Tafuta

Taa inayoangaza mwaka wa kukesha lampada. Taa inayoangaza mwaka wa kukesha lampada. 

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 32 ya Mwaka A:Kesheni kwa maana hamjui siku ya kufa

Tunapoelekea mwisho wa mwaka wa Kanisa,Mama Kanisa anatuelekeza kujiandaa,kujitayarisha na kujiweka tayari kwa maisha yajayo ya uzima wa milele mbinguni.Tunaalikwa kukesha, kuwa tayari wakati wowote kwa ujio wa mjumbe wa Mungu kuja kutuita wakati na muda tusioujua. Hivyo tunapaswa kukesha.Upo mfano wa wanawali kumi wanaomngojea Bwana arusi anayetajwa kama mwana wa mfalme.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vaticani, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 32 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Tunapoelekea mwisho wa mwaka wa Kanisa, Mama Kanisa anatuelekeza kujiandaa, kujitayarisha na kujiweka tayari kwa maisha yajayo ya uzima wa milele mbinguni. Tunaalikwa kukesha, kuwa tayari wakati wowote kwa ujio wa mjumbe wa Mungu kuja kutuita wakati na mda tusioujua. Hivyo tunapaswa kukesha.

Somo la kwanza kutoka kitabu cha Hekima ya Sulemani latufundisha dhamani ya Hekima ya Mungu ipatikanayo katika neno lake. Sulemani anatueleza kuwa Hekima ina thamani kuliko utajiri na nguvu za mwili, kwani ina uwezo wa kujua siri za nguvu za asili na kufumbua mafumbo ya Mungu kwa ufunuo wake Mungu kwa wale wanaofungua mioyo yao na kumruhusu Roho wa Mungu kufanya kazi ndani yao. Hekima hii humpa mtu uvumilivu, umakini na uaminifu kwa maneno na matendo yake, unyenyekevu na kiasi. Hivyo mtu anayekubali hekima kuwa mwongozo wake ana amani maishani mwake. Hekima hii ya Mungu ndiye Kristo Bwana na mwokozi wa maisha yetu ambaye hung’aa wala hafifii, huonekana upesi nao wampendao, hupatikana nao wamtafutao. Tumtafute basi huyu Hekima hasa katika sala na sakramenti za Kanisa ili maisha yetu ya sasa na yajayo yawezekuwa ya furaha na amani milele yote.

Katika somo la pili la waraka wake wa kwanza kwa wathesalonike, mtume Paulo anawaambia kuwa wasibweteke na maisha ya dunia hii bali wakeshe kwani ujio wa Yesu ni muda wowote. Hii ni kwasababu waamini wa kwanza waliamini kuwa Yesu atarudi mapema sana kwa mara ya pili kuwachukua wafuasi wake na kuwapeleka mbinguni kwa Mungu Baba. Waliamini hivyo kwasababu ya majanga makubwa na mateso yaliyokuwa yanawapata wakristo. Kwa Wathesalonike hali hii ilisababisha baadhi yao waache kufanya kazi kwa kuona akiba ya chakula walichokuwa nacho kinatosha kuwafikisha mwisho wa dunia. Muda ukapita na watu wakaanza kukata tamaa, uvumilivu ukawashinda na baadhi yao wakaacha imani yao ya kikristo. Ndipo sasa Paulo anawatia moyo wasikate tamaa waendelee kuchapa kazi huku wakiwa tayari kwa ujio wa Kristo. Ujumbe huu ni wetu sote hata nyakati zetu kuwa tuishi na kufanya kazi kwa bidii huku kana kwamba tutaishi milele yote hapa duniani lakini tukiwa tumejiandaa kwa ujio wa ndugu yetu kifo wakati wowote atakapokuja kutuita kila mmoja kwa jina lake na kwa wakati wake kwenda kwa Baba mbinguni kushiriki uzima wa milele.

Sio mara chache Yesu ameufananisha Ufalme wa Mbinguni na Sherehe kwa mifano mbalimbali. Leo anatupatia mfano wa wanawali kumi wanaomngojea Bwana arusi anayetajwa kama mwana wa mfalme lakini Bibi arusi kamwe hatajwi. Kufichwa kwa jina la Bibi arusi chimbuko lake ni tangu Agano la Kale ambapo uhusiano kati ya Mungu na taifa teule la Israeli ulielezwa kama uhusiano wa Mume na Mke na kazi ya kumkomboa mwanadamu inalinganishwa na kumposa kwa upya mke aliyeasi na kumrudisha tena katika nyumba ya mume wake ndiyo maana Mungu alimwambia nabii Hosea; “Nenda tena ukampende mwanamke anayependwa na mume mwingine na ambaye ni mzinzi. Mpende kama mimi Mwenyezi ninavyompenda Israeli, ingawa yeye anaigeukia miungu mingine…” (Ho.3:1). Ni lugha ngumu kweli tukiiangalia katika maisha ya kawaida. Ni vigumu mwanamume kumbembeleza mke aliyemsaliti. Lakini Mungu anasisitiza kuwa kumpenda Israeli aliyeasi kama mwanamke mzinzi. Hii ni faraja kubwa kwetu, kuwa Mungu daima anatutafute na kutuita turudi kwake licha ya dhambi zetu, tukitubu yeye daima yuko tayari kutusameheme na kutupokea tena na kutushirikisha uzima wa milele.

Kudhihirisha upendo na huruma yake anamtoa na kumtuma kwetu mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo kuja ulimwenguni kutukomboa. Tendo hili linafananishwa na mwanamume kuanza utaratibu mpya wa kumwoa mwanamke aliyemsaliti na kutembea na wanaume wengine. Mungu kwa njia ya Yesu Kristo anakuja kutuletea tena furaha kama furaha za harusi tulizozipoteza kwa kutenda dhambi. Ndiyo maana kwa ishara ya harusi ya Kana ya Galilaya (Yoh.2:1-11), Yesu alibadili maji kuwa divai ikiwa ni ishara ya kuleta neema na baraka katika maisha ya mwanadamu yaliyopoteza ladha kwa sababu ya dhambi. Ile karamu aliyoagua Nabii Isaya akisema; Katika mlima huu, Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta (Is.25:6-10) inatizwa katika Kristo.

Bwana wetu Yesu Kristo anatualika katika sherehe za uzima wa milele kwanza kabisa kwa wale wanaompokea anawapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu (Yoh.1:12). Lakini sherehe hizi ukamilifu wake ni mbinguni kama Yohane anavyotuambia akisema; “Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo (1Yoh.3:1-2). Anaendelea kusema; “Tufurahi na kushangilia; tumtukuze Mungu kwani wakati wa harusi ya Mwanakondoo umefika, na Bibi arusi yuko tayari. Amepewa uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na yenye kung’aa! Kisha malaika akaniambia; “Andika haya: Heri wale walioalikwa kwenye karamu ya harusi ya Mwanakondoo!” (Uf.19:7-9). Hawa ndio wale watakaokuwa na vazi la harusi (Mt.22:12) na watakaokesha mpaka mwisho kwa maneno na matendo yao.

Ndiyo maana katika Injili ya domenika hii ya 32 A, kama ilivyoandikwa na Matayo tunapewa mfano wa wanawali kumi unaotukumbusha wajibu wetu wa kukesha, yaani kudumu katika hali ya neema ya utakaso, kwani hatujui siku wala saa ya kifo chetu. Ili kuulewa mfano huu, yatubidi tuelewe mila na desturi za kuoa za Wayahudi kipindi hicho. Sherehe za harusi zilifanyika nyumbani kwa bwana harusi, zilianza jioni kwa maandamano kutoka nyumbani kwa wazazi wa bibi arusi na kuishia nyumbani kwa bwana arusi. Kimila bibi arusi aliwaalika marafiki wanawali wenzake wasiopungua kumi, wamsindikize wakiwa na taa kuelekea nyumbani kwa mumewe. Wanawali hao walipaswa kuwa na kichupa cha akiba ya mafuta ili ikiwa bwana harusi atachelewa wasitindikiwe. Kama injili isemavyo bwana arusi alikawia kuja. Ilipofika usiku ndipo ulipoonekana msafara wa bwana arusi akija kumchukua bibi-arusi. Wanawali wakaamshwa na kuambiwa waziandae taa zao, waende kumlaki bwana arusi ili waandamane naye wakimsindikiza bibi arusi kwenye makazi yake mapya. Watano wenye busara walijaza taa zao mafuta na wakaweka na akiba. Watano waliopewa sifa ya upumbavu hawakuwa na mafuta ya akiba na walipotindikiwa waliomba kwa wenye busara nao wanaambiwa washike njia wakanunue kwa wauzao. Waliporudi walikuta maandamano yamekwishafika kwa Bwana harusi, waliokuwa kwenye maandamano wameingia ndani na milango imefungwa naye Bwana harusi hakuwa tayari kuwafungulia.

Mama Kanisa ana maana kubwa sana anapotupa mfano huu hasa tunapokaribia mwisho wa mwaka wa Kanisa. Tulipobatizwa tulipewa taa inayowaka ndio neema ya utakaso tuipatayo kwa sakramenti ya ubatizo iliyo mlango wa sakramenti zingine zote. Pale tunapotindikiwa kwasababu ya dhambi tunapaswa kwenda mara kwa wauzao yaani makuhani kujinunulia katika sakramenti ya kitubio na kujiimarisha katika sakramenti ya Ekaristi Takatifu, sala, sadaka na majitoleo mbalimbali huku tukizishika na kuziishi amri za Mungu na za Kanisa kwa kufuata mifano yamaisha ya wakatifu huku tukiishi maisha ya kumpendeza Mungu. Siku ya ujio wa mjumbe wa Mungu itakuja kama mwizi. Kumbe tunapaswa kujiandaa kwelikweli. Tusiwe wapumbavu kwani maisha ya leo ni ya hatari kwelikweli. Wapo watu wanaokufa ghafla kwa magonjwa yanayozuka na yasiyoponyeka na hata wengine kwa ajali. Kumbe sasa ndio wakati wa kulia:” Bwana, Bwana tufungulie!” Kanisa liko macho muda wote na linatualika kukesha katika kuwahudumia masikini, wagonjwa kimwili na kiroho, kuwafariji yatima kwa upendo huku tukimwombe Mungu atujalie Hekima ya kujua mambo ya nyakati za mwisho.

DOMINIKA YA 32
06 November 2020, 17:23