Sherehe ya Noeli 2020: Fumbo la Umwilisho Ni Fumbo la Mshangao!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Noeli inatualika sote kuwa wema na wakarimu! Ni upendo unaotokana na mshangao wetu kuona Neno wa Mungu, Mungu anatwaa mwili wetu na kuishi kati kati yetu. Kwa namna ya pekee kabisa, mwaka huu, Baba Mtakatifu Francisko anatualika sote kuomba neema ya mshangao, ndio neema ya kuja mbele yake Mtoto Yesu na kuutafakari kwa kina upendo wake wa Kimungu kwetu wanadamu. Tena amefanyika mwanadamu sio kwa ajili ya watu wenye haki bali sisi tulio wadhambi na wakosefu. Ni mwaliko wa kila mmoja wetu katika maadhimisho ya Noeli kufika na kutafakari mbele ya pango la mtoto Yesu. Ni hapo tunabaki na mshangao, kumuona Mungu anazaliwa katika hali duni kabisa, ishara tunayoalikwa kama wachungaji kwenda kuiona pangoni, si nyingine bali ni Mungu anayekuwa zawadi kwa kila mmoja wetu, ni Mungu anayetwaa ubinadamu wetu, anayekubali kujimwilisha na kuwa na hali duni sawa na kila mmoja wetu. Ni fumbo linalotuacha na mshangao!
Wachungaji walitoka na kwenda kwa haraka Bethlehemu, ndivyo nasi leo tunaalikwa kutoka kwa haraka na kuelekea Bethlehemu. Ni mwaliko wa kufanya safari hiyo kiroho ili tukaone hiyo ishara kubwa, ya Maria amezaa mtoto wa kiume na kumvisha mavazi ya kitoto na kumlaza katika hori la kulishia wanyama. Mtoto aliyezaliwa ni mtoto kama watoto wengine, lakini tunapochukua muda wa kumtafakari zaidi ni hapo tunapogundua kukutana na upendo wa Mungu katika hali ile duni na dhaifu kubwa. Noeli ya kweli inatualika tangu awali kuingia ndani na kulitafakari fumbo hilo, itakuwa ni bahati mbaya sana kuacha kutenga muda wa kuutafakari wema na upendo wa Mungu kwa mwanadamu hasa katika maadhimisho haya ya Noeli. Leo hii, Noeli imekuwa sherehe kubwa inayosherekewa sio tu na waamini wakristo bali hata na wale wasioamini katika Kristo. Lakini, sisi kama waamini tunaalikwa kutoishia katika mashangilio ya juu juu na badala yake kuona ni katika Noeli kwa jicho la Injili.
Ni maadhimisho ya Mungu kuingia katika historia ya mwanadamu, katika maisha ya kila mmoja wetu. Ni Neno wa Mungu anayetwaa mwili na kuwa mwanadamu isipokuwa hakuwa na dhambi, ni uumbaji mpya wa ulimwengu wa nuru ya Mungu kuja na kukaa kati yetu, ni Mungu anakuja ili kututoa katika giza la dhambi na maovu. Noeli ni kukubali Mungu kubadili maisha yetu. Kwa bahati mbaya sana, leo Noeli imekuwa ni sherehe ya kimwili zaidi kuliko ya kiroho. Noeli imeanza kupoteza umaana wake, kwani wengi wetu tumebaki kuiangalia Noeli kwa kuongozwa na mantiki za kiulimwengu hasa ulimwengu wa vitu zaidi, ndio inabaki kuwa Noeli ya mavazi mapya, kula na kunywa, kupeana zawadi na kufanya kila aina ya anasa na starehe. Huko ni kushindwa kuonja upendo wa Mungu kwa kila mmoja wetu, ni kupotoka kwa kuacha kuongozwa na tangazo lile la malaika kutoka mbinguni. Malaika wanatualika leo nasi tutoke katika maisha yetu ya kila siku, maisha ya kubaki gizani ili twende kumuona aliye nuru na mwanga wa kweli.
Baba Mtakatifu anatualika tena kujitafakari katika maadhimisho ya mwaka huu ili kuepuka na mtego wa kupoteza maana halisi ya Noeli, kwani wengi leo tunaishia katika kutakiana matashi na salamu za Noeli, kupeana zawadi, kuvaa vizuri, kula na kunywa na kusahau utajiri wa maadhimisho ya Noeli. Noeli ni maadhimisho yanayotualika kuutafakari tena ubinadamu wetu. Na ndio kiini cha maadhimisho haya ya kumtafakari Mungu anayejitoa zawadi kwetu wanadamu, anayechukua ubinadamu wetu na kuishi kati kati yetu, yaani, Emanueli, Mungu pamoja nasi. Kiini cha maadhimisho ya Noeli ni: “Naye Neno akawa mwanaadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli.” Yohane 1:14. Maneno haya ambayo tumeyasikia katika somo la Injili ya leo, ndio hasa kiini cha maadhimisho ya sherehe za Noeli. Na ndio tunaalikwa kwenda kwa haraka pangoni ili tunaione ishara ya Mungu kukaa kati kati yetu, ya Neno anayetwa mwili na kuwa sawa nasi isipokuwa hakuwa na dhambi.
Noeli ni kutafakari tena historia yetu wanadamu, historia iliyojeruhiwa na dhambi, ndio tunaalikwa sasa kwenda kumtafakari yule aliyejaa neema na ukweli, aliyejaa huruma ya Mungu, aliye pia Mwokozi na Mkombozi wetu wanadamu. Ni pangoni tunakutana na upendo wa Mungu kwetu, anayekuja ili kutukomboa na kututoa katika utumwa wa kila hali na namna na hivyo kutujalia kuwa na uzima wa kweli. Ni mwaliko wa kuwa rafiki zake Mungu, kwani Mungu anakuja ili mwanadamu aingie katika historia ya mahusiano ya upendo naye. Mungu anajitoa kwetu kama zawadi, ni neema, hivyo sio mastahili yetu, sio malipo ya wema wetu bali ni wema usio na masharti wala mipaka wake Mungu mwenyewe. Noeli ni nafasi ya kuutafakari tena wema na upendo wake Mungu kwetu. Nasi tukiwa mbele ya pango la mtoto Yesu, hakika hapo tunabaki na mshangao utakanao na ukweli wa Mungu kukubali kuutwaa mwili duni ili aingie katika mahusiano mapya na mwanadamu aliye mdhambi na mkosefu.
Leo duniani inaposherehekea Noeli katikati ya janga la homa kali ya mafua inayosababisha na Virusi vya Corona, COVID-19, tunakubali sote jinsi tulivyo duni na dhaifu kwa kuwa wanadamu, lakini tunafarijiwa na ujumbe au tangazo la Noeli, la Mungu anayetwaa mwili na kukaa kati kati yetu. Ni Mungu anayekuja ulimwenguni kama mtoto mchanga aliye duni na dhaifu, asiye na uwezo wa kujitetea yeye mwenyewe. Ni huyu tunaalikwa kwenda kumuona pangoni Bethlemu, ndio ishara ya Noeli, ndio kiini cha maadhimisho ya Noeli. Ni katika uduni na unyonge wetu, Mtoto Yesu anatwaa unyonge na uduni wetu. Mungu hamwangalii mwanadamu kutoka mbali, juu mbinguni, bali anakuja na kukaa kati yetu na hata kutwaa hali yetu duni na dhaifu ya kuharibika na kutabika na kuteseka, na kuugua kama sisi. Yesu si alionekana kama mwanadamu bali ni mtu kweli sawa na mimi na wewe, ndio mshangao tunaobaki nao kila mara tunapolitafakari fumbo la Noeli, fumbo la Umwilisho wake Yesu Kristo.
Noeli ni maadhimisho ya upendo wa Mungu kufanyika mwanadamu, ni katika mtoto Yesu hapo tunauona upendo wa Mungu kwetu. Mungu anayetaka kubaki na kusafiri na historia ya mwanadamu, ya kuwa pamoja nasi, sio Mungu anayetuacha na kutuangalia kwa mbali bali anayetaka kuwa na hisia na hali moja nasi isipokuwa hakuwa na dhambi. Ni Mungu anayebaki nasi siku zote katika Kanisa lake, kwa njia ya Neno lake na masakramenti yake. Mtoto anayezaliwa ni nuru ya ulimwengu, inayokuja ili kutuangazia wanadamu, ili tuweze kutembea katika nuru na mwanga wa kweli. Ni nuru inayokuja ili kufukuza giza katika maisha ya kila mmoja, ili tuweze kutembea kwa uhakika kwa uwepo wa hiyo nuru, ndio Neno lake linalopaswa kuongoza maisha yetu ya siku kwa siku. Mtoto Yesu anazaliwa ili sisi tuweze kuwa kweli wana wa nuru, kwa maisha yetu. Noeli ni kukubali kuwa wana wa mwanga wa kweli, mwanga utokao kwa Baba wa mbinguni. Ni nuru inayotoa maana ya kweli ya maisha yetu.
Baba Mtakatifu anatualika kukaa mbele ya pango la mtoto Yesu ili hapo kwa mshangao tuweze nasi kama wachungaji kuutafakari upendo wa Mungu, na pia hapo tuweze kumwabudu Mtoto Yesu, aliye Mungu kweli na Mtu kweli. Ni hapo tunakiri nasi Kanuni ile ya Imani ya Nicea, ni hapo tunakutana na Mungu kweli na Mtu kweli, na yule aliyetwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na kufanyika mwanadamu na kukaa kati yetu. Pango la kuzaliwa Mtoto Yesu, ambayo baadhi tunayo katika makanisa yetu na hata majumbani, ni mahali pa katekesi ya kweli, katekesi ya fumbo la Umwilisho, kama ambavyo tunasoma katika Injili juu ya masimulizi ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo katika mji ule wa Bethlehemu miaka elfu mbili iliyopita. Ukweli huo unabaki kuwa halisi hata leo kila mara tunapokubali kufika na kuongozwa na neema ya mshangao ili tuweze kuuonja nasi upendo wa Mungu anayejitoa zawadi ya Noeli kwa kila mmoja wetu. Ni hapo mbele ya pango tunatambua zawadi ya kweli ya Noeli, si kitu bali ni Mungu mwenyewe anayejitoa kwako na kwangu, anayetaka kuwa Neno la uzima katika maisha yetu, anayetaka kuwa nuru na mwanga wa maisha yetu, zaidi sana nasi tuweze kuomba neema ya kumpokea ili neema na utukufu wake Mungu utawale maishani mwetu.
Leo katika ulimwengu ambapo upendo wa kweli umekuwa ni bidhaa adimu, tunaalikwa tena kufika mbele ya Pango la Mtoto Yesu, kwa msaada wa neema ya mshangao, nasi ndani mwetu iweze kuamka ile shauku na hamu ya kuwa watu wenye upendo wa kweli, upendo wa kujishusha na hata kujisadaka kwa ajili ya wengine na hasa wanaokuwa wanyonge na duni zaidi. Ni kwa njia yetu wengine waweze kuuonja wema na upendo wa Mungu kwa watu wake. Noeli, kama sherehe ya upendo basi basi hatuna budi siku hizi za Noeli kuonesha upendo wetu kwa wengine, iwe katika familia zetu, jumuiya zetu, mitaa yetu, maparokia yetu, makazini na kadhalika na kadhalika. Tunapokula na hata kunywa tuwakumbuke watu wengi popote duniani wanaokuwa na dhiki na njaa na kiu. Je, ni ujumbe wa Noeli kula na kunywa na hata kusaza wakati wengine wakifa kwa njaa na kiu, au wakitembea uchi kwa kuwa mimi nimejinunulia mavazi na zawadi za gharama kubwa? Kila mmoja wetu anaalikwa kuingia ndani mwake na kujiuliza, kila mmoja achukue wasaa na muda mbele ya pango la Mtoto Yesu kuutafakari upendo wa Mungu, Mungu anajitoa zawadi sio kitu bali ni yeye mwenyewe kwa ajili yetu. Je, nasi tuna nini cha kujifunza tunapokuwa mbele ya pango la Mtoto Yesu? Nawatakia maadhimisho mema yenye kila neema na baraka zake Mtoto Yesu.
“Et Verbum caro factum est et habitavit in nobis ; et vidimus gloriam eius, gloriam quasi Unigeniti a Patre. Plenum gratiae et veritatis. YOHANE 1 :14