Neno la Mungu Dominika ya 31 ya Mwaka A:Kutumikiana kidugu ni sharti la kufika mbinguni kwa Baba
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vaticani, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 31 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Katika Dominika hii tunakumbushwa kuwa,kutumikiana kuliko kwema ni njia ya kufika mbinguni kwa Baba. Hili ndilo jukumu tulilopewa tulipobatizwa na kumpokea Roho Mtakatifu kwa njia ya sakramenti ya Kipaimara tulipoimarishwa ili kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu mema. Katika somo la kwanza Nabii Malaki anatoa maonyo kutoka kwa Mungu, Bwana wa majeshi na Mfalme mkuu kwa maovu yaliyotendwa na Makuhani katika Hekalu jipya lililojengwa Yerusalemu baada ya kutoka uhamishoni Babeli. Tukumbuke kuwa kitabu cha nabii Malaki ni cha mwisho katika agano la kale na maana ya jina Malaki ni mjumbe wangu. Malachi aliishi miaka 450 kabla ya Kristo na aliandika kitabu chake miaka 80 baada ya wayahudi kurudi kutoka uhamishoni Babeli akieleza kuwa sababu kubwa iliyopelekea ubaridi wa imani ya wana wa Israeli ni mifano mibaya ya makuhani ambao hawakuishi utakatifu wa ahadi zao, na kuongoza ibada katika hekalu kwa hali isiyoridhisha. Makuhani hawa walishindwa kuwaongoza watu katika sheria ya Musa. Matokeo yake maadili yao na ya watu wao yalishuka na hivyo kupelekea maskini, wajane, yatima na wageni kuwa wahanga wa kukosekama kwa mizani ya maadili mioyoni mwa watu na kutokuwa na hofu ya Mungu.
Nabii Malaki anatangaza matokea ya hali hii kwa makuhani kuwa Mungu atawapelekea laana na kuzilaani baraka zao na kuwa siku inakuja wakati ibada inayompendeza Mungu itaadhimishwa tena, ibada ambayo watashiriki watu wote, wayahudi na watu wa mataifa yote; kutoka mashariki ya mbali hadi magharibi ya mbali jina la Mungu litatukuzwa na kila mahali sadaka safi ya ubani itatolewa kwa ajili yake na jina lake litatukuzwa kati ya mataifa. Sadaka hii ya thamani haitakuwa kama sadaka zile ambazo makuhani wa nyakati za Malaki walizitoa, bali zitatolewa na kuhani mkuu ambaye ni mtakatifu, asiye na doa, aliye safi, aliyejitenga na dhambi na hivyo kukwezwa juu ya mbingu (Heb 7:26). Huyu kuhani siyo mwingine ni masiya, Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe ambapo sadaka yake msalabani imechukua nafasi ya sadaka zisizofaa zilizowahi kutolewa na mwanadamu kwa Mungu na kwa sasa sadaka hii inatolewa katika kila adhimisho la Misa Takatifu.
Katika somo la pili la waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa wathesalonike tunaona tofauti ya makuhani nyakati na Malaki na Paulo mtume ambapo Paulo anaelezea namna alivyowatumikia na kuwapenda wakristo wathesalonike kwa maneno na matendo yake mema akiwatangazia habari njema kwa upendo mwingi na kuwaongoza vyema wakristo katika mambo ya roho na mwili na hivyo kuwafanya wakristo wa Thesolonike walipokee neno lake si kama neno la binadamu bali kama neno la Mungu. Hivyo mtume Paulo pamoja na wafuasi wake wanamshukuru Mungu kwa kuwafanya wakristo walipokee vema neno lake na kuwa ndugu zao na mwisho anawaasa kudumu katika imani ili neno la Mungu liendelee kutenda kazi yake ndani yao. Kumbe tunapaswa kulipokea kila mara neno la Mungu kwa moyo wa imani na matumaini.
Katika Injili ilivyoandikwa na Matayo kama alivyofanya Malaki katika somo la kwanza, Yesu naye anatoa karipio kali kwa waalimu wa dini wasiofaa na kutoa ushari wanaolipokea neno la Mungu waliishi neno hilo. Tukumbuke kuwa nyakati za Yesu, kazi ya makuhani na walawi ilikuwa kuongoza ibada hekaluni. Kazi ya kuwafundisha watu sheria ya Musa ilikuwa kazi ya waandishi na mafarisayo ambao kimsingi walikuwa ni walei. Yesu anawaonya kwa mambo manne; kwa kuongeza sheria ambazo hazikuwekwa na Mungu na hivyo kufanya maisha ya watu kuwa magumu, kutokushika yale waliyoyafundisha na hivyo kutokuwa mfano bora wa maisha ya imani na maadili kwa watu, kuwa na majivuno wakitafuta sifa mbele za watu na kumuweka Mungu pembeni, hivyo wakajaa unafiki, uchoyo na ubinafsi (Marko 12:40 na Luka 20:47). Sheria walizozitunga zilikuwa mzigo mzito kwa watu mabegani mwao wakati wao wenyewe hawakuzifuata wasitake hata kuigusa hata kwa vidole vyao.
Sambamba na hilo Yesu anawaonya wafuasi wake wasipende sifa na heshima za nje kama Mafarisao wanavyofanya, kwa kupendelea viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika Masinagogi, kusalimiwa masokoni na kuitwa walimu. Anawataka wafuasi wake wawe waadilifu katika kumtumikia Mungu kwa kuonyesha matendo ya huruma kwa watu wote hasa walio wanyonge kwani sisi sote ni ndugu na watoto wa Mungu mmoja, sote tumeumbwa kwa sura na mfano wake Mungu. Yesu anasema kuwa waandishi na mafarisayo waliketi katika kiti cha Musa kwa maana kuwa walirithi kazi ya Musa ya kuwaelekeza na kuwaongoza watu lakini hawakuishi kile walichohubiri na hivyo kujivika unafiki ambao Kristo aliukemea waziwazi kwani unafiki u kinyume kabisa na ukweli. Unafiki unamfanya mtu kufanya matendo ili aonekane na watu kwa nje tu lakini ndani mwake ni tofauti kabisa na anavyoonekana.
Kwa waandishi na mafarisayo majivuno yao yaliendana na unafiki wao; walitaka waonekane wenye hekima na watu watakatifu ndiyo maana walipanua matamvua yao na kuongeza hirizi zao. Haya matamvua yalikuwa ni vyombo vidogo vya ngozi vyenye kurasa zilizoandikwa sheria ya Musa. Kila myahudi mkereketwa, alizivaa kwa kujifunga juu ya paji la uso na mkono wa kushoto wakati wa sala na wakati wa kwenda katika sinagogi. Lakini waandishi na mafarisayo walivaa wakati wote na walivaa saizi kubwa kumaanisha kwamba walifuata sana sheria ya Mungu kwa makini kuliko watu wengine. Vivyo hivyo kwa hirizi walizovaa kwenye upindo wa vazi ambazo zilifungwa katika pande nne za kanzu zikizoning’inia. Tukumbuke kuwa mambo haya Mungu alimwamuru Musa ayaweke kama ishara kwamba wale walizozivaa ni watu wateule wa Mungu na pia kuwakumbusha wajibu wao wa kuziishi sheria zake kama tunavyosoma katika kitabu cha Hesabu 15:38-39; Bwana akamwambia Mose, Sema na Waisraeli uwaambie: Kwa vizazi vyote vijavyo jifanyieni vifundo katika pindo za mavazi yenu vikiwa na uzi wa buluu kwenye kila kifundo. Mtakuwa mkivitazama vifundo hivyo ili mpate kukumbuka amri zote za Bwana, ili mpate kuzitii msije mkajitia uzinzi wenyewe kwa kuzifuata tamaa za mioyo yenu na za macho yenu. Ndipo mtakumbuka kuzitii amri zangu zote nanyi mtawekwa wakfu kwa Mungu wenu. Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewatoa Misri niwe Mungu wenu. Mimi ndimi Bwan, Mungu wenu. Na kitabu cha Kumbukumbu la Torati 22:12 kinasema: Fanya vishada kwenye pembe nne za joho unalovaa. Lakini Mafarisayo waliharibu maana yake na kuvaa hirizi kubwa na ndefu kuonesha kwamba wao walikuwa watakatifu zaidi kuliko watu wengine na hivyo kuchukua nafasi ya Mungu.
Kwa ubatizo sisi sote tunashirikishwa unabii, ukuhani na ufalme wa Kristo hivyo tunaitwa na kutumwa kutangaza habari njema ya wokovu kwa mataifa yote na kuwafanya kuwa wafuasi wa Yesu. Kumbe mafundisho haya ya Yesu kwa wanafunzi wake yanatuhusu sisi sote tuliobatizwa ambao tumeitwa na kutumwa kuwa watumishi wa neno la Mungu kwa mataifa na hivyo tunapaswa kuvitumia vipaji vyetu mbalimbali tulivyozawadiwa na Mungu katika kuwatumikia wengine kwa unyenyekevu na upendo mkuu. Na hivyo tutumikiane kidugu kama watoto wa Baba mmoja kwa maneno na matendo kuelekea kwenye wito wetu wa utakatifu. Zaidi katika kufanikiwa tusilewe sifa pale tunapofanikiwa, wala tusibweteke na mambo ya kimwili bali tutafute ya roho na kuwa wajasiri katika kujishikiza kwa Mungu.