Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, "Theotokos": Mtaguso wa Efeso wa Mwaka 431
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tarehe Mosi Januari 2021, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, “Theotokos” sanjari na Siku ya 54 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2021. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya unaongozwa na kauli “Utamaduni wa Utunzaji Kama Njia ya Amani”. Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema kwamba, Mwenyezi Mungu ni kiini cha wito wa binadamu kutunza. Mwenyezi Mungu Muumbaji ni mfano bora wa wito wa utunzaji unaoshuhudiwa pia katika utume wa Kristo Yesu na hatimaye, kunafsishwa katika utamaduni wa utunzaji unaoshuhudiwa na wafuasi wa Yesu. Utunzaji ni kiini cha Mafundisho Jamii ya Kanisa mintarafu utamaduni wa utunzaji unaohimiza: utu na haki msingi za binadamu; utunzaji wa mafao ya wengi; utunzaji kwa njia ya mshikamano pamoja na mchakato wa utunzaji bora wa mazingira, dira ya njia ya pamoja. Kumbe, kuna haja ya kuwafunda watu utamaduni wa utunzaji kwani hakuna amani, ikiwa kama hakuna utamaduni wa kutunza na kujaliana!
Bikira Maria Mama wa Mungu: Kwa lugha ya Kigiriki: Theotokos, Θεοτόκος; kwa Kilatini “Deipara” au “Dei genetrix”. Katika tafakari hii tungependa kugusia kwa ufupi historia kuhusu: kiri ya imani kwa Bikira Maria Mama wa Mungu, Bikira Maria Mama wa Kristo; mfano bora wa kuigwa katika kulinda na kudumisha imani inayomwilishwa katika ushuhuda. Ilikuwa ni tarehe 26 Juni 431 katika maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso, Mababa wa Kanisa walipotamka kwamba, yule ambaye Bikira Maria amemchukua mimba kama mtu na ambaye amekuwa ni Mwana wake kadiri ya mwili, ndiye Mwana wa milele wa Baba, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linaungama kwamba, kweli Bikira Maria ni “Mama wa Mungu” “Theotokos, Θεοτόκος”. Hiki ndicho kiini cha Taalimungu na Ibada kwa Bikira kwa sababu mhusika mkuu ni Mwenyezi Mungu. Katika Agano Jipya, Bikira Maria anatambulikana kuwa ni Mama wa Yesu.
Tangu mwanzo, Kanisa lilimtambua Bikira Maria kuwa ni Mama wa Mungu lakini kiri hii ya imani ikaendelezwa na kufikia kilele chake kwenye Mtaguso wa Efeso ili kukukabiliana na changamoto zilizoibuliwa na wazushi wa nyakati zile, waliokuwa wanapinga Umungu wa Kristo. Mtaguso wa Efeso ukaweka mafundisho haya kuwa ni sehemu ya Kanuni ya Imani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kanisa. Kristo Yesu alitungwa mimba tumboni mwa Bikira Maria kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kumbe, Kristo Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli. Katika karne ya tatu kulizuka mgogoro kuhusu Umungu wa Kristo na Ubinadamu wake. Mtaguso wa Efeso ulifafanua kwa kina na mapana kuhusu imani ya Kanisa na kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Waamini wa Efeso wakashangilia sana na huo ukawa ni mwanzo wa kukua na kuendelea kuimarika kwa Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu tangu wakati huo hadi sasa.
Bikira Maria ni Mama pia wa maisha ya kiroho kama alivyofafanua Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Bikira Maria alitekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, akawa ni zaidi ya mfuasi wa Kristo kwa sababu alikuwa kwanza kabisa ni Mama wa Kristo. Huu ni uhusiano wa ndani kabisa uliojengeka kati ya Bikira Maria na Kristo Yesu kutokana na imani thabiti ya Bikira Maria. Bikira Maria Mama wa Mungu ni cheo kikubwa kutokana na upendeleo na neema aliyopata kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hiki ni kiini cha imani ya Kanisa. Bikira Maria Mama wa Mungu kama anavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu anapaswa kuwa ni kiungo cha umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo na kamwe asiwe ni sababu ya mipasuko na utengano.