Tafakari Jumapili 24 ya Mwaka A: Msamaha Hauna Ukomo! Masharti!
Na Padre Gaston George Mkude, Roma.
Amani na Salama! Hata nyakati za Yesu, Marabi waliwafundisha watu umuhimu na hata ulazima wa kuishi maisha ya amani na wengine, kuombana msamaha na kusameheana pale wanapokoseana katika maisha. Anayekosea alipaswa kuomba msamaha kwa yule aliyemkosea. Na kama aliyekosewa anakataa kutoa msamaha basi mkosaji alipaswa hapo kuita mashahidi ili nao waweze kuwepo katika jitihada hizo za kuomba msamaha. Na kama aliyekosewa alifariki kabla ya kuombwa msamaha, hapo mkosaji alipaswa kufika katika kaburi la yule aliyekosewa na kuweka jiwe juu ya kaburi lenye maandishi, ‘’Nimefanya yaliyo mabaya kwako’’. Hivyo, tunaweza kuona tayari hata kabla ya Ukristo kati ya Wayahudi kumekuwa na ulazima wa kuomba msamaha na wajibu wa kusamehe. Hata hivyo, msamaha huo ulipaswa kutolewa kwa wanawaisraeli tu na si kwa watu wa mataifa mengine. Hivyo ni msamaha uliokuwa na masharti kadha wa kadha. Msamaha pia ulikuwa na mipaka, mmoja angeweza kusamehe sio zaidi ya mara tatu, ikiwa ndugu yako atakukosea mara ya nne, basi hapo unapaswa kumpeleka mahakamani na huko sheria ichukue mkondo wake.
Somo la Injili ya leo, Mtume Petro anamuuliza Yesu swali juu ya msamaha: ‘’Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe?’’. Ni swali linaloonesha kuwa tayari Mtume Petro anatambua umuhimu na ulazima wa kusamehe, lakini bado anakuwa naye na mashaka juu ya mara ngapi anapaswa kusamehe. Mtume Petro anakumbuka hotuba ya Yesu mlimani; ‘’Basi, ukipeleka sadaka yako mbele ya madhabahu na hapo ukakumbuka kwamba ndugu yako ana ugomvi nawe, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako, ndipo urudi utolee sadaka yako’’ (Mathayo 5:23-24). Na tena tunasoma: ‘’Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia. Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu’’ (Mathayo 6:14-15). Pia kuhusu msamaha tunasoma: ‘’Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, muonye; akitubu, msamehe. Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema, Nimetubu, lazima umsamehe’’ (Luka 17:3-4).
Na ni hapo tunaona swali la Mtume Petro ni kutaka kupata uthibitisho juu ya uhalali na wajibu wa kusamehe kila mara bila mipaka, kusamehe bila kuweka masharti, bila kuangalia idadi wala ukubwa wa kosa. Ni mwaliko leo kutambua, sisi wanafunzi na marafiki zake Yesu Kristo kusamehe na kusamehe bila masharti wala kuweka idadi, au mipaka yoyote ile. Jibu la Yesu kwa Petro, ni jibu kwa kila mmoja wetu: ‘’Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini’’. Dominika iliyopita tulialikwa kutafakari jinsi ya kumsaidia ndugu anayekuwa mbali na Mungu na jamii, na leo tunaalikwa wajibu wetu mwingine wa kusamehe. Kusamehe sio kama ulimwengu unavyotaka bali sisi tunaalikwa kusamehe kama Mungu anavyosamehe, bila masharti wala kiwango au idadi. Yesu anatumia msemo ule tunaokutana nao kwa Lameki. Aliyekuwa wa uzao wa Kaini: ‘’…Mimi niliua mtu kwa kunijeruhi, naam, nilimuua kijana kwa kuniumiza. Ikiwa Kaini atalipizwa mara saba, kweli Lameki atalipizwa mara sabini na saba’’. Ndio kusema adhabu ya Lameki ni ile isiyokuwa na mipaka wala mwisho, ni adhabu au hukumu ya milele yote.
Na ndio Yesu anatualika na kututaka nasi sio kulipiza kisasi bali kusamehe saba mara sabini, kusamehe daima bila mipaka wala masharti yoyote yale. Ni kusamehe kama Mungu anavyotusamehe bila kutuwekea mipaka au masharti. Ili kutufundisha zaidi juu ya ulazima wa kusamehe, Yesu leo anaongea nasi kwa lugha ya mfano. Mfano unaokuwa na wahusika wakuu wawili, mfalme na mtumwa mdeni wake, na sehemu ya pili mtumwa aliyesamehewa deni kubwa na mjoli wake aliyemwia dinari mia moja. Mfalme analetewa mbele yake mtumwa mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Labda naomba hapa tuelewe maana ya talanta. Talanta moja ni sawa na kilo 36 za dhahabu, hivyo kusema talanta elfu kumi tunaweza kuona ni kiasi kikubwa sana cha deni alilokuwa nalo mtumwa yule. Ni mshahara wa zaidi ya miaka laki mbili, hivyo ni deni kubwa hivi isingewezekana kabisa kulilipa kwa mtumwa yule. Ni lugha ya picha anayotumia Yesu leo kutuonesha jinsi mfalme yule alivyokuwa tayari kusamehe deni kubwa kiasi tusichoweza hata kutolea mahesabu yake, ni deni la thamani kubwa kiasi kile, lakini anakuwa tayari kumsamehe mtumwa yule.
Kwa Wayahudi makosa na dhambi zao kwa Mungu yalifananishwa na madeni ya kulipa, na ndio tunaona ni dini inayokuwa na sheria nyingi za kulipa madeni yao iwe kwa njia ya sala, sadaka, majitoleo, kufunga, matendo mema na bado kila mara walijiona hawakulipa vya kutosha kwani makosa na dhambi ni madeni makubwa mbele ya Mungu. Kila mara mmoja alijisikia ni mkosefu na mdhambi mbele ya Mungu na hivyo hana budi kufanya kitu ili kulipa madeni yake. Kila mmoja kama anavyotufundisha Mtakatifu Augostino kuwa tumesamehewa, na hapo lazima kusamehe wengine, ni kutoka kwa Mungu kwa nafasi ya kwanza kila mmoja wetu amepokea msamaha na hivyo tuna wajibu pia wa kusamehe wengine, kuwa wenye huruma na msamaha kama Mungu alivyo na huruma na msamaha kwa kila mmoja wetu. Mfalme anayesamehe bila masharti katika mfano anaoutumia Yesu ni Mungu mwenyewe. Mungu anatusamehe bila kuweka mipaka, anasamehe deni kubwa kiasi hiki cha dhambi na makosa yetu, ndio kusema hakuna dhambi kubwa kiasi cha kukosa kupokea msamaha kutoka kwa Mungu, hata dhambi zile tunazozifikiria na kudhania ni kubwa kiasi cha kushindwa kuelezeka kwa lugha ya kibinadamu.
Mfano wa Yesu ni faraja kwa kila mmoja wetu, kwani tunatambua jinsi Mungu anavyotupenda bila mipaka wala masharti. Ni ukuu wa huruma ya Mungu isiyokuwa na masharti wala kikomo kwa kila mmoja wetu. Ni mwaliko kwetu pia kuwa na huruma kama Mungu alivyo na huruma, kusamehe kama Mungu anavyotusamehe. Pamoja na ombi la mtumwa yule la kuweka ahadi ya kulipa deni lile, tunaona Mfalme anamsamehe na kulifuta deni kubwa kiasi kile. Ndio kusema Mungu daima anafuta makosa na madhambi yetu yote kila mara tunapofika mbele yake na kukiri na kumuomba msamaha. Mungu anafuta deni bila kutuwekea masharti makubwa na magumu, sharti la Mungu leo ni moja la kututaka nasi kufanana naye, kuwa wenye huruma na msamaha kama Yeye. Sehemu ya pili ya Injili ya leo tunakutana na mkasa mwingine unaotushangaza: ‘’Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia; akamkamata, akamshika koo, akisema, nilipe uwiwacho.’’ Dinari mia nyakati zile za Yesu ilikuwa sawa na ujira wa siku moja tu, ndio kusema mtumwa huyu alipokea msamaha sawa na mshahara wa miaka laki mbili na yeye anashindwa kusamehe deni dogo tu sawa na ujira wa siku moja tu.
Mjoli wake anatumia maneno sawa na yale alipomwomba mfalme msamaha wa deni lake, lakini hakujali, tunasikia alimkamata na kumshika koo akitaka alipwe deni lile na hata aliposhindwa akamtupa kifungoni. Ni wazi Yesu leo anatuonesha waziwazi tofauti kubwa iliyopo kati yetu wanadamu na Mungu, jinsi Mungu anavyotusamehe sisi kila mara bila kutuwekea masharti wala mipaka nasi kwa upande wetu tunashindwa kuwasemehe wengine waliotukosea kitu au jambo dogo tu. Utofauti wa huruma na upendo wa Mungu kwetu na jinsi sisi tunavyotendeana baina yetu. Jinsi tunavyoweza kukabana koo, ndio kusema kuwakosesha wengine amani na furaha katika maisha kwa kukosa kuwasamehe makosa yao, jinsi tunavyoweza kufanya maisha ya wengine kuwa magumu, kiasi cha kuwaua kwa kuwakosesha pumzi, kuwakosesha furaha ya maisha na kuishi kwa amani. Mfano anaoutumia Yesu, pia unatukumbusha jinsi sisi tunavyosamehewa deni kubwa la dhambi na makosa yetu, na upande wa pili jinsi tunavyokosa kuwa wenye huruma na msamaha kwa wenzetu katika maisha ya kila siku.
Ni upendo wa Mungu ulio mkubwa kiasi cha kusamehe deni kubwa, na ugumu wa mioyo yetu kusamehe wengine hata makosa madogo wanayoweza kutukosea katika maisha. Ni mfano unaotuonesha jinsi gani makosa yetu ni makubwa sana mbele ya Mungu na bado anatusamehe, hivyo hatuna budi kuwasamehe wengine wanatuokosea. Yesu hana nia ya kuanza kufanya hesabu ya uzito na ukubwa wa makosa na madhambi yetu, bali kuangalia ukubwa usiopimika wa huruma na upendo wa Mungu kwetu. Mungu anatupenda na kutusamehe kiasi kile ambacho mimi na wewe hatuwezi hata kuelezea kwa maneno na vipimo vyetu vya kibinadamu. Dhambi sio tu kosa tunalolitenda katika maisha bali zaidi sana ni kuvunja maagano ya kufanana na Mungu, kupenda na kusamehe kama Mungu. Maana sisi tumeitwa kama wafuasi na rafiki zake Kristo kuwa: ‘… wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu’’ (Mathayo 5:48). Deni ni kubwa kiasi hicho kwani kipimo cha ukamilifu wetu sio mwanadamu bali ni Mungu mwenyewe, lakini umbali wa mtu mtakatifu kabisa na yule mdhambi kabisa kabisa sio mkubwa kwani kipimo hapo sio Mungu aliye mkamilifu kabisa.
Na ndio maana hatuna budi kuupokea upendo na huruma ya Mungu kwa moyo wa shukrani, kwani katika kila dhambi tunayoifanya hata ile ndogo kabisa inavunja maagano yetu na Mungu, maagano ya kuwa wakamilifu kama Yeye. Na makosa wanayotufanyia wengine ni kuvunja urafiki kati yao walio wadhambi na sisi tunaokiri kuwa tu wadhambi pia, wenye kupungukiwa na utukufu wa Mungu Baba. Utusamehe makosa yetu, ndio sala yetu tunayomwomba Mwenyezi Mungu atusamehe yale yote maovu tuliyomkosea, ni sehemu tu ya makosa yetu kwani hatusali kwa makosa ambayo kwa hakika bado hatujayatenda, ni makosa na madhambi yetu ya zamani, yale ambayo tayari tumekwishayatenda. Lakini sala hii mara zote tunamuomba Mungu atusamehe si tu makosa yale ya zamani bali kwa kweli hata na yale ambayo tutayatenda katika maisha yetu, makosa ya sekunde na dakika, na siku na miaka inayofuata kutoka leo. Ni makosa yetu mpaka siku ile ya mwisho ya safari ya maisha yetu hapa duniani.
Je, Mungu anatarajia nini kutoka kwetu? Si kingine, bali ni moyo wa huruma na msamaha kwa wengine, kusamehe kama Mungu anavyotusamehe, kusamehe bila masharti wala kikomo, kusamehe na kuonea huruma wengine kwa daima. Kutokusamehe ni kuwakaba kooni wengine, ni kuendelea kuwaweka wengine katika utumwa wa makosa yao ya zamani, ni kuwakosesha pumzi, kuwakosesha furaha na amani katika maisha yao, katika mahusiano yao nasi. Na ndio leo Yesu anatualika kuwasamehe sio mara saba tu, sio mara nyingi tu bali kuwasamehe daima, kuwa watu wa kuwafanya wengine wapate pumzi na furaha na amani katika maisha. Kila mmoja wetu hana budi kuomba neema ya kuwa watu wa msamaha, yawezekana kuna watu katika maisha yetu bado tunawabeba katika nafsi zetu, kwa kukosa kuwasamehe, na hata kujisamehe sisi wenyewe kwa makosa na madhambi yetu tuliyotenda maishani, leo tunaalikwa kusamehe sio mara saba tu bali sabini mara saba, kuwa daima watu wenye huruma na msamaha.
Kutokusamehe hakumkoseshi tu pumzi ya furaha na amani mwingine bali hata nasi wenyewe tunajiweka katika hali ya kukosa pumzi ya furaha na amani. Kutokusamehe ni kukosa kupumua amani katika maisha yetu, kukosa furaha ya kweli maishani, ni kupoteza urafiki na ukaribu wangu kwa Mungu na kwa jirani. Ni kukosa mahusiano mema hata na nafsi zetu wenyewe, kwani tunakuwa kifungoni, tunakosa uhuru wa kweli wa kuishi maisha yetu kama wana huru wa Mungu. Kutokusamehe ni kifungo cha nafsi na maisha pia. Msamaha ni dawa kwa nafsi si tu za wengine bali hata kwetu sisi wenyewe. ‘’Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma’’ (Luka 6:36). Ndio sifa ya wana wa Mungu, ni wana wenye huruma kama Baba yetu wa mbinguni alivyo na huruma, ndio sifa kubwa ya kila mfuasi wa kweli wa Kristo Mfufuka. Mfuasi wa Kristo haongozwi na mantiki ya kisasi na chuki na kutokusamehe ya ulimwengu huu, bali ni yule anayekubali kuongozwa na mantiki ya mbinguni, mantiki ya huruma na upendo bila masharti. Hatusamehe kwa kuwa sisi ni wanyonge na dhaifu, bali kwa kuwa tunaalikwa kufanana na Mungu Baba yetu mwingi wa huruma na upendo. ‘’Mwenye upendo…wala hana wepesi wa hasira; haweki kumbukumbu ya mabaya…upendo hauna kikomo kamwe’’ (1 Wakorintho 13:5-8).
Upendo unasamehe yote, unafurahi kuona huyu ndugu yangu yu mtu huru, na sio mfungwa wa makosa na madhambi yake aliyonikosea katika maisha. Ni mantiki ya upendo pekee inayopaswa kuongoza maisha yetu kama wafuasi na marafiki zake Kristo Yesu. Hitimisho la somo la Injili yetu ya leo linatuachia maswali mengi, kwani ni baada ya kutoka kusikia huruma ya Mungu na upendo wake usiokuwa na masharti mara moja tunaona kuwa Mungu ili atusamehe basi nasi hatuna budi kuwa watu wa huruma na msamaha. ‘’Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake’’. Na kama ndivyo tunaweza kuona au kusema kuwa basi Mungu hana huruma na msamaha usiokuwa na masharti kama tulivyotoka kutafakari na kusikia katika sehemu ya Injili ya leo inayotangulia. Yafaa kutambua kuwa sio tabia ya Mungu kulipiza kisasi, ila mwandishi anatumia mtindo wa uandishi wenye matisho makali kuonesha jinsi gani msamaha unapaswa kupewa uzito katika maisha ya kila mmoja wetu. Ni muhimu kuwa watu wa msamaha kwani kushindwa kusamehe kama nilivyotangulia kuonesha hapo juu, hakumnyimi tu mwingine hewa na pumzi ya kuishi maisha ya furaha na amani bali hata na sisi wenyewe. Ni maumivu na kuangamiza sio tu maisha ya mwingine bali hata na yangu mimi mwenyewe. Mungu daima anabaki na sifa ya kuwa mwenye huruma na upendo bila masharti nasi kila mmoja wetu tunaalikwa kuwa wenye huruma kama Baba yetu wa mbinguni.
Kutenda makosa ni ubinadamu, ila kusamehe daima tunaweza kwa neema na msaada wa Mungu, hivyo basi tunaalikwa kila mara kuomba neema hiyo, neema ya kufanana na Mungu, ya kuwatendea wengine kwa huruma na upendo kama Mungu anavyonitendea mimi na wewe. Kuna mengi tukiyasikia au kuyaangalia kwa jicho la kibinadamu tunakosa ujasiri wa kusamehe, ni kwa neema pekee ya Mungu tunaweza nasi kufanana naye kwa kuwasamehe wengine wanaotukosea hata na wale wasiotutakia mema, wasiotunenea mema, wasiotaka kuona tunafanikiwa hata kwa jambo dogo kabisa katika maisha yetu, labda hata na wale waliojaribu kuangamiza maisha yetu iwe kwa ndimi zao, iwe kwa fikra zao, iwe hata kwa majaribio ya mashambulio ya miili yetu, daima tunaweza kuwasamehe wote kwa msaada wa neema ya Mungu. Ukristo unatuingiza kuishi ufalme ambapo amri kuu na ya msingi sio haki bali ni upendo, msamaha unatamalaki kwa haki, kinachotangulia yote ni upendo tena bila masharti, huo ndio ukristo na ndio maana tunaalikwa leo kuwa daima watu wa msamaha bila kutanguliza haki au masharti fulani fulani yanayoweza kwenda kinyume na mantiki ya Kristo mwenyewe. Niwatakie tafakari na Dominika njema.