Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili 27 ya Mwaka A wa Kanisa: Uasi wa mwanadamu na huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili 27 ya Mwaka A wa Kanisa: Uasi wa mwanadamu na huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. 

Tafakari Jumapili 27: Uasi Wa Mwanadamu na Huruma ya Mungu!

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 27 ya Mwaka A wa Kanisa, inatuasa tuzae matunda mema na tumpe Mwenyezi Mungu mavuno wakati unaofaa, hii ni alama na ishara ya wana wapendwa wa Mungu. Matunda yetu mema ni kumjua Mungu, kumpenda na kumtumikia Yeye katika ndugu zetu hasa walio wanyonge. Ujumbe huu unaelezwa kwa mfano wa mkulima wa mizabibu! Wema!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 27 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Kuanzia domenika hii ya 27 A mpaka mwishoni mwa mwaka wa kawaida wa kiliturujia, Injili tutakayokuwa tukiisoma itakuwa inaongea juu ya matukio yaliyojitokeza katika siku za mwisho za maisha ya Yesu hapa duniani kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake na kupaa mbinguni. Sehemu hii ni ya majadiliano makali na viongozi wa Wayahudi ambapo Yesu anawafundisha na kuwaonya viongozi hawa ili nao wapate kuipokea Habari Njema ya Wokovu. Hata hivyo walibaki na shingo ngumu wakakataa kuipokea habari njema ya wokovu. Katika mifano mitatu, Yesu aliwaambia matokeo ya kutokuupokea ujumbe aliowahubiria: mfano wa wana wawili tuliousikia Jumapili ya 26 A, mfano wa watumishi waovu tunaousikia domenika hii ya 27 A, mfano wa Karamu ya Arusi tutakao usikia domenika ya 28 A na kuanzia domenika ya 29 ndipo Mafarisayo wanapoanza mashauri na kupanga mikakati ya namna ya kumkamata, kumshitaki ili auawe. Katika mifano hii ujumbe unaelekezwa kwa makundi mawili: kwanza kwa watu wa Israeli, hususani viongozi wao na pili ni kwa Jumuiya ya Wakristo ambao Mathayo aliwaandikia Injili yake na pamoja nao, kwa Jumuiya ya Wakristo wa nyakati zote, ikiwa ni pamoja na sisi.

Masomo ya domenika ya 27 ya Mwaka A wa Kanisa yanatuasa tuzae matunda mema na tumpe Mungu mavuno wakati unaofaa, hii ni alama na ishara ya wana wapendwa wa Mungu. Matunda yetu mema ni kumjua Mungu, kumpenda na kumtumikia Yeye katika ndugu zetu hasa walio wanyonge. Ujumbe huu unaelezwa kwa mfano wa mkulima wa mizabibu ambao unatolewa na Nabii Isaya katika somo la kwanza kama utabiri na unatolea na mwinjili Mathayo kama utimilifu wa utabiri wa Nabii Isaya kwa njia ya Yesu Krsito. Sio mara chache manabii katika Agano la Kale na Yesu katika Agano jipya kutumia mfano wa shamba la mizabibu katika kufikisha ujumbe kwa watu wake akilinganisha taifa teule la Israeli kama shamba na Mungu kama Mkulima. Ni wazi shamba ni sehemu ambayo mkulima ana mategemeo makubwa sana katika maisha yake. Furaha ya mkulima daima huwa ni kupata mavuno mengi na mazuri, na hufurahia pia wafanyakazi au vibarua ambao hufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanampatia mavuno mazuri kwa wakati ufaao. Kinyume na hapo mkulima huwa na masikitiko makubwa kwa kukosa mazao na pengine huwalaumu au kuwafukuza kazi wafanyakazi wake.

Katika somo la kwanza Nabii Isaya anawafananishwa Waisraeli na shamba zuri la mizabibu alipendalo Mungu. Somo hili laweza kufananishwa na wimbo wa mapenzi alioutunga kijana kwa msichana ampendaye. Wimbo wenye hisia ya furaha na huzuni. Kijana aliyempenda msichana huyu na ametumia mbinu zote kuonesha upendo ila msichana huyu amemtoroka na kwenda kutembea na makahaba. Anajiuliza; nilipaswa kukutendea nini ambacho sijakutendea? Mungu ambaye anafananishwa na mkulima hodari wa zabibu na ndiye mmiliki wa shamba ambalo ni taifa la Israeli aliwatendea mema mengi watu wake Isaraeli; aliwatoa utumwani Misri kwa mkono wa nguvu zake na maajabu mengi, akiwaongoza jangwani na kuwalisha mana, hatimaye akawapa nchi ya ahadi na kufanya nao agano na kuwapa ulinzi na usalama. Badala ya shukrani waisraeli na zaidi mno viongozi wao wanakosa uaminifu kwa maagano, wanavunja amri na maagizo yake. Wanazaa zabibu mwitu yaani dhambi, laana na uasi kwa kuabudu sanamu za miungu ya uwongo, wakawatesa wanyonge na maskini na wakaishi maisha ya ufisadi, uasherati, rushwa na ushirikina.

Nabii Isaya anawasihi waisraeli kuwa wamwongekee Mungu na waache uasi wao, ama sivyo Mungu atawaadhibu kwa kuwaondolea ulinzi na usalama na baraka zake kwa mfano wa mvua juu ya mashamba yao. Viongozi na waisraeli walipoendelea kukaidi maongozi ya Mungu, wanaadhibiwa; wanavamiwa na maadui, wanapelekwa uhamishoni na falme zao zinasambaratishwa. Ndivyo inavyokuwa kwetu tunapokosa uaminifu kwa Mungu wetu na kuabudu miungu mingine. Katika somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi, Paulo anatushauri tutolee mahangaiko na taabu zetu kwa Mungu kwa ajili ya sala, ndipo tutapata amani, huku tukiyafikiria na kuyatenda mambo mema ili tuendelee kujenga uhusiano mwema na Mungu. Paulo anafafanua mambo ambayo mkristo anatakiwa ayaishi ili awe jirani na Mungu ikiwa ni kudumu katika kutenda matendo mema, kutenda haki, kutenda yanayompendeza Mungu, na kudumu katika sala. Mtu anayeishi yanayompendeza Mungu anaishi bila wasiwasi, anakuwa na furaha daima, kwani anakuwa ameunganika na Mungu.

Katika Injili ya Mathayo ya domenika hii inaonesha uaminifu wa Mungu katika ahadi zake. Baada ya kupelekwa utumwani Babeli, Mungu aliwarudisha waisraeli katika nchi yao toka uhamishoni kwa njia ya mfalme wa Persia/uajemi, Cyrus/Koreshi, akawarudishia usalama, akawaandaa wampokee masiha. Masiha anakuja kuwakomboa toka utumwa wa dhambi. Viongozi wa Israeli walirudia matapishi ya dhambi na uasi badala ya kumpokea masiha kwa kuzaa matunda ya toba na upendo wanazaa zabibu mwitu yaani kiburi, majivuno na chuki. Ndiyo maana Yesu kama nabii Isaya ana ujumbe ule ule lakini yeye ni Mwana wa Mungu alietabiriwa na Manabii. Katika ujumbe wa Yesu mwenye shamba ni Mungu, shamba la mizabibu ni ufalme wa Mungu, wakulima ni waisraeli na viongozi wao, watumwa ni manabii na mwana pekee ni Yesu Kristo mwenyewe ambaye wao wanapanga kumuua. Mungu ni mvumilivu, hata baada ya kuona watumwa wake wameua hatumi jeshi kuwaangamiza bali anamtuma mwanae wa pekee tena bila jeshi wala ulinzi wa askari. Kwa kutompokea Yesu ufalme unaondolewa kwao.

Sisi ndio wakulima katika shamba la Bwana nyakati hizi. Kila mmoja wetu amekabidhiwa shamba alitunze na azalishe mazao bora kwa ajili ya nafsi yake, kwa ajili ya Mungu, kwa ajili ya ulimwengu na kwa ajili ya watu wote. Shamba tulilokabidhiwa ni moyo wetu. Tujiulize ndani ya mioyo yetu kuna zabibu gani? Zabibu bora au pori? Zabibu bora zinajulikana kwa matendo yake; upendo kwa Mungu na jirani. Zabibu pori hali kadhalika zinajulikana kwa matendo yake; ubinafsi na dhambi za wizi, ujambazi, ufisadi, ulevi, uasherati, uzinzi, ukahaba, ndoa za jinsia moja, ulawiti wa watoto, utoaji mimba, matumizi ya dawa za kuzuia mimba kwa mwavulia wa uzazi wa mpango, mauaji ya viongozi, ushirikina, uongo na ulaghai wa imani mbalimbali zinazodai kufanya miujiza ya kuwapa watu mali na utajiri, watoto kwa walioharibu vizazi, kuvunja na kufungua mti wa ukoo, kutoa laana, mikosi na balaa, kurudisha vitu vilivyopotea, ubishi kwa viongozi wetu wanapotukumbushwa wajibu wa imani yetu, tunaacha kusali, tunaacha kumpa Mungu shukrani kwa sadaka zetu; haya yote ni magugu na zabibu mwitu ambayo ndiyo yalimfanya mwenye shamba aliache shamba liharibiwe na waovu na ndivyo itakavyokuwa kwetu tukizaa zabibu pori.

Tukitaka kuzaa zabibu bora ni lazima kukubali maongozi ya Mungu, kumpokea Kristo kama Bwana na mwokozi, kusulibisha hali yetu ya mwili na tamaa zake na kuweka hali zetu sawa ili Roho Mtakatifu afanye maskani ndani yetu. Matunda ya maongozi ya roho ni mapendo, furaha, amani, uvumilivu, uaminifu, fadhili, haki, kiasi, upole na uchaji wa Mungu. Lazima tuwasaidie ndugu zetu, kaka, dada na wazazi wetu ili nao waweze kuzaa matunda hayo kwa kuwasaidia waishi injili. Kristo ni mzabibu wa kweli nasi tu matawi yake. Mtume Paulo anatufundisha kuwa; kwa kusali, kuomba na kushukuru, Mungu atakidhi haja zetu. Mungu atatujalia amani katika kutenda yaliyo ya kweli na haki, yenye kupendeza, safi na yenye sifa njema. Yesu anatusisitizia kuwa waaminifu katika kazi tunazokabidhiwa. Uaminifu unapotoweka katika jambo lolote lile, madhara yake ni kuvunjika kwa uhusiano mwema uliopo kati ya marafiki. Tunapokosa uaminifu kwa mwenyezi Mungu uhusiano mwema uliopo kati yetu na Mungu huvunjika.

Ndiyo maana kutokana na kutomwamini Yesu kama ni Masiha, utawala wa Mungu unaondolewa baina yao na kupewa watu wa Mataifa mengine. Taifa teule la Israeli halikuwa na uaminifu juu ya Yesu Kristo kwamba ni Masiha wakamhukumu kuwa ni mwenye makosa, walimtoa nje ya mji na kumwua kama jambazi. Lakini siku ya tatu akafufuka na kuwa jiwe kuu la msingi ambalo kabla yake lilikataliwa na waashi. Hivyo uhalali wa Waisraeli kuwa watoto wa Mungu unaondolewa baina yao na unaelekezwa kwa watu wa mataifa mengine. Hawa ndio wale ambao Yesu anasema kuwa watazaa matunda kwa wakati unaofaa. Basi tumwombe Mungu atudumishe daima katika kutenda yale yaliyo mema, yanayompendeza na yanayotufanya daima tuitwe watoto wa Mungu. Tumsifu Yesu Kristo. 

Jumapili 27 ya Mwaka A
03 October 2020, 15:11