Tafakari Jumapili 30 Mwaka A: Upendo Na Utu wa Binadamu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na kuyatafakari masomo ya dominika ya 30 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (Kut 22:20-26) ni kutoka Kitabu cha Kutoka. Baada ya Mwenyezi Mungu kuwapa Waisraeli amri zake 10, ulifuata ufafanuzi wa amri hizo kuendana na mazingira ya maisha yao ya kila siku. Somo hili la leo linaeleza na kufafanua mambo mawili. La kwanza ni wajibu walionao juu ya wageni na la pili ni wajibu walionao wao kwa wao. Wajibu huu tunaweza kuuelezea katika neno moja tu “uungwana” unaofumbatwa katika utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwenyezi Mungu anawataka watu wake waishi kiungwana katika mahusiano yao na wageni na katika mahusiano yao wao kwa wao. Katika uungwana na utu huo, anaagiza kutokumtendea ubaya mgeni yeyote anayewafikia. Anaongeza katika kundi hili la wageni, wajane na yatima. Mungu anawakumbusha kuwa wao nao walikuwa wageni katika nchi ya Misri lakini Yeye mwenyewe aliwatendea wema hadi kuwatoa salama kutoka Misri.
Hapo Mungu anatukumbusha nasi kuwa tuangalie vema namna tunavyowatendea wale tusiofahamiana nao. Tujihadhari dhidi ya kuwa wakatili kwao kwa sababu yeye ni Mungu awahifadhiye wageni. Hasira yake isije ikawaka juu yetu kwani ni kwa wema huo huo ametutendea nasi katika nyakati tofauti za maisha yetu. Mungu anawataka pia kuendeleza uungwana hata katika yale ambayo sheria ingewataka kutokuwa hivyo. Ilikuwepo sheria iliyoongoza masuala ya mikopo na madeni. Kimsingi aliyekopa alipaswa na alikuwa na wajibu wa kulipa. Na ndivyo ilivyo hadi sasa. Hata hivyo tunaona kuwa tangu mwanzo Mungu anawaalika kuzishughulikia sheria hizo kwa kuzingatia uungwana au utu. Sio kwamba mdeni asilipe deni lake ila isifike mahala akaondolewa utu wake kwa sababu ya deni. Anatumia lugha rahisi kabisa anapowaambia, ikiwa mtu amekukopa na ameweka rehani kwako shuka lake. Ni uungwana kumrudishia shuka lile walau limfae kwa baridi ya usiku hasa ikiwa kwamba ndilo shuka pekee alilonalo kwa ajili ya kujisitiri. Utu na uungwana katika mahusiano.
Somo la pili (1Thes 1:5c-10) ni kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike. Waraka huu ndio unaosemekana kuwa ndio Waraka wa kwanza kuandikwa na Paulo kati ya nyaraka zake zote ambazo zipo katika Agano Jipya. Ni hapa ndipo alipoanzisha utamaduni wa kuwaandikia waamini wa makanisa aliyohubiri ili pamoja na kuwasalimu aweze kuendelea kuwalisha Neno la Mungu lililo Habari Njema ya wokovu. Katika somo hili la leo, Mtume Paulo anawakumbusha Wathesalonike maisha waliyoishi katika kipindi walipokuwa pamoja. Anawakumbusha ule uungwana, utu na heshima aliyowaonesha hata wakavutiwa kumuiga kama yeye naye alivyokuwa akimuiga Kristo. Na kwa jinsi hiyo, Wakristo hao wa Thesalonike wakawa mfano kwa waamini wote wa makanisa ya jirani – Macedonia na Akaia. Mtume Paulo amelihubiri Neno lakini pia amewavuta kwa uungwana na utu wa maisha yake. Na kwa uungwana na utu huo anapenda akumbukwe. Mtume Paulo anatukumbusha jambo muhimu wakristo wote hasa sisi watangazaji na wahubiri wa Neno la Mungu. Jambo hilo ni mwenendo mwema wa maisha, hasa ule mwenendo unaoacha alama kwa mahusiano ya kiungwana na watu, ni msaada mkubwa sana katika utangazaji wa Neno.
Injili (Mt 22:34-40) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Mathayo. Ni Injili ambayo Yesu anautangaza upendo kuwa ndiyo ufupisho wa amri zote. Amri iliyo kuu kuliko zote ndiyo hiyo – mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote. Na ya pili inafanana nayo. Ni upendo kwa jirani: mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe”. Wayahudi walikuwa na dhana pana sana juu ya sheria. Walipenda sheria. Na kwa kupenda kwao huku sheria walijikuta wanajitengenezea sheria ndogo ndogo nyingi sana. Karibu kila kitu walichofanya, kilikuwa na sheria inayoeleza jinsi gani kifanyike. Ndivyo ilivyokuwa pia kwa amri za Mungu. Kutoka katika amri hizo kumi walijituka wametengeneza sheria ndogondogo zaidi ya 600. Kwa sababu hii kulikuwa na hitaji la kuwa na waalimu wa sheria. Hawa kazi yao kubwa ilikuwa ni kuelekeza nini kifanyike iwapo mtu atavunja sheria hizo lakini pia kueleza sheria zipi ni za msingi na zipi ni zile ndogo ndogo. Kumbe ilikuwa mtu akitaka kumtambua mwalimu wa kweli wa sheria, basi alimuuliza maoni yake kuhusu zipi ni sheria kuu na zipi ni ndogondogo. Ndivyo walivyokwenda na kwa Yesu kumuuliza afafanue kadiri ya mwono wake zipi ni amri kuu.
Yesu anapolijibu swali hilo na kuonesha mwono wake juu ya amri iliyo kuu, kwanza kabisa anajitambulisha na kujipambanua kuwa kweli ni mwalimu wa sheria. Ni mwalimu wa sheria kama Musa aliyezitoa na kuzifafanua. Lakini pia yeye anaenda mbele zaidi. Walimu wa kawaida wa sheria walipoulizwa ipi ni amri kuu, wao walitaja kati ya amri au sheria zilizopo kuwa hii na hizi ndizo kuu. Yesu yeye hataji hizo zilizopo bali ni kana kwamba anatoa amri nyingine. Katika amri 10 za Mungu haipo amri ambayo inataja moja kwa moja upendo. Kumbe, Yesu anatoa kiini cha amri zote badala ya kutaja amri moja au mbili kati ya zile kumi ambazo ni kuu na kuacha nyingine ambazo si kuu. Yesu ni Mwalimu wa sheria lakini hasa ni mtoaji wa sheria na ndiye yule anayealika kushika kiini cha sheria bila kubaki katika maneno yake ya juu juu.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu ya dominika hii ya 29 ya mwaka A wa Kanisa yanatupatia kwa mara nyingine tena, nafasi ya kuutafakari upendo kama msingi wa kuishi vema kati yetu sisi kwa sisi lakini pia kama msingi wa kuishi vema katika mahusiano yetu na Mungu kwani ni upendo unaotusaidia kuzishika vema amri zake kwa kuishi kile kilicho kiini cha amri hizo. Dominika hii ni ya mwisho katika mwezi huu wa Oktoba, mwezi ambao Kanisa limeutenga kama mwezi wa Rosari Takatifu na pia mwezi wa kuhamasisha maisha na utume wa Kanisa, yaani mwezi wa kuombea, kukuza ufahamu na kualika majitoleo kwa kazi za kimisionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Tumshukuru Mungu kwa upendo wake mkuu kwetu na tuombe neema ili nasi tutawaliwe na upendo katika maisha yetu. Upendo huo utusukume kutafuta kudumisha mahusiano mema na wenzetu na upendo huo utusukume katika ibada na majitoleo yetu kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kama kielelezo cha imani tendaji!