Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Neema za Mwaka Mpya!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Heri na baraka tele zake Mtoto Yesu tunapomaliza na kuanza mwaka mpya! Kabla ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Liturujia ya Januari mosi ilikuwa ni juu ya kutahiriwa kwake Mtoto Yesu maana ni siku ya nane baada ya kuzaliwa kwake Mtoto Yesu. Rejea Luka 2:21 Liturujia baada ya Mtaguso Mkuu wa Oili wa Vatican inaitenga siku ya kwanza ya Mwaka kuwa ni Sherehe ya Bikira Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu. Ni mwendelezo wa fumbo la Noeli la Mungu kufanyika mwili na kukaa kwetu na hivyo Mariamu ni Mama wa Mungu. Pia Baba Mtakatifu Paolo VI mwaka 1968 akaitenga siku hii kuwa pia ni siku ya kuombea amani ulimwenguni maana ujumbe wa Malaika siku ya Noeli ni Amani kwani Mtoto aliyezaliwa ni mfalme wa amani.
Katika Maandiko Matakatifu siku ya leo tunasikia juu ya maudhui mbalimbali, mathalani, Baraka za kuanza Mwaka Mpya, Bikira Maria kama kielelezo cha kila mama na kila mfuasi wa Yesu Kristo, Amani, Uana wa Mungu, Upendo wa kimungu na utambulisho wa jina la Mwana wa Mungu. Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha Hesabu, tunaona Musa anapokea kutoka kwa Mungu kanuni ya jinsi ya kubariki, inayopaswa kutumiwa na ukoo wa kikuhani wa Haruni. Kanuni hii ilitumika kila siku na makuhani katika Hekalu kwa kuwabariki Wanawaisraeli. Kuhani alisimama katika lango la patakatifu na kuwanyooshea watu mikono yake na kuwabariki kwa maneno tuliyosikia katika somo la kwanza. Uso wa Mungu unaotung’alia ni ishara ya urafiki na kupokea upendeleo wa Mungu katika maisha yetu. Hivyo kuhani aliruhusiwa kutamka Jina la Mungu yaani YHW mara tatu, ili kumuomba Mungu awabariki watu wake na kuwafadhili, kuwajalia upendeleo.
Kubariki ni kumnenea mema mwingine, ndio kumtakia matashi mema, ni maneno ya upendo kwa mwingine, ni kumtakia mafanikio mwingine, ni kumzungumzia vizuri mwingine. Hivyo, tunapouanza mwaka mpya, kila mmoja wetu anamtakia mwingine matashi mema, lakini kwetu sisi wakristo tunatambua kila mema yanatoka kwa Mungu, na ndio maana tunakuja kwake ili atubariki, ili atunenee yaliyo mema katika mwaka mpya. Na wanawaisraeli walipaswa pia kumbariki Mungu na ndio kuenenda kadiri ya Neno na Maagizo na amri zake. Wapendwa tunapomuomba Mwenyezi Mungu atubariki kwa Mwaka Mpya nasi hatuna budi kumbariki Muumba kwa kuishi kadiri ya Neno lake. Kumbariki Mungu ndio kuziimba na kuzinena sifa zake kwa maneno na hata kwa maisha yetu ya siku kwa siku. Ni matamanio yetu kuwa maisha yetu kila siku yawe ya kutangaza makuu ya Mungu, Huruma na Upendo wake kwetu.
Waraka wa Mtume Paolo kwa Wagalatia unatuonesha kuwa nasi tumefanyika wana wa Mungu kwa njia ya Ubatizo wetu. Ni kushirikishwa maisha ya neema ya Kimungu. Ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu tuliyempokea ile siku ya Ubatizo wetu nasi tunamuita Mungu, Abbà, yaani Baba. Fumbo la Noeli, ni fumbo la kufanyika nasi wana wa Mungu kwani Mwana wa Mungu ameutwaa ubinadamu wetu kwa kuja na kukaa kati yetu. Katika Injili leo tunasikia tena sehemu ya Injili ya Luka, linaloeleza juu ya simulizi la kuzaliwa kwake Mtoto Yesu. Wachungaji walienda kwa haraka na kumkuta mtoto amevishwa nguo za mtoto mchanga na kulazwa sehemu ile ya kulishia wanyama. Hakuna la ajabu au la pekee wanaloliona maana ni kawaida mtoto mchanga kuvishwa nguo na hasa iliyozungushiwa kufunika mwili mzima ili kumkinga na baridi ila pia kadiri ya mila za kiyahudi alikuwa bado najisi mpaka siku ile ya kutakaswa kwao hekaluni. Wachungaji pamoja na kumkuta mtoto Yesu kama watoto wengine ila waliweza kumtambua mtoto Yesu kama Masiha. Wachungaji waliotengwa na kuonekana najisi na wadhambi na hata wasiofaa kukaribiwa kwa harufu zao mbaya za wanyama, ndio wanakuwa wa kwanza kukutana na Mtoto Yesu.
Ni fumbo la upendo wake Mungu kwa mwanadamu. Ni Mungu anajionesha kwanza kwa wadhambi na watu duni. Wachungaji walibaki na mshangao na furaha. Na ndivyo Mungu anavyojionesha kwetu na kujidhihirisha kwetu. Yatosha kuomba kuwa na jicho la imani kuona ukuu wake unaotuacha mara nyingi wenye mshangao na furaha. Mwenyezi afiki kwetu mara moja na kuanza kutupa amri na maagizo, badala yake anaonesha upendo na ukuu wake kwako na kwangu. Na ndio Habari Njema kuwa tunakutana na upendo wa Mungu kwa mwanadamu aliye mdhambi na dhaifu. Mama yetu Bikira Maria tunasikia kuwa aliyaweka haya yote moyoni mwake, kuyaweka moyoni mwake maana yake ni nini? Kwa kweli sio tu kuyakumbuka bali kuyaweka pamoja maana hakuelewa haya yote pale mwanzoni. Kuyaweka pamoja ili mwishoni kutambua mpango wa Mungu kwa huyu Mtoto aliyezaliwa na hata kwake pia. Na ndio mwaliko wa maisha yetu ya kiimani kumuona Mungu katika maisha ya siku kwa siku, ni Mungu anayesafiri na kutembea nami katika maisha ya kawaida kabisa. Ni kuomba jicho la imani kama Mama yetu Bikira Maria ili kumuona Mungu katika maisha yetu.
Mwanzoni Bikira Maria haelewi nini maana yake ila anaangalia kwa makini, anasikiliza, anatafakari na hivi baada ya fumbo la Pasaka ndipo atakapoelewa nini maana yake haya yote. Ni fumbo la upendo wa Mungu katika historia ya mwanadamu. Mtoto Yesu kwa kutahiriwa kwake siku ya nane anaingia rasmi katika jamii au taifa lile la wanawaisraeli. Mwinjili Luka hasa sio tu anataka kutuambia juu ya kutahiriwa kwake Mtoto Yesu bali hasa juu ya Jina la Mtoto ambalo ni YESU au kwa Kiebrania YESHUA, maana yake BWANA ANAYEOKOA. Jina kwa wayahudi lilimtambulisha pia aina gani ya mtu aliyebeba jina fulani na ndio maana hata Mungu alipowateua na kuwaita watu mbalimbali pia aliwapa majina. Jina linabeba utambulisho wa misheni na aina ya mtu. Rejea Matayo 1:21 kwani atawakomboa watu wake kutoka dhambi zao. Tunaposoma Injili ya Luka tunabaki na mshangao pia kwao wanaomtambua Mwana wa Mungu kwa jina la Yesu ni wale waliokuwa wanasumbuliwa na nguvu giza au kila uonevu; mathalani wenye pepo wachafu Luka 4:34, wenye ukoma Luka 17:13, kipofu Luka 18:38, mwizi aliyeteswa pamoja na Yesu pale msalabani na kuomba aokolewe na Yesu Kristo Luka 23: 42. Mifano hii inatosha kutukumbusha kuwa nasi pale tunapopita katika magumu na mateso ya maisha ya siku kwa siku hatuna budi kumuita Jina lake aliye Mwokozi wetu naye kwa hakika atatuokoa. Nawatakia nyote mwaka mpya wenye kila neema na baraka zake Mtoto Yesu na tujiweke sote chini ya maombezi ya Mama yetu Bikira Maria, Mama wa Mungu na Mama yetu pia.