Tafakari Jumapili 28 Mwaka A: Karamu ya Uzima wa Milele!
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 28 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya leo yanatukumbusha kuwa mwaliko wa kushiriki karamu ya uzima wa milele ni kwa wote. Na kila anayefanya maandalizi yanayopaswa kufanyika ana haki ya kuingia na kushiriki. Nasi kwa ubatizo tulipewa mwaliko huu. Ni mwaliko wa kuwa raia wa ufalme wa Mungu na kushiriki furaha za mbinguni. Lakini kwa kuwa Mungu amemjalia kila mmoja uhuru na utashi kamili hamlazimishi yeyote kushiriki na ndiyo maana wapo wanaokataa mwaliko wakibaki kuhangaikia shughuli za maisha ya hapa duniani na kuutupilia mbali mwaliko wa ufalme wa Mungu. Tulipobatizwa tulipewa vazi jeupe la kuingia katika ufalme wa mbinguni. Vazi hili liliashiria neema ya utakaso. Lakini vazi hili, tukilivaa tu bila kulifua linachafuka na kupoteza sura. Likipoteza sura halitafaa tena kuvaliwa
Somo la kwanza la Kitabu cha Nabii Isaya ni msingi wa sehemu ya Injili ya leo juu ya karamu. Mungu ameandaa karamu; Wayahudi na watu wa mataifa wamealikwa. Kuna vyakula na vinywaji kwa ajili ya uzima na uhai wa kimungu. Waliokubali mwaliko wana mang’amuzi mapya; hawana huzuni, hawataonja mauti, watamwona Mungu uso kwa uso kwani kilema cha huzuni hofu ya kifo vyote vitaondolewa. Kwa kuwa watafanyika wana wa Mungu, na kazi yao itakuwa ni moja tu, kumsifu na kumwabudu Mungu; wataimba oneni huyu ndiye Mungu wetu, tunayemtumainia kwa wokovu wetu. Nabii Isaya aliagua nyakati za furaha ambapo Bwana atawaandalia karamu watu wake na kufuta machozi katika nyuso zote. Utimilifu wa uaguzi huu umetimia kwa njia ya Yesu Kristo katika nyakati. Bwana tayari ameandaa karamu na anataka kufuta machozi kutoka nyuso za watu. Kukataa mwaliko huu ni kujitakia hukumu yaani, mauti ya milele.
Katika somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi, Mtume Paulo anasema kwamba wakristo yawapasa kumshukuru na kumtukuza Mungu daima katika yote, yaani katika matamu na magumu. Tutaweza hayo sababu kati yetu yupo mmoja atutiaye nguvu, ndiye Yesu Kristo mkuu wa karamu ya uzima wa milele. Mtakatifu Paulo anasisitiza akisema: Najua kudhilika, tena najua kufanikiwa; katika hali yoyote, na katika mambo yoyote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Lakini ni kitu gani kinampatia uwezo huo? Paulo anasema; Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Kristo ambaye alikuwa yu namna ya Mungu lakini akaachilia hayo yote akawa mtii hata mauti naam mauti ya msalaba (Wafil 2:6ff) huyo ndiye anayenitia nguvu katika mateso kwa sababu yeye hakuishia msalabani au kaburini. Hii ndiyo initiayo nguvu kwa sababu tunajua kuwa yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu (2Kor 4:14). Kwa hiyo tutambue kuwa hata tukiwa katika matatizo ya namna gani maishani: iwe ugumu wa maisha, iwe kuteseka kwa imani yetu, iwe kunyanyaswa na wengine, iwe ni kudhulumiwa kwa sababu ya uongozi au misimamo yetu katika imani na maadili, tunapata kitulizo kwamba tutapokea uzima wa milele kwani; baada ya dhiki ni faraja na Mchumia juani hulia kivulini.
Ukristo ni furaha. Hivyo tunawezakuseme kama Mtume Paulo kuwa; Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nakamilisha kile kilichopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake yaani Kanisa (Kol 1:24). Ni wazi mateso yana sababu nyingi; lakini ni mateso yale yatokanayo na kutenda mema ndiyo yanayotupatia uzima wa milele kama anavyotuonya Petro: Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema kama Mungu amependa hivyo, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu (1Pet 3:17). Katika Injili ya leo ilivyoandikwa na Mathayo Yesu anatupa mfano wa karamu unaotufundisha kuwakaramu ya uzima wa milele sote tunaalikwa bila ubaguzi na kadi ya mwaliko ni moja tu, ndio ubatizo ambao ni mlango wa sakramenti zingine zote. Katika mfano Yesu anasema kuwa mfalme aliwatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini nao wakakataa kuja, akatuma tena watumishi wengine kuwaita walioalikwa waje arusini lakini hawakujali kila mmoja akaendelea na shughuli zake na waliosalia wakawakamata wale watumwa wakawapiga na kuwaua.
Basi yule mfalme akapeleka jeshi akawaangamiza wale wauaji, akawaambia watumwa wake waende hata njia panda na wote watakaowaona wawaite arusini. Wakafanya hivyo arusi ikajaa wageni. Alipoingia mfalme ili kutazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiye na vazi la arusi, akawaamuru watumishi wake wamtoe nje. Huyu alikuwa mzamiaji. Katika arusi watu kama hawa hawakosekani. Na inaelekea huyu mzamiaji hakupitia mlango mkuu wa ukumbi maana waliopitia mlango huu walipewa vazi rasmi la arusi kama ilivyokuwa desturi ya wayahudi ambapo mavazi rasimi yaliandaliwa na waliokuwa wanaingia ukumbini walipewa vazi hilo na kulivaa. Kumbe huyu alipitia mlango wa nyuma. Mfalme aliyemfanyia mwanae arusi ni Mwenyezi Mungu. Huyu mwana ni Yesu Kristo. Bibi arusi ni Kanisa ndiyo kila mmoja wetu. Wale watumishi ndio manabii na manabii waliohubiri Neno la Mungu ili kuwaleta watu katika arusi ya ufalme wa Mungu. Wale waliokataa kufika arusini ni wayahudi na wale wote walioikataa injili. Walioalikwa mwishoni kuja arusini ni watu wote waliohubiriwa injili au habari njema wakaamini na kubatizwa.
Yule aliyeingia bila vazi la arusi yaani yule "mzamiaji" anawakilisha wadhambi au wakosefu. Huyu mzamiaji alikubali mwaliko, akaenda lakini hakuvaa vazi la kuingia katika arusi, akaingia ukumbini bila vazi. Namfananisha huyu mzamiaji na mtu anayeingia kwenye sherehe bila kadi ya mwaliko. Huyu mtu hakueleweka wala na mwenyeji wake wala na wageni wenzake lakini yeye akajionea sawa. Katika mfano huu alioutoa Yesu kuna makundi matatu ya watu; kwanza wapo wale waliokataa mwaliko wakaendelea na shughuli zao. Pili wapo wale waliokubali mwaliko na kuingia katika arusi kadiri ya masharti wakachukua vazi la arusi na tatu aliyeitikia akawa tayari kuingia katika arusi lakini hakufuata masharti hakuchukua vazi la arusi. Huyu wa kwanza na wa tatu wanatuwakilisha wengi wetu. Mungu ametuandalia na kutualika twende kwenye karamu ya ufalme wake. Kuwa mkristo, ni ishara ya kukubali huu mwaliko. Lakini ili kuingia katika sherehe hii tunahitaji vazi rasmi.
Tulipobatizwa tulipewa vazi kama wale waliokuja arusini walivyopewa vazi la arusi. Tulipewa kitambaa cheupe, tukaambiwa kitambaa hiki ndicho vazi la arusi na tukifikishe au tuingie nacho katika ufalme wa Mungu kama kilivyo bila doa lolote. Kitambaa hiki au vazi hili ni neema ya utakaso. Tunakumbushwa wajibu wetu wa kukifua kitambaa au vazi hili mara kwa mara kwa toba ili Bwana arusi atakapokuja atukute tumevaa vazi hili likiwa safi tupate kustahili kuingia katika karamu ya ufalme wa Mungu. Ingawa tumeitikia mwaliko huu na vazi tunalo lakini vazi tulilopewa linachafuka mara kwa mara na kupoteza sura hata haijulikani lilikuwa la rangi gani. Limekuwa na madoa tupu kwa sababu ya dhambi. Tunapaswa kulifua. Kutenda dhambi ni kukataa mwaliko wa kushiriki karamu ya ufalme wa Mungu. Au ni kulitia lile vazi madoa. Matendo yetu yanaonyesha kuitikia kwetu au kukataa mwaliko. Tufue mavazi yetu kwa toba na tumgeukie Mungu na kuitikia mwaliko wa kuingia katika karamu ya ufalme wake kwa matendo yetu mema.