Neno la Mungu Dominika ya 33 ya Mwaka A:Tutumie vema karama zetu
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vaticani, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 33 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Tunakaribia mwishoni mwa kipindi cha mwaka A. Katika domenika hii tunaadhimisha siku ya nne ya maskini duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Fransisko umebebwa na maneno yanayotoka katika kitabu che Hekima ya Sulemani 7:32 yakisema: Mnyooshee masikini mkono wako naye Bwana atakubariki ndio kipimo msingi cha hukumu ya mwisho atakapoketi mwana wa Adamu katika kiti chake cha enzi (Mt. 25:40). Somo la kwanza la katika kitabu cha Mithali linaeleza jinsi mwanamke mwenye hekima na mwenye uchaji kwa Mungu alivyolicha; kuwa daima anafanya kila awezalo ili ampendeze bwana wake. Sisi wakristo tutakuwa wenye hekima, iwapo tutakesha na kutenda mema kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Na hekima ya Mungu inatudai kuwahudumia ndugu zetu kadiri ya uwezo aliotujalia mwenyezi Mungu kwani kila tulichonacho chatoka kwake kwa ajili yetu na kwa ajili ya wengine.
Somo la pili la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike linatukumbusha kuwa wajibu wetu mkubwa katika maisha ya sasa ni kuwa tayari daima kila wakati kwa ujio wa Kristo. Si lazima tujue siku ipi atakuja; Kama anavyosema Paulo; ndugu zangu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, hakika hawataokolewa. Kumbe wajibu wetu ni kujua kwamba tumeokolewa gizani kwa ubatizo basi yatupasa kutunza nuru hiyo tuliyopata kila siku ya maisha yetu kama anavyosema Paulo mtume; Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.
Wazo kuu tunalolipata katika Injili ya leo ilivyoandikwa na Mathayo ni kwamba Mwenyezi Mungu ametujalia karama mbalimbali ambazo tunapaswa kuzitumia katika kuujenga ufalme wake duniani. Talanta hizi zinaelezwa kwa mfano wa talanta ambazo zimegawiwa na Bwana mmoja kwa watumwa wake watatu; wa kwanza amepata talanta tano, wa pili talanta mbili na wa tatu amepewa talanta moja. Kila mmoja amepewa kulingana na uwezo wake! Talanta ni vipaji, vipawa au karama ambazo Mwenyezi Mungu anamjalia kila mtu kwa kadiri ya uwezo wa kila mmoja alivyomuumba. Kila mtu amejaliwa karama kwa viwango tofauti na mwingine. Tumepewa karama hizo ili tuzitumie kwa manufaa yetu na kwa manufaa ya wengine. Mfano huu unatukumbusha kwamba kipawa au karama uliyojaliwa na Mungu iwe kubwa au ndogo lazima itumike katika kumtumikia Mungu katika viumbe wake. Kadiri tunavyotumia vizuri vipaji na karama tulizojaliwa ndivyo tutakavotunukiwa taji ya utukufu mbinguni kama kwa wale watumwa wawili waliofanya vizuri.
Na tusipovitumia vizuri vipaji tulivyojaliwa, tutaadhibiwa na kunyang’anywa uzima wa milele tulioahidiwa. Mara nyingine tunashindwa kutumia karama zetu tulizojaliwa kwa kisingizio kwamba ni chache, kwa hiyo hatuwezi kufanya lolote au hatuwezi kuchangia chochote. Hakika tutafanana na yule mtumwa aliyeshindwa kuitumia talanta moja aliyopewa. Tukumbuke kuwa kipawa chochote ulichonacho ukikitumia ipasavyo katika mazingira mbalimbali kipawa hicho kitakua na kustawi vizuri zaidi. Tofauti na yule ambaye amejaliwa kipawa fulani halafu hakitumii au hakifanyii kazi hatimaye kitakufa. Jinsi tunavyojituma kwa akili na nguvu zetu zote kuvitumia vipawa vyetu ndivyo tutakavyofaidi zaidi matunda yake. Tunaalikwa tunapoendelea kumsubiri Kristo, kila mmoja kwa kadiri ya karama au vipawa alivyojaliwa, kuvitumia kwa nguvu zote ili alete mabadiliko ya kiroho, kimwili na kijamii. Vipawa vyetu vitusaidie katika kumtumikia Mungu na jirani. Pia vitusaidie katika kupambana na umaskini, njaa, ujinga na magonjwa mbalimbali. Tukitaka kutumia vema karama zetu, hatuna budi kuondoa hofu, uvivu na ubinafsi na kujivika moyo wa kudhubutu, kujaribu na ujasiri na majitoleo. Basi kila mmoja afanye jitihada za kutambua vipawa alivyopewa na Mungu na avitumie ipasavyo katika kumtumikia Mungu na jirani. Hatimaye tuweze kupata tuzo toka kwa Kristo atakapotwambia; “Vema mtumwa mwema na mwaminifu, ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi. Ingia katika furaha ya Bwana wako.”
Kumbe tunakumbushwa kuwa mwisho wa yote hata kwa kidogo ulichojaliwa na Mungu utatakiwa kutoa hesabu yake ni jinsi gani ulivyokitumia kwako mwenyewe na kwa ajili ya wengine. Hivyo, tumwombe Mungu atusaidie tuwe watumishi wema na waaminifu tunaokaa macho ili siku ya hukumu isitupate ghafla bali tuwe tayari kutoa faida kwa vipawa tulivyopewa. Kama somo la kwanza kutoka kitabu cha mithali linavyosisitiza kuwa mke mwema, mwenye hekima na uchaji kwa Mungu kuwa daima anafanya kila awezalo ili ampendeze bwana wake ndivyo ulivyo uhusiano wa Kristo na Kanisa (Ufu 19:7-9; Eph 5:25-27). Kama mke mwema na mwenye hekima anavyokuwa mwaminifu kwa mme wake, ndivyo mkristo anavyopaswa kuwa mbele za Mungu. Jinsi mke mwema anavyojitahidi kumpendeza bwana wake, ndivyo mkristo anavyopaswa kumpendeza Mungu kama mtumishi mwema na mwaminifu aliyetumia vyema talanta alizopewa. Kama ilivyo kwa mke mwema kuwa moyo wa mume wake humwamini ndivyo ilivyo kwa mkristo mwema, Mungu humwamini na kumpatia majukumu zaidi na kumjaza neema na baraka zake, imani yake haitatetereka hata nyakati za majaribu na siku ya mwisho haitampata ghafla. Mkristo mwenye hekima anafanya kazi na kutimiza wajibu wake kwa kanisa, kwa familia yake na kwa jamii yake kwa kuwakunjulia maskini mikono yake. Anaweka vipawa vyake viwanufaishe wengine na kuwasaidia wahitaji. Bwana atamsifia kama mke mwema asifiwavyo na bwana wake naye Mungu atamwambia: vyema mtumishi mwema na mwaminifu umekuwa mwaminifu katika machache nitakuweka juu ya wengi.
Mungu humjalia kila mtu vipawa vyake tofauti na vya mwingine kama vile anavyomuumba kila mtu tofauti na mwingine na kila mmoja anapewa wajibu wake binafsi na kila mmoja ana nafasi ya pekee kabisa katika maisha yake (Rum 12:6) kama vile mmoja alivyopewa talanta 5, mwingine 2 na mwingine 1. Hii inatufundisha: Usijilinganishe na wengine. La muhimu si kuwa na vitu vingi bali namna unavyovitumia. Usilalamike kwamba una vitu vichache. Mungu hatakudai zaidi ya uwezo wako. Usiogope kutumia kidogo ulichonacho kwa faida ya wengine. Usiogope kutoa zaka au moja ya kumi kwasababu wewe huna mshahara mkubwa. Usiogope kumsaidia mtu eti kwasababu hauna vitu vingi. Utafute utakatifu kwa namna ya maisha yako. Kama umeoa au umeolewa usitafute utakatifu kama Mtawa au Padre. Utakatifu upo katika ndoa yako na familia yako. Na kama ni mtawa au padre usitafute utakatifu kama mtu wa ndoa. Utakatifu wako uko katika wito wako wa utawa au upadre. Kama ni mfanyabiashara, utafute utakatifu katika biashara yako. Kama ni mtoto au kijana, usiseme nitakuwa mtakatifu nikiwa mzee bali uuishi utakatifu katika hali yako ya sasa uliyonayo.
Tuzo ya kufanya kazi vizuri ni kupewa kazi zaidi. Wale walioleta faida kwa talanta walizopewa hawakuambiwa njooni mpumzike; walipewa majukumu makubwa zaidi. Tunapomtumikia Mungu vizuri tusitegemee maisha rahisi; yanaweza hata yakawa magumu zaidi na majukumu yakaongezeka. Hii ni kwasababu Mungu akituona kuwa tu wema na waaminifu kwa kazi yake anatuongezea majukumu zaidi. Kama tumeonyesha uvumilivu, kwa mfano, atatuongezea magumu zaidi ili tuendelee kuwafundisha wengine kuwa wavumilivu. Kipaji usipokitumia kina kufa. Ni vipawa gani tumepewa: ni jumla yetu tulivyo na tulivyonavyo ni zawadi kutoka kwa Mungu uhai, afya, ujuzi, imani, fadhila, muda, cheo, elimu, nafasi yako katika jamii na mengine mengi. Kumbe kila ulichojaliwa yakupasa kikufae wewe, kiwafae na wengine ili waone uwepo wa Mungu katika maisha yao na hivyo wamtukuze Mungu. Uwezo wowote unahitaji mazoezi ili kuuendeleza. Usipojitokeza na kuyafanyia kazi uliyopewa utabaki ulivyo wala hutaendelea.
Basi tumuombe Mungu atujalie ujasiri tusiogope kujaribu na kuthubutu kama aliyepewa talanta moja alivyogopa kuifanyia kazi na kwa sababu hiyo aliadhibiwa. Usiogope kujitokeza na kuonyesha vipaji vyako ukichelea kupewa majukumu makubwa zaidi. Usiogope kusaidia hata kama una kidogo ukichelea kikiisha utafanyaje. Usiogope kuanzisha kitu fulani kizuri ukichelea kuwakitatumia muda wako mwingi au kukuingiza katika gharama. Jaribu, fanya kadiri ya uwezo wako na Mungu atamalizia. Mungu humsaidia anayejaribu. Usitafute maisha rahisi kwa kuficha uwezo wako. Utabaki hivyo, hautakuwa au kuendelea.