Tafakari Jumapili 28: Ufalme wa Mungu na Karamu ya Bwana!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Ufalme wa Mungu ndio lengo kubwa katika mahubiri yake Kristo Yesu. Yesu anaanza utume wake kwa kutualika akisema: ‘’Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Injili’’ (Marko 1:15). Na taratibu kwa kutumia njia ya mifano anafafanua juu ya ufalme wa Mungu kama tunavyosoma katika sura ile ya 13 ya Mwinjili Mathayo. Lakini kati ya mifano yote ule wa wafanyakazi katika shamba la mizabibu wanaoajiriwa saa tofauti kati siku ndio haswa unatuonesha wema na upendo wa Mungu kwa kila mmoja. Pamoja na kuwa sisi sote tunapokea mwaliko wa bure wa kushiriki katika shamba lake la mizabibu kwa upande mwingine tunaona wajibu tunaopewa kila mmoja wetu, tunaalikwa kwenda na kufanya kazi katika shamba hilo hata kama kwa lisaa limoja la mwisho wa siku. Ni upendo kutoka kwa Mungu lakini nasi tunaalikwa kuwajibika kwa upande wetu. Leo Yesu anaonesha pia upande mwingine wa ufalme wa Mungu, anaufananisha na sherehe, na karamu iliyoandaliwa na mwaliko kutolewa bure. Nyakati za Yesu, marabi walifundisha watu kusubiri kwa hamu na shauku ufalme wa Mungu kwani ni kushiriki furaha ya milele pamoja na Mungu.
Marabi walitafakarisha watu kwa kujihoji maswali; Je, kuna mtu anayeweza kuandaa karamu nzuri kwa ajili ya wageni wake na kisha akaketi pembeni na kuwaacha wageni wale wakila na kunywa? Na jibu lao lilikuwa ni katika maisha baada ya hapa duniani, Mungu atawaandalia muziki mzuri wale wenye haki na Mungu ataketi pamoja nao huku wakisema, huyu ni Mungu wetu, ambaye ukombozi wake tumekuwa tukiungoja na kuusubiri kwa hamu. Ni ufalme unaozungumziwa baada ya maisha ya hapa duniani, ni ufalme wa Mungu wanakutana nao baada ya kifo. Yesu leo anaonesha utofauti na mafundisho hayo ya Marabi. Yesu tofauti na marabi hazungumzii ufalme wa Mungu kama kitu kitarajiwacho, bali upo kati yetu, ni sasa! Ni maisha ya sasa kwa kila mmoja anayempokea na kukubali kuongozwa na Roho wa Mungu, kweli za Injili na kweli za imani yetu, anayekubali kuishi maisha kwa mantiki mpya ya Mungu mwenyewe, ni kwa kila anayekubali kubadili kichwa na kumvaa Kristo. Ufalme wa Mungu sio jambo la baadaye bali ni la sasa, ni mwaliko wa kuuishi ufalme huo leo katika maisha yetu. Ni kukubali maisha yetu kutawaliwa na Mungu, kuongozwa na Neno lake kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
Somo la Injili ya Jumapili ya 28 ya Mwaka A wa Kanisa linatupa picha ya mazingira ya furaha, muktadha wa sherehe, muktadha wa kushirikishana furaha, lakini kwa upande mwingine tena tunastuka tunasikia matukio mawili yasioendana na sherehe. Ndio matukio ya mji kuangamizwa kwa moto na pili mmoja anayekutwa bila vazi la harusi na kutupwa nje kwenye vilio na kusaga meno. Ninawaalika pia kutafakari vema sehemu ya Injili hii ili tuweze kupata ujumbe kusudiwa. Harusi katika Maandiko Matakatifu ni lugha ya picha inayotumika kuonesha makutano ya upendo kati ya Mungu na watu wake, yaani taifa teule la Israeli. Katika somo la leo Bwana harusi ni Yesu mwenyewe, Mwana wa Mungu na mchumba wake ni watu wote wa ulimwengu mzima, ni mwaliko kwa kila mmoja wetu bila ubaguzi wowote ule. Karamu ya harusi inawakilisha furaha ya nyakati za kimasiha. Ni furaha ya wokovu wetu ambayo Mungu anatualika ili kutushikirisha, ni mwaliko wa kuishi maisha pamoja na Mungu.
Ni kwa kukubali kuongozwa na Neno la Mungu hapo nasi tunaweza kupata furaha ya kweli na inayodumu. Yesu leo anauelezea ufalme wa Mungu sio kwa kutumia mfano wa mikusanyiko yetu ya kiibada makanisani, mahali ambapo tunaalikwa kufika na kukusanyika kwa heshima na moyo wa ibada, sio sawa na nyumba ya tafakari, mahali ambapo watu wanakusanyika kusali na kutafakari kwa ukimya mkuu. Lakini Yesu anaufananisha na karamu ya harusi, mahali ambapo watu wanakusanyika na kula na kunywa, na kucheza na kufurahi. Ndio kusema wito wa kushiriki ufalme wa Mbinguni ni kushiriki maisha ya furaha daima. Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika Waraka wake wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, anatualika kuangalia tena upya mahusiano yetu iwe katika familia, jumuiya zetu, parokia zetu, mitaani kwetu, katika taifa na nchi yetu na kadhalika na kadhalika. Je, mwingine ana nafasi gani katika maisha yangu, Je, mimi katika nafasi yangu ni mtu ninayewajali wengine na kuwaona ndugu zangu?
Ni mwaliko wa kujiangalia tena na hasa siku hizi za kuelekea uchaguzi mkuu kama taifa hatuna budi kujihoji na kujiuliza tena juu ya mahusiano baina yetu. Je, tumeruhusu itikadi zetu zitugawe? Je, tumeruhusu tofauti zetu za kimtazamo au kisera kutufanya kumwona mwingine kama adui na mtu hatari? Kumbe, ufalme wa Mungu ni mwaliko wa kumwona mwingine kuwa ni ndugu, kumpenda mwingine bila masharti, kumuona Kristo katika sura ya mwingine, na ni hapo dunia yetu itakuwa paradiso, ni hapo furaha na amani ya kweli itatawala. Kila Dominika, yaani Siku ya Bwana, tunaalikwa kufanya sherehe ya ushindi, karamu ya wokovu wetu. Kila Dominika ni Pasaka ndogo, ni sherehe ya ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Katika somo la kwanza Nabii Isaya anazungumzia juu ya karamu inayoandaliwa na Mungu kwa ajili ya watu wote. Karamu ya kusherehekea ushindi dhidi ya kifo, maana umauti utakuwa umemezwa. Ni karamu ya vinono watakayoiadhimisha katika mlima wa Bwana. Karamu hii tunaweza leo kuifananisha na maadhimisho yetu ya Kiekaristia kila Dominika, kwani tunaalikwa kusherehekea ushindi dhidi ya kifo, kwani ni sherehe ya ufufuko wake Kristo.
Watumwa wanaozungumziwa katika somo la Injili tunaweza kuwagawa katika makundi matatu. Kundi la kwanza na la pili wanawakilisha manabii wale wa kale mpaka Yohane Mbatizaji; Ni wao waliotumwa ili kumwandalia njia Masiha, mchumba anayekuja kwa watu wake, kulikomboa taifa lake, lakini hawakuwa tayari kuupokea mwaliko huo. Na kundi la tatu ndio lile la Mitume na wabatizwa wengine wote, tunaokuwa tayari kumpokea Kristo ili awe mtawala na kiongozi wa maisha yetu, ili tuongozwe na Injili yake. Waalikwa wale wa kwanza hawakuitikia wito, na hivyo wakakosa kushiriki karamu ile ya harusi. Hawakuwa tayari kubadili vichwa vyao, kuacha maisha yao na shughuli zao za siku kwa siku. Hawakuona sababu ya kuupokea mwaliko kwani walijiona kutosheka na maisha yao ya siku zote, walijiona kumiliki ya kutosha kwa maisha yao na hivyo hawakuwa wamepungukiwa na kitu kadiri ya mtazamo wao. Kwa kweli Yesu anazungumzia pale wakuu wa dini kati ya Waisraeli, kwani daima walijihesabu kuwa watu wa haki na hivyo hawana uhitaji wa Masiha wa Mungu. Daima walijiona kuwa ni wenye haki mbele ya Mungu na wanadamu.
Hawakutambua umaskini na kupungukiwa kwao, hawakutambua kupungukiwa kwao hivyo kuwa wahitaji wa chakula na kinywaji, kwa kukubali na kuupokea mwaliko wa kuingia karamuni na kuketi na kufurahi pamoja na Mwana wa Mfalme. Ni wale tu wanaotambua uduni na udogo wao hao ndio pekee wanakuwa tayari kuupokea mwaliko wa kwenda kushiriki karamu katika ufalme wa Mungu. Ni wale tu wanaokuwa kama watoto wadogo, waotambua kuwa bila Mungu hawawezi kitu chochote, wanaokubali kukabidhi maisha yao ili Mungu mwenyewe awaongoze. Mfalme anawatuma tena watumwa wake sasa kwenye njia panda za barabara ili kuwaalika watu wote waweze kushiriki harusi. Wema na waovu, ndio kusema Mungu anatualika kwake sisi sote bila ubaguzi, kila mmoja wetu anayepokea wito hatuna budi kujikubali kuwa tu wema na waovu, kila mmoja wetu ana sifa zote hizi mbili. Hakuna hata mmoja wetu anayeweza kusema yeye ni mwema tu au yeye ni muovu tu. Sifa ya kushiriki kumbe sio kuwa mwema au kuwa muovu bali kuwa na utayari kwa kutambua uduni na umaskini wetu na hivyo kuwa wahitaji wa huruma na upendo wa Mungu.
Mwinjili Mathayo kila mara anatukumbusha kutambua kuwa katika Jumuiya ya wanakanisa, kila mara kuna wema na waovu. Ni shamba lenye ngano na magugu, na vyote havina budi kukua pamoja. Ndio kusema ni kwa kukubali kila siku kupiga hatua katika mahusiano yetu na Mungu, hapo mbegu ile mbaya inazidi kupotea ndani mwetu. Ni kwa kukubadili kubadili vichwa, kukubali kuongozwa na mantiki mpya, hapo mbegu njema inashamiri na kukua na pole pole ule uovu kupotea kabisa. Ni kwa kuruhusu Roho wa Mungu atuangazie kila siku ili tuweze kukua katika safari yetu ya ufuasi. Na ndio mwaliko ambao Baba Mtakatifu anatupa katika waraka wake wa ‘’Sisi sote ni ndugu’’. Kanisa sio mahali kwa ajili ya wema na watakatifu bali anatukumbusha kuwa sehemu kwa kila mmoja, hata wale wanaoonekana kuwa ni wadhambi na waovu, sisi sote tunaalikwa karamuni ili tuweze kuonja na kuipata furaha ya kweli. Kamwe hata mara mmoja asitokee mtu kutengwa na jumuiya ya wanakanisa, Kanisa ni mahali kwa kila mmoja anayekimbilia huruma na upendo wa Mungu.
Ni changamoto tunayopewa sisi sote kwani kuna nyakati tunapata kishawishi cha kudhani sisi ni bora na wenye haki kuliko wengine wanaoonekana wadhambi na wakosefu. Kanisani daima pawe ni mahali ambapo maskini, waliotengwa na wale wote wanaojiona kuwa wapweke wapokelewe kwa furaha na wajisikie nyumbani. Kanisa ni jumuiya ya furaha kwa watu wote, ni jumuiya inayoalikwa kuwaambukiza wengine furaha ambayo tumeipata kwa kukutana na Kristo Mfufuka. Mwinjili Mathayo pia anatuonesha kuwa katikati ya sherehe kuna kuangamiza mji kwa moto. Kwa kweli ni ngumu kupata picha yenye mtiririko mzuri na wenye mantiki kwa mfano wa leo, kuwa sherehe au karamu imeshaandaliwa na ipo tayari mezani, halafu wanaacha kwanza ili kwenda kuangamiza mji ule kwa moto. Kwa kweli Mwinjili Matayo hapa anatupa ujumbe wa kiteolojia, kwani wakati anaandika Injili yake tayari mji wa Yerusalemu ulishakuwa umekwishavamiwa na kuharibiwa na adui. Waamini wa kwanza waliamini kuwa kuangamizwa kwa mji ule ni adhabu iliyotokana na ghadhabu ya Mungu kwa kukataa kumpokea Masiha.
Kwa kweli ni kumzungumzia Mungu mwenye sifa kama za mwanadamu ilikuwa ni kawaida katika nyakati zile za Yesu, lakini kwa kweli Mungu hatendi kama sisi wanadamu na kamwe hamlaani mwanadamu kwani Mungu ni upendo wenyewe na kumfikiria Mungu vingine ni karibu sawa na kukufuru, niwasihi sana tuepuke kishawishi cha aina hiyo katika mahusiano yetu na Mungu. Daima Injili ni Habari Njema, ni Habari ya Furaha na yenye matumaini kwa kila mtu aliyepondeka na kuvunjika moyo! Kwa kila anayekataa mwaliko wa kushiriki karamu ya harusi huyo anayaangamiza maisha yake mwenyewe. Kujiweka mbali na Mungu ni kujiangamiza mwenyewe, kwa kukosa chakula na kinywaji kutoka katika meza ya Mungu mwenyewe. Mungu daima anatumia kila njia katika kumtafuta mwanadamu ili aweze kushiriki furaha yake ya milele. Hata katika mazingira ya dhambi hapo Mungu anatumia nafasi hizo kwa ajili ya kumwokoa mwanadamu. ‘’Wakati ule nyinyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu yoyote katika lile agano la zile ahadi’’ (Waefeso 2:12).
Ila sasa hata watu wa mataifa mengine, waliohesabika kama wapagani nao wamefunguliwa milango ya kuweza kushiriki katika karamu ya harusi ya Mwana wa mfalme, yaani karamu ya Kristo mwenyewe, karamu ya furaha ya milele. Harusi ikajaa wageni, ndio kusema hakuna aliyekosekana kati ya wana wa Mungu, na sasa karamu i tayari. Tunaweza kuona kuwa sasa kila kitu ki tayari, waalikwa wapo tayari na chumba chote kimejaa wageni, tungetegemea furaha kubwa kwa upande wa aliyetoa mwaliko. Ila tunakutana tena na picha nyingine inayotupa maswali mengi na labda bila majibu ya moja kwa moja. Kwa masikitiko makubwa, alipoingia mfalme na kuwaangalia wageni wake anagundua mmoja asiyekuwa na vazi la harusi. Na hata yule mtu tunasikia alitekewa, alifadhaika, alijiona kuwa yu sawa na uchi bila nguo. Lakini tena mbaya zaidi tunaona hata anavyomchukulia ni kwa ukali na ghadhabu kubwa hata kumfunga kamba miguuni, na kutupwa nje kwenye giza na vilio na kusaga meno. Je, isingetosha kumwamuru mtu yule atoke nje, kwa nini adhabu kubwa kiasi hiki, na pili tunaambiwa hawa tu walialikwa walipowaona katika barabara kuu, Je, wale wengine walipata muda gani wa kurudi majumbani na kuvaa mavazi ya harusi? Lakini pia hata mhusika mkuu wa simulizi huyu tunagundua ni mtu aliyegawanyika ndani mwake, mwanzoni anatupa picha ya mtu mwema na mkarimu anayetoa mwaliko wa kuwashirikisha wengine furaha yake lakini tena mara hii tunapata picha ya mtu katili na asiye na huruma wala msamaha.
Lengo la Mwinjii Mathayo ni kutuonesha kuwa si wote wanaoupokea mwaliko wa kuingia karamuni wanakuwa tayari kwa sherehe ya harusi, ni kushindwa kukubali kubadili kichwa, kubadili nguo, nguo za harusi ni kukubali kuvaa mantiki mpya, mantiki ambayo leo Papa Francisko anatualika kumwona mwingine ni ndugu bila kujali imani yake, rangi yake, itikadi yake, kabila lake na tofauti zozote tunazoweza kuwa nazo. Maisha ya kikristo katika Agano Jipya yanafananishwa na vazi jipya, vazi la harusi, vazi tulilopewa siku ya ubatizo wetu na ndilo vazi la kutembea na neema ya Mungu, urafiki na Mungu kwa kukubali kuongozwa naye katika maisha yetu. Maisha yetu hayana budi kudhihirisha na kuonesha kuwa sisi ni watu wapya na sio wa kale. Haitoshi kubatizwa tu au kupokea masakramenti bali maisha yetu kuendana na kuyafananisha na neema tuzipatazo katika masakramenti. Mwinjili Mathayo anawaandikia hasa wakristo wale wa kwanza wenye asili ya kiyahudi, hivyo anatumia lugha inayozoeleka na kueleweka kwao. Lugha ya vitisho na kali: kutupwa nje gizani na kilio na kusaga meno. (Mathayo 8:12, 25:30, 24:51). Wainjili wengine hawatumii lugha ya aina hii. Ni lugha iliyokuwa ikitumika na marabi na hata kumuonesha Mungu kuwa mkali na asiye na huruma kwa wanaokataa mwaliko wake.
Na hata sasa wapo wanaokuwa na sura ya namna hiyo ya Mungu, nikiri kuwa si sawa na hatuna budi kubadili vichwa na kumuona Mungu kama anavyotuandikia Baba Mtakatifu Francisko ‘’Jina la Mungu ni Mwenye Huruma’’ Kinyume chake kwa kweli ni kukufuru kwa kumuonesha Mungu na sura ya ukatili na bila huruma. Waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache. Maneno haya hayamaanishi kuwa watakaoingia mbinguni ni wachache, kwani Yesu hazungumzii juu ya paradiso kama nilivyotangulia kusema, bali ufalme wa Mungu. Wote tunaalikwa ila wachache tu ndio wanaokuwa na ujasiri wa kukubali kubadili mavazi, kubadili vichwa, kubadili mitazamo yao na kuruhusu kuongozwa na mantiki ya mbinguni, yaani ya Mungu mwenyewe. Tarehe 10.10.2020 Mama Kanisa anatarajia kumtangaza kijana mdogo Carlo Acutis kuwa Mwenyeheri, ni hatua muhimu kabla ya kutangazwa kuwa mtakatifu. Carlo Acutis ni mfano wa vijana watakatifu wa enzi na nyakati zetu, alifariki mwaka 2006 akiwa na miaka 15 tu kwa ugonjwa wa saratani ya damu (Leukemia). Ni kijana aliyejulikana kuwa na kipaji kikubwa cha kutumia kompyuta, na alitumia kipaji chake kuinjilisha vijana wenzake. Kwa kutambua maisha ya fadhila ya Mwenyeheri Carlo Acutis, nimetenga pia muda wangu kuandika kitabu kidogo chenye masimulizi ya maisha yake.
Na kitabu hiki kwa namna ya pekee kinazinduliwa rasmi tarehe 11 Oktoba 2020 hivyo niwaalike iwe watoto, vijana, watu wazima na hata wazee kujipatia nakala ya kitabu hicho ili tuweze kukutana na Mwenyeheri Carlo ili atuambukize nasi utakatifu. Mwenyeheri Carlo aongee na kila mmoja wetu iwe ni wazazi, vijana, watoto na hata wazee, ni kwa kukutana naye kwa njia ya masimulizi ya maisha yake nasi tunajifunza mbinu na njia za kuishi kitakatifu katika maisha yetu ya kila siku. Mtakatifu Francisko wa Assisi, utuombee! Mwenyeheri Carlo Acutis, utuombee! Nawatakia Dominika na tafakari njema.