristo Yesu, wanalazimishwa kukimbia”. Masomo ya domenika hii yanatukumbusha kuwa kila mtu atahukumiwa kwa matendo yake mwenyewe na ukristo wa kweli si maneno ya nasadiki tu, bali ni kutimiza mapenzi ya Mungu kwa utii, unyenyekevu, na uaminifu katika kutimiza ahadi zetu za ubatizo. Katika somo la kwanza Nabii Ezekieli anawaambia Waisraeli kuwa sababu ya wao kuwa utumwani ni dhambi zao wenyewe kwa kuwa wao walifikiri kuwa wao kuwa utumwani Babeli ni adhabu ya dhambi za babu zao. Hii ni kwa sababu mfumo wa maisha katika agano la kale adhabu zilitolewa siyo tu kwa aliyekosa bali familia nzima hata ukoo mzima ulikuwa unawajibika. Wazazi walipaswa kulipa kwa dhambi za watoto wao na watoto kwa dhambi za wazazi wao na mara nyingine familia yote iliweza kuangamizwa.
Sheria hii ya kosa la pamoja ilikuwa maarufu kati ya mataifa yaliyokuwa jirani na Israeli. Katika Kitabu cha Kutoka Kut 20:5 tunasoma; mimi Bwana Mungu wako ni Mungu mwenye wivu na naadhibu makosa ya wazee kwa watoto wao na wajukuu kwa watoto wa wajukuu wa wale wanaonichukia. Sababu ya Mungu kutoa maneno haya makali hivi ni kuwaonesha watu wake ubaya wa dhambi ya kuabudu miungu mingine ndiyo maana Nabii Ezekieli anawafundisha kuwa Mungu ni mwenye haki, hivyo anamwadhibu kila mtu dhambi zake binafsi nasio kwa dhambi za watu wengine. Kila mtu atapata hukumu kadiri ya haki ya moyo wake na matendo yake. Ndiyo maana baadae Mungu anasema; wazazi wasiuawe kwa sababu ya dhambi ya watoto wao wala watoto wasiuawe kutokana na dhambi ya baba zao; kila mmoja auawe kwa dhambi yake mwenyewe. Hata hivyo wazo hili liliendelea hata katika agano jipya, ndiyo maana Mitume walimuuliza Yesu kuhusu habari za mtu kuzaliwa kipofu wakisema; Bwana ni nani aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake kwa yeye kuzaliwa kipofu? (Yoh 9:2). Yesu anajibu; Siyo yeye wala wazazi wake waliotenda dhambi; alizaliwa kipofu ili kazi ya Mungu ionekane kwa njia yake (Yoh 9:3).
Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi limegawanyika katika sehemu mbili. Katika sehemu ya kwanza Paulo anatuonya tuwe na nia moja bila ugomvi wala majivuno. Tukiwa na unyenyekevu tutashinda majivuno na mafarakano na hivi tutakuwa na amani, umoja na mapendano. Katika sehemu ya pili Paulo anatualika tuufuate mfano wa Yesu. Yeye alijinyenyekeza akawa mtii na kutimiza mapenzi ya Mungu Baba. Bwana wetu Yesu Kristo alionyesha mfano kamili wa unyenyekevu kwa kutwaa mwili wa kibinadamu, kutii, kuteswa na kufa msalabani, ili sisi tupate kukombolewa. Baada ya kujinyenyekesha hivyo Mungu alimtukuzwa. Hivyo tunaalikwa kuufuata mfano wake kwa maneno na matendo ili kwayo nasi tuweze kutukuzwa. Injili inasisitiza kuwa katika kuutafuta ufalme wa Mungu ni lazima maneno na matendo yetu yaendane. Ukristo ni kutii hima mapenzi ya Mungu na huko ndiko kumpendeza Mungu Baba yetu wa Mbinguni.
Ujumbe huu unaelezwa kwa mfano wa watoto wawili wakaidi kwa baba yao ambapo yule wa kwanza hakutimiza kabisa alichoambiwa licha ya kuwa aliitikia kwa maneno tu atafanya aliyoagizwa na wa pili licha ya kumjibu vibaya baba yake kuwa hataki kufanya kazi alijirudi na kutimiza kile alichombiwa. Mtoto wa kwanza ni mfano wa wakristo ambao ukristo wao ni wakutimiza tu ibada na kusema nasadiki lakini matendo yao ni kinyume kabisa na imani yao. Yakobo anasema Imani bila matendo imekufa (Yak 2:14-26), ndiyo maana Yesu anatuuliza katika injili ya Luka 6:46 akisema; Mbona mnaniita Bwana, Bwana lakini hamtimizi ninayowaambia? Katika injili ya Matayo 7:21 anatuonya akisema; Si wote waniitao Bwana, Bwana watakaoingia katika ufalme wa Mungu bali ni wale wanaotimiza mapenzi ya Baba yangu. Kwa hiyo basi tujitahidi kuufanya ukristo wetu usiwe tu namna ya kusali bali uwe namna yakuishi. Imani yetu ionekane katika namna tunavyoishi katika familia, tunavyoendesha shughuli na biashara zetu, tunavyoendesha siasa zetu na tunavyohusiana katika maisha ya kijamii.
Injili pia inatuhimiza kutimiza ahadi zetu na kuacha ahadi za uongo. Mtoto wa kwanza ni mfano wa watu wanaotoa ahadi nyingi lakini hawazitimizi. Katika ulimwengu wa sasa tunashuhudia sana ahadi za uongo, hivyo kutokana na kukosa uaminifu katika ahadi zetu, tunakuwa na unafiki na ugeugeu katika aina ya maisha tuliyochagua iwe maisha ya miito mitakatifu kama upadre, utawa na katika maisha ya ndoa. Kumbe tunaalikwa kuishi na kutimiza ahadi zetu tunazoziweka mbele za Mungu na mbele za watu. Tunashuhudia mara nyingi wanasiasa wakitoa ahadi za uongo kwa wananchi hasa nyakati za uchaguzi lakini hawatimizi wanayoahidi hivyo kukosekana kwa uaminifu katika utendaji kazi na kujaa ukigeugeu na kukosa msimamo na mwelekeo. Mara nyingine tunakuwa wanafiki wa kutaka kuwafurahisha wakubwa au wakutaka kuonekana wazuri kwa kusema ndiyo, ndiyo, ndiyo lakini kwa ndani haturidhishwi, hatukubaliani na wakati mwingine hatutimizi tunayoyakubali kwa mdomo.
Huku ni kuwa na sura mbili sio wa moto wala si wa baridi bali uvuguvugu ambao ni hatari sio tu kwa maisha ya imani bali hata maisha ya kijamii. Tunalolifikiria ni tofauti na tunalolisema; tunalolisema ni tofauti na tunalolitenda. Tunapaswa kuwa watu wa kweli, tutoe ahadi za kweli na tunazoweza kutimiza. Kama kuna ulazima wa kubadilisha iwe ni kwa ajili ya kutenda lililo jema zaidi. Tujitahidi kuwa watu wa ukweli. Tunalolisema lilingane na tunalolifikiria na tutimize kwa matendo yale tunayosema kwa maneno. Tukisema “Ndiyo” iwe ni ndiyo na tukisema “Hapana” iwe ni hapana.” Tusiwe wepesi wa kuahidi tusiloweza. Tuwe na moyo wa sadaka. Hii itatusaidia kuwa waaminifu katika ahadi zetu. Tusiwe vigeugeu. Tudumu katika kutenda mema. Tusikubali kuharibu mazuri tuliyokwisha tenda kwa faida au furaha ya muda mfupi. Waswahili wanasema: Usiache mbachao kwa msala upitao. Mungu ametuambia katika somo la kwanza kuwa Mwenye haki akiacha njia yake njema akatenda uovu, yale mazuri aliyotenda zamani hayatakumbukwa; na katika uovu wake atakufa.
Mtakatifu Polycarp alipolazimishwa katika uzee wake kukana imani yake alisema; Nimemtumikia Kristo kwa muda wote huu wa miaka 86 naye hakunikana; unadhani ninaweza kumkana kwa muda huu?” Kama tumeanza vizuri tusikubali chochote kitutenge katika msimamo wetu. Paulo anawauliza warumi: Nini kitakachotutenga na upendo wa Kristo? Na anatoa jibu hakuna (Rum 8:35), kwa Wagalatia aliwauliza; Enyi Wagalatia, ni nani amewaloga? Mlianza katika Roho sasa mnamalizia katika mwili (Gal 3:1). Basi na sisi tudumu katika kutenda mema katika roho na kweli. Tusing’ang’anie ubaya tulionao, tunaweza kubadilika na kuwa wema kabisa. Mtoto wa pili katika Injili ni mfano mzuri wa kuwa na moyo wa toba na kuanza maisha mapya. Inawezekana kwa sababu fulani tumekuwa hatuishi maisha yanayofaa. Kama tulivyoambiwa jumapili iliyopita hata saa kumi na moja watu waliajiriwa shambani na wakalipwa dinari moja sawa na waliofanya kazi kutwa nzima. Hivyo, tunaalikwa kupiga moyo konde, kutubu na kurudi tena. Mungu ametuahidi kuwa; Mtu mwovu akighairi njia yake mbaya na kuanza kutenda mema, maovu yake yote aliyotenda hapo zamani hakuna hata moja litakalokumbukwa. Mtume Paulo anatuambia; Ninachokifanya nikusahau yote ya zamani na kuchuchumilia yale yajayo” (Wafilipi 3:13) kwa sababu Ya kale yote yamepita tazama sasa yamekuwa mapya (2Kor 5:17).
Hii itufundishe pia kuwapatia watu nafasi ya kujaribu tena na wanaporudi tuwe tayari kuwasamehe na kuwapokea. Kumbe basi Ukristo ni kutii hima mapenzi ya Mungu kwa matendo si kwa maneno tu. Aidha, tunaalikwa kuwa waaminifu kwa ahadi zetu na kuacha kutoa ahadi za uongo. Basi, tumwombe Mungu atujalie moyo wa unyenyekevu na utii ili tuwe waaminifu na kutimiza ahadi zetu za Ubatizo na zile tunazozitoa kwa Mungu na wenzetu na pale tunapokosea tuwe wepesi wa kuomba msamaha, kufanya toba na kuanza upya.