Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXVI ya Mwaka: Imani inapaswa kumwilishwa katika matendo! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXVI ya Mwaka: Imani inapaswa kumwilishwa katika matendo! 

Tafakari Jumapili 26 ya Mwaka A: Imani Katika Matendo Adili

Onyo kutoka kwa Kristo Yesu: Tusiwe tu wakristo wa Dominika au wa Kanisani na tunapotoka tu katika malango yake tunabaki kuwa wapagani kwa maisha yetu ya siku kwa siku. Ni Yesu anatualika kila siku kwenda kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu yaani kuvuna matunda mema na adili kwa kuwa mashuhuda wa Injili, wa Habari njema ya wokovu inayomwilishwa katika matendo.

Na Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Nchi ya ahadi iliyoahidiwa na Mungu kwa taifa lile la Israeli sio tu ilitiririka maziwa na asali bali pia: ‘’Nchi yenye ngano na shayiri, mizabibu, mitini, mikomamanga, mizeituni na asali’’ (Kumbukumbu la Torati 8:8,10). Na kwao si tu kwamba nchi yao ilijaa mizabibu bali pia nchi hiyo inatambulika kama shamba la mizabibu. ‘’Naam! Shamba la mizabibu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi ni jumuiya ya Waisraeli, na mizabibu mizuri aliyoipanda ni watu wa Yuda’’ (Isaya 5:1-7). Ndio kusema katika Maandiko Matakatifu na hasa kwa hadhira ya nyakati za Yesu kila mara inapotumika lugha ya picha yenye kutumia shamba la mizabibu, watu wale walielewa mara moja kuwa muhusika mkuu ni taifa zima la Waisraeli na watu wake. Katika Agano Jipya tunoana Yesu anatumia mara kadhaa lugha hii ya picha; Dominika iliyopita tulisikia juu ya Mfalme mwenye nyumba, mwenye shamba na aliyetoka katika mida tofauti katika siku ili kuajiri vibarua kwenda kufanya kazi shambani mwake, (Mathayo 20:1-15), vibarua wabaya wanaokataa kukusanya mazao ya shamba na hivyo kuamua kumuua mwana wa mwenye shamba, (Mathayo 21:33-40) na hata Yesu mwenyewe anatumia lugha hiyo ya zabibu na kujitambulisha kuwa ni Yeye aliye mzabibu wa kweli nasi tu matawi yake. (Yohane 15:1-8)

Lugha ya picha ya somo la Injili ya leo, tunaona Yesu anatumia wahusika wakuu watatu, ndio baba pamoja na wana wake wawili. Ni lugha ya picha inayoweza kuwa rahisi sana kueleweka kwetu leo kwani inatumia picha ya watu wa familia, baba na wana wake. Lakini lugha hii inaweza kutushangaza haikuwa rahisi kwa hadhira ya Yesu, ilikuwa ni mfano unaoleta maswali yenye mashaka mengi kuliko majibu, ni mfano wa kichokozi kwani uliwataka wasikilizaji wake kuutafakari zaidi ili kupata ujumbe uliokusudiwa na Yesu Kristo. Yesu alikuwa anazungumza na wakuu wa makuhani na wazee, ndio kusema wasikilizaji wake walikuwa ni watu wa dini na taifa lile la kiyahudi. Baba kuwa ni Mungu kwao haikuwa shida kuelewa mara moja ila walipata shida pale waliposikia kuwa huyu baba alikuwa na wana wawili. Kwao mwana wa Mungu ni mmoja, ni Taifa pekee teule la Waisraeli. Kwa kinywa cha Nabii Hosea tunasoma: ‘’Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda, kutoka Misri nilimwita mwanangu’’ (Hosea 11:1). ‘’Nawe utamwambia Farao kuwa Mwenyezi-Mungu asema hivi, Israeli ni mzaliwa wangu wa kwanza wa kiume’’ (Kutoka 4:22). Hivyo kwa myahudi yeyote kusikia simulizi la wana wawili tayari kwao ilikuwa ni makwazo na kupoteza nini hasa Yesu anataka kuwaambia, kwani wao waliamini kuwa mwana pekee wa Mungu na ndio lilifananishwa pia na shamba zuri la mizabibu, taifa lile teule la Waisraeli pekee, na wengine wote sio wana wa Mungu, walihesabika kuwa adui wa Mungu na wapagani na wadhambi.

Baba alimsogelea mwana mkubwa na kumwalika kwa nafasi ya kwanza kwenda na kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu, naye kwa bashasha kaitikia ndio nakwenda katika shamba na asiende. Kwa kweli jibu la yule mwana wa kwanza sio tu kusema ndio bali anatumia maneno ya lugha ya Kigiriki, ‘’Εγω, κυριε’’ (Ego kurie), kwa kweli yakiwa na maana sisisi ‘’mimi hapa bwana’’ niangalie na kunijali mimi pekee na wala usipoteze muda wako kuangalia au kuwajali wengine, ni mimi pekee ninayeweza kutenda kadiri ya mapenzi yako daima na hivyo usiangahike na wengine, nitazame na niangalie mimi pekee. Lakini mwana huyu wa kwanza pamoja na kutoa jibu linaloweza kuonekana ni la mwana mtiifu na mwenye heshima na upendo mkubwa kwa baba yake, bado hakwenda, jibu lake lilianzia na kuishia mdomoni tu na hakuliweka katika matendo, kwa kushindwa kwenda katika shamba la baba yake. Mwana huyu hatusikii zaidi ya kuwa labda baada ya kukutana na marafiki zake au watu wengine ndio alibadili msimamo wake, hivyo ni kuonesha tangu awali alikosa utii wa kweli kwa baba yake. Ni mwana aliyempendeza baba yake kwa maneno matupu bila matendo, alikosa upendo wa ndani kwa baba yake bali alikuwa ni mzuri wa maneno matamu bila matendo. Ni wazi jibu lake lilimfurahisha baba yake ila baadaye kumuacha katika masikitiko makubwa.

Yesu anatuonya hata nasi leo tunaotafakari Injili hii: ‘’Si kila aniambiaye, Bwana, Bwana, ataingia katika ufalme wa mbinguni, ila ni yule tu anayetimiza matakwa ya Baba yangu aliye mbinguni’’ (Mathayo 7:21). Ni onyo kwetu kila mara tunaalikwa kutambua kuwa `ndiyo` yetu haina budi kuwa ndiyo si tu mdomoni bali katika maisha yetu, imani yetu haipaswi kuwa ni ya maneno tu bali kuiishi katika maisha yetu ya siku kwa siku, tusiwe tu wakristo wa Dominika au wa Kanisani na tunapotoka tu katika malango yake tunabaki kuwa wapagani kwa maisha yetu ya siku kwa siku. Ni Yesu anatualika kila siku kwenda kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu na ndio kusema kuvuna matunda mema kwa kuwa mashuhuda wa Injili, wa Habari njema kwa kuishi kadiri ya imani yetu. Yesu leo anazungumza na wakuu wa makuhani na wazee, anazungumza na wale waliokuwa wamejawa na dini ya maumbile, ndio dini ya kushika mambo ya nje nje na kuacha yale ya muhimu ya kumuunganisha na Mungu na jirani, ni dini ya kujionesha na kujihesabia haki mbele ya wengine, wengine waone kuwa mimi ninasali, ninatoa sadaka hekaluni na ninalipa zaka na kadhalika na kadhalika, ni dini ya nje nje, dini ya kujionesha na kujiridhisha kuwa inatosha mimi kufanya hayo tu wakati maisha yangu hayaakisi kabisa imani, yanakuwa kinyume na Injili. Kwa maneno machache hii ni dini ya kutaka “kujimwambafai” mbele ya wengine.

Mwana huyu mkubwa tunaweza kumtambua akiwa anawakilisha taifa lile teule, taifa lilikengeuka na kuwa kinyume na Mungu, na mapenzi ya Mungu kwa kukosa kuwa waaminifu kwa maagano yao. ‘’Lakini nyinyi mmekosa uaminifu kwake, nyinyi sio watoto wake tena kwa sababu ya uovu, nyinyi ni kizazi kiovu na kipotovu’’ (Kumbukumbu la Torati 32:5,20). Dini ya sadaka, sala na matendo ya nje pekee haitoshi kwani Mungu daima anataka kutuona daima tunaungana naye na jirani kwa upendo usio na masharti. Na ndio kama tulivyoanza kuona Nabii Isaya 5:7 akilitambulisha taifa la Israeli kama shamba la Mungu la mizabibu sehemu ya pili ya aya hiyo tunasoma: ‘’…Yeye alitazamia watende haki, badala yake wakafanya mauaji, alitazamia uadilifu, badala yake wakasababisha kilio’’. Mfano wa Yesu hauishii na mwana mkubwa na badala yake, baba pia anamsogelea mwana wa pili na kumpa mwaliko ule ule na ulio sawa na wa yule wa mwana mkubwa. Mwana mdogo anajibu kwa jeuri na kukosa heshima, sitaki ila baadaye akatubu na kwenda. Kwa Waisraeli, mwana wa kwanza ndiye mwana pekee na daima aliwakilisha na kutajwa yeye pekee na si mwingine.

Ila tunaona leo Mungu pia ana mwana mwingine, ana mwana wa pili, mwana mdogo, ndiye yule aliyeonekana kuwa hafai, ni mpagani na mdhambi, ni mmoja anayekuwa mbali na Mungu, ni mmoja anayeishi katika ukaidi na kusema daima hapana kwa Mungu, ndio jibu lake sitaki, kwa maneno mengine, mimi sio wa thamani mbele yako, mimi ni sawa na mwana yule asiyekuwa katika mawazo yako, hivyo ni heri ukaniacha niendelee na maisha yangu ya siku zote ya kukaa na kuishi mbali nawe. Mungu alimsogelea mwana yule wa pili, mwana wa pili naye anakaribishwa kushiriki katika uzuri na utajiri wa baba yake, kwenda naye na kuhesabika mrithi sawa na yule mkubwa, ni kwa kuonja upendo na huruma ya baba yake, anatubu na kukubali kwenda shambani na kufanya kazi kama ilivyokuwa mapenzi ya baba yake. Kama tulivyosikia katika somo la Injili la Dominika iliyopita, ni Mungu daima anatoka na kumwendea mwanadamu, kama mwenye shamba alivyotoka katika saa tofauti za siku ili kuajiri vibarua, na leo pia ni baba anayetoka na kuwasogelea wana wake wawili na kuwapa mwaliko ule ule wa kwenda kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu. Ni Mungu daima anayetoka na kuja kutupa mwaliko wa kwenda na kushirikia katika shamba lake, katika furaha yake ya milele. Mwana huyu wa pili au mdogo tunaweza kumfananisha na watu wa Mataifa, watu waliohesabika kuwa ni wapagani “watu wa kuja” na hivyo wadhambi na mbali na Mungu.

Ni wale walioonekana mbali na Mungu kwani maisha yao yalionekana na kuhukumiwa kuwa hayakuendana na sheria na amri za Mungu. Ni hawa ambao katika somo la Injili ya Dominika iliyopita Yesu anatuambia wa mwisho watakuwa wa kwanza na wale wa kwanza watakuwa wa mwisho. Ni huruma na upendo wa Mungu unaomkomboa mwanadamu, ni mwanadamu kujibu na kuitikia wito wa upendo na huruma ya Mungu nasi hapo tunapokea wokovu. Mwinjili Mathayo, anaandika Injili hii tayari miaka zaidi ya 50 imepita tangu baada ya tukio la mateso, kifo na ufufuko wake Kristo. Ndio kusema anawaandikia jumuiya ile ambayo wengi wao wala hawakupata kumuona Yesu kwa macho, lakini ni wakati ambapo jumuiya ya waamini ilikuwa na waamini si tu wa asili ya Kiyahudi bali na watu wa mataifa mengine, watu walioonekana na kuhesabika kuwa ni wapagani, kuwa wapo mbali na Mungu na hivyo wokovu haukuwahusu wao, Masiha ametumwa si kwa wengine bali kwa wana wa Israeli waliopotea.

Pamoja na kufananisha wana wale wawili kwa wana wa Israeli na watu wa mataifa, bado tunaona kila mmoja kama muumini kila mara tunakuwa aidha mwana mkubwa na kuna nyakati tunakuwa kama mwana mdogo. Kuna nyakati ambazo ndiyo yetu inakuwa kweli ndiyo, ni pale imani yetu inaporandana na kushabihiana na matendo yetu, na vile vile kuna nyakati maisha yetu hayajaakisi kabisa imani yetu. Ni kwa kila mmoja wetu kuingia katika maisha yake na kujiuliza kwa dhati kabisa, ni kwa kuchunguza mahusiano yetu na Mungu na jirani, Je, kila mara nimeishi kweli za Injili, kweli kila mara nimesema ndiyo kwa Mungu na kwenda na kuishi hiyo ndiyo, kufananisha maisha yangu na kweli za Injili, kuwa shahidi sio tu wa maneno bali kwa maisha yangu. Je, maisha yangu yanaendana na kweli za Injili ninazozisikia kila Dominika, au maisha yangu kila ninapotoka kushiriki meza ya Neno na ile ya Ekaristi yanabaki mabaya zaidi kuliko hata kabla ya kushikiri? Je, nafananisha maisha yangu na yale ninayoyaadhimisha iwe katika sala zangu binafsi, zile za familia, zile za jumuiya ndogo ndogo na zile za jumuiya ya parokia au kigango?

Mtume Paulo anatuonesha kuwa Yesu hakuwa mtu wa ndiyo na siyo bali daima ni ndiyo kwa Mungu. Na ndio sifa ya mfuasi wa kweli wa Kristo mfufuka, kuishi kiaminifu kwa kushika maagano yale tuliyoweka siku ya ubatizo wetu. ‘’Maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi na Silwano na Timotheo, tulimhubiri kwenu, hakuwa mtu wa Ndiyo na Siyo, bali daima ni Ndiyo ya Mungu’’ (2 Wakorintho 1:19). Mfuasi wa Kristo hapaswi kuwa mtu wa ndimi mbili, bali daima mkweli kwa Mungu na nafsi yake, anayejitahidi kila siku kufananisha maisha yake na Injili ya Kristo, kujitahidi kuishi kadiri ya kweli za imani yetu. Makwazo makubwa kwa wengine ni hasa pale wanapotuona sisi tulio wafuasi wa Kristo tunaishi kinyume na kile tunachokikiri na kukiamini kwa kinywa, ni kwa kushindwa kufananisha maisha yetu na kile tunachokiamini. Ni kuwa na maisha ya kifarisayo, Dominika au kila siku wanatuona tunasali ila maisha yetu yanajaa chuki, masengenyo, kuwanenea na kuwatakia wengine mabaya, kuwa watu wa kisasi na kukosa msamaha, lugha zetu kushindwa kuwabariki wengine na hivyo kuwa kikwazo cha kuwaambukiza wengine uzuri wa imani, uzuri wa upendo na huruma ya Mungu kwa wengine. Mfuasi wa kweli ni yule anayeambukiza wengine ufuasi sio kwa maneno yake bali kwa harufu nzuri ya maisha yake, maisha katika familia zetu, sehemu zetu za kazi, mashuleni, kwenye jumuiya zetu na mahali popote tunapokuwepo, tunaalikwa leo kuhakikisha tunakua na kukomaa katika kuishi imani yetu.

Sehemu ya mwisho ya Injili ya leo nayo pia ni tafakarishi si tu kwa wasikilizaji wa nyakati zile bali hata nasi kwetu leo: ‘’Amin, nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu’’. Ndio kusema watoza ushuru na wadhambi wao tayari wamepiga hatua ya kwanza na ya muhimu katika kuupokea wokovu, wao wanatambua uduni na udogo wao kwani hata nao wanajua kuwa wapo mbali na Mungu na hivyo wanahitaji huruma na upendo wa Mungu, wanajitambua kuwa ni wadhambi, ni kwa kukubali kuwa sote kuwa wadhambi na tunaopungukiwa na utukufu wa Mungu, vinginevyo hatuwezi kupiga hatua ya pili, ile ya mwana mdogo aliyetubu na kwenda. Ili kupata wokovu lazima kutambua kuwa tu wadhambi na wakosefu na hivyo wenye kuhitaji wokovu na ndio upendo wa Mungu. Kila anayejihesabia haki anabaki katika hali ya mwana mkubwa, aliyedhani inatosha kusema ndio na kushindwa kwenda katika shamba la baba yake, ni kwa kutambua kuwa tupo mbali na tunahitaji kutubu na ndio hapo tunaweza nasi kushiriki katika karamu ile ya milele.

Watoza ushuru na makahaba wanajiona ndani mwao kuwa wana uhitaji wa Mungu, wanajiona hawana haki wala mastahili yoyote hivyo ni kwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu pekee. Katika tafakari yetu ya Dominika iliyopita tuliona hatari ya dini ya mastahili, dini ya kujihesabia haki, na leo Yesu anazidi kutukumbusha umuhimu na ulazima wa kuwa wadogo na duni mbele ya Mungu ili tuweze kupata wokovu wake. Mwana mkubwa naye anaweza tu kwenda na kufanya kazi katika shamba la mizabibu mara pale atakapotambua kuwa naye yu mbali na baba yake na hivyo anapaswa kutubu na kubadili maisha yake, kila mara kiburi na kujihesabia haki na kujiona kuwa sisi ni bora kuliko wengine, kinakuwa ni kikwazo kwetu katika kupiga hatua katika mahusiano mema na Mungu na jirani. Hakuna utakatifu bila unyenyekevu wa nafsi, kujikubali na kujiona hatuwezi kitu bila kwanza kuitegemea neema itokayo kwa Mungu, kuikimbilia neema yake, ndio huruma na upendo wake usio na masharti.  Mungu anamsogelea kila mmoja wetu na wito wake kwetu daima ni kutualika kubadili vichwa vyetu, kubadili mioyo yetu, namna zetu za kufikiri ili tuweze kuongozwa sio kwa mantiki zetu bali ile ya Mungu, ndio hiyo inayotutaka kila mara kuwa na moyo wa unyenyekevu katika mahusiano yetu na Mungu na jirani. Nawatakia Dominika na tafakuri njema.

23 September 2020, 08:17