Tafakari Jumapili 24 ya Mwaka A: Msamaha na Udhaifu wa Binadamu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na kuyatafakari masomo ya dominika ya 24 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (YbS 27:30-28:1-7) ni kutoka Kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira. Ni mojawapo ya vitabu vya Agano la Kale vinavyojulikana kama vitabu vya Hekima. Hii ni hekima ambayo ilikuwa inamsaidia Myahudi kuzifikia kweli za kimungu zilizo katika Torati kupitia mang’amuzi ya maisha ya kawaida ya watu, ukiachilia mbali ile njia ya ufunuo wa moja kwa moja au wa kupitia kwa Manabii. Katika somo la leo, mwandishi anazungumzia juu ya msamaha. Hapo tupo katika kipindi cha kihistoria ambapo Wayahudi walikuwa chini ya utawala wa Wayunani. Pamoja na mateso ya ukoloni, Wayahudi walitiwa hofu zaidi baada ya kugundua nia ya Wayunani ni kufuta kabisa kumbukumbu na rejea za Torati ya Wayahudi. Wakaazimia kumrudia Mungu kumwomba toba na msamaha hasa kwa makosa yote waliyofanya dhidi ya Torati yenyewe, ili basi Mungu awapiganie dhidi ya Wayunani wawe salama. Ni katika kipindi hicho, Hekima ya Yoshua bin Sira inawakumbusha kuwa husamehewa dhambi zake yule ambaye humsamehe pia jirani yake yale makosa anayomfanyia. Anasema “mwanadamu humkasirikia mwanadamu, Je? Atatafuta kuponywa na Bwana?” Anachokazia kusema Yoshua bin Sira ni kuwa kuishi msamaha kati ya jirani na jirani pamoja na kutokuwa na moyo wa kulipiza kisasi ni hatua muhimu sana katika kuishika Torati nzima.
Ikiwa basi Wayahudi wanataka kuishika Torati wamrudie Mungu na ikiwa wanategemea kusamehewa naye, basi wao kwanza waanze kuuishi msamaha. Somo la pili (Rum 14: 7-9) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Somo hili ni mwendelezo wa mausia ya Mtume Paulo kwa Warumi katika kuwasaidia kuiimarisha jumuiya yao ya Kikristo. Leo anawaambia kuwa msingi na kipimo cha maisha ya jumuiya yoyote inayojitambua kuwa ni jumuiya ya kikristo ni Kristo mwenyewe. Ni Kristo anayetoa maana na mwelekeo wa maisha ya jumuiya. Kwa jinsi hii basi, Kristo ndiye anayepaswa kuwa rejea ya maisha ya wanajumuiya wote. Anasema Mtume Paulo kuwa “hakuna mtu aishiye kwa nafsi yake wala hakuna mtu anayekufa kwa nafsi yake. Tunaishi si kwa uwezo wetu bali wa Bwana na tunakufa si kwa matakwa yetu bali ya Bwana. Anachokisisitiza Mtume Paulo katika somo hili ni kuwa matakwa binafsi ya mtu au mtindo wa maisha unaotokana na vionjo binafsi vya mtu, kamwe haviwezi kuwa ndio msingi wa kuijenga jumuiya ya kikristo. Wanajumuiya wanapaswa kumuiga Kristo na kuchota daima kutoka kwake msingi na maana ya yote wanayopaswa kuyafanya na kuyaishi.
Injili (Mt 18:21-35) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo. Katika injili hii, Yesu anafundisha na kuwaalika wanafunzi wake kuwa ni watu wa kusamehe. Yesu anatoa fundisho hili kwa kutumia namna mbili tofauti. Katika namna ya kwanza anatumia lugha ya picha. Anamwambia Mtume Petro kuwa inapasa kusamehe “hata saba mara sabini”. Namba saba kibiblia ni namba ya ukamilifu. Kumbe kabla ya kuangalia idadi ya kutoa msamaha anamwalika Petro, kwa jina la wanafunzi na wafuasi wote, kusamehe kikamilifu, sio kusamehe nusu nusu wala kwa shingo upande, wala kusema nimekusamehe ilhali bado hajasamehe. Anapoongeza sasa neno “mara sabini” ndipo anapozungumzia idadi ya misamaha. Idadi hii haibanwi na namba fulani ya misamaha bali humaanisha utayari usiokoma wa kusamehe. Katika namna ya pili, Yesu anatoa mfano au hadithi fupi kuhusu watu hao wawili waliokuwa wanadaiwa. Yule aliyekuwa anadaiwa deni kubwa (elfu kumi) aliomba akasamehewa. Lakini baada ya yeye kusamehewa alishindwa kumsamehe mdeni wake aliyekuwa anamdai deni dogo (mia).
Fundisho analotaka kulitoa Yesu linakuja sasa pale ambapo yule aliyemsamehe deni kubwa aliposikia kuwa huyu aliyekuwa mdeni wake ameshindwa kusamehe deni dogo (mia), alilifufua deni alilokuwa amesamehe na akamuwajibisha hadi alilipe. Kwa Wayahudi hiki hakikuwa kitu cha kawaida. Madeni yalikuwa ni mojawapo ya mambo yaliyokuwa na sheria na taratibu kali na zilizokuwa zinafahamika. Mtu alipolipa deni au kuondolewa deni, mdai na mdaiwa waliandikishiana na deni hilo lililolipwa au kuondolewa hakuweza mtu kulidai tena. Sasa Yesu anapowapa mfano huu anawaonesha kuwa kutokusamehe kunaweza kurudisha deni lililokwishafutwa kisheria. Kwa maneno mengine, kutokusamehe ni kosa na tena kwa mfuasi wa Kristo ni kosa linaloweza kuuharibu uhusiano mwema kati ya mkristo na Mungu Muumba wake.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika ya leo yanatupatia tafakari kuhusu msamaha na hapo hapo yanatualika tuwe ni watu wa msamaha ili kuboresha mahusiano yetu na Mungu na pia mahusiano yetu na binadamu wenzetu. Ni ukweli usiopingika kuwa makosa na kukoseana vimeshakuwa ni sehemu ya maisha yetu kama binadamu. Na hii inatokana ukweli kuwa hakuna mwanadamu aliye mkamilifu. Sote tunaalikwa kujibidiisha kuelekea ukamilifu. Msamaha tunaoalikwa leo kuutafakari na kuuishi ni tunu basi ya kutusaidia ili makosa na kukoseana kati yetu kusiwe ndio kikomo cha udugu wala kusiwe ndio mwisho wa maisha yenyewe. Kwa sababu kukosa na kukoseana ni ubinadamu, kusamehe na kusahau ni mwanzo wa mchakato wa utakatifu wa maisha. Msamaha ni tunu inayotusaidia kuvuka vikwazo vya udhaifu wa ubinadamu wetu ili tusonge mbele tuufikie ukamilifu tulioitiwa na Mungu mwenyewe.
Ni kwa mantiki hii basi, hatuwezi kuuchanganya msamaha na hali ya kupuuzia kosa au kutenda kana kwamba kosa halikufanyika. Tena msamaha sio kupuuzia uchungu au maumivu yanayosababishwa na kosa. Kufanya hivyo kunaweza kuleteleza hatari ya baadhi kuhalalisha makosa na mwenendo usiofaa kwa kisingizio cha msamaha. Msamaha huyachukulia yote hayo katika uzito wake lakini pia huenda mbele zaidi, huruhusu maisha kuelekea ukamilifu yaendelee. Msamaha una nguvu ya kurekebisha makosa kwa kumpa mtu nafasi ya kutubu na kubadilika. Lakini kwa namna ya pekee kabisa, leo tunahimizwa kutambua kuwa kusamehe ndio kigezo cha sisi nasi kusamehewa makosa yetu na Mungu. Si rahisi kusamehe, hasa pale ambapo kosa au madhara ya kosa alilotufanyia mtu ni makubwa. Katika nyakati kama hizo tunapaswa kukumbuka pia kuwa msamaha ni mchakato.
Msamaha ni tendo linaloweza kuhitaji muda hadi ile nia ya kusamehe iweze kufikia ukamilifu wa tendo lenyewe la kusamehe. Katika nyakati hizi basi tukumbuke kuwa kisasi ni cha Mungu, sio kazi yetu wala hata kukusudia kukilipa. Hali kadhalika pia msamaha ni sifa ya kimungu na ni Yeye awezaye kutufikisha katika kutoa msamaha wa kweli. Tujikabidhi mikononi mwake Mwenyezi Mungu tukiomba neema zake ili kufikia kuwa watu wa msamaha. Kwetu sisi yatosha tu kuweka nia ya kusamehe na kuwa watu wa msamaha na kuomba neema ya Mungu itusindikize katika mchakato huo wa kufikia kusamehe wenzetu ili nasi tuweze kusamehewa makosa yetu na kupokea baraka na neema za Mungu maishani mwetu.